Friday, December 31, 2021

Waziri Mhagama: Serikali Kuendelea Kuchukua Hatua Stahiki Dhidi ya Majanga na Maafa Nchini


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watendaji kutoka katika ofisi yake alipotembelea na kukagua Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula kilichopo katika ofisi hiyo hii leo Desemba 31, 2021 Jijini Dodoma.

Na: Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya Majanga na Maafa nchini kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa cha kisasa (Tanzania Centre of Excellence in Disaster Management).  

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea na kukagua Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula kilichopo katika ofisi hiyo hii leo Desemba 31, 2021 Jijini Dodoma kwa lengo la kupokea taarifa na hatua zinazochukuliwa katika kuboresha utendaji wa kituo hicho.

Waziri Mhagama alieleza kuwa kati ya mambo mazuri yaliyofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa katika mwaka wa 2021 ni pamoja na ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa cha kisasa kinachojengwa eneo la Nzuguni ‘B’ Jijini Dodoma.

“Ofisi ya Waziri Mkuu tunajivunia na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa ambacho kitasaidia kuimarisha uwezo wa usimamizi wa maafa katika sekta zote hapa nchini kwa ajili ya maendeleo endelevu,” alisema Waziri Mhagama

“Ujenzi wa kituo hicho ni dhamira ya serikali katika kuhakikisha inazingatia namna njema ya hatua za kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na maafa yanapojitokeza,” alisema

Aliongeza kuwa, Katika kutekeleza mpango huo Serikali imeendelea na azma ya ujenzi wa Kituo cha Tiafa cha Usimamizi wa Maafa nchini kwa kuingiza tena mpango wa ujenzi wa kituo hicho katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020 – 2025) katika Ibara ya 107 kipengele (h) ikiwa na lengo la kuhakikisha vyombo vinavyoshughulika na maafa vinakuwa na mpango wa utayari wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alieleza kuwa kituo hicho kitasaidia kuimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa na kuwezesha uwepo wa vifaa na zana za kisasa katika utoaji wa huduma za usimamizi wa maafa nchini, kuwa na mfumo wa kisayansi wa kufuatilia mwenendo wa majanga na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukua kwa wakati kwa ajili ya tahadhari za awali, kuimarisha mfumo wa kitaasisi wa kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya maafa, kuwa na rasilimali za kutosha na kuimarisha ushirikiano na wadau katika utekelezaji wa dhana nzima ya mzingo wa maafa kwa ajili ya kuwa na jamii yenye uchumi stahimilivu pamoja na kituo hicho cha usimamizi wa maafa kuwa cha mfano kwa ajili ya jamii yenye ustahimilivu na uchumi endelevu nchini.

Akiwa katika ziara hiyo ya kutembelea na kukagua Kituo hicho cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula, Waziri Mhagama amewataka wadau kutoka katika sekta mbalimbali wanashughulikia masuala ya majanga na maafa kuwa na mfumo wa Kanzi Data (Data Base) ili kujua namna walivyorejesha hali katika maeneo yaliyokubwa na majanga na maafa. 

Read More

Monday, December 6, 2021

Serikali kushirikiana na EAC kuendeleza Wajasiriamali Wadogo


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akieleza jambo kuhusu maonesho hayo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza.


Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba ya 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wa kuratibu vizuri maandalizi ya Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali) kwa Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bw. Ally Msaki (kulia) ambaye ni mwenyekiti wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza Desemba 5, 2021.

*******************************

Na: Mwandishi Wetu - MWANZA


Serikali kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimejipanga kuwa na sera ya kuendeleza wajasiriamali wadogo kwa lengo la kukuza haraka sekta ya biashara ndogo, kuongeza ajira, vipato vya wajasiriamali, pato la Taifa na kupunguza umaskini katika jamii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati akifungua Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki yanayofanyika Rock City Mall, Jijini Mwanza Desemba 5, 2021.

Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na nchi 5 ikiwemo Burundi, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini na Uganda zimeazimia na kujipanga kuwa na sera itakayosaidia kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati sambamba na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa shughuli zao.

