SERIKALI imeutaka Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN),
ufanye mapitio ya gharama za afya katika hospitali ya Aga Khan ili
wananchi wa kawaida waweze kumudu na kunufaika na huduma za tiba
wanazozitoa.
Imeelezwa
kuwa pamoja na jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya, pia
inatambua mchango unaotolewa na taasisi zisizo za Kiserikali ikiwemo
Hospitali ya Aga Khan katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisasa.
Hayo
yamesemwa leo (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan
jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Amesema
upanuzi wa hospitali hiyo ni miongoni mwa jitihada za kuwafikishia
Watanzania huduma za afya katika maeneo yao na kwa ngazi zote na kwa
gharama nafuu, hivyo amewataka watoa huduma wote nchini waangalie upya
gharama zinazotozwa katika huduma mbalimbali hususan za matibabu.
“Mtakubaliana
nami kuwa gharama zikiwa kubwa hazitawanufaisha wananchi hususan wa
kipato cha chini na wananchi hawataona unafuu wa kutibiwa nchini na nje
ya nchi, hivyo fanyeni mapitio ya gharama hizo.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali inatambua gharama kubwa za uwekezaji na
uendeshaji wa shughuli za afya nchini hususan kwa sekta binafsi. “Lengo
la Serikali kutoa misamaha ya kodi kwa baadhi ya taasisi zisizo za
kiserikali kama Aga Khan ni kuwezesha huduma zinazotolewa kuwa nafuu.”
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema Serikali imeanzisha na kuhamasisha wananchi
kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mwitikio wa ni
mkubwa na lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya
matibabu tena kwa uhakika.
“Nitoe
wito kwa taasisi zote zisizo za Serikali kuunga mkono jitihada hizi za
Serikali na kuhakikisha wananchi wote wananufaika na huduma zenu kupitia
mfumo huu bila kubaguliwa.”
Pia
ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan na Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya wakamilishe majadiliano yao katika matumizi ya NHIF kwenye
hospitali hiyo ya rufaa. “Dr. Konga Mkurugenzi Mkuu wa NHIF upo hapa
kamilisheni mjadala.”
Amesema
nia ya Serikali ni kuona wananchi wanakwenda hapo kwenye jengo hilo
zuri na wanapata huduma kupitia bima ya afya. “Ni matumaini yangu kwamba
jambo hili litafanyiwa kazi kwa kuzingatia maslahi mapana ya pande zote
mbili.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira
mazuri ya uwekezaji, kuimarisha amani na utulivu, ambapo ametoa rai kwa
sekta binafsi ziendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika
kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo nchini kwa kuzingatia sheria
za nchi, utamaduni na mila za Watanzania.
Awali,
Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika
jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya
wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake
sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka
Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Kwa upande wake,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ameupongeza Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan kwa upanuzi wa
hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwani unakwenda kuboresha
huduma za afya nchini.
Amesema
Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan
katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya kutolea huduma za afya ambapo kwa
sasa imeanzisha ushirikiano na sekta ya umma na binafsi kwenye mikoa ya
Dar es Salaam na Mwanza.
NayeBalozi
wa Ufaransa nchini, Balozi Frederic Claiver amesema awamu ya pili ya
upanuzi wa hospitali hiyo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya
Tanzania.
Pia
Balozi huyo amesema Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
kuhakikisha inatimiza mkakati wake wa kukuza uchumi kutoka wa chini
kwenda wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.