Thursday, March 5, 2020

MAKAMU WA RAIS MHESHIMIWA SAMIA SULUHU AMEWATAKA MAWAZIRI NA WADAU WA UTATU WA SADC SEKTA YA KAZI NA AJIRA KUWA NA MIKAKATI YA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Wadau wa Utatu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) sekta ya Kazi na Ajira kuweka Mazingira wezeshi yatakayowajengea vijana uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri.
Hayo yameelezwa wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri na Wadau wa Utatu  wa SADC wa Sekta ya Kazi na Ajira pamoja na uzinduzi wa Programu ya Taifa ya Mafunzo kwa Vitendo Mahala pa Kazi (Internship) iliyofanyika katika Kitio cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ikiwa ni “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu”.
Makamu wa Rais alieleza kuwa ni muhimu nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wakawa na mikakati ya kuiwezesha nguvukazi ya Jumuiya hiyo na hasa vijana kupata ujuzi stahiki utakaowawezesha kufanya kazi zenye staha.
Alifafanua kuwa taarifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu mwenendo wa soko la ajira kwa mwaka 2020, zaidi ya watu milioni 187.7 ikiwa sawa na asilimia 5.5 duniani hawana kazi na takribani wafanyakazi bilioni 2 ikiwa sawa na 61.2% wanafanyakazi kwenye sekta isiyo rasmi na zaidi ya watu milioni 267 ikiwa ni sawa na asilimia 22 ambao kati yao wana umri wa miaka 15 hadi 24 na hawapo kwenye mafunzo wala ajira.
“Sisi kama Jumuiya ya SADC tunalazimika kuwa na mikakati itakayowezesha nguvukazi ambao kwa idadi kubwa ni vijana na wanakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 60 katika jumuiya yetu, hivyo kama Jumuiya hatuna budi kuwekeza katika kuwajengea uwezo vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika ukuzaji wa uchumi wa nchi za ukanda huo,” alisema   
Alisema kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua changamoto ya ajira kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu nchini iliamua kuanzisha programu ya taifa ya kukuza ujuzi kwa lengo la kuwawezesha vijana kuweza kujiajiri na kuajiriwa.
“Niwasihi wenzetu katika nchi za SADC ambao bado hawajaanzisha utaratibu huu, wajifunze kutoka Tanzania na wakiona utaratibu huo unafaa wautelekeze kwa manufaa ya vijana wa jumuiya hiyo,” alisema
Sambamba na hayo Makamu wa Rais amewapongeza waajiri katika sekta binafsi na sekta ya umma kwa kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo vijana kujifunza maadili, mtazamo chanya kuhusu kazi pamoja na tamaduni za kuishi mahali pa kazi na Kuwapatia uzoefu wa kazi unaohitajika na waajiri.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini kwa vijana wa kitanzania imewasaidia vijana wengi kujiandaa na kuingia katika soko la ajira ikiwemo sekta muhimu za kipaumbele kama vile Ujenzi, Ukarimu, teknolojia ya habari, mawasiliano na utalii.
Aliongeza kuwa Programu ya Mafunzo kwa Vitendo Mahali pa Kazi kwa wahitimu imewanufaisha vijana zaidi ya 5,967 ambapo vijana 3,967 wamehitimu mafunzo na kati yao vijana 1,827 wamepata ajira moja kwa moja na vijana 2,000 bado wanaendelea na mafunzo hayo.
Naye, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stergomena Tax alieleza kuwa Serikali ya Tanzania imeonesha nia thabiti ya kutatua changamoto ya ajira kwa kuanzisha programu ya kukuza ujuzi kwa vijana lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo vijana.
“Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi inazozifanya katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, kwa kuwapatia mafunzo yatakayowajengea uzoefu katika soko la ajira,” alisema Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Tax
Mkutano huo wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeshirikisha pia Wadau wa Utatu wa Jumuiya hiyo ikiwemo Jukwaa la Vyama vya Waajiri Kusini mwa Afrika (SPSF), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Kusini mwa Afrika (SATUCC), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji kanda ya Kusini mwa Afrika (IOM).

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.