“Sekta isiyo rasmi inachukua sehemu kubwa ya Uchumi na Uzalishaji katika nchi nyingi hasa nchi zinazoendelea, hivyo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatekeleza azma ya kurasimisha biashara kwa kuweka mazingira wezeshi ya Wajasiriamali kupata huduma stahiki za usajili na kufanya biashara,” alisema

“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwa kuwa nchi zote duniani ujasiriamali unachukua nafasi kubwa hali inayopelekea umuhimu wa uwepo wa sera zitakazosaidia kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati,” alisema Waziri Mkumbo

Aliongeza kuwa, Maonesho hayo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali ni kiashiria kuwa serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuwezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupata fursa ya kutangaza biashara zao na kutafuta masoko.

Sambamba na hayo, Waziri huyo alipongeza wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo kwa kuwa na bidhaa zenye ubora na ubunifu wa hali ya juu.

Katika hatua nyingine, alipongeza wajasiriamali wanawake na vijana kwa kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali).

“Biashara ndogo zinafanywa zaidi na Wanawake na Vijana jambo ambalo ni muhimu na katika maonesho haya Zaidi ya asilimia 60 ya wajasiriamali walioshiriki ni wanawake ambapo tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 90 ya mapato yatakayopatikana katika biashara zao zitasaidia familia na kutatua changamoto mbalimbali,” alieleza

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa

maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi / Jua Kali) yamechangia kwa kiasi kikubwa kudumu kwa umoja na mshikamano wa jumuiya hiyo.

“Ni vyema kuendelea kuwaunga mkono na kuwashukuru Viongozi wetu kwa kutuletea mfumo huu wa ufanyaji biashara ambao umewaunganisha wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa wamoja,” alisema Waziri Mhagama

Pia alitumia fursa hiyo kuwasihi wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo kutumia kama nyenzo ya kubadilishana ujuzi ili kupunguza tatizo la ajira kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Nimetembelea mabanda mengi katika maonesho haya na nimefurahishwa na teknolojia ya mashine zilizopo katika banda la Kenya, ninaamini kwamba tukiamua sisi watanzania kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kufundisha vijana kutengeneza mashine hizo tutawawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao,” alisema

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel alisema kuwa maonesho hayo yamekuwa ni chachu kwa wakazi wa Mwanza na wananchi kutoka maeneo ya jirani kupata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kuimarisha biashara zao.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Peter Mathuki amepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maandalizi mazuri na kwa namna ilivyoshirikisha vijana wabunifu katika maonesho hayo.

Read More

Saturday, November 20, 2021

Mafunzo ya Ufundi Stadi Suluhisho la Tatizo la Ajira Nchini – Naibu Waziri Katambi

 

Mnufaika wa mafunzo ya Uanagenzi Pili Hussein (wa pili kutoka kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kulia) alipotembelea fani ya ushonaji katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akizungumza katika mahafali ya 22 ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help yaliyofanyika Jijini Arusha, Novemba 19, 2021.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kushoto) akigawa cheti kwa mwanafunzi bora wa mafunzo ya Uanagenzi Bw. Frank Kijangwa (kulia) katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help wakati wa hafla hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo hicho cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help na baadhi ya wanafunzi waliohitimu mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali.

Na: Mwandishi Wetu - ARUSHA

Vijana wameaswa kuthamini na kutumia ipasavyo fursa ya mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu maana ni suluhisho la kuzalisha wataalamu mahiri wenye ujuzi na stadi zinazohitajika soko la ajira ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha kujiajiri, kuajirika na kuajiri wenzao.

Ameyasema hayo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi aliposhiriki katika mahafali ya 22 ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help kilichopo Mtaa wa Sakina, Arusha Novemba 19, 2021.

