*Ni baada ya Serikali kusikia kilio kutoka kwa wafanyabiashara
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza jitihada za kufuta tozo
zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini
zikiwemo za kwenye pembejeo ili kuwawezesha wafanyabiashara kuzifikisha
hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima.
Ametoa
kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 23, 2019) Bungeni jijini Dodoma wakati
akijibu swali la mbunge wa Madaba, Kizito Mhagama katika kipindi cha
maswali kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango
gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza pembejeo ili kumwezesha
mkulima kupata pembejeo.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara
mbalimbali wakiwemo na wauzaji wa pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika
uendeshaji wa shughuli nzima wa biasharazao.
“Serikali
imesikia vilio vyenu na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo na
itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni aina
gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha ili muendelee kufanya
biashara zenu katika mazingira rahisi.”
Waziri
Mkuu amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali kwa sasa ni kufanya
mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa wafanyabiashara na
kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini, ikiwemo ya
pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba tayari Mawaziri wa kisekta wenye
dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye wizara zao zinazokwamisha
ufanyaji biashara katika mazingira rafiki wameshakutana kwa ajili ya
kujadili namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Hata
juzi nilikuwa na mawaziri hao kupata taarifa zao kwa pamoja kuona
maeneo yote waliyoyapitia na tozo zote zinazokusudiwa kupitiwa upya na
kazi hiyo ikikamilika watakutana na Kamati ya Bajeti ya Bunge, Wizara ya
Fedha ili kuona namna nzuri ya kuondoa tozo hizo. Lakini baadaye suala
hilo litaenda kwenye mamlaka inayotoa ridhaa ya kuondoa au kupunguza
tozo.”
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema miradi mingi ya maji ambayo inatekelezwa kwenye
maeneo mbalimbali nchini baadhi yake haitekelezwi kwa viwango
vilivyokusudiwa, hivyo haiwiani na thamani halisi ya kiasi cha fedha
kinachotolewa.
Hata
hivyo Waziri wa Maji wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2019/2020 alieleza hatua mbalimbali
zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote ambayo haiwiani na kiasi cha fedha
kilichotolewa pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote.
“Moja
kati ya hatua ambazo amezifanya ni pamoja na kuunda timu inayopita
kukagua miradi yote nchini na kujiridhisha kama matengenezo yake
yanakidhi thamani ya fedha iliyotolewa katika mradi huo na kama haukidhi
hatua kali zinachukuliwa kwa wahusika.”
Waziri
Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Korogwe Mjini
Mary Chatanda aliyetaka kujua Serikali kama ipo tayari kuchunguza na
kuchukua hatua kwa watendaji walioshindwa kusimamia miradi ya maji na
kuisababishia hasara pamoja na wananchi kukosa huduma waliyokusudiwa.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.