Na. OWM, DODOMA
Ujumbe wa maafisa waandamizi wa serikali kutoka
nchini Sudani umekuja hapa nchini kujifunza masuala ya Uratibu wa Vuguvugu la
Lishe na urutubishaji wa Vyakula. Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu
masuala ya lishe nchini kutokana na mamlaka iliyonayo kikatiba ya kuratibu
shughuli zote za Serikali pamoja na masuala mtambuka. Uratibu huo unafanywa
kupitia Kamati ya kitaifa ya Lishe chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko.
Tanzania kupitia Ofisi hiyo imefanikiwa kuandaa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe ambao
hutoa mwongozo wa utekelezaji wa masuala ya Lishe nchini, ikiwemo kupambana na
upungufu wa ukosefu wa virutubishi kwa kuongeza virutubishi hivyo kwenye
vyakula, pamoja na uanzishwaji wa majukwaa
mengine ya lishe katika ngazi ya kitaifa hadi ngazi ya mkoa na wilaya likiwemo
jukwaa la sekta binafsi linalojikita sana kwenye masuala ya urutubishaji wa
vyakula.
Akiongea mara baada ya kikao cha
kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Urutubishaji wa vyakula, mjini
Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Paul Sangawe, ambaye pia ni Mratibu wa
Vuguvugu la lishe nchini, amefafanua kuwa Tanzania ilikuwa miongoni
mwa nchi za awali duniani kujiunga na Vuguvugu la Lishe, ambalo linahimiza
ushiriki wa sekta zingine na wadau wa lishe kupambana na utapiamlo wa watoto wa
chini ya miaka mitano hasa aina ya udumavu, ambapo kwa sasa Tanzania imefanikiwa kupunguza udumavu kutoka 42% mwaka 2010 hadi 32% mwaka 2018.
“Kutokana na utekelezaji mzuri wa Vuguvugu la Lishe
tumefanikiwa kuwa na mtandao mzuri wa Lishe wa kisekta kwa sekta binafsi,
lakini pia utashi wa kisiasa umeongezeka hapa nchini ambapo tayari takribani
wabunge 55 wamejitanabaisha kujihusisha na masuala ya lishe. Masuala ya lishe
tayari yameingizwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa
miaka mitano (2016-2021) na Mwongozo wa Mpango na Bajeti ambao umesaidia
masuala ya lishe kuingizwa kwenye mipango ya kisekta ya nchi ”
amesisitiza Sangawe.
Aidha, Sangawe amebainisha kuwa tayari Tanzania
imefanikiwa kuwa na Kanuni za Urutubishaji wa Vyakula za mwaka 2011, ambapo
kanuni hizo zinavihusu viwanda vikubwa vya uzalishaji wa vyakula hususan unga
wa ngano na mafuta ya kupikia.
Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, imeendelea kulipa kipaumbele
suala la lishe kwa kutoa muongozo kwa Halmashauri zote nchini
kutenga fedha za lishe kwa kila mtoto, ambapo awali ilikuwa
Shilingi 550/=, kwa kila mtoto na kwa sasa ni shilingi 1,000/= kwa
kila mtoto.
“Kwa sasa serikali
imefanikiwa kuajiri wataalamu wa masuala ya lishe katika ngazi ya Wizara na
Halmashauri ambapo kwa sasa 57% ya Halmashauri 185 zote nchini zimeajiri
wataalamu wa masuala ya lishe huku Halmashauri zilizobaki zina maafisa viungo
tu wa masuala ya lishe ” Amesisitiza Sangwe.
Amebainisha kuwa serikali
imeamua suala la lishe kuwa agenda ya Kitaifa ambapo kwa sasa imeandaa
makubaliano maalum (mikataba ya lishe) kwenye ngazi za serikali za mitaa ambayo
ni kati ya ngazi hizo na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), lengo ni kuongeza uwajibikaji kwenye masuala ya lishe.
Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe wa Maafisa
Waandamizi kutoka nchini Sudani, Kutoka Wizara ya Afya nchini Sudani, Huda
Kambal, amefafanua kuwa wamechagua kuja Tanzania kujifunza uratibu wa kisekta
wa masuala ya lishe na Urutubishaji wa vyakula hususani kwenye unga wa ngano na
mafuta ya kupikia.
“Sisi katika nchi ya Sudani hatuna huu Uratibu wa
kisekta katika masuala ya lishe na Urutubishaji wa vyakula. Lengo la kuja hapa
ni kujifunza na kutaka kupata uzoefu wa namna ya kuratibu na kutekeleza
shughuli za Urutubishaji wa Vyakula hasa kwa wazalishaji wakubwa wa vyakula ili
twende tukaboreshe nchini kwetu shughuli hizo” Amesisitiza Kambal
Amebainisha kuwa katika kuhakikisha
wanafanikiwa kwenye kuanzisha Utaratibu huo wanatarajia kujifunza na kupata
uzoefu katika maeneo ya Udhibiti na Usimamizi wa vyakula vilivyorutubishwa,
ushiriki wa sekta binafsi kwenye masuala ya lishe, ufuatiliaji wa mara kwa mara
na mawasiliano kwa umma juu ya masuala ya lishe.
Kikao hicho kilihudhuriwa na maafisa kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za serikali, Taasisi ya
Lishe Tanzania, Shirika la Viwango Tanzania pamoja na maafisa waaandamizi
kutoka nchini Sudani ambao wametoka Wizara ya Afya, Shirika la Chakula
Duniani, Shirika la Afya Duniani, Mamlaka ya Viwango na Ubora Sudani, Mamlaka
ya utafiti na Viwanda, Wizara ya Viwanda na Shirika la Biashara Sudani
Mnamo mwaka 2012 Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa
nchi za kwanza Duniani kujiunga kwenye Vuguvugu la Lishe Duniani, ambapo mnamo
mwaka 2011 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipindi hicho ,
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa kwanza kuingia
kwenye kikundi cha viongozi wa Vuguvugu la Lishe Duniani. Kuanzia Kipindi hicho
Agenda ya kitaifa ya masuala ya lishe ilianza kuratibiwa na Ofisi ya Waziri
Mkuu kama Ofisi yenye dhamana ya kuratibu shuguli za Serikali kwa mujibu wa
sheria.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.