Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Tanzania Bara, Philip Mangula (kulia) akieleza jambo alipokuwa kwenye Kitalu nyumba kilichopo Ihemi, Mkoani Iringa. (Wenye shati ya Bluu) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde.
Na; Mwandishi Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa utekelezaji wa programu ya taifa ya kukuza ujuzi ambayo imekuwa ni chanzo cha kuwajengea uwezo vijana nchini.
Pongezi hizo zimetolewa jana Disemba 18, 2019 na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Tanzania Bara, Philip Mangula wakati alipokuwa akizindua Chuo cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Ihemi, Mkoani Iringa.
Alieleza kuwa utekelezaji wa programu hiyo umeleta mabadiliko makubwa sana kwa vijana ambapo wamekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo kwa mustakabali wa taifa lao.
“Serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa vijana na ndio maana inatekeleza programu hii kwa kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi yatayowasaidia vijana wa kitanzania kuondokana na changamoto ya ajira,” alisema Mangula
Aliendelea kuelezea kuwa Mafunzo ambayo yatakuwa yakitolewa katika chuo hiko yatahamasisha vijana kushiriki kwa wingi kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na pia kuinua ari ya vijana katika utendaji kazi wao.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde alifafanua kuwa Ofisi hiyo inatekeleza Programu hiyo ya kukuza ujuzi kwa njia mbalimbali ikiwemo uanagenzi, mafunzo ya vitendo mahali pa kazi, mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliyopatikana nje ya mfumo rasmi na mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.
“Programu hii imekusudia kuwezesha vijana ambao kwa asilimia kubwa ndio nguvukazi ya taifa, hivyo kuwapatia ujuzi na stadi za kazi stahiki kutawasaidia kujiajiri au kuajiriwa katika soko la ajira,” alieleza Mavunde
Akitolea mfano Mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (Greenhouse) yaliyokuwa yakitolewa kwa vijana waliopo kituoni hapo yametoa fursa kwa vijina kutambua kuwa kilimo kinaweza kuwapatia ajira na kipato.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde amesisitiza vijana kuchangamkia fursa ya mafunzo yatakayokuwa yanatolewa katika chuo hiko ili waweze kupata ujuzi wa fani mbalimbali zitakazowafanya waweze kujiajiri na kupata kipato.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.