Na;
Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama ametoa maagizo kwa viongozi wa Shamba la Katani la Hassan Sisal
Estate kuhakikisha wanatatua migogoro na wafanyakazi pamoja na kusimamia haki
zao ipasavyo.
Waziri Mhagama ametoa
maagizo hayo wakati wa ziara yake Wilayani Same alipofanya ziara katika Shamba
la Hassan Sisal Estate ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe.
Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi aliyoyatoa Julai 20, 2019 alipotembelea
shamba hilo lililopo Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same.
Akizungumza na wafanyakazi
pamoja na viongozi wa shamba hilo, alieleza kuwa waajiri wanatakiwa kutekeleza
matakwa yote ya Sheria za ajira na mahusiano kazini kwa kuzingatia miongozo na
kanuni ambayo inasimamia haki za msingi kwa wafanyakazi.
“Tunataka kuona ninyi kama
waajiri mnakuwa na vikao vyenye tija na wafanyakazi katika kuleta suluhu ya
masuala mbalimbali ya kazi,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa Kampuni mbili
zilizopo katika shamba hilo yaani Unique Consultancy na UPAMI kuhakikisha
wanatoa huduma bora kwa wafanyakazi hao, ikiwemo kuwasilisha michango kwa
wakati kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF). Pamoja na hayo alishauri pia kampuni hizo kuwaweka wazi wafanyakazi
kuhusu mikataba yao.
“Malalamiko na Manung’uniko
ya wafanyakazi ni mengi, mnatakiwa kukaa na kujadili pamoja namna bora ya
kutatua matatizo yao yanayojitokeza hususani kwenye mikataba,” alisema Mhagama.
Katika hatua hiyo, Mhe.
Mhagama alimuagiza Meneja wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA),
kufanya kanguzi za mara kwa mara katika shamba hilo na kuangalia kama wafanyakazi
wanakabidhiwa vifaa vya kujinginga na madhara kazini (Protective gears) kwa
wakati, pamoja na kusimamia zoezi la upimaji afya kwa wafanyakazi hao.
Pia, alitoa maelekezo kwa
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Kilimanjaro, kukabidhi
kadi za uwanachama kwa wafanyakazi wa shamba hilo la Hassan Sisal Estate na
kufuatilia uwasilishaji wa michango yao kutoka kwa waajiri wao.
Sambamba na hilo, Waziri
Mhagama ametaka Afisa Kazi Mfawidhi wa
Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea shamba hilo na maeneo mengine mbalimbali katika
mkoa huo ili kuelimisha wafanyakazi sheria mbalimbali za kazi na ajira zitakazo
wawezesha kutambua haki zao za msingi.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa
maelekezo juu ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwenye mashamba yote ya katani
yaliyopo nchini, vitakavyosadia kuongeza tija na ufanisi katika shughuli
mbalimbali za utendaji kazi.
Pamoja na hayo, Mheshimiwa
Mhagama aliwataka viongozi wa shamba hilo kuendelea kusimamia vizuri maslahi ya
wafanyakazi wao ili waweze kutekeleza majukumu ya kila siku wanapokuwa katika
maeneo yao ya kazi.
Naye, Meneja Mshauri wa
Shamba hilo, Bw. Ndekirwa Nnyari aliahidi kufanyia kazi maagizo yote
yaliyotolewa ikiwemo kuwa na majadiliano ya mara kwa mara na wafanyakazi kwa
itakayowapa munufaa ya pamoja.
Kwa upande wake, Meneja wa
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Victor Luvena amesema kuwa watatekeleza
maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwa kuchukua hatua za kisheria kwa
wale watakaoshindwa kutekeleza.
Pia mmoja wa Wafanyakazi wa
Shamba hilo, Bi. Cheshi Juma alisema kuwa ujio wa Waziri na wataalamu
alioambatana nao utasaidia kuondoa kero za wafanyakazi na kujenga mahusiano
mazuri na waajiri wao.
“Tumehamasika sana kuona
Serikali yetu ipo pamoja nasi katika kutetea maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia
kero tulizokuwa tukikabiliana nazo katika maeneo ya kazi,” alisema Cheshi
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Large Mature akifafanua jambo kuhusu uwasilishaji
wa michango ya wafanyakazi wa Shamba la katani la Hassan Sisal Estate.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.