WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa
Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ukamilishe majadiliano yao na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhusu matumizi ya kadi za NHIF kwenye
hospitali zao ili Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 28, 2019) alipokutana na viongozi
kadhaa wa taasisi hiyo pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu, ofisini kwake bungeni
jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango
unaotolewa na taasisi ya AKDN katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya.
“Nilijionea kazi kazi kubwa inayofanyika pale
Hospitali ya Aga Khan Machi, mwaka huu, niliongea na wagonjwa na kupata maoni
yao, lakini kikubwa tu mpunguze gharama na muimarishe huduma zenu,” amesema.
Amewapongeza
viongozi hao kwa utoaji wao wa huduma kwenye sekta nyingine kama elimu, maji na
kilimo. “Tunategemea mtaendelea kuimarisha huduma hizo ili ziwasaidie
Watanzania wengi zaidi,” amesisitiza.
Viongozi
hao walikutana na Waziri Mkuu ili kumuarifu juu ya mpango wa taasisi hiyo wa
kuanzisha kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini (Specialised Cancer Care
Facility) ambao unatarajiwa kugharimu dola za marekani milioni 15. Kituo hicho
kitaendeshwa kwa ubia baina ya hospitali za Ocean Road, Muhimbili, Bugando na
Aga Khan.
Kwa upande
wake, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alimweleza Waziri
Mkuu kwamba hospitali za Ocean Road na Bugando zinatoa huduma za radiotherapy na chemotherapy, wakati hospitali ya KCMC inatoa huduma ya chemotherapy tu. “Hospitali ya Rufaa ya
Mbeya bado huduma hizo zinaadaliwa ili ziweze kutolewa,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Ummy alisema hivi sasa kwa nchi
nzima, kuna vituo zaidi ya 120 ambavyo vinatoa huduma ya utambuzi wa saratani
(cancer screening).
Mapema, akitoa maelezo kuhusu mpango wa kujenga kituo hicho, Mwakilishi Mkazi wa
AKDN, Bw. Amin Kurji, alisema wameshawasiliana na hiospitali zote tajwa na sasa
wanashirikiana na wataalamu wa wizara ya afya ili kukamilisha suala hilo.
“Tatizo la
saratani hapa nchini ni kubwa kwa sasa. Lakini tunataka watu watambue kwamba
ukiugua saratani haimaanishi kwamba utakufa mara moja (it’s not a death
sentence). Inaweza kutibika endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu,” alisema
Bw. Kurji.
Alisema kwa
sasa hivi hapa nchini hakuna kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini
lakini kitu cha pekee kuhusu kituo hicho ni uwepo wa huduma zinazotembea za
upimaji na utoaji tiba hadi mikoani. “Huduma hizi zitakuwa zinatolewa kwenye
mikoa yote kupitia njia ya mtandao, ilhali vituo vikuu vya Dar es Salaam na
Mwanza vitakuwa vikitoa majibu kwa madaktari husika,” alisema.
Alisema
lengo lao pia ni kutoa elimu juu ya kuzuia, upimaji wa mapema na upatikanaji wa
tiba (prevention, early diagnosis and cure).
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.