Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.
Jenista Mhagama amezindua rasmi Baraza la Taifa la ushauri
kwa Watu wenye Ulemavu huku akilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa weledi na
ushirikiano ili kuleta tija na mafanikio makubwa kwa Watu wenye Ulemavu nchini.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi huo alisema kuwa baraza linajukumu kubwa katika kuhakikisha usimamizi wa
sekta ya watu wenye ulemavu pamoja na kuishauri Serikali juu ya masuala mbalimbali
ya kundi hilo maalumu.
“Mtambue nafasi mliyopewa
ni dhamana kubwa katika kuwahudumia watu wenye ulemavu ambao ni takribani asilimia
5 ya watanzania, hivyo ni vyema mkashirikiana na Serikali kubuni mikakati
itakayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili wenye ulemavu”, alisema Mhagama
Alifafanua kuwa Baraza hilo
limeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010 na
Sheria hiyo imeeleza majukumu ya Baraza ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri.
“Ni matumaini yangu
mtakuwa washauri wazuri wa masuala ya watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa
kwa wote na si maslahi binafsi,” alisisitiza Mhagama.
Sambamba na hilo alimpongeza
Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Dkt. Lukas Kija kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Wajumbe
wengine kutokana na uaminifu na uwezo walionao katika kusimamia masuala ya Watu
wenye Ulemavu.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea
kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanapata haki zao za msingi na kwa ajili ya ustawi
wao katika Nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, uchumi,
kuwa na miundombinu rafiki pamoja na nyenzo za kujimudu.
Aidha Waziri Mhagama
alitoa rai kwa watendaji wa Baraza hilo kuwa na miongozo yote inayohusu masuala
ya Watu wenye Ulemavu itakayo wawezesha kufanikisha utendaji wao wa kazi.
Kwa Upande wake Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe.
Stella Ikupa amesema kuwa Serikali katika mwaka 2019/2020 itaanza mapitio ya
Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 ili kuwawezesha watu wenye
ulemavu kwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Baraza
la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu Dkt. Lukas
Kija alieleza kuwa wapo tayari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia
sheria, kanuni na miongozo inayosimamia haki na ustawi wa Watu wenye Ulemavu.
Aliongeza kuwa Baraza hilo
lipo tayari kutoa ushauri na hoja zenye tija kwa Serikali juu ya masuala mbalimbali
ya Watu wenye Ulemavu.
Pia, Katibu Mkuu wa Ofisi
hiyo Bw. Andrew Massawe alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kutoa
ushirikiano mkubwa kwa Baraza hilo na kufanya kazi pamoja katika kutatua
changamoto zinazowakabili Watu wenye Ulemavu nchini ikiwemo migogoro na
migongano kwa wadau.
Uzinduzi wa Baraza la Taifa
la Ushauri kwa Watu wenye Ulemavu umefanyika Juni 2, 2019 jijini Dodoma ambapo Baraza
hilo litaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu (2019 hadi 2021) likiongozwa na Mwenyekiti
Dkt. Lukas Kija. Awali Baraza hilo lilikuwa likiongozwa na Dkt. Edward
Bagandanshwa ambalo limemaliza muda wake mwaka 2017.
MWISHO
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.