Na. OWM, Arusha.
KWA mara ya kwanza Barani Afrika,
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kufanya mafunzo katika ngazi ya mkoa na
Halmashauri kwa kutumia dhana ya Afya moja kuwajengea uwezo wadau wa
Afya moja juu ya namna ya kufanya tathmini ya vimelea hatarishi vya
magonjwa. Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau wa Afya moja na wataalam kutoka
sekta za afya ya binadamu, wanyama pori, mifugo, kilimo na mazingira. Wadau hao na wataalam
kutoka sekta hizo za afya wamepata mafunzo ya namna ya kufanya
tathmini hiyo kwa magonjwa ya Kichaa cha mbwa, Kimeta na Ugonjwa wa Brusela
(Ugonjwa wa Kutupa mimba kwa wanyama).
Kufuatia nchi ya Tanzania kuwa imepiga hatua katika
uratibu wa masuala ya Afya moja, ambayo ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori,
mifugo, kilimo na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na
kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Dawati la
Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa (FAO) imeratibu mafunzo hayo yaliyotolewa na
wakufunzi wa hapa nchini waliojengewa uwezo na wataalamu kutoka
Makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa (FAO), pamoja na Shirika linaloshughulika na Afya ya
Wanyama (OIE).
Akiongea
wakati wa kufunga mafunzo hayo tarehe 22 Novemba 2019,Jijini Arusha, Mkurugenzi
wa Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, amebainisha kuwa
ushirikiano wa wadau wa Afya moja na wataalam na sekta za Afya kwa
kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha amefafanua
kuwa dhana hiyo inapunguza gharama katika kushughulikia tishio la
magonjwa yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama
na kwenda kwa binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na
hata usugu wa vimelea vya magonjwa.
“Wadau wa afya moja wanawajibika kupanga mikakati mbalimbali ya udhibiti, ulinzi na usalama katika kuzuia, kujiandaa na kukabali magonjwa ambukizi. Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na kimataifa ni kujiandaa kwa kuwafundisha wataalam wa sekta mbalimbali za afya jinsi ya kufanya tathmini ya hatari ya vimelea vya magonjwa ambukizi kwa ushirikiano.” Amesema . Kanali Matamwe.
Kwa upande wake, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa (FAO), Tanzania, Bi. Niwael Mtui amefafanua kuwa Shirika
hilo moja ya kipaumbele chake ni kupunguza umasikini na kuongeza kipato cha
wananchi, hivyo Shirika hilo linashirikiana na serikali ya Tanzania kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu, katika kujenga
uwezo wa ndani ya nchi kwa kuwafundisha wataalam wa sekta za Afya
katika kudhibiti magonjwa ambapo uwezo huo utasaidia kuimarisha afya ya binadamu
na mifugo na hatimaye kipato kitaongezeka na umasikini utapungua
Wakiongea
kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamebainisha
kuwa wamekuwa wakifanya tathmini za vimelela hatarishi vya magonjwa
hapa nchini lakini tathmini hizo zimekuwa ni za kisekta kwani hazikuwa
zinazingatia ushirikiano kwa maana ya dhana ya Afya moja. Aidha walifafanua
kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutumia Dhana ya Afya moja kwa
kuwa inapunguza gharama katika
kushughulikia tishio la magonjwa yanayotokana na vimelea vyenye
uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu na hata mimea (mazingira) na
kusababisha magonjwa na hata usugu wa vimelea vya magonjwa.
Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la
Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na
kuratibu shughuli za Afya moja nchini. Kwa
kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia
Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa (FAO) na wadau waliandaa na kuratibu mafuzo hayo, ambapo
wataalamu wa sekta za Afya na Wadau wa Afya moja kutoka Halmashauri nne za mkoa
wa Arusha (Halmasahauri ya Arusha, Monduli, Ngorongoro na Karatu) walishirki
mafunzo hayo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.