Saturday, March 30, 2019
MAFUNZO YA TATHIMINI YA VIMELEA HATARISHI VYA MAGONJWA KWA DHANA YA AFYA MOJA YAFANYIKA KWA MARA YA KWANZA BARANI AFRIKA NCHINI TANZANIA.
Kwa mara ya kwanza Barani Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza
kufanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Afya moja juu ya namna ya kufanya tathmini ya vimelea hatarishi vya
magonjwa kwa kutumia dhana ya Afya moja. Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalam
na wadau wa Afya moja kutoka sekta mbalimbali, hususan sekta za afya ya binadamu,
wanyama, kilimo na mazingira.
Kufuatia nchi ya Tanzania kuwa imepiga hatua
katika uratibu wa masuala ya Afya moja,
ambayo ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo
na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa
yanayoathiri binadamu, hali hiyo imechagiza kuchaguliwa kuwa nchi ya kwanza
barani Afrika kwa wataalam wa sekta za
Afya hapa nchini kupewa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 25-28 Machi, 2019, Jijini
Dar es salaam, yaliendeshwa na wataalamu kutoka Makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Makao makuu ya
Shirika la Chakula Duniani (FAO), pamoja na Shirika linaloshughulika na Afya ya
Wanyama (IOE). Wataalamu hao wameweza kuwapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya
hapa nchini juu ya namna ya kufanya tathmini hiyo kwa magonjwa ya Kichaa cha
mbwa, Kimeta na Homa ya Mafua ya ndege.
Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uratibu
Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, alibainisha kuwa ushirikiano
wa wataalam na sekta za Afya kwa kutumia
dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha amefafanua
kuwa dhana hiyo inapunguza gharama
katika kushughulikia tishio la magonjwa
yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa
binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na hata usugu wa
vimelea vya magonjwa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamebainisha kuwa wamekuwa wakifanya tathmini za vimelela
hatarishi vya magonjwa hapa nchini lakini tathmini hizo zimekuwa ni za kisekta
kwani hazikuwa zinazingatia ushirikiano kwa maana ya dhana ya Afya moja. Aidha
walifafanua kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuandaa nyenzo ya kitaifa ya
kufanya Tathimini kwa Dhana ya Afya Moja ambayo itawaongoza Wataalamu hususani wanapokuwa katika maeneo halisi
yanakotokea magonjwa.
Aidha, washiriki hao
walieleza kuwa Dhana ya Afya Moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea
vingi vinavyo sabababisha magonjwa kwa binadamu asilimia (60%) vinatoka kwa wanyama pori na mifugo na maambukizi
yanatokea pale binadamu anapoingilia maskani ya wanyama hao bila tahadhari.
Hata hivyo, kwa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuzingatia kuwa Bara
la Afrika hususan sehemu zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama (Congo Basin)
ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa(RVF),
Marburg na mengineyo.
Walibainisha kuwa, Kupitia matokeo ya
mwingiliano kati ya wanyama na binadamu, wadau wa afya moja wanawajibika
kupanga mikakati mbalimbali ya udhibiti, ulinzi na usalama katika kuzuia,
kujiandaa na kukabali magonjwa ambukizi. Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na
kimataifa ni kujiandaa kwa kuwafundisha
wataalam wa sekta mbalimbali za
afya jinsi ya kufanya tathmini ya
hatari ya vimelea vya magonjwa ambukizi kwa ushirikiano.
Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya
moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo
Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya
moja kwa kushirikiana na WHO, FAO, IOE na wadau wengine wa Afya moja waliandaa na kuratibu mafuzo
hayo.
Wednesday, March 27, 2019
UJENZI WA MJI WA SERIKALI WAKAMILIKA KWA 99%-MAJALIWA
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema nia ya dhati ya Rais Dkt. John Magufuli ya
kujenga upya mji wa Serikali imetekelezwa baada ya mji huo kukamilika
kwa asilimia 99.
Ameyasema
hayo leo (Jumatano, Machi 27,2019) alipotembelea mji mpya wa Serikali
unaojengwa katika eneo la Mtumba, Jijini Dodoma. Majengo ya wizara 20
yamekamilika.
