Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amehimiza
wawekezaji katika sekta mbalimbali kuongeza uzalishaji zaidi hususani katika
kipindi hiki ambacho mahitaji ya bidhaa mbalimbali yanazidi kukua katika soko
la ndani. Ameyasema hayo leo tarehe 18 Mei 2020 alipotembelea Kiwanda cha OK Plast Ltd kilichopo Vingunguti, Dar
Es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amepata fursa ya kujionea shughuli
mbalimbali za uzalishaji zinazoendelea kiwandani hapo na kusikiliza changamoto
zao.
Kiwanda
hicho cha OK Plast Ltd ni moja ya viwanda vichache vinavyochakata skrepaza
shaba
na kuzalisha bidhaa za mwisho kama vile nyaya za aina mbalimbali za umeme
pamoja na malighafi za viwanda vingine kama vile ingoti za betri, kathodi na
rodi za shaba.
Wakati
akimpatia maelezo ya uwekezaji wa kiwanda hicho, Meneja wa Kiwanda Bw. Fadl
Ghaddar ameeleza kuwa hadi sasa wameshawekeza takribani Shilingi bilioni 10 kwa
ajili ya kuendeleza mradi huo ambapo amebainisha kuwa tangu waliposajili mradi
huo Mwaka 2005 umekuwa ukijiendesha kwa mafanikio ikiwemo kuweza kuzalisha
bidhaa zenye uhakika wa soko la hapa nchini huku wakiendelea kupokea oda za
bidhaa kutoka nchi jirani hususani kutoka Kenya.
Meneja
huyo aliongeza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kuajiri jumla ya wafanyakazi 600
ambapo kati yao 595 ni Watanzania na 5 tu ndiyo raia wa kigeni. Aidha,
alifafanua kuwa wanajivunia kuweza kuendelea kutoa mafunzo ya ujuzi wa
kushughulikia aina mbalimbali za metali kwa waajiriwa wao na hata wale
wanaoamua kuacha kazi huondoka wakiwa na ujuzi wa kuweza kuanzisha karakana zao
na kujitegemea. Kiwanda hicho kinalipa Kodi taribani Shilingi bilioni 2 kwa
mwaka, alieleza.
Hata
hivyo, Bw. Ghaddar alibainisha kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni
uhaba wa malighafi ya skrepa ya shaba jambo ambalo limepelekea Kiwanda
kuzalisha chini ya uwezo wake ambapo kwa sasa huzalisha takriban tani
150 za
bidhaa mbalimbali za shaba kwa mwezi huku uwezo wa kiwanda kuzalisha ukiwa tani
zaidiya
500 kwa
mwezi. Alieleza kuwa changamoto hiyo inatokana na ukweli kwamba licha ya
utafiti uliofanywa na Taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuonesha
kuwa kuna upatikanaji wa kutosha wa skrepa ya shaba hapa nchini kutosheleza
mahitaji ya viwanda vya kuchakata malighafi hiyo, kuendelea kuuzwa nje ya nchi
kwa skrepa kumesababisha uhaba wa malighafi hiyo kwa viwanda vinavyoihitaji
hapa nchini. Hivyo, alishauri na kutoa ombi kwa Serikali kupitia kwa Waziri wa
Uwekezaji kuliangalia suala hilo ili kulinda viwanda vya ndani kwa
kuvihakikishia upatikanaji wa malighafi ya kutosha ili kuepuka kutumia fedha za
kigeni kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.
Kwa
upande wake Waziri Kairuki aliupongeza uongozi wa Kiwanda hicho kwa kuhakikisha
uzalishaji kiwandani hapo unaendelea kama kawaida licha ya changamoto ambazo
wanakabiliana nazo. Alipongeza pia hatua ya Kiwanda hicho kuitikia wito wa
Serikali kwa wawekezaji wa kuajiri Watanzania kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa
na wazawa pamoja na kuweka program nzuri kwa wataalamu wa kigeni kutoa mafunzo
ya ujuzi mbalimbali kwa wafanyakazi wa kitanzania. Alitumia pia fursa hiyo
kuwapongeza kwa kulipa kodi za Serikali kwa mujibu wa Sheria na kuwataka
wawekezaji wengine pia kuiga mfano huo ikiwa ni sehemu ya wajibu wao kwa
Serikali.
Aidha
alitoa wito kwa wawekezaji waliojisajili Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC) kuendelea kuwasilisha taarifa za
maendeleo ya miradi yao kila baada ya miezi 6 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni
za usajili TIC ili Kituo kiweze kufahamu na kufuatilia kwa karibu changamoto
mbalimbali wanazokabiliana nazo kwa wakati.
Waziri
Kairuki anatarajia kuendelea na ziara ya kutembelea miradi ya uwekezaji katika
sekta mbalimbali katika Mikoa ya Dodoma na Singida kwa lengo la kusikiliza
chanmagamoto zao na kuhamasisha
uzalishaji hususani wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini badala ya
kuagizwa kutoka nje ya Nchi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.