WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema viongozi wa dini waendelee kuimarisha
malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana na kuepusha mmomonyoko wa
maadili ili Taifa liendelee kung’ara, kuheshimika na kusifika duniani
kwa utulivu, amani na umoja.
Amesema
Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo CCT katika
kutengeneza mustakabali mwema na ustawi wa familia kupitia mahubiri ya
injili na malezi ya kiroho kwa waamini. “Mtakubaliana nami kuwa siku
zote Taifa imara msingi wake hujengwa na familia imara.”
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 5, 2019) wakati alipomwakilisha
Rais Dkt. John Magufuli kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ulioambatana na harambee ya kukusanya
fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitegauchumi cha jumuiya hiyo. Mkutano huo
umefanyika jijini Dodoma.
Amesema
Serikali inatambua mchango wa malezi ya kiroho katika ustawi wa
wananchi na Taifa kwa ujumla na mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga
watumishi wa umma ambao wamelelewa katika misingi bora ya kumcha
Mwenyezi Mungu.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inaamini kwamba watumishi wa namna hiyo watachapa
kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu na kupiga vita vitendo vyote vya
rushwa na ubadhilifu wa mali za umma. Serikali itaendelea kushirikiana
na Taasisi za kidini kwa ajili ya ustawi wa Taifa na watu wake.
Akizungumzia
kuhusu harambee hiyo ambayo jumla ya sh. milioni 357.35 zilipatikana,
Waziri Mkuu amesema ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa CCT wa miaka
mitano (2017 – 2022) wenye lengo la kuiwezesha CCT kujitegemea kwa kuwa
na vitega uchumi vyake ambavyo vitawawezesha kujiendesha kwa asilimia
80.
Waziri
Mkuu ameipongeza CCT kwa kuanza kuchukua hatua za kujenga uwezo wa
ndani wa kujitegemea kiuchumi kwani zinahitajika nguvu za pamoja katika
kuhakikisha wanawahudumia Watanzania na kuwaletea maendeleo.
“Kujizatiti
kwa CCT katika kufikia malengo yake ya kujitegemea kiuchumi ni muhimu
katika kutimiza kusudio na agizo la Mungu la kuwahudumia wahitaji ambao
ni Watanzania lakini pia mtakuwa mnajaliza juhudi za Serikali katika
wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.”
Waziri
Mkuu amesema kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za
CCT na madhehebu mengine ya dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia
sekta za elimu, maji, afya na shughuli za ujasiriamali.
Amesema
suala la kujitegemea ndiyo msingi wa uongozi wa Rais Dkt. Magufuli wa
kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 na
katika kufanikisha hilo, Serikali imeendelea kupunguza kiwango cha
utegemezi.
Amesema
kiwango cha utegemezi kutoka kwa Washirika wa Maendeleo katika bajeti
kimepungua kutoka asilimia 12.5 mwaka 2017/2018 hadi asilimia nane
2019/2020. “Kuimarika huko kwa bajeti yetu kunakwenda sambamba na
kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kupungua kwa
umaskini wa mahitaji muhimu.”
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Moses Matonya, amesema jumuiya hiyo
imeanzisha mkakati wa kuwa na vitegauchumu vyake kwa lengo kuondokana
na utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi
mwaka.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.