WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatakaviongozi
wote na watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa,
wilaya, mkoa hadi wizara kuwajibika ipasavyo na kudumisha nidahmu katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Amesema
ili kufikia lengo na dhamira ya kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali
ya 2019/2020 kwa ufanisi, viongozi hao wanatakiwa waendelee
kuwasisitiza wananchi washiriki ipasavyo kulinda miundombinu inayojengwa
kwa gharama kubwa na Serikali.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa
15 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Septemba
tatu mwaka huu.
Pia,
Waziri Mkuu amezitaka mamlaka husika zishirikiane na wadau wengine
katika kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kukomesha ukataji hovyo wa
misitu, uchafuzi wa bahari, mito na maziwa na taka za plastiki ili
kulinda mazingira asilia.
Akizungumzia
kuhusu bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Waziri Mkuu
amesema Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 33.11, kati yake
sh. trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na
asilimia 63. “Aidha, sh. trilioni 12.25, sawa na asilimia 37 ya bajeti
yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania pamoja na Washirika wa
Maendeleo waiunge mkono Serikali katika kutekeleza vipaumbele
vilivyowekwa kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 ili viweze kutoa mchango
wa haraka katika maendeleo ya uchumi na ya watu.
Wakati huo huo,Waziri
Mkuu amezungumzia kuhusu uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga
kura, ambapo amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha
maandalizi hayo ikiwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu
utakaofanyika mwakani.
“Uboreshaji
huo, unatarajiwa kuanza tarehe 18 Julai, 2019 katika mikoa ya Arusha na
Kilimanjaro ambapo litafanyika kwa muda wa siku 7 kwa kila kituo na
kuendelea hadi tarehe 5 Machi, 2020 litakapohitimishwa katika mkoa wa
Dar es Salaam.”
Waziri Mkuu amesema uboreshaji
huo hautahusisha wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 isipokuwa
utawahusu wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au
watakaotimiza umri huo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu ujao.
Ametaja
kundi lingine litakalohusika na zoezi hilo kuwa ni pamoja na wale
watakaoboresha taarifa zao, kama waliohama jimbo au kata na kuhamia
katika maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza au kadi zao kuharibika,
watakaorekebisha taarifa zao pamoja na kuwaondoa waliopoteza sifa kama
vile kufariki.
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito
kwa wananchi wote wenye sifa kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la
wapiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema kuwa Novemba mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa, ambao ni sehemu muhimu katika kuimarisha utawala bora
na demokrasia ambayo imeendelea kunawiri nchini. Amewataka wananchi
wenye sifa kujitokeza wakati utakapofika.
Amesema
Serikali imeendelea kutumia mbio za mwenge kuhamasisha wananchi
washiriki uchaguzi huo kupitia kaulimbiu isemayo “Maji ni haki ya kila
mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa”.
“Napenda
kutumia fursa hii kutoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa
ujumla hususan wale wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na
kupiga kura ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au
kuchaguliwa katika uchaguzi huo.”
Kwa wananchi wenye nia ya kugombea katika uchaguzi huo, Waziri Mkuu amesema ni
lazima wajue majukumu wanayoomba kwamba yanahitaji umakini mkubwa na
uchapaji kazi kwa sababu Serikali imewekeza miradi mingi kote nchini,
hivyo wanahitajika watu walio tayari kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo
ili itoe matokeo yanayokusudiwa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha
uwepo wa mazingira salama na tulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.