Naibu Waziri Katambi alieleza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inalenga kuimarisha nguvukazi iliyo katika soko la ajira kwa kuipatia ujuzi na stadi za kazi.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu imeendelea kuwatengenezea vijana mifumo maalumu ya kupata ujuzi ili waweze kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwapatia mafunzo yenye ujuzi staki unaohitajika katika soko la ajira,” alisema Naibu Waziri Katambi

Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iliingia makubaliano na Vyuo 72 ambavyo vinatoa mafunzo ya ufundi stadi na jumla ya vijana 14,440 katika mikoa yote ya Tanzania bara wamenufaika na programu hiyo kwa kulipiwa ad ana serikali asilimia 100.

“Mafanikio tunayoyaona katika utekelezaji wa programu hii yanatupa hamasa ya kuendelea kutoa fursa zaidi ya mafunzo haya ili kuwezesha nguvukazi ambayo asilimia kubwa ni vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi,” alisema

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa vijana hususan katika kuongezeka kwa fursa za ajira na uwezo wa kuajirika pamoja na baadhi yao wamepata ajira kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

“Ukienda kwenye mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji - Julius Nyerere, mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta asilimia kubwa ya vijana walioajiriwa ni wanufaika wa mafunzo haya ya uanagenzi,” alisema

Aidha, Naibu Waziri Katambi ametaka vijana wanaohitimu mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi wao kujiajiri na kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na umaskini. Sambamba na hayo amezitaka Halmashauri zote nchini kuwa na kanzi data ya vijana wanaopatiwa mafunzo ya ufundi stadi katika meneo yao ili kuwawezesha mikopo ya asilimia 4 kupitia mapato ya ndani.  

“Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alielekeza wakati wa uzinduzi wa programu hii ya awamu ya tatu kule Jijini Mbeya vijana hawa waliosomeshwa kwa ufadhili wa serikali wapatiwe mikopo hiyo ili waweze kuanzisha miradi au shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazo wawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao na kujiingizia kipato,” alisema Katambi

Pamoja na hayo alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana hao waliohitimu mafunzo hayo na aliwasihi kuwa mfano wa kuigwa katika utendaji wa kazi zao kwenye jamii zinazowazunguka kwa kuonyesha uwezo wao katika kumudu kazi.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Help to Self Help Bw. Amani Sam alitumia fursa hiyo kuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia nafasi ya kutoa mafunzo ya uanagenzi.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza mpango huu wa kuwapatia vijana ujuzi katika fani mbalimbali na jumla ya Vijana wapatao 150 wamepatia mafunzo ya uanagenzi toka mwezi juni 2021,” alisema   

Mnufaika wa Mafunzo hayo Bi. Dina Lukasi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na kutambua mchango wa vijana katika jamii kwa kuwapatia ujuzi ambao utakuwa na manufaa katika kuwawezesha kuondokana na changamoto ya ajira.

“Tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake kwa kutupatia fursa hii, hakika mafunzo tuyopata yamekuwa na faida mno kwetu,” alisema Mwanagenzi huyo.

Read More

Wednesday, November 17, 2021

Serikali kuendelea kufungua fursa kwa Wanawake - Naibu Waziri Katambi


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kushoto) akijadiliana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Wiebe de Boer (kushoto) na wanufaika wa mradi wa WAENDELEZE wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika Novemba 17, 2021 Jijini Dar es Salaam.


Na: Mwandishi Wetu – DAR ES SALAAM

SERIKALI imeazimia kuendelea kufungua fursa zaidi kwa wanawake nchini katika kufanya biashara, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya kukuza biashara na mitaji, kufungua masoko na kuwatambua vitendea kazi muhumu kwa ajili ya kufanyia biashara zao.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi wakati akizindua mradi wa WAENDELEZE unaoratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fursa kwa wanawake kujiendeleza kibiashara ili kuinua uwezo wao na kuwawezesha katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Mradi huu wa Waendeleze ni moja ya jitihada za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri na wadau wa maendeleo ambao unalenga kumuinua mwanamke anayefanya biashara aweze kufikia hatua za juu zaidi,” alisema Naibu Waziri Katambi

Aliongeza kuwa katika kufanikisha mradi huo wa WAENDELEZE, Ubalozi wa Uholanzi nchini umewezesha mafunzo kwa wafanyabiashara wanawake kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi ambapo wanawake kutoka kanda ya ziwa, kanda ya nyanda za juu kusini, kanda ya kati, kanda ya magharibi na kanda ya mashariki wamenufaika.

