Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na waganga wakuu wa mikoa
|
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akiwa na Naibu Katibu Mkuu
OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof.
Muhammad Bakari Kambi wakati wa mkutano huo
|
Afisa kutoka kitengo cha magonjwa ya milipuko wizara ya afya
Dkt. Vida Makundi akitoa mada kwenye mkutano wa waganga wakuu wa mikoa
|
Baadhi wa waganga wakuu wa mikoa na maofisa kutoka wizara ya
afya walioshiriki mkutano wa kujadili tishio la ugonjwa wa Corona
|
Na. WAMJW - Dar es Salaam
Wananchi wanatakiwa kupewa elimu
ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaoletwa na kirusi wa
Corona (COVID-19) ili kuepusha usisambae endapo atatokea muhisiwa wa ugonjwa
huo hapa nchini.
Maelekezo hayo yametolewa leo na
Katibu Mkuu - Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto:
Idara Kuu Afya Dkt. Zainab Chaula, wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Waganga
Wakuu wa Mikoa (RMOs) wa kujadili utayari, changamoto na hatua za
kukabiliana na tishio la mlipuko wa
COVID-19 uliofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la
Mloganzila jijini Dar es slaam , tarehe 10 Machi 2020.
“Katika mkoa wewe mganga mkuu wa
mkoa ndio mtaalam namba moja wa afya kwenye mkoa wako ambalo ndilo eneo lako la
kazi, hivyo mnatakiwa kushauri viongozi katika kukabiliana na ugonjwa huu”. Amesisitiza
Dkt. Chaula
Amesema upashanaji elimu juu ya
kujikinga na maambukizi kwa wananchi ni jambo muhimu sana kwani jamii inapaswa
kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya ugonjwa huo unavyoambukizwa pamoja na
dalili zake ili kila rika iweze kuwa na ufahamu na hivyo itasaidia kuepusha
magonjwa ya mlipuko yasiingie nchini.
“Kama nchi za Afrika hivi sasa
hatupo kwenye hatua ya utayari bali kwenye hatua ya kukabiliana. Kwani utaona
ugonjwa huu umezikumba nchi nyingine, hivyo kama nchi lazima wataalam wote
tujiandae kukabiliana na virusi hivi vya Corona ili endapo tutapata mgonjwa
basi vyanzo vyote vya maambukizi vinatakiwa kudhibitiwa ili usienee.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI
anayeshughulikia afya Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa TAMISEMI wapo tayari
kupokea maelekezo na mafunzo yote ya kisekta ili kutimiza lengo tarajiwa la
Serikali la kudhibiti na kukabiliana ugonjwa huo.
Dkt. Gwajiama amesema kuwa mkutano huu utasaidia waganga
wakuu wa mikoa nchini kutoka na mkakati wa pamoja wa namna ya kukabiliana na
ugonjwa huu hususan mikoa ya mipakani kama Kagera, Katavi, Songwe, Kigoma,
pamoja na mikoa mingine ambayo ipo kwenye hatari ya kuingia kwa magonjwa ya
mlipuko.
Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka waganga wakuu
hao kutoa mafunzo kwa wataalam wengine wa chini yao na viongozi wa mikoa na
halmashauri ili kwenda pamoja katika kukabiliana na magonjwa wakati wa dharura.
Kwa upande wake Mratibu wa
Masuala ya maafa, Idara ya Menejimenti ya Maafa, ofisi ya Waziri Mkuu, kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Idara hiyo amefafanua kuwa, katika ngazi ya mkoa na wilaya
hadi kwenye vijiji zipo Kamati za maafa hivyo wataalamu hao hawanabudi kuwap
elimu ili waweze kuwelimisha wananchi walionao katika ngazi zao na hatimaye
uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo utakuwa umeimarika.
-MWISHO-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.