Tuesday, May 19, 2020

WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WATATU TEMESA

* Atoa onyo kwa Mtendaji Mkuu wa TEMESA
* Taasisi za Serikali zapewa miezi miwili kulipa deni la sh. bil 25

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa sh. milioni 780 zinazotokana na zabuni.

Vile vile, Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi miwili kwa taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na TEMESA kiasi cha sh. bilioni 25.88 ziwe zimeshalipa na iwapo kuna taasisi itashindwa kulipa deni lake hadi Julai 30, 2020 apewe taarifa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Mei 19, 2020) alipotembelea karakana ya mitambo ya TEMESA jijini Dodoma na amewasisitiza watumishi hao wafanye kazi kwa uadilifu na Serikali haihitaji wala haitowavumilia watumishi wazembe.

Watumishi waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Hans Lyimo, Kaimu Mhasibu Mkuu, Jonas Bakuza na Lecian Mgeta aliyekuwa Mhasibu wa Wakala huo ambaye aliandika barua ya kuacha kazi Aprili 6, 2020. Waziri Mkuu ameagiza mtumishi huo arudishwe kazini ili akajibu tuhuma zinazomkabili.

“Kazi hii imefanywa kwa ushirikiano na Afisa wa benki ya CRDB asiyekuwa muaminifu ambaye naye tutamtafuta hadi tumpate. Fedha hizo zilikuwa kwenye mfumo wa hundi wao wakazibadilisha na kuziweka katika mfumo wa fedha taslimu. Umakini usipokuwepo fedha zote zitakuwa zinaliwa tu.”

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemuonya Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Japhet Maselle kutokana na usimamizi wake usioridhisha, ambapo amesema Mtendaji huyo alikuwa anajua kuhusu upotevu wa fedha katika wakala huo na hakuchukua hatua kwa wahusika.

 “…si mzuri kwenye usimamizi unapenda kuacha watu wanaofanya maovu wakiwemo na watumishi hawa watatu. Mtendaji ulikuwa unajua, ulikuwa hauchukui hatua hadi uliposikia nakuja, hii si sahihi sheria zipo na maelekezo ya Serikali yapo. Upotevu wa sh. milioni 780 katika taasisi ni doa.”

Waziri Mkuu amesema kufuatia na matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa TEMESA, amemuagiza Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akafanye ukaguzi katika wakala huo kutokana na upotevu wa sh. milioni 780 zilizotakiwa zipelekwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na wakala huo ziwe zimelipa madeni yote katika kipindi cha miezi miwili ili kuiwezsha TEMESA kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Tukishapata bilioni 25 TEMESA hii tukapeleka walau bilioni moja moja kila mkoa watanunua mitambo, watanunua vipuri na magari yatatengenezwa kwa haraka. Magari yote ya Serikali lazima yatengenezwe TEMESA kwa sababu ya uhakika wa usalama wake.”

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wakala huo ufanye maboresho makubwa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya sehemu ya magari kwa kuwa inalalamikiwa zaidi hususani suala la utengenezaji wa magari yanayopelekwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa wanalalamikia gharama kubwa wanazotozwa kwa ajili ya utengenezaji wa magari, hivyo lazima ziangaliwe kama ni halisi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wakala huo ujiridhishe kila kivuko kama ni kizima ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea na wavifanyie ukaguzi wa mara kwa mara.

Awali, Mtendaji Mkuu wa TEMESA alisema wakala huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo madeni makubwa yanayotokana na huduma zao kutolipwa kwa wakati au kutolipwa kabisa.

“…kwa mfano hadi mwezi Machi 2020 tunazidai taasisi za Serikali kiasi cha shilingi 25,882,593,038 na wakati huo huo tukidaiwa na wazabuni mbalimbali kiasi cha shilingi 18,959,630,408.”

Changamoto nyingine aliyoitaja ni uchakavu wa karakara nyingi zinazomilikiwa na wakala huo katika makao makuu ya mikoa mbalimbali nchini, hivyo kuathiri ufanisi katika matengenezo ya magari ya Serikali.


(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.