Friday, September 27, 2019

MAAFISA VIUNGO WA AFYA MOJA WAPIGWA MSASA





Na.  OWM, Morogoro

Dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu imeendelea kufundishwa kwa maafisa viungo wa sekta hizo za Afya, ikiwa ni Sekta ya Afya  ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na Mazingira, ili maafisa hao watumie dhana hiyo kuchukua tahadhari kwa wakati.

Tafiti mbalimbali duniani zinaonesha  kuwa asilimia 60% ya vimelea vya magonjwa ambayo huambukizwa binadamu vinatoka kwa wanyama hususani  wanyamapori na baadae kusababisha magonjwa kwa binadamu.

Tayari Tanzania imeainisha magonjwa sita ya kupewa kipaumbele ambayo ni; Kimeta, Kichaa cha mbwa, Mafua ya ndege, Homa ya Bonde la ufa, Malale na Ugonjwa wa  kutupa mimba  kwa wanyama (Brusela) , hivyo maafisa hao wakiitumia dhana ya Afya moja kwenye sekta zao  itasaidia kuimarisha udhibiti wa magonjwa hayo.


“Akiongea wakati akifunga rasmi warsha hiyo tarehe 27 Septemba, 2019,   mjini Morogoro, Mkurugezi wa Idara ya Menejimenti  ya  Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amefafanua kuwa maafisa hao ni muhimu katika kuhakikisha sekta za Afya zinashirikiana katika
 kuzitatua  changamoto zilizopo kwenye sekta  za afya  ya binadamu, wanyama, na mazingira” amesisitiza Kanali. Matamwe.

Aidha, katika hatua nyingine maafisa hao ambao wameteuliwa  kutoka katika Wizara , Idara , Taasisi za serikali, Vyuo vikuu  na mitandao ya Afya moja nchini wamepata fursa ya kuelewa namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Afya moja wa hapa nchini.

Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo  Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja  kwa kushirikiana na Program ya HRH2030 kupitia Chemonics International,  wamendaa na kuratibu warsha hiyo.
MWISHO.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.