Friday, March 6, 2020

WAFICHUENI WAFANYABIASHARA WA MAGENDO-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wananchi washirikiane na Serikali katika kuwafichua wafanyabiashara wa magendo wanaoingiza bidhaa kwa kupitia bandari bubu.

Pia ameiagiza Idara ya  Uvuvi wilaya ya Pangani ihakikishe inadhibiti uvuvi haramu wa kutumia mabomu na nyavu zisizo stahili kwa kuwa unahatarisha mazalia ya samaki.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 6, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Bomani, wilayani Pangani.

Amesema uwepo wa bandari bubu katika wilaya hiyo unasababisha kuingizwa kwa bidhaa ambazo viwango vyake havijathibitishwa na mamlaka husika hivyo kuhatarisha afya za watumiaji.

“Wananchi shirikianeni na Serikali katika kuwataja wanaoingiza bidhaa kupitia bandari bubu kwani licha ya bidhaa hizo kutokuwa na uhakika wa ubora, pia hata wakwepakodi nao wanapitia huko.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu malalamiko ya wafanyakazi wa mkonge ambapo amesema atamuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aende kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Pangani na Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu, maji na umeme kwani kati ya vijiji 33 vya jimbo hilo vitatu tu ndio havina umeme.

Pia mbunge huyo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani yenye urefu wa kilometa 50 pamoja na ulipaji fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha mradi huo.

Awali, Waziri Mkuu alizindua mradi wa ujenzi wa ujenzi wa ukuta wa mto Pangani kwa upande wa kaskazini wenye urefu wa mita 950 uliogharimu sh. Bilioni 2.9. Pia alizindua kituo cha polisi cha wilaya ya Pangani pamoja.

Mwisho

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.