Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki ametembelea
kiwanda cha kuchakata mifuko chakavu na kuzalisha mipya cha SAMAKI investment ili
kukagua mazingira ya wawekezaji nchini pamoja na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia
ufumbuzi ili kuendelea kuwa na mazingira
rafiki kwa wawekezaji nchini.
Waziri huyo ametembelea kiwanda hicho
kilichopo katika Kata ya Zinga Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani Januari 16,
2020 ili kujionea mazingira yao pamoja na kupokea changamoto wanazokabiliana
nazo ili kuona namna ya kushirikiana nao katika kuzitatua ili kufikia malengo.
Katika ziara hiyo aliambatana na
viongozi wa Wilaya ya Bagamoyo, Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete
pamoja na watendaji wa Ofisi yake ambapo alifurahishwa na utendaji kazi wa
kiwanda hicho kwa kuchakata mifuko chakavu na kuzalisha mipya pamoja na mifuko
ya kisasa na kusema kuwa ni ya kuridhisha.
“Niwapongeze sana kwa kuendelea
kuzalisha mifuko katika ukubwa tofauti, ikiwemo ile ya Kilo 25, 50 na 100 na
hii itasaidia kuwafikia wateja wenye mahitaji tofauti tofauti kwa kuzingatia
ubora unaotakiwa,” alisema Waziri Kairuki
Alisema licha ya kazi nzuri
inayoendelea katika kiwanda hicho bado kuna kazi kubwa ya kuwajengea uwezo
vijana wa Kitanzania kwa kuhakikisha wanapewa mafunzo na ujuzi wa kutosha ili
waweze kuleta tija katika nchi yao.
Aidha waziri aliwataka waendelee
kuzalisha kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo nchini ili kuendelea kuwekeza
kwa uhuru bila uvunjifu wa sheria za uwekezaji zilizopo.
Aidha akijibu changamoto
zilizoainishwa ikiwemo ya kukosekana kwa huduma za umeme wa uhakika,
ucheleweshwaji wa vibali vya wafanyakazi, kukosa kibali cha kuingiza malighafi
kutoka nchi za nje na ufinyu wa eneo la kiwanda, Waziri alieleza Serikali
itahakikisha inaboresha mazingira kwa kuhakikisha changamoto za umeme
zinatatuliwa na kumwagiza Mhandisi Mkuu wa Mkoa TANESCO, Kenneth Boymanda
kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa ifikapo Machi, 2020.
“Nimetembelea viwanda vingi mkoa wa
Pwani na vingi vimeongelea changamoto hii ya ukosefu wa umeme wa uhakika, hivyo
Mhandishi mkuu wa mkoa, hakikisheni mnamaliza changamoto hii mapema ili
kutowakwamisha wawekezaji wetu kwa kukosa umeme wa uhakika,”alisema Waziri
Kairuki.
Naye Mmiliki wa kiwanda hicho Bw. Xiawei
Yu alimshukuru waziri kwa kutembelea kiwandani hapo na kuahidi kuendelea
kuzalisha kwa kuzingatia sheria kama zinavyoelekeza kwa kuzingatia mradi huo ni
mkubwa na una tija kwa jamii yote kwa kuzingatia umuhimu wa mifuko ya kisasa.
“Tutaendelea kuzingatia taratibu
zilizopo na kampuni yetu imedhamiria kuzalisha mifuko bora ya kubebea nafaka
mbalimbali na kuhakikisha wateja wanapata bidhaa bora zenye uhakika,”alieleza
Bw. Yu.
Aliongezea kuwa, uwepo wa kiwanda
hicho umechangia upatikanaji wa ajira kwa vijana wapatao 126 kati yao 71 ni
wenye ajira rasmi na 55 ni vibarua kwa kazi ndogondogo za msimu zinazojitokeza
kiwandani hapa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.