Katika
ziara yake hiyo, Waziri Mkuu ametembelea na kukagua majengo ya Wizara
13, ambapo amesema ameridhishwa na hatua za ujenzi zilizofikiwa katika
maeneo mengi.
Hata
hivyo katika maengo hayo ya wizara 13 aliyoyatembelea, Waziri Mkuu,
alibaini kasoro kwenye mlango wa kuingilia katika Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira.
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Mkuu amemuagiza mkandarasi anayejenga jengo hilo
auondoe na aweke mwingine kwa kuwa mbao zilizotumika zipo chini ya
kiwango na haupendezi.
Kadhalika,
kuhusu ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
ambayo bado haikamilika, Waziri Mkuu amemuongezea siku 10 mkandarasi na
kumtaka akamilishe.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu wahakikishe kazi
iliyosalia ambayo ni ya kuboresha mazingira ya nje ya ofisi hizo iwe
imekamilika ifikapo Apriri 15, mwaka huu. Mji huo unatarajiwa
kuzinduliwa na Rais Dkt. Magufuli.
Awali,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema ujenzi wa mji huo ulianza
Desemba mwaka jana na ulitarajiwa ukamilike Februari mwaka huu lakini
utakamilika Mei mwaka huu.
Waziri
Jenista alisema ujenzi wa majengo ya wizara tatu ambayo hayajakamilika
ikiwa ni pamoja na OR-TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Wenye
Ulemavu yatakamilika Mei mwaka huu.
Tuesday, March 26, 2019
WIZI WA MITIHANI UNALIVUNJIA TAIFA HESHIMA-MAJALIWA
*Awaonya Maafisa wanajihusisha na wizi waache mara moja
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wanaoshirikiana na waliamu kujihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji wa mitihani waache mara moja tabia hiyo na mwenendo huo kwa sababu unalivunjia heshima na hadhi Taifa.
“Kamati za Mitihani za Mikoa na Wilaya ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila ya woga, upendeleo na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na kiutumishi kwa mujibu wa sheria.Hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa”.
Waziri Mkuuametoa onyo hilo leo (Jumanne, Machi 26, 2019) wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya(REDEOA), uliofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma. Kauli mbiu ya mkutano huo inasema “Elimu Bora Itatufikisha Katika Uchumi wa Kati Ifikapo 2025”
AmesemaBaraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ni chombo ambacho kwa muda mrefu kimejijengea sifa kubwa sana nchini na barani Afrika, ambapo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha rasilimali ili kukifanya chombo hiko kuwa imara na cha kisasa.
Waziri Mkuu amesema hali hiyo imezifanya nchi mbalimbali kuja nchini kujifunza masuala ya upimaji na uendeshaji wa mitihani. “Nimejulilishwa pia hivi sasa hapa nchini wapo Viongozi wa Mabaraza ya mitihani kutoka nchi za Afrika Mashariki”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema suala la tatizo la nidhamu mbaya ya wanafunzi ni jukumu la walimu wote, hivyo wanatakiwa watekeleze majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kuzingatia sheria.
Waziri Mkuu amesema Serikali imesikitishwa sana na matukio ya hivi karibuni ya athari ya viboko kwa wanafunzi shuleni ikiwemo kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu pamoja na tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa shule ya msingi Kibeta Mkoani Kagera.
“Ninatambua si kusudio la walimu kuwadhuru wanafunzi lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni. Maafisa Elimu kawakumbusheni walimu wote nchini wazingatie mwongozo wa kutoa adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 cha sheria ya Elimu sura 353 pamoja na kanuni zake”.
“Adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Na adhabu hii itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi. Nina hakika tukisimamia utaratibu, matukio haya yaliyoanza kuonekana yatakoma”.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo amewapongeza maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya hao kwa sababu wanafanya kazi kubwa ambayo imechangia kupandisha ufaulu wa kidato cha sita na cha nne nchini. Amewasisitiza waendelee kufanya kazi kwa bidii.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka maafisa hao wawe wanatoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Awali, Mwenyekiti wa REDEOA, Germana Mung’aho amesema umoja wao unatekeleza majukumu yao ya kusimamia elimu kikamilifu nchini, lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli, ambaye anasisitiza watu wafanye kazi.
