WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka menejimenti ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) ijizatiti na kuweka mbinu mpya za kuongeza makusanyo.
Ametoa
agizo hilo leo jioni (Alhamisi, Aprili 18, 2019) wakati alipokutana na
menejimenti ya mfuko huo kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa PSSSF
jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu ambaye aliamua kutembelea ofisi za mfuko huo ili afahamiane na menejimenti
hiyo, amesema amepokea taarifa ya Mkurugenzi Mkuu na kubaini kuwa ukusanyaji wa
michango hauridhishi.
“Mfuko
huu ni wa tofauti na wa NSSF kwa sababu umeunganisha mifuko mingine ya GEPF,
PSPF, LAPF na PPF. Mifuko yote hii ilikuwa na malengo na majukumu yake ya
awali, lakini sasa imeunganishwa kwa hiyo jukumu letu ni moja,” amesema.
“Natambua
mna kazi kubwa ya kusajili wanachama wapya lakini pia tunayo kazi ya kuwafikia
wanachama wa zamani ambao tumewachukua kutoka mifuko mingine na kuhakikisha
kuwa wanaingizwa katika mfuko mpya,” amesisitiza.
“Napenda
kusisitiza kuwa jukumu la kukusanya michango ni la muhimu sana. Ni lazima mjue wastani
wa makusanyo kwa mwezi ni kiasi gani, na kama zimepungua, ni kwa kiasi gani na pia
mtafute ni kwa nini zimepungua,” amesema.
Ameitaka
menejimenti hiyo pia ijiridhishe juu ya uhakiki wa mali walizorithi kutoka
mifuko mingine na izitambue ziko katika hali gani. “Menejimenti peke yenu
hamuwezi kufuatilia mali zote, kwa hiyo wapeni hiyo kazi wajumbe wa Bodi,
wagawane maeneo ili waende kuzitathmini hizo mali na kisha nipate hiyo taarifa,”
amesema.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya utendaji wa
mfuko huo kuanzia Agosti Mosi 2018 hadi Machi 31, 2019, Mkurugenzi Mkuu wa
PSSSF, Bw. Hosea Kashimba alimweleza Waziri Mkuu kwamba majukumu makuu wa mfuko
huo ni kusajili wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa
wanachama.
Alisema
baada ya kuunganishwa kwa mifuko, uandikishwaji wa wanachama uliendelea ambapo
hadi kufikia Machi 2019, jumla ya wanachama wapya 7,575 walikuwa wamesajiliwa.
“Hapo
awali mfuko ulikuwa na wanachama 962,871. Kati ya hao, wanachama 279,564
wanatoka sekta binafsi ambao wamehamishiwa NSSF. Hadi kufikia Machi 31, 2019,
mfuko ulikuwa na jumla ya wanachama 750,943 ambao ni watumishi wa umma
ikijumuisha na wanachama 67,636 waliohamia kutoka NSSF,” alisema.
Kuhusu
ukusanyaji wa michango, Bw. Kashimba alisema moja ya jukumu la mfuko ni
kukusanya michango na tangu Agosti 2018 hadi Machi 2019, mfuko huo ulikuwa
umekusanya jumla ya sh. bilioni 928.31 ikilinganishwa na lengo la lililowekwa
la kukusanya sh. trilioni 1.05 sawa na asilimia 88.62.
Kuhusu
malipo ya mafao, Bw. Kashimba alisema katika kipindi kilichoishia Machi 31,
2019, mfuko huo umelipa mafao ya jumla ya sh. trilioni 1.65.
Alisema
mfuko huo hivi sasa una wafanyakazi 839 ambao kati yao, wanaume ni 470 na
wanawake ni 369.
Kikao
hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, (OWM – Sera, Uratibu, Bunge na wenye
Ulemavu), Bibi Jenista Mhagama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Menejimenti ya PSSSF, katika jengo la ofisi hiyo, jijini Dodoma Aprili 18, 2019. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.