“Tumeshuhudia hapa wafanyabiashara wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji, usindikaji na kadhalika namna mafunzo hayo yalivyowasaidia kufungua fursa nyingi ikiwa ni pamoja na kukuza mtandao wa biashara zao na masoko,” alisema

Aidha, Naibu Waziri Katambi aliwasihi wanawake walionufaika na mafunzo hayo kutoa elimu na kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo wanayofanya biashara ili kuwapa hamasa wengine.

Sambamba na hayo alitumia fursa hiyo kuwahimiza Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kuchangamikia fursa ya mikopo ya asilimia 10 (4% Vijana, 4% Wanawake na 2% Wenye Ulemavu) kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuanzisha na kuendeleza shughuli au miradi itakayowaingizia kipato na kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Wiebe de Boer alisema kuwa serikali ya ufalme wa Uholanzi itaendelea kushirikina na Serikali katika kuboresha na kuendeleza wafanyabiasha wanawake nchini kupitia mradi huo wa WAENDELEZE.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lindam Bi. Zuhura Muro, alisema kuwa mradi huo umewawezesha wafanyabiashara wanawake kupata hamasa ya kuchangia pato la Taifa na pia kupitia shughuli zao za kiuchumi wameweza kutoa fursa za ajira kwa wengine.

Pamoja hayo, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara kutoka Benki ya NMB, Bw. Issack Masusu alieleza kuwa benki hiyo ya NMB imepunguza riba katika eneo la sekta ya kilimo na kilimo biashara ambapo riba hiyo imeshuka kutoka asilimia 18 hadi 10.

“Benki ya NMB imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 100 kwa ajili ya kuwezesha mikopo kwa wafanyabiashara ambapo kiasi cha laki 2 hadi bilioni 10 zimekuwa zikitolewa kwa mkopaji mmoja, hivyo ni vyema wanufaika wa mradi huu wakakimbilia fursa hiyo ambayo itakuwa chachu katika ukuaji wa biashara zao,” alisema Masusu

Read More

Sunday, November 14, 2021

Serikali Imepiga Hatua Kubwa katika Kudhibiti VVU na UKIMWI Nchini – Waziri Mhagama


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Mkoani Mbeya, Mosi Desemba, 2021. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko (kulia) wakati mkutano huo uliofanyika Novemba 14, 2021 katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), UNAIDS na Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOFA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya akieleza jambo wakati wa mkutano huo. Kulia ni 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama.


Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko (kulia) akieleza jambo wakati wa mkutano huo. 

Na: Mwandishi Wetu – DODOMA

Serikali imepiga hatua kubwa katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mujibu wa kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 hadi asilimia 83 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU).

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Novemba 14, Jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba 1, 2021.

Waziri Mhagama alieleza kuwa kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilima 61 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019.

“Serikali kupitia uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU na UKIMWI nchini,” alisema Waziri Mhagama

Alifafanua kuwa, matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARV) kwa WAVIU wanaojua hali zao za maambukizi yameongezeka kutoka 95% mwaka 2016 hadi 98% mwaka 2019 na Kiwango cha kufubaza VVU kwa wale wanaotumia ARV kimeongezeka kutoka 87% mwaka 2016 hadi 92% mwaka 2019.

 

Pia alieleza kuwa vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa 50% kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020.wakati takwimu za kiwango cha maambukizi katika jamii (HIV prevalence) zinaonyesha kiwango kilishuka kutoka 7% mwaka 2003/04 hadi 4.7% manamo mwaka 2016/17.  

 

Mhe Mhagama amefafanua kuwa Maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) nchini Tanzania yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020. Wakati Maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (Mother to child transmission) yameshuka kutoka 18% mwaka 2010 hadi 7% mwaka 2020.

