Tuesday, June 30, 2020

TIMU YA WATAALAMU YAENDESHA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UELEWA WADAU KUHUSU HIFADHI YA JAMII

Baadhi ya wadau waliohudhuria mafunzo hayo wakiwa wamewaka daftari “Notebook” kichwani kama ishara ya kumkinga wananchi na changamoto mbalimbali.
Mtaalamu wa Kinga ya Jamii, Dkt. Flora Miyamba akitoa mada kwa wadau kuhusu masuala ya Kinga ya Jamii.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka TAMISEMI, Bi. Mariam Nkumbwa (kushoto) akichangia mada wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa PSSSF, Jijini Dodoma.
Sehemu ya wadau wakijadili jambo wakati wa mafunzo hayo ya kuwajengea uelewa kuhusu masuala hifadhi ya jamii.

Sehemu ya wadau wakijadili jambo wakati wa mafunzo hayo ya kuwajengea uelewa kuhusu masuala hifadhi ya jamii.
Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Sarah Mshui akieleza jambo kuhusu masuala ya Hifadhi ya Jamii kwa wadau walipokutana kwa ajili ya mafunzo maalumu ya kujengewa uelewa kuhusu Kinga ya Jamii katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF, Jijini Dodoma.
Afisa Maendeleo ya Jamii, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bi. Herieth Mwamba (kushoto) akieleza jambo wakati wa mkutano huo.   


Wednesday, June 24, 2020

SERIKALI ITASHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA WATANZANIA WOTE BILA YA UBAGUZI-MAJALIWA


                                       
                                                                                             
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania wote zikiwemo za afya, maji, miundombinu na elimu bila ya kujali itikadi zao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 24, 2020) alipozungumza na wananchi baada ya kutembelea Zahanati ya kijiji cha Nandagala akiwa katika ziara ya kikazi wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, ambapo amewataka wananchi washikamane na Serikali katika kuboresha maendeleo yao.

“Suala la maendeleo halina chama, maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni kwa ajili ya wananchi wote, hivyo watu wote tunatakiwa tushikamane kwa pamoja kumshukuru na kumuunga mkono Rais Dkt. Magufuli kwani shule, hospitali anazojenga zinatumika na watu wote.”

Amesema wananchi wanatakiwa watambue jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. Magufuli katika kuboresha huduma za afya. “Leo nimeshuhudia wagonjwa wakiwa wamelazwa katika zahanati yetu ya Nandagala. Haya ni mafanikio makubwa awali hatukuwa na Zahanati hapa.”

Amesema awali kijiji hicho hakikuwa na Zahanati na wakazi wake waliuguzwa majumbani kwa kushindwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, ujenzi wa zahanati hiyo umekuwa mkombozi mkubwa hususani kwa wajawazito kwani huduma zote zikiwemo za mama na mtoto zinatolewa hapo.

Vilele, Waziri Mkuu ametembelea kijiji cha Luchelegwa na amekabidhi gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya cha kata ya Luchelegwa. Gari hilo limetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ufadhili wa Global Fund.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa vijiji vyote ambavyo havina zahanati viongozi wake waanzishe miradi ya ujenzi wa zahanati na watakapokamilisha ujenzi wa maboma Serikali itawapelekea vifaa vya viwandani yakiwemo mabati na misumari.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Luchelegwa Dkt. Codratus Mutabihirwa ameishukuru Serikali kwa kuwapa gari la kubebea wagonjwa kwani awali walikuwa wanapata tabu pale wanapokuwa na mgonjwa anayetakiwa kuhamishiwa hospitali ya wilaya.

Amesema gari hilo litatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kwamba watalitunza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha linakuwa na mafuta wakati wote. “Tayari tumeshatenga fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya gari hili, hivyo hata matengenezo kinga yatakuwa yanafanyika kwa wakati.”

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Luchelegwa walitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la kubebea wagonjwa kwa sababu walikuwa wanapata tabu sana hususani kwa wajawazito ambao walikuwa wakihamishiwa hospitali ya wilaya kwani walikuwa wanatumia pikipiki.

Mmoja wa wananchi hao Sauda Kaisi amesema anaishukuru Serikali kwa kuwapelekea gari hilo kwa kuwa Kituo cha Afya cha Luchelegwa hakikuwa na gari la kubebea wagonjwa jambo ambalo lilisababisha baadhi ya ndugu zao kupoteza maisha kwa kushindwa kupata huduma kwa wakati.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Joyce Chimela amesema anamshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali kwenye wilaya yao kikiwemo Kituo chao cha Afya cha Luchelegwa ambacho kimepewa gari la kubebea wagonjwa litakalowafikisha kwa wakati hospitali ya wilaya.

Mwisho.

KUSHUKA KWA BEI YA MAZAO KUSIWAKATISHE TAMAA-MAJALIWA


*Awataka wakulima waendelee na kilimo katika kipindi hiki cha mpito    
                                                                                                
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa mazao mbalimbali ya biashara wakiwemo wakulima wa ufuta nchini waendelee na kilimo na kwamba suala la kushukuka kwa bei lililotokea kwenye msimu wa mwaka huu lisiwakatishe tamaa kwani jambo hilo litakwisha.

Amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo na kwamba bei ya mazao nchini itaimarika baada ya kuongezeka kwa ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao nchini, ambapo wakulima watakuwa na masoko na uhakika na pia nchi itauza bidhaa zitokanazo na mazao hayo na si malighafi.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Juni 24, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa, Lindi alipokuwa katika ziara ya kikazina aliwasihi wakulima kutoacha kulima.

