*Ni katika
mashamba ya mkonge, apokea kilio cha wafanyakazi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri
wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Kazi, Ajira
na wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama aende Makanya, wilayani Same, kwenye
mashamba ya mkonge akatatue kero za wafanyakazi.
“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya
kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, manake watumishi wameweka
malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona wanaoendesha mitambo hawana gloves, wengine wamevaa kandambili
badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu…” alisema Waziri Mkuu.
Ametoa ahadi hiyo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati
akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye
shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro, mara
baada ya kukagua uzalishaji kwenye kiwanda hicho.
Alifikia uamuzi huo baada ya kusoma mabango yaliyokuwa
yakitoa ujumbe juu ya hali mbaya kiwandani zikiwemo malipo ya sh. 3,800 kwa siku;
mikataba mibovu ya kazi; wafanyakazi kutothaminiwa wanapougua na kutoridhika na
mawakala wawili ambao ni UNIQUE na UPANI waliowekwa kusimamia uendeshaji wa
shamba hilo. UNIQUE inasimamia wakata mkonge na UPANI inasimamia kazi ya
upandaji na upanuzi wa mashamba.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alimweleza Meneja wa
Mashamba ya METL likiwemo la Hasani, Bw. Ndekiwa Nyari kwamba uamuzi wa kuweka
mawakala unawapunguzia wenye kampuni mzigo wa usimamizi kwenye mashamba lakini
unaipa hasara kampuni yao.
“Kwa sasa unashughulika na watu watatu au wanne
ambao ni mawakala wakati watu wote wanaokuzalishia wako hapa. Ni vema ungeajiri
hao watu wanne, ukawasimamia kwa karibu na unaweza kuwapa motisha wakifanya
vizuri au kuwafukuza wakiharibu. Lakini kwa sasa hawa mawakala huna mamlaka
hayo, sababu ulishaweka mkataba nao,” alisema.
“Ni bora uwe na idara mbili za upandaji na uvunaji,
kisha uweke wasimamizi watatu au wanne ambao watawajibika kwako moja kwa moja.
Hii system uliyotumia ina walakini
hasa kwenye maslahi ya wafanyakazi. Unawalipa fedha lakini haifiki yote kwa
wafanyakazi,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyakazi hao.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Makanya wajipange
na kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili nao waanze kulima mkonge ambao
alisema watakuwa wanauuza kwenye kiwanda hicho.
“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji jirani ingieni
kwenye kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na nje ya nchi. Tafuteni
maeneo ya ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha mkonge sasa. Zao hili lipo
kwenye mazao ya nyongeza ya mkakati ambayo ni chikichi na mkonge.”
“Na uzuri wake unalima mara moja tu, halafu kila
mwaka unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji simamieni jambo hili,”
alisisitiza.
Mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya
tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa
pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na korosho.
Mapema, akitoa
taarifa juu ya uzalishaji kwenye kiwanda hicho, Bw. Nyari alisema shamba lote
lina ukubwa wa ekari 2,453 na kwamba uzalishaji umekuwa ukiongezeka kidogo
kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani za mkonge 713 na hadi kufikia mwka
2018 walifikisha tani 890 za mkonge. “Mwaka huu tunatarajia kufikisha tani
1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge limeongezeka,” alisema.
Alisema moja ya changamoto inayowasumbua ni tabia ya
wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge mchanga hali ambayo
alisema inaua miche hiyo michanga.
Aliitaja changamoto nyigine kuwa ni ukosefu wa maji
ya uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha singa za katani ambazo
ni safi.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani
Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na
kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same -
Mwanga - Korogwe.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.