 

Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka huu 2021 amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kitaifa Jijini Mbeya kuanzia Novemba 24 hadi Disemba 1, 2021 katika Uwanja wa Luanda Nzovwe ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

 

Aliongeza kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutoa fursa ya kutathimini hali halisi na mwelekeo wa kudhibiti Virusi va UKIMWI (VVU) na UKIMWI kitaifa na kimataia, kutafakari na kutekeleza kauli mbiu inayotolewa kila mwaka kulingana vipaumbele vya kidunia kwa muktadha wa kitaifa, pamoja na kuwakumbuka watu wote waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI.

“Katika wiki ya maadhimisho hayo kutakuwa na matembezi ya hisani kwa ajili ya kutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund – ATF) ambayo yatafanyika tarehe 24 Novemba, 2021 Mbeya. Pia kutakuwa na kongamano la kisayansi kwa ajili ya kutathmini hali na mwelekeo wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini,” alisema

Sambamba na hayo alieleza kuwa kutakuwa na Kongamano ambalo litahusisha mawasilisho ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI nchini. Pia kutakuwa na mdahalo wa vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vilivyopo Mkoani Mbeya ambapo watajadiliana masuala mbalimbali yanayo husiana na afua za VVU na UKIMWI kwa vijana, mafanikio yaliyofikiwa vyuoni katika kukabiliana na changamoto hizo. Pamoja na hayo ameongeza kuwa kutakuwa na Mdahalo wa Viongozi wa Dini na Viongozi wa Jadi (Machifu), utakaohudhuriwa na vijana na jamii kwa ujumla

 

Aidha, Waziri Mhagama ameagiza  wakuu wa Mikoa  yote nchini kusimamia utekelezaji wa shughuli za maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani katika mikoa yao kwa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU na UKIMWI walioko katika Mikoa husika.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahimiza Wakazi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani watumie fursa ya maonesha hayo kupata elimu ya afya,ushauri nasaha,upimaji wa hiari wa VVU , Upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi, Sukari, Uwiano wa Urefu na Uzito wa Mwili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko aliishukuru Serikali kwa kuendelea kupambana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Naye Mwenyekiti wa Baaza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bi Leticia Kapela aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita namna inavyoendelea kuwajali watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na mikakati iliyojiwekea katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambayo yameleta mafanikio makubwa na maambukizi kupungua.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutujali sisi watu tunaoishi na virusi vya UKIMWI na sisi Baraza tutahakikisha tunashirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI,” alisema Mwenyekiti huyo

kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka huu 2021 ni “Zingatia Usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko

MWISHO

CAPTIONS

R 1


R 2

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko (kulia) wakati mkutano huo uliofanyika Novemba 14, 2021 katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma.

R 3

Sehemu ya washiriki kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), UNAIDS na Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOFA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.

R 4

Sehemu ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma.

Read More

Saturday, November 13, 2021

Tanzania Mwenyeji wa Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba, 2021 kwenye viwanja vya Rock City MallJijini Mwanza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Jamal Katundu wakati mkutano huo uliofanyika Novemba 13, 2021 Jijini Dodoma.


Sehemu ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.


Na: Mwandishi Wetu – DODOMA

*Zaidi ya Wajasiriamali 1,000 kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Tanzania kushiriki.

*****************************

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba, 2021 kwenye viwanja vya Rock City MallJijini Mwanza.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Bunge, leo Novemba 13, 2021 Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alieleza kuwa, Maonesho hayo ya Nguvu Kazi au Jua Kali yamekuwa yakijulikana hivyo kwa sababu yanawalenga wajasiriamali wa kati na wadogo waliopo katika sekta isiyo rasmi na lengo kubwa la maonesho haya ni kuwawezesha wajasiriamali kurasimisha shughuli zao kwa kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa pamoja na kuongeza fursa za ajira za staha nchini.