“Kushuka kwa bei ya ufuta kusiwakatishe tamaa na kuwafanya muache kulima kwa sababu bei haijashuka kwa zao hilo tu bali na mazao mengine kama chai, tumbaku, kahawa, chai na mazao mengine. Hali hii imetokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambao umeikumba dunia.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali inatarajia kwamba kadiri ugonjwa wa COVID-19 unavyoendelea kupungua katika Mataifa mbalimbali duniani hali bei ya mazao nayo itaimarika, hivyo wakulima waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho ni cha mpito.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi waje wawekeze katika viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali kwa sababu watakuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi pamoja na nishati ya kutosha.

Alisema moja ya msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuboresha sekta ya kilimo ili iweze kujitosheleza kwa chakula. “Suala la bei ya mazao linapangwa na wanunuzi Serikali inasimamia tu.”

Pia, Waziri Mkuu ameendelea kuwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa umoja na mshikamano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na amewasisitiza waendelee na ushirikiano huo kwa ajili ya maendeleo ya wilaya yao na Taifa kwa ujumla.

Mwisho.

ZIARA YA MAJALIWA RUANGWA JUNI 24

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama picha yake iliyochorwa na Tabibu wa Meno wa Kituo cha Afya cha Kingorwila Morogoro, Sanjame Kayoka  wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Nachingwea, Wilayani Ruangwa Juni 24, 2020. 
Mwimbaji wa nyimbo za Sengeli, Hassan marufu kwa jina la  Dogo H akitumbuiza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Nachingwea, Wilayani Ruangwa, Juni 24, 2020. 
Mwimbaji wa nyimbo za Sengeli, Hassan marufu kwa jina la  Dogo H akitumbuiza wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Nachingwea, Wilayani Ruangwa, Juni 24, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia wimbo kutoka kwa mwimbaji wa nyimbo za Sengeli, Hassan maarufu kwa jina la Dogo H. wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Nachingwea, Wilayani Ruangwa Juni 24, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea picha yake iliyochorwa na Tabibu wa Meno wa Kituo cha Afya cha Kingorwila Morogoro, Sanjame Kayoka (kulia) wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Nachingwea, Wilayani Ruangwa Juni 24, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama picha yake iliyochorwa na Tabibu wa Meno wa Kituo cha Afya cha Kingorwila Morogoro, Sanjame Kayoka (kulia) wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Nachingwea,Wilayani Ruangwa Juni 24, 2020. 



Tuesday, June 23, 2020

WIKI YA UTUMISHI WA UMMA -OWM

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi:Dorothy Mwaluko awakumbusha watumishi wa Ofisi yake wajibu wa majukumu yao wawapo kazini na kuwataka kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa kila moja kwenye eneo lake.

Katibu Mkuu amesema hayo kwenye mkutano na watumishi wa  Ofisi yake katika kukamilisha wiki ya Utumishi wa uuma kwa mwaka 2020, iliyobeba kauli mbiu isemayo  “jukumu la mtumishi wa umma katika kujenga na kudumisha amani iliyopo miongoni mwa jamii”

Katika kikao hicho aliwakumbusha kuwa na nidhamu ya kutosha katika uwajibikaji wa kazi na kila mtumishi kuzingatia sheria na taratibu za kazi awapo kazini.

Aidha aliwakumbusha pia watumishi kukamilisha ujazaji fomu za upimaji utendaji kazi yani (OPRAS) ambacho ndicho kipimo sahihi cha uwajibikaji wa mtumishi wa umma.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw:Greyson Mwaigombe  alimshukuru Katibu Mkuu kwa niaba ya watumishi wote na kuahidi kutekeleza yale yote aliyo elekeza.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa hazina jijini Dodoma uli hudhuriwa na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu na mada mbalimbali zilitolewa za kuwakumbusha watumishi wajibu wao na kuzingatia maadili ya kazi na Usalama mahala pakazi.
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu Bi Dorothy Mwaluko katika Mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu Bi Dorothy Mwaluko katika Mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu Bi Dorothy Mwaluko katika Mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.


MWISHO




VIJIJI VYOTE NCHINI KUFIKIWA NA UMEME-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vijiji 25 vya wilaya ya Ruangwa ambavyo bado havijafikiwa na umeme.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi walio katika vijiji ambavyo bado havijaunganishiwa nishati ya umeme wafanye maandalizi kwa sababu maeneo mengine tayari wakandarasi wameshapatikana.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 23, 2020) wakati alipozungumza na wananchi katika vijiji vya Nanjaru, Nambilanje, Mkaranga, Namichiga na Mbekenyera akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Amesema wilaya ya Ruangwa ina jumla ya vijiji 90 kati yake vijiji 25 tu ndio bado havijafikiwa na huduma ya umeme lakini tayari mkandarasi ameshapatikana na ameshaanza kazi, hivyo aliwataka wananchi wajiandae kuunganisha umeme kwenye nyumba zao za makazi na biashara.

“Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme na amepunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 ili kila mwananchi aweze kumudu gharama hizo.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa licha ya gharama za kuunganishiwa umeme kupunguzwa, pia wananchi hatolazimika kulipia gharama za nguzo pamoja na gharama za fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari zimeshalipiwa na Serikali.
      
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Serikali imeboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya na kwamba haitaki kuona mwananchi anakwenda maeneo hayo na kukosa huduma.

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipoingia madarakani aliongeza bajeti ya dawa kutoka sh bilioni 31 na kufikia sh. bilioni 269, hatutarajii kusikia mgonjwa amekwenda zahanati akaandikiwa cheti na kisha akaelekezwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi.”

Waziri Mkuu amesema ni lazima dawa zipatikane katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya kulingana na hadhi ya eneo husika kama zahanati lazima dawa zinazotakiwa kuwepo kwenye zahanati ziwepo, kadhalika kituo cha afya na hospitali.

Mwisho.