Wednesday, September 25, 2019

ZAIDI YA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI 390 WASIKILIZWA KERO ZAO RUVUMA


NA.MWANDISHI WETU
Zaidi ya wafanyabiashara na wawekezaji 390 mkoani Ruvuma wamekutana katika mkutano wa mashauriano baina ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo katika mazingira ya biashara.
Kongamano hilo lililofanyika Septemba 24, 2019 lililoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kwa kushirikiana na ofisi ya mkoa wa Ruvuma na  kufanyika  katika Ukumbi wa mikutano wa Bomba mbili Mkoani Ruvuma .
Kongamano hilo lilihudhuriwa na Mawaziri kutoka Wizara saba ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Wizara ya Fedha,  Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati na Wizara ya Viwanda
Akizungumza wakati wa kufunga kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masualaya Uwekezaji nchini Mhe.Angellah Kairuki alieleza nia thabiti ya Serikali katika kuwafikia wawekeza wote nchini kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli aliyoyatoa tarehe 7Juni, 2019 alipokutana na wafanyabiashara Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“mikutano ya Mashauriano kati ya Serikali na sekta Binafsi imejikita kusikiliza na kutatua kero za wawekezaji na wafanyabiashara katika kada mbalimbali ili kutengeneza mazingira ya kuwekeza zaidi ili kukuza uchumi wetu kwa ustawi wa biashara zenu kwa kutambua na kuthamini michango yenu ndani ya jamii na nchi kwa ujumla,”alieleza Waziri Kairuki.

Alieleza kuwa, mikutano hiyo ya mashauriano itaendelea kwa nchi nzima ili kuhakikisha mazingira bora  ya wafanyabiasha na wawekezaji nchini kwa lengo la kufikia adhima ya uchumi wa kati na kuendeea kuwa na nchi yenye maendeleo.

“Mikutano hii inaenda sambamba na utekelezaji wa Kauli Mbiu aliyoitoa Mheshimiwa Rais kuwa Mwaka 2019 ni Mwaka wa Uwekezaji, hivyo nasi Waheshimiwa Mawaziri tumeamua kutekeleza hilo kwa Kauli mbiu ya kwamba “Mwaka 2019 ni Mwaka wa Uwekezaji: Tunasikiliza na Tunatatua”.alisisitiza Waziri Kairuki.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliwahakikishia wawekezaji kuhusu maboresho yanayoendelea kufanywa na serekali kwa kuwa na punguzo za tozo, ada na kodi mbalimbali walizoainisha kuwa ni kero kubwa kwa wafanyabiashara hao.
“Mhe. Rais alipoingia madarakani alianza kuboresha viwango vya kodi kwa kuhakikisha anaondoa na kufanya marekebisho kwa kodi ikiwemo zile za madini, na hii ni dhamira njema”alieleza Dkt.Kijaji
Aidha alifafanua kuwa, wameendelea kutekeleza kwa vitendo sheria ya fedha  ya mwaka 2019 ambayo imebainisha orodha ya tozo na ada zilizopunguzwa na zilizofutwa na  kuahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa ukusanywaji wa tozo zote nchini na kushughulikia kero za kodi, ada na tozo zinazotozwa bila kufuata sheria na taratibu zilizopo.
“Katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2018/2019 zaidi ya kodi, tozo na ada mbalimbali zipatazo 109 zilifutwa na nyingine zipatazo 54 zilifutwa ili kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji,”alisisitiza Dkt. Kijaji
Alimalizia kwa kutoa rai kwa wananchi kuendelea kufuatilia kila taarifa muhimu zinazohusu maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu ulipaji wa kodi ili kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza.
=MWISHO=

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.