 

“Tanzania imekua mwenyeji wa maonesho haya mara tano na mwaka huu 2021 itakuwa ni mara ya sita ambapo maonesho hayo yatafanyika Mkoani Mwanza,” alieleza Waziri Mhagama

 

“Kwa kutambua umuhimu wa maonesho haya tunategemea kuwa na zaidi ya Wajasiriamali 1,000 kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Tanzania ambao watashiriki katika maonesho haya ambapo Tanzania itawakilishwa na Wajasiriamali zaidi ya 450,” alisema

 

Alisema kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha haiwaachi nyuma Wajasiriamali na imekuwa ikiwawezesha kushiriki katika Maonesho mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo hayo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kwa jina la Jua Kali au Nguvukazi.

 

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanikisha maonesho haya kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali wakiwemo vijana, wanawake na wenye ulemavu wanatumia fursa hii kutafuta masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Waziri Mhagama

 

“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 kupitia Ibara ya 26 imeilekeza Serikali kuwezesha wajasiriamali na makundi yao ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine,” alisema

 

Akizungumzia historia ya Maonesho hayo alieleza kuwa, onesho la Nguvu Kazi au Jua Kali hufanyika kila mwaka katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Desemba kama sehemu ya kumbukumbu ya kuanzishwa tena Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

“Wajasiriamali wadogo na wa kati nchini ni vyema wakatumia fursa ya maonesho haya ili waweze kujifunza mbinu za kutengeneza bidhaa na kutafuta masoko kutoka kwa wenzetu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema

 

Aliongeza kuwa, Maonesho hayo hufanyika sambamaba na makongamano ya kuwajengea uwezo Wajasiriamali kuhusu masoko, ubora wa bidhaa, urasimishaji biashara na kuongeza thamami ya bidhaa. Pia, maonesho hayo yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka Sitini 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hivyo alihimiza Vijana wajasiriamali kutumia fursa hiyo kuonesha kazi zao za ubunifu katika sekta ya teknolojia ya habari, viwanda, kilimo, biashara, na huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya.

 

Waziri Mhagama alifafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - Kazi, Uchumi na Uwezeshaji - Zanzibar, Wizara, Taasisi nyingine za Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali (CISO) imeunda Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu maandalizi ya Maonesho hayo na fomu za maombi pamoja na maelekezo kwa Wajasiriamali wanaokusudia kushiriki maonesho hayo zinapatikana kupitia Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji kote nchini, Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali (CISO) na katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu www.pmo.go.tz.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kufanikisha maonesho hayo. Pia alitumia fursa hiyo kuhimiza Shirika la Viwanda vidogo (SIDO) kuendelea kusaidia na kuwaibua Wajasiriamali mahiri kushiriki maonesho hayo.

“Nitumie fursa hii kuwasihi wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho haya bila wasiwasi wowote kwa kuwa tumejipanga kuhakikisha masuala ya afya yanazingatiwa wakati wote wa maonesho hususan tahadhari dhidi ya changamoto ya UVIKO – 19,” alisema

MWISHO


Read More

Wednesday, November 10, 2021

Mawaziri Sekta Zinazotekeleza Mpango wa Lishe Wakutana Jijini Dodoma


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika Kikao cha Mawaziri wa Sekta zinazotekeleza Mpango wa Lishe kilichofanyika Novemba 10, 2021 katika Ukumbi wa mkutano katika Ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki katika Mkutano huo wakisikiliza taarifa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akihutubia mkutano huo uliofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma. 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama.

Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Sera na Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Paul Sangawe akiwasilisha Mkakati wa Serikali katika kuboresha Lishe nchini wakati wa Kikao hicho cha Mawaziri wa Sekta zinazotekeleza Mpango wa Lishe kilichofanyika Novemba 10, 2021 katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Ngome, Jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (kushoto) akipitia Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe (2020/21-2025/26) na Mkakati wa Utafutaji Rasilimali Fedha wakati wa Mkutano huo. 


*Waziri Mhagama abainisha Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe (2020/21 – 2025/26) na Mkakati wa Utafutaji Rasilimali fedha kukamilika.


