*Akemea ujenzi mbovu wa kuta, aagiza zibomolewe na kurekebishwa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa,
mkoani Lindi na kusema kwamba hajaridhishwa na baadhi ya majengo.
Amemwagiza
Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Tengamaso Wilson abomoe
kuta zenye hitilafu na kurekebisha kasoro zilizopo kwenye majengo hayo
ikiwemo kutonyooka kwa kuta za majengo hayo.
Alitoa agizo hilo jana (Jumatano,
Oktoba 16, 2019) wakati akikagua majengo ya hospitali hiyo, na
kumweleza mhandisi huyo kwamba kuta zimepishana unene kwa sababu
hakusimamia kazi yako ipasavyo. “Ukuta huu ni mbovu kwa sababu
hukuwasimamia vizuri mafundi wako. Kuna mahali juu unaona ukuta ni mdogo
na huku chini ni mnene.”
Majengo
ambayo Waziri Mkuu aliyakagua na kuonesha kutoridhishwa nayo ni ya
utawala, wagonjwa wa nje (OPD) na maabara. Majengo mengine yanayojengwa
ni jengo la wazazi, la X-ray, la utoaji dawa na la kufulia nguo.
Alipouliza
ni kwa nini kumetokea tofauti baina ya kuta hizo, Waziri Mkuu alijibiwa
kwamba tatizo ni upigaji wa lipu. “Mhandisi wa Wilaya simamia hili,
kagonge upya kuta za jengo hili na lile. Hatuwezi kuwa na jengo la
Serikali la aina hii. Tukitoa fedha ya Serikali ni lazima mjiridhishe
kama kilichojengwa ndicho sahihi.”
“Tunahitaji majengo yote yawe smart, hata ujenzi wake nao uwe smart. Usikubali kutoa certificate kama kazi haijakamilika. Kama kuna kazi haujaridhika nayo, usikubali certificate
itoke. Zile sentimeta 30 ni lazima zirekebishwe la sivyo, itaonekana
huku uliweka matofali mengi kuliko upande ule,” alisisitiza.
Akiwa
hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba katika awamu ya kwanza,
Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya
kipaumbele ambayo ni jengo la wazazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara,
la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.
Ujenzi
wa hospitali hiyo unafanyika kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa
‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri
mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa
halmashauri na kamati mbalimbali.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amemwagiza mweka hazina wa Halmashauri hiyo, Bw. Frank Chonya
ajiridhishe na kazi za ujenzi zinazofanyika kabla hajaamua kutoa fedha
za malipo.
“Mweka hazina, wakati wote ukiambiwa kuwa certificate imeletwa
ni lazima uende ukakague mradi na kama haujaridhika, sema wazi kwamba
hujaridhika na kazi iliyofanywa,” alisema Waziri Mkuu.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Andrea Chezue alisema
kiasi chote kilichotolewa na Serikali cha sh. bilioni 1.5 kimeshatumika,
na kwamba Halmashauri illitumia zaidi ya sh. milioni 100 ili kusafisha
eneo na kulipa fidia ili wapate eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 56.
“Mchango
wa Halmashauri ya Wilaya kwenye ujenzi wa hospitali hii, mpaka sasa ni
kwamba tumelipa sh. milioni 88.266 zikiwa ni fidia ya eneo la ujenzi na
sh. milioni 14.418 zimetumika kusafishia eneo lote,” alisema.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.