WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Magufuli inahitaji watumishi waadilifu wenye uwezo wa
kufanyakazi kwa uaminifu na waliotayari kuwahudumia wananchi wote bila
ya ubaguzi.
Amesema
Serikali inataka kuona watumishi wa umma wakitumia taaluma zao katika
kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi kwenye maeneo yao
hususani wa vijijini, hivyo amewataka watenge muda wa siku nne kwa ajili
ya kukutana nao.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na
Halmashauri ya Mji wa Mafinga pamoja na Madiwani kwenye mkutano
uliofanyika Halmashauri ya Mufindi.
Amesema
watumishi hao wanapaswa kutekeleza matakwa ya ilani ya CCM, ambayo
imeainisha kila kitu kinachotakiwa kufanyika katika halmashauri, hivyo
wakuu wa idara hawanabudi kuisoma kwa makini ili waweze kupata mafanikio
kwenye utendaji wao.
Waziri
Mkuu amesema ni lazima watumishi hao wafanye kazi za Serikali na waache
itikadi zao watekeleze ilani ya CCM. “Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri hakikisheni wakuu wa idara na wasaidizi wao wanawahudumia
wananchi.”
“Tuelewane
vizuri hapa, msimamo wa Serikali hii ni kuchapakazi mtu atakaye
vurugavuruga hana nafasi katika Serikali hii na hatuta muundia tume
tutamalizana naye hapo hapo. Rais wetu anataka kuona wananchi
wakihudumiwa katika maeneo yao.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amezitaka halmashauri nchini zinapotoa huduma
zihakikishe zinapotoa huduma kwa wananchi wasisahau kutenga asilimia 10
ya mapato yao kwa ajili ya makundi maalumu kama wanawake, vijana na
wenye ulemavu.
Pia,
Waziri Mkuu amewataka watendaji hao kutofanyakazi kwa mazoea, ambapo
amemtaka Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Mufindi kuhakikisha anasimamia
vyanzo vyote vya maji na kuwachukulia hatua watu wote wanaolima au
kufanya shughuli katika vyanzo vya maji. Amesema kata ya Igowole iwe
imepata maji ifikapo 2020.
Katika hatua nyingine,Waziri
Mkuu amesema suala la ukusanyaji wa mapato limepewa kipaumbele na
Serikali kwa sababu linasaidia katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo. “Madiwani msimamie ukusanyaji mapato na hakuna kumlinda mtu
anayetafuna fedha hizo.”
Amesema
watendaji nao wahakikishe wanawasimamia vizuri mawakala waliopewa
zabuni za ukusanyaji wa mapato na watakaobainika kushindwa kutekeleza
vizuri jukumu hilo wasipewe tena zabuni na badala yake watafutwe
wazabuni watakaokusanya vizuri.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Joseph Kandege amesema
utendaji wa kazi katika hospitali ya wilaya ya Mufindi si wa kuridhisha
hasa siku za Jumamosi, amewataka watumishi wabadilike kwani huduma
zinatakiwa wakati wote.
Awali,Mbunge
wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema hali ya upatikanaji wa huduma za
afya katika halmashauri ya Mji wa Mafinga si ya kuridhisha kutokana na
uhaba wa watumishi kwani waliopo ni 204 huku mahitaji yakiwa 310. Waziri
Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa kazi, Serikali inaendelea kuajiri.
Naye,
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi amesema halmashauri za wilaya ya
Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga zinafanya vizuri katika sula
zima la ukusanyaji wa mapato pamoja na kutenga asilimia 10 ya mapato
yake kwa ajili ya wanawake, vijana na wenyeulemavu.
Akizungumzia
kuhusu hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga amesema inachangamoto
ya utoaji wa huduma kwa sababu ya kuhudumia halmashauri mbili ya
Mufindi na Mafinga lakini mgawo wa dawa wanaopewa ni kwa ajili ya wakazi
wa Mafinga pekee.
Pia,
Mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kupeleka zaidi
ya sh. bilioni saba katika wilaya hiyo kwa ajili ya kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na
Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
Baada
ya kuzungumza na watumishi, Waziri Mkuu amekagua na kuweka jiwe la
msingi la ujenzi wa hospiyali ya wilaya ya Mufindi inayojengwa katika
Kijiji cha Nzivi kata ya Igowole. Ujenzi wa hospitali hiyo utagharimu
sh. bilioni 1.5 na upo katika hatua za umaliziaji.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.