Amesema umoja huo una wanachama zaidi ya 400 na ulianzishwa ili kusimamia utoaji wa elimu nchini. Katika mkutano huo wanatarajia kujadiliana changamoto mbalimbali za sera ya elimu na namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali iwapatie magari maafisa hao watakayoyatumia kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao ya kazi, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.
(mwisho)
Monday, March 25, 2019
YAMETIMIA TANZANIA YAFUZU MICHUANO YA AFCON
*Ni baada ya kuifunga Uganda the Craines magoli 3-0
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars, imekuwa miongoni mwa timu nne zilizofuzu kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kuifunga Uganda 'The Crane' magoli matatu kwa sifuri.
Mechi
hiyo dhidi ya Taifa Stars na Uganda the Craines imechezwa katika Uwanja
wa Taifa leo (Jumapili, Machi 24, 2019) ambapo Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa aliwaongoza Watanzania kushuhudia mechi hiyo.
Taifa
Stars imefuzu michuano hiyo itakayofanyika mwaka huu nchini Misri baada
ya kupita miaka 39 tangu mara ya mwisho kucheza michuanohiyo.Timu hiyo
kwa sasa imeungana na Burundi, Kenya na Uganda kufuzu michuano hiyo.
Magoli ya Simon Msuva, Erasto Nyoni na Agrey Morris yalichangia kuivusha Taifa Stars, ambapoMsuva
alianza kwa kuipatia gori timu ya Taifa ya Tanzania dakika ya 20 baada
ya mechi hiyo kuanza, Nyoni aliipatia Taifa Stars goli la pili dakika ya
50 na dakika sita baadae Moris aliipatia timu ya Taifa goli la tatu.
Kufuatia
ushindi huo wachezaji wote wa Timu ya Taifa ya Tanzania
wamejihakikishia kila mmoja kuondoka na kitita cha shilingi milioni 10
kutoka kwaKamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Akizungumza
na wachezaji hao jana wakati Waziri Mkuu alipotembelea kambi yao,
Makonda ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kamati yake
itatoa sh. milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu
kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kwa upande wake,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala yeye aliwaahidi
kuwapeleka katika mbuga yoyote ya wanyama watakayoichagua kwa ajili ya
mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi dhidi ya
timu ya Taifa ya Uganda.
(mwisho)
Sunday, March 24, 2019
MAJALIWA ASHUHUDIA USHINDI WA TAIFA STARS DHIDI YA YA UGANDA
WAZIRI MKUU ATEMBELEA KAMBI YA STARS
*Kamati yaahidi milioni 10 kwa kila mchezaji, iwapo watavuka
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa na
kuwaeleza kwamba Serikali na wananchi wanamatumaini makubwa kwa timu
yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu
ya Taifa ya Uganda.
Pia,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa
maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana katika soka nchini.
Waziri
Mkuu ametembelea kambi hiyo leo (Jumamosi, Machi 23, 2019) jijini Dar
es Salaam na amewaeleza kuwa Serikali inaimani nao na kwamba wasiwe na
wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine
duniani.
“Macho
yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho na Serikali
inamatumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo waelewe kwamba kesho ni
siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine
yamefikia”.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati yake itatoa sh. milioni 10
kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza michuano ya
Mataifa ya Afrika (AFCON)
Makonda
amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu
yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa
furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi
wamehamasika kwenda kuwashangilia.
Nae,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala ameahidi
kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo
wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya
Taifa ya Uganda hapo kesho.
Dkt.
Kigwangala amesema Serikali ipo pamoja na wanamichezo, ambapo amewataka
wachezaji hao wa timu ya Taifa wakapigane kweli kweli kwa ajili ya
Taifa lao. “Kesho muingie uwanjani kama askari wa nchi. Mkapiganie
ushindi wa Taifa letu”.
Awali,
Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata amesema,”Ninafuraha si kwa sababu
ya ukubwa wa mechi ya kesho bali ni kwa sababu naona kesho nakwenda
kuongoza nchi. Tupo tayari kuliletea Taifa ushindi”.
