Monday, March 23, 2020

KATIBU MKUU MWALUKO AWAASA WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU KUENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA CORONA


NA. MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziti Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwekezaji Bi. Dorothy Mwaluko amewaasa watumishi wa ofisi yake kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mlipiko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona nchini ili kuendelea kupambana na maambukizi ya virusi hivyo.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichohusu Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na Makadirio ya Mpango na Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2020/2021kilichofanyika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma tarehe 23 Machi, 2020.
Katibu Mkuu aliwaeleza watumishi kuendelea kujilinda katika mazingira yote kwa kuhakikisha wanafuata maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kulinda na janga hilo lililopo nchini.
“Watumishi lazima muwe kielelezo kwa kuzingatia ofisi hii ndiyo inayoratibu na kusimamia shughuli zote za Serikali hivyo lazima mzingatie tahadhari zote ili kuepuka mlipuko wa virusi vya Corona katika nchi yetu ”alisema Mwaluko
Aliongezea kuwa, kila Mtanzania ana nafasi ya kujilinda kuanzia ngazi ya mtu mmoja hadi Taifa kwa kuangalia namna ugonjwa ulivyoathiri nchi zingine na kusababaisha vifo vya watu wengi.
Mwaluko aliwaasa watumishi waendelee kunawa mikono na kuepuka makusanyiko yasiyo ya lazima huku wakijihadhari kwa kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa saidiizi katika kujikinga na maambuki ya virusi vya Corona.
Aliongezea kuwa, nchi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuona inakabiliana na mlipuko wa COVID 19 kwa kutoa elimu kwa umma juu ya kujikinga na maambukizi na kuhakikisha idadi ya wanaoathiriwa na Corona inapungua badala ya kuongezeka.
“Kila mtumishi aelewe kuwa hadi sasa hakuna dawa wala chanjo ya virusi hivyo, na ugonjwa huu upo nchini, hili silipuuzwe na lazima tuzingatie tuwapo kazini kila mmoja wetu awe makini na endapo ukiona una dalili moja wapo ya ugonjwa huu ni vyema kutoa taarifa ili kuepuka madhara kwa wengine,”alisisitiza Mwaluko
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE wa ofisi hiyo, Bw. Mohamed Athuman alimpongeza Katibu Mkuu kwa kuchukua fursa ya kuwakumbusha watumishi na kuendelea kutoa elimu juu ya kujikinga na kuwalinda wengine.
“Leo tumepata nafasi ya kukumbushwa na kiongozi wetu kuhusu namna bora ya kuendelela kuwa makini na kuzingatia maelekezo ya Serikali ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona,”alisema Athuman
Aidha aliendelea kutoa wito kwa watumishi wa ofisi hiyo kuona namna bora ya kuyazingatia maelekezo yanayotolewa ili kuendelea kuwa na  afya bora katika utekelezaji wa majukumu wawapo kazini.
“Sisi viongozi wa TUGHE tunaunga mkono tahadhari zinazotolewa na viongozi wetu , hivyo ni vyema tukazingatia na kukumbuka kuwa kinga ni bora kuliko tiba,”alieleza
Sambamba na hilo alieleza kuwa kila mtumishi wa umma ana nafasi nzuri ya kuendelea kuunga mkono na kuwa kinara namba moja katika vita kwa kuachana na mizaa na kuendelea kuelimishana kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo hilo.
Naye mmoja wa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Numpe Mwambenja alieleza wameendelea kuchukua tahadhari zote zinazotolewa kwa kuzingatia mchango wa watumishi wa umma katika nchi na maendeleo kwa ujumla.
“Ofisi imetimiza wajibu wake kwetu, na sisi tunapaswa kuwajibika na tuhakikishe tunapambana na wanaopotosha umma kwa kuhakikisha tunasambaza taarifa sahihi zinazotolewa na Serikali yetu,”alifafanua Bi.Numpe.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.