Na: Mwandishi Wetu – DODOMA 

Mawaziri sekta zinazotekeleza Mpango wa lishe wamekutana leo tarehe 10 Novemba, 2021 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kujadili na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Lishe utakaofanyika Mkoani Tanga.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mkutano huo kwa kushirikiana na Wizara zinazotekeleza mpango wa lishe pamoja na wadau wa lishe (Joint Multisectoral Nutrition Review) kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe pamoja na mikakati ya Serikali katika kupunguza changamoto ya utapiamlo nchini. 

“Suala la lishe ni mtambuka linalosimamiwa kwa ujumla wet una mkitizama sekta ambazo zipo hapa zinaguswa moja kwa moja kwenye suala hili la lishe bora na kupambana na udumavu, utapiamlo na mambo mengine yanayohusu lishe,” alisema Waziri Mhagama

Alifafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu katika kufanikisha hayo imekamilisha maandalizi ya Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe (2020/21-2025/26) ambao utatoa mwongozo wa utekelezaji wa afua za lishe hapa nchini kwa miaka mitano.

Waziri Mhagama aliongeza kuwa, Mkutano huo wa mwaka utafanyika Mkoani Tanga kwa lengo la kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kuongeza jitihada katika masuala ya lishe na hivyo kurudisha mkoa huo katika nafasi iliyokuwa awali na ikiwezekana kufanya vizuri zaidi.

“Zamani mkoa wa Tanga ulikuwa unafanya vizuri kwenye masula ya lishe lakini hivi karibuni imeonekana kuwa na kiwango cha udumavu katika masuala ya lishe, hivyo mkoa huu unahitaji uhamasishaji wa hali ya juu katika masuala ya lishe ili kuwa ni moja ya Mikoa ambayo itakuwa kielelezo cha mafaniko katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe,” alisema Waziri Mhagama

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Mhagama alipongeza juhudi zilizochukuliwa katika kusimamia mapambano dhidi ya utapiamlo ambapo alieleza jitihada hizo za wazi zitawezesha kufikia malengo waliyojiwekea katika kupunguza viwango vya utapiamlo nchini.

Pia alipongeza mchango na juhudi katika kuimarisha masuala ya lishe ikiwemo sekta ya Kilimo kwa kuandaa Kilimo kwa Mpango Mkakati wa Kujumuisha Masuala ya Lishe kwenye Kilimo ambao utasaidia kuimarisha uratibu wa sekta ya kilimo katika kupambana na utapiamlo nchini. Upande wa sekta ya Afya ni kuratibu maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa ambayo hutumika kutoa uelewa wa masuala ya lishe kwa jamii. Pamoja na kuandaa Mkakati wa Kupambana na Magonjwa yasiyoambukiza ambao utazinduliwa hivi karibuni. Upande wa sekta ya Elimu ni uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi ambao una lengo la kuwawekea watekelezaji na wadau wa utoaji wa huduma hiyo ya chakula na lishe shuleni namna bora ya kutekeleza, kusimamia na kuboresha utoaji wa huduma hiyo nchini. 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Jamal Katundu alisema kuwa, Tanzania ni nchi mwanachama wa Vuguvugu la Lishe Duniani “Scaling Up Nutrition (SUN) Movement”, kama taifa lilipokea mwaliko wa kushiriki katika Mkutano huo wa Wadau wa Lishe wa Mwaka 2021 unaojulikana kama Nutrition for Growth Summit (N4G) utakaofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 7 na 8 Desemba 2021, Tokyo – Japan. 

“Katika kuhakikisha nchi yetu inashiriki kikamilifu kwenye mkutano huo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau imeratibu maandalizi ya ushiriki huo kwa kuandaa maeneo ambayo Nchi yetu itaahidi kutekeleza katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo,” alisema Naibu Katibu Mkuu Prof. Jamal

Mkutano huo wa Mawaziri Sekta zinazotekeleza Mpango wa Lishe umependekezwa kufanyika tarehe 17 hadi 18 Novemba, 2021 Mkoani Tanga na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Kassim Majaliwa (Mb). Kauli mbiu ya mkutano huo ni; “LISHE BORA NI MSINGI WA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU KATIKA UCHUMI SHINDANI”.

Read More