Wataalam wa sheria kutoka katika sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameshauri kutungwa kwa sheria mpya itakayohusika na ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi ili kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa sampuli za vimelea hivyo kutoweza kueeneza magonjwa kwa binadamu.
Sheria hiyo imeshauriwa kuzingatia dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu, lengo nikusaidia katika kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa kuvichukua vimelea kwa wanyama, binadamu na mimea au wakati wa kuvisafirisha na kuvipeleka maabara kwa ajili ya Uchunguzi na wakati wa kuviharibu mara baada ya kuvifanyia uchunguzi.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano wa kujadili masuala ya kisheria ya Ulinzi na Usalama wa vimelea hatarishi, uliofanyika kwa siku tatu na kufungwa leo tarehe 31 Mei , 2019, Jijini Arusha, kwa pamoja, wataalam wa sekta za Afya na wanasheria wa sekta hizo wamebainisha kuwa uwepo wa sheria hiyo utasaidia kuimarisha usalama na ulinzi kwa wanaohusika na shughuli za vimelea hivyo, mafunzo kwa wataalamu hao, miundo mbinu ya maabara, pamoja na kuainisha orodha ya vimelea hivyo.
Wataalamu wa sekta za Afya walioshiriki mkutano huo, wamebainisha kuwa, sheria hiyo ni ya muhimu kwa kuzingatia kuwa, Dunia imekuwa na tishio kubwa la magonjwa ya kuambukiza yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi na kusababisha madhara makubwa kwa binadamu, mifugo, wanyama pori na kuleta uharibifu wa mazingira. Wamefafanua kuwa, Tafiti zinabainisha kuwa kila mwaka huibuka magonjwa ambukizi mapya kati ya matano hadi Nane duniani. Hivyo inakadiriwa ifikapo mwaka 2030, dunia itakuwa na magonjwa ambukizi mapya 30.
Aidha, wamebainisha kuwa, Tafiti mbalimbali duniani zinaonesha pia, kuwa asilimia 60% ya vimelea vya magonjwa ambayo huambukizwa binadamu vinatoka kwa wanyama hususani wanyamapori na baadae kusababisha magonjwa kwa binadamu.Tayari Tanzania kupitia Dhana ya Afya Moja, imeainisha magonjwa sita ya kupewa kipaumbele ambayo ni; Kimeta, Kichaa cha mbwa, Mafua ya ndege, Homa ya Bonde la ufa, Malale na Ugonjwa wa kutupa mimba wanyama.
Akiongea wakati wa akifunga mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe amebainisha kuwa serikali imedhamiria kuijenga jamii ya watanzania yenye Afya bora kwa kuikinga na majanga yatokanayo na magonjwa ya mlipuko, hivyo ushauri huo wa wanasheria na wataalam wa sekta hizo za afya utaratibiwa kwa uhakika ili kuweza kuijenga jamii salama.
Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.