WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa uongozi wa Mahakama nchini
uhakikishe unakamilisha ujenzi wa miundombinu ya Mahakama ili
kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu na kutumia gharama
kubwa katika kutafuta haki zao.
Amesema
kuna wilaya 139 Tanzania Bara, kati ya wilaya hizo wilaya 111 zilizo na
huduma ya Mahakama za Wilaya na wilaya nyingine 28 bado zinahudumiwa na
Mahakama za Wilaya za jirani ambazo zimepewa mamlaka ya kisheria
kuhudumia Mahakama zisizo na majengo ya Wilaya.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Januari 13, 2020) wakati akizindua jengo la Mahakama
ya wilaya ya Ruangwa. Amesema ni vema uongozi wa Mahakama uhakikishe
kuwa yale yote waliyojipangia kwenye mpango wao wa Miaka Mitano wa
Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama 2016/17 – 2020/21 unatekelezwa kwa
wakati.
Waziri
Mkuu amesema kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Wilaya Ruangwa mwaka
2009, wananchi wa wilaya hiyo walilazimika kusafiri umbali wa kilomita
180 kufuata huduma za mahakama wilayani Lindi. Mahakama hiyo
itarahisisha upatikanaji wa haki wilayani Ruangwa.
“Umbali
huo mrefu ulisababisha wananchi wengi kupoteza muda mwingi ambao
wangeutumia kwa shughuli za uzalishaji mali. Wakati mwingine wananchi
hao walikosa haki zao kwa kushindwa kumudu gharama za usafiri kuhudhuria
mashauri yao wilayani Lindi.”
Waziri
Mkuu amesema Mahakama ni muhimu katika kudumisha amani na kuleta
maelewano ndani ya nchi au jamii ambayo huwa ni kichocheo cha shughuli
za kiuchumi, hivyo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuamua kujenga
Mahakama hiyo Wilayani Ruangwa pamoja na sehemu nyingine nchini.
Amesema kupitia Mahakama, migogoro mingi hupata usuluhishi na hivyo kuimarisha hali ya amani na utulivu. “Kwa lugha nyingine,Mahakama
inapokuwa imara Taifa letu huvutia uwekezaji kwa kuwa wawekezaji
wanakuwa na uhakika na usalama wao pamoja na mali zao.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na
Mahakama kuhakikisha kuwa mipango yake iliyojiwekea inatekelezwa kama
ilivyokusudiwa, kwani bado kuna kazi kubwa mbele yao.
Wakati hu huo, Waziri Mkuu ameipongeza Mahakama
ya Tanzania kwa kukusanya mapato kupitia mfumo wa Kielekitroniki wa
Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali (Government electronic Payment
Gateway, GePG) kwani Serikali ilielekeza kila taasisi itumie mfumo huo
ili kupunguza mianya ya rushwa na upotevu wa fedha.
Amesema
amefurahi kusikia kuwa kwa kutumia mfumo wa GePG, Mahakama iliweza
kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka sh. bilioni 1.6 mwaka 2017 hadi
sh. bilioni 2.5 mwezi Desemba 2019 baada ya kuanza kutumia GePG. “Fedha
hizi zitatumika kuchangia ujenzi wa mahakama na miundombinu mingine ya
kiuchumi unaoendelea katika kila kona nchini.”
“Ni
ukweli usiofichika kwamba hata wananchi nao wanafarijika kuona kuwa
kile mnachowatoza kinaenda moja kwa moja kwenye mfuko mkuu wa Serikali,
na baadaye kiasi fulani kinarudi kwenu kujenga miundombinu ya kisasa kwa
ajili ya kuwahudumia wananchi.”
Waziri
Mkuu amesema kuwa hayo ndiyo malengo na dhamira ya Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. “Aidha, kwa kufanya
hivyo, mnachangia utekelezaji wa malengo yaliyoainishwa vema kwenye
Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.”
Kwa upande wake,
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma amesema kwa muda mrefu,
Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba,
na uchakavu wa majengo katika ngazi zote za Mahakama, yaani Mahakama za
Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi (Mahakamaza Mikoa),
Mahakama Kuu na hata Mahakama ya Rufani.
Amesema
ili kukabiliana na ukubwa wa changamoto ya upungufu na uchakavu wa
majengo yake, Mahakama ya Tanzania ilitayarisha Mpango wa Miaka Mitano
wa Maendeleo ya Miundombinu (2016-2021). “Mpango huu umetathmini hali ya
majengo ya Mahakama katika Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara.”
Jaji
Mku amesema mpango huo umelenga kupunguza au kuondoa kabisa uhaba na
uchakavu. Jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa ni kielelezo cha
utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya
Mahakama ya Tanzania.
Pia,
Jaji Mkuu ametumia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa watumishi wa
Mahakama, majengo kwamba hayo ya kisasa na miundombinu bora, iambatane
na upatikanaji wa huduma bora kwa mwananchi.
“Kila
mtumishi wa Mahakama (kama walivyo watumishi wote wa umma) anao Mkataba
na watumiaji wa huduma za Mahakama. Kipimo chetu cha kutimiza masharti
ya Mkataba huu, ni nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ambayo ni
‘Upatikanaji na Utoaji wa Haki kwa Wakati’, hivyo siku zote watumishi
wa Mahakama tukumbuke kuwa Mahakama hii ni mali ya wananchi na wananchi
wana haki ya msingi ya kupata huduma iliyo bora kwa wakati.”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.