WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu
wa Kampuni ya Russian Railways, Bw. Alexander Misharin na kumweleza
kuwa Tanzania inahitaji sana kuimarisha usafiri wa ndani wa reli hasa
katika Majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga.
Amesema
kampuni hiyo yenye uwezo mkubwa wa kujenga reli mpya, kukarabati reli,
kutengeneza injini za treni na mabehewa pamoja na ukarabati wake
inahitajika sana nchini ili kufanikisha mpango wa Serikali wa kuimarisha
reli za zamani za TAZARA, Reli ya Kati na kufugua reli ya Kaskazini
inayounganisha mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Waziri
Mkuu alizungumza na Mkurugenzi huo jana (Oktoba 22, 2019) kwenye hoteli
ya Marriot iliyopo Sochi nchini Urusi, ambapo alitumia fursa hiyo
kuikaribisha kampuni ya Russian Railways kuwekeza nchini hususani katika
sekta ya ujenzi, ufundi na mafunzo ikishirikiana na makampuni ya
Watanzania.
Waziri
Mkuu yuko nchini Urusi kuhudhuria mkutano baina ya Wakuu wa Nchi na
Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi (Russia-Africa Summit),
unaotarajiwa kuanza leo Oktoba 23 hadi 24, 2019 katika jiji la Sochi. Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli.
“Katika
kipindi hiki ambacho Tanzania inajenga reli ya kiwango cha kimataifa
ya SGR pamoja na kufufua reli ya Kaskazini, inaikaribisha Kampuni ya
Russian Railways kwa mikono miwili ije ifanye mazungumzo rasmi na Wizara
husika. Pia Serikali inao mkakati wa kujenga reli mpya katika ukanda
wa Kusini kutoka Mtwara hadi Ruvuma ili kuiunganisha bandari ya Mtwara
na mikoa ya Kusini pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia.”
Alisema
Tanzania kwa sasa inahitaji sana kuimarisha usafiri wa ndani wa reli
hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na
Tanga hivyo endapo mazungumzo kati ya Wizara husika na kampuni hiyo
yataonekana kuwa na tija na yana maslahi kwa Watanzania, kampuniyo
itapewa fursa ya kuwekeza nchini.
Kadhalika,
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara wa
Tanzania, wito wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kuwataka watumie
fursa lukuki zilizopo nchini kuanzisha makapuni ya pamoja na makampuni
ya nje ili kuunganisha nguvu kwa kuendesha kwa pamoja makampuni
yatakayoanzishwa.
Alisema
utaratibu wa makampuni ya Tanzania kuanzisha makampuni ya pamoja na
makampuni ya nje utawapa Watanzania fursa ya kujipatia kipato pia
wataweza kulinda maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Russia Railways, Bw. Misharin
alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana na
wafanyabiashara wa Kitanzania katika kuanzisha makapuni ya pamoja ili
kuipatia Tanzania tekinolojia ya masuala ya reli na kubadilisha ujuzi.
Awali,
Waziri Mkuu alizungumza na Wakurugenzi wa Kampuni ya kutengeneza
matrekta ya BTP, Bw. Alexsey Punkov na Bw. Ignat Dydyshkoa ambaye
alisema kuwa kampuni yake inakusudia kuwekeza nchini Tanzania katika
sekta ya kilimo kwa kuleta nchini mashine mbalimbali kama vile matrekta
na mitambo ya ujenzi wa barabara.
Viongozi wote wa
makampuni ya Urusi waliozungumza na Waziri Mkuu waliahidi kuja
Tanzania mwaka huu ili kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na kufanya
mazungumzo yenye lengo la kushirikiana na wafanyabiashara wa Kitanzania
katika uwekezaji wao wanaokusudia kuufanya nchini.
Mheshimiwa
Majaliwa pia alizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta na
Gesi ya Zarubezhnefe, Bw. Sergey Kundryashov ambaye pia alionyesha nia
ya kutaka kuwekeza nchini Tanzania.
Katika
safari hiyo Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Balozi wa
Tanzania nchini Urusi, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi na Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James
Matarajio.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.