OWM,
DODOMA.
Ofisi
ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Uwekezaji imekutana na wadau wa uwekezaji
wa sekta ya Umma kwa lengo la kuidhinisha taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa
Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996. Wadau hao ni kutoka Wizara, Idara,
Taasisi na Wakala wa Serikali. Baada ya kupokea taarifa ya Tathmini ya
Utekelezaji wa Sera hiyo,wameridhishwa kwa jinsi ilivyobainisha nchi inavyoweza
kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa
ndani na nje.
Wakipongeza
wakati wa kujadili taarifa hiyo, leo tarehe 11 Septemba, 2020 jijini Dodoma. Wadau
hao wamesisitiza Tathmini hiyo iliyojikita kwenye masuala ya kisera, kisheria
na kiutendaji inaendelea kutoa mapendekezo ya kuendelea kutatua changamoto za
uwekezaji nchini hususani kwenye maeneo ya Uratibu wa Masuala ya Uwekezaji,
Utangazaji wa Fursa za Uwekezaji, Uwezeshaji Uwekezaji, pamoja na Vivutio vya
kikodi na visivyo vya kikodi.
Akiongea
wakati akifungua kikao kazi hicho, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Uwekezaji), Bibi Dorothy Mwaluko amesisitiza kuwa upo umuhimu wa
wadau hao kubainisha masuala ya kisera, kiutendaji na kisheria, ili kuhakikisha
kuwa Sera ya Taifa ya uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji nchini haikinzani na
sheria nyingine za kisekta kwenye masuala ya uwekezaji.
“Serikali
imekuwa ikitunga Sera na Sheria kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya
uwekezaji na biashara nchini, tunahitaji kuwa na Sera madhubuti za kuvutia na
kuwezesha uwekezaji katika sekta zote ili kutumia vilivyo fursa za uwekezaji
zinazopatikana nchini.”Amesisitiza Mwaluko.
Akiongea
kwenye kikao kazi hicho Mtaalamu wa Utafiti wa masuala ya sheria ya uwekezaji
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt. Saudin Mwakaje, amefafanua kuwa
kukutana kwa wadau hao kujadili taarifa ya tathmini hiyo kutawezesha kujua
changamoto wanazozipata wakati wa utekelezaji wa sera hiyo na hatimaye utatuzi
wake, utawezesha uwekezaji na kuleta tija kwa mwananchi wa kawaida.
Naye Mkurugenzi wa Uwezeshaji
Uwekezaji, kutoka Mamlaka ya Uzalishaji kwa Mauzo ya nje (EPZ), James Maziku
amefafanua kuwa, sera hiyo imetungwa kwa muda mrefu hivyo tathmini hiyo
itasaidia kuhuisha (Review) Sera na Sheria za uwekezaji za kisekta, kupunguza
migongano ya kiutendaji na kuelewa namna ya kuboresha utendaji wa pamoja wa
kisekta.
Sera
ya Taifa ya Uwekezaji imebainisha malengo mahsusi sita (6) na malengo nane (8)
ya kisekta. Baadhi ya malengo hayo ni kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa
kwa ajili ya mauzo ya nje; Kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi; Kuhimiza na
kuvutia matumizi ya teknolojia za kisasa katika uwekezaji; Kuweka mfumo mzuri
na wa wazi wa kisheria; na kuondoa urasimu katika taratibu za upatikanaji wa
vibali vya uwekezaji.
Sera
ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997
iliyoanzisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), vinaratibiwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa, Idara, Taasisi na Wakala wa Serikali. Kituo cha Uwekezaji Tanzania
kimepewa jukumu la kuratibu, kuvutia, kutangaza na kuwezesha wawekezaji hapa
nchini.
MWISHO.
Mratibu wa Masuala ya Uwekezaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jumanne Gomera, akiwasilisha wasilisho la taarifa ya Tathmini ya sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996, wakati wa warsha ya wadau wa uwekezaji sekta ya Umma kujadili taarifa hiyo, kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, leo tarehe 11 Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha wadau wa uwekezaji sekta ya Umma wakifuatilia Warsha iliyolenga kuidhinisha taarifa ya Tathmini ya sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996, kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, leo tarehe 11 Jijini Dodoma.Mkurugezi wa Idara ya Maendeleo ya Uwekezaji, Aristides Mbwasi na Mtaalamu wa Utafiti wa masuala ya sheria ya uwekezaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt. Saudin Mwakaje wakiteta jambo wakati wa kikao kazi cha wadau wa uwekezaji sekta ya Umma iliyolenga kuidhinisha taarifa ya Tathmini ya sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996, kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, leo tarehe 11 Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.