(mwisho)
MAJALIWA AZUNGUMZA NA WACHEZAJI NA VIONGOZI WA TAIFA STARS
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Soka - Taifa Stars, Mbwana Samata baada ya kuzungumza na wachezaji na viongozi wa timu hiyo jijini Dar es salaam, Machi 23, 2019. |
Saturday, March 23, 2019
WAZIRI MKUU AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA ZAMBIA, ITALIA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia, Mhe. Hassan Simba Yahya kabla ya mazungumzo yao, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Machi 23, 2019. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Italia Nchini, Mhe. Roberto Mengoni, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Machi 23, 2019. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Italia Nchini, Mhe. Roberto Mengoni, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Machi 23, 2019. |
Friday, March 22, 2019
MAJALIWA AFUNGUA KIWANDA CHA KUCHAKATA MUHOGO LINDI
aziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kufungua kiwanda cha kuchakata muhogo cha Cassava Starch of Tanzani Corporation Limited (CSTC) kilichopo katika kijiji cha Mbalala kwenye jimbo la mtama mkoani Lindi, Machi 22, 2019. Wa tatu kulia ni Balozi wa Ufaransa nchini, Frederick Clavier, wa pili kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa CSTS, Christophe Gallean. |
Thursday, March 21, 2019
SEKTA ZA AFYA NCHINI ZA SHAURIWA KUITEKELEZA AFYA MOJA
Na. OWM, MOROGORO
Afya Moja ni dhana
inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu , wanyamapori, mifugo na
mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri
binadamu ,wanyamapori na mifugo.
Kwa kutambua umuhimu wa Afya moja nchini, sekta za
Afya zenye kujumuisha wataalam wa sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya
wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wametakiwa kuanza kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia dhana hiyo ili uimarishaji wa Afya ya binadamu uwe
wa Ufanisi na matokeo bora.
Akiongea wakati wa warsha ya maafisa viungo wa Afya moja kutoka
Wizara, Idara, Taasisi, Mashirika ya
serikali na ya Kimataifa, mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019,
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Matamwe Jimmy, amefafanua
kuwa tayari wataalamu hao wanao Mkakati wa kuzileta pamoja Sekta za Afya kwa ajili ya kuzuia, kukinga na
kuthibiti madhara na magonjwa yanayoikumba nchi yetu, yaani magonjwa ambukizi
kati ya wanyama na binadamu pamoja na usugu wa vimelea vya magonjwa hivyo ni
wakati wa kutekeleza mkakati huo kwa kuitumia dhana ya Afya moja.
“Ninaamini kwamba, wote mnafahamu kuhusu tishio kubwa la magonjwa kama
vile homa ya bonde la ufa, kwenye nchi za Afrika Mashariki , virusi vya Ebola
Afrika Magharibi, kusambaa kwa kiasi kikubwa cha ugonjwa wa mafua ndege,
(HPAI), matatizo ya kupumua yanayosababishwa na virusi vya Corona, mlipuko wa
homa ya Lassa huko Africa Magharibi na homa ya Zika huko Amerika ya Kusini, kwa
hiyo mifano michache magonjwa hayo yamekuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu
na wanyama duniani kote.” Amesisitiza Kanali Matamwe.
Wakiongea
wakati wa warsha hiyo wataalamu wa sekta za Afya hizo wamebainisha kuwa tayari wamekubaliana mfumo wa kutoa taarifa na kuhuisha
utekelezaji wa mpango mkakati wa afya moja nchini.
Tarehe 13 Februari 2018,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa
na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini. Kwa kutambua
umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati
la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana na USAID na Chemonics
International wameandaa mkutano wataalam hao.
MWISHO.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akieleza jambo wakati wa warsha ya maafisa viungo wa Afya moja mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019. |
Mtaalamu wa Afya moja toka sekta ya Afya ya Mifugo, Dkt. Joseph Masambu akichangia juu ya umuhimu wa dhana ya Afya moja nchini wakati wa warsha ya maafisa viungo wa Afya moja mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019. |
Tuesday, March 19, 2019
MAJALIWA AFUNGUA BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO KANDA YA ZIWA JIJINI MWANZA
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Kanda ya Ziwa lililofunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Mtaa wa Posta jijini Mwanza, Machi 19, 2019. |