Tuesday, April 21, 2020

WAZIRI MKUU AONGOZA MAOMBI YA KITAIFA KUKABILIANA NA VIRUSI VYA CORONA

*Idadi ya wagonjwa yafikia 284, ataka tahadhari zaidi iongezwe
*Aomba viongozi wa dini wahakikishe mikusanyiko ibadani inapungua
*Akemea wanaopandisha bei za vyakula hasa sukari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia jana (Aprili 21, 2020) jumla ya wagonjwa 284 wamethibitika kuwa na virusi vya ugonjwa wa corona (Covid-19) ambapo wagonjwa 256 wanaendelea vizuri, saba wako kwenye uangalizi maalum, 11 wamepona na 10 wamefariki.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 22, 2020) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa dini walioshiriki maombezi ya Kitaifa dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) yaliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Amesema jumla ya watu 2,815 waliokuwa karibu na wagonjwa wamefuatiliwa afya zao ambapo kati yao, watu 1,733 walikutwa hawana maambukizi na watu 12 walikutwa na virusi hivyo (wapo kwenye orodha ya watu 284).

“Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa ifikapo mwishoni wa Aprili, 2020 nchi yetu ingekuwa na wagonjwa 524,716 lakini tunamshukuru Mungu kwa kuwa kadirio hilo hatujalifikia.”

Kuhusu hali ya maambukizi ilivyo nchini, Waziri Mkuu amesema Jiji la Dar es Saalam na kisiwa cha Zanzibar, yanaongoza kwa maambukizi na akataka tahadhari zaidi zichukuliwe. “Jiji la Dar es Salaam ndio lina maambukizi makubwa hivyo nawasihi wananchi kama huna jambo lolote la kufanya huna sababu ya kuzurura na kwa wafanyabiashara siyo lazima mje Kariakoo, unaweza kufanyia biashara katika eneo lako,” amesisitiza.

“Ni wakati kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari vya kutosha ili kuepuka maambukizi. Epuka misongamano isiyokuwa ya lazima, huna sababu ya kumuamini yeyote, ona kuwa kila mmoja ana ugonjwa.”

Kipekee, Waziri Mkuu amewaomba viongozi wa dini waendelee kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na ugonjwa huo kwa kuwaelimisha waumini wachukue tahadhari zote muhimu. “Ninawaomba viongozi wa dini wachukue tahadhari zaidi kwa kuhakikisha mikusanyiko kwenye nyumba za ibada inapungua ikiwemo waumini kukakaa kwa nafasi, umbali wa angalau mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine na kuweka maeneo ya kunawa kwa maji na sabuni pamoja na vitakasa mikono katika nyumba zote za ibada.

“Kupunguza idadi ya siku za kukutana kufanya ibada na masaa ya ibada au mahubiri kila inapobidi. Kwa mfano, mikutano au shughuli za mikusanyiko za vikundi vya uimbaji, vijana, akinamama au waumini kwa ujumla ni vema zikasitishwa katika kipindi hiki,” amesisitiza.

Kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa huu zikiwemo za kutoa elimu ya namna ya kujikinga, kuunda Kamati za Kitaifa kwa ngazi za Mawaziri, Makatibu Wakuu, Timu ya Wataalam wa afya pamoja na kutoa maelekezo kwa Kamati za Ulinzi na Usalama.

“Tumetenga maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huu, tumenunua vifaa vya kukabiliana na ugonjwa huu hususani kwa watoa huduma wa afya. Tumeimarisha maabara zetu kwa lengo la kupanua wigo wa kufanikisha upimaji wa sampuli, vituo zaidi ya saba nchini ambapo upimaji wa awali unaanzia huko na kwenda kuhakikishwa katika Maabara Kuu ya Taifa,” amesema.

Wakati huohuo, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetaja mikoa ambayo imepata wagonjwa wapya 30 kutoka idadi ya 254 iliyotangazwa mara ya mwisho.

Wagonjwa hao na idadi yao kwenye mabano wanatoka mikoa ya Dar es Salaam (10), Zanzibar (9), Mwanza (4), Pwani (2), Dodoma (2). Mingine ni Kagera, Manyara na Morogoro ambayo yote ina mgonjwa mmoja mmoja.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wanaopenda kupandisha bei za vyakula wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Wiki hii waumini wa Kiislamu wanaanza mfungo wa Ramadhan, hivyo natoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha vyakula muhimu katika kipindi hiki vinauzwa kwa bei ya kawaida, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wafanye ukaguzi wa mara kwa mara kwenye masoko ili kuhakikisha bei ni ile ile.”

Amesema kuwa hivi sasa kuna sukari ya kutosha nchini hivyo bei itaendelea kuwa ileile bila kujali msimu. “Ninaawagiza Wakuu wa Mikoa, yeyote atakayekutwa anauza sukari kwa bei ya sh.4,500, chukua hatua dhidi yake kwani hayo si malengo ya Serikali yetu,” amesisitiza.

Kwa upande wao, wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa dini walioshiriki maombi hayo, wameipongeza Serikali kwa hatua ambazo imezichukua hadi sasa katika kukabiliana na ugonjwa huo.

(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.