WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na
Viwanda Bw. Juma Hassan Reli ahakikishe anazuia utoaji wa vibali vya
kuingiza sukari kutoka nje hadi sukari inayozalishwa na kiwanda cha
sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda iishe.
Amesema
haiwezekani kiwanda hicho cha pekee kinachozalisha tani 6,000 za sukari
kwa mwaka kikakosa wateja wakati mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani
36,000 kwa mwaka.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 18, 2020) wakati apotembelea
kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo katika eneo la
Mahonda wilaya ya Kaskazini ‘A’ mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema
ni vizuri wizara ikahahakikisha sukari inayozalishwa na kiwanda hicho
inapewa kipaumbele cha kwanza kwa kununuliwa kwa sababu wanauhakika na
ubora wake kwa kuwa wameshuhudia uzalishaji wake kuanzia hatua ya awali
miwa ikiwa shambani.
“Wizara
ya Viwanda lazima mbadilike na muweke utaratibu mzuri wa kusimamia
uingizwaji wa sukari kutoka nje. Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani
ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hatuwezi
kumfurahisha mtu mmoja huku wengi wakiumia.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali imeamua kukuza uchumi kwa kupitia sekta ya
viwanda hivyo ni lazima viwanda vya ndani vikalindwa. “Viwanda
vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la
uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya uhakika.”
Amesema
kitendo cha wizara hiyo kushindwa kuratibu vizuri suala la uingizwaji
wa sukari kutoka nje ya nchi kutakwamisha uwekezaji jambo ambalo ni sawa
na kuihujumu Serikali kwa kuwa itasababisha wananchi kupoteza ajira
pamoja na Serikali kukosa mapato.
Waziri
Mkuu amesema “haiwezekani sukari inayotengezwa na kiwanda hicho ambayo
ubora wake umethibitishwa na Shirika la Viwango Zanzibar ikakosa soko
hii haiwezekani tukashindwa kununua tani 6,000 huku mahitaji yetu ni
tani 36,000.”
Amesema
sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao
bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda
wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika pamoja na
kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa hizo.
Awali,
Mkurugenzi Mkaazi wa kiwanda cha Sukari Zanzibar, Bw. Rahim Bhaloo
alisema kiwanda chao kinazalisha tani 6,000 kwa mwaka huku kikiwa na
uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 20,000 kwa mwaka ila tatizo ni soko
pamoja na ardhi ya kutosha kulima miwa.
Alisema
kutokana na uhaba wa soko sukari waliyozalisha katika msimu wa mwaka
2010/2020 wameuza tani 2,800 tu na kiasi cha tani 3,200 bado kipo
kiwandani hapo, hivyo ameiomba Serikali iwasaidie kwa kuwatafutia masoko
pamoja na ardhi ili waweze kuongeza uzalishaji.
Mkurugenzi
huyo aliiomba Serika iwe inazuia utoaji wa vibali vya uagizaji wa
sukari kutoka nje hususani kipindi cha uzalishaji ili waweze kuuza
sukari yao na itakapoisha ndio vibali hivyo vianze kutolewa. Kiwanda
kimeajiri wafanyakazi 300, pia wakulima wa nje zaidi ya 800 wanauza miwa
yao kiwandai hapo.
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, Bw. Juma Hassan
Reli amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba sukari yote iliyopo kiwandani
hapo itakuwa imeshanunuliwa ifikapo Februari mwaka huu. Pia maelekezo
yote aliyoyatoa kuhusu utoaji wa vibali vya uagizaji wa sukari
watayafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.