Saturday, November 17, 2018

VIJIJI VYOTE NCHINI KUPATIWA HUDUMA ZA MAJI SAFI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamesema Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wakiwemo wa wilaya ya Nachingwea wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao, hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 17, 2018) alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Namatula ‘A’ na kijiji cha Mtua ambao waliosimamisha msafara wa Waziri Mkuu wakati akiekea Kata ya Kilimarondo wilayani Nachingwea.

“Serikaliya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini vikiwemo vijiji vya wilaya ya Nachingwea ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo.”
Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.
Amesema mbali na huduma ya maji, pia Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini vitaunganishiwa katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu, hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Nachingwea. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Pia Waziri Mkuu ameesema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Awali, Waziri Mkuu alimkabidhi Mwenyekiti wa kijiji cha Mpiluka saruji tani mbili na nusu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule ya Msingi Mpiluka.
 (mwisho)
Read More

MAJALIWA AWASALIMIA WANANCHI WA KIJIJI CHA NYAMATULA WILAYANI NACHINGWEA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Nyamatula wilayani Nachingwea akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo, Novemba 17, 2018.  
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Nachingwea wakati  alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Nachingwea kwa ziara ya kazi wilayani humo, Novemba 17, 2018.  Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango.Read More

MAJALIWA AWASILI NACHINGWEA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Viongozi wa Mkoa wa Lindi wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea, Novemba 17, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na mkewe Mary (wapili kushoto) wakiitazama ngoma ya Nsolopa iliyotubuizwa na Kikundi cha Mshikamano wakati walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea mkoani Lindi, Novemba 17, 2018.


Read More

Friday, November 16, 2018

WAZIRI MKUU: MAONESHO YA VIWANDA, BIASHARA NA MADINI YANAPASWA KUIGWA NA MIKOA MINGINE


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maonesho ya viwanda vidogo na biashara ndogondogo pamoja na yale ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yanayofanyika nchini ni ubunifu muhimu na hauna budi kuigwa na mikoa mingine.

“Ubunifu huu wa kufanya maonesho ya viwanda ya kimkoa, kikanda na kitaifa ni jambo muhimu sana. Maonesho haya, yanatupa fursa ya kujitangaza na kutathmini hatua tuliyofikia katika utekelezaji wa ajenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kubaini changamoto zilizopo,” amesema.

Akizungumza wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge leo (Ijumaa, Novemba 16, 2018) bungeni mjini Dodoma,Waziri Mkuu amesema maonesho hayo yanahamasisha wananchi wengi zaidi washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Napenda kuielekeza mikoa mingine iige mifano hiyo ya mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita ili kuhamasisha wananchi na wadau wengine washiriki ipasavyo katika ujenzi wa viwanda na kuleta teknolojia mpya za viwanda na sekta ya madini,” amesema.

Amesema mbali ya kujifunza teknolojia mpya, maonesho hayo yanatoa fursa kwa wadau husika kukutana na kubadilishana utaalam na uzoefu mbalimbali.

“Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita kwa ubunifu wao huo. Vilevile, niwapongeze sana wazalishaji wenye viwanda na madini pamoja na wadau wote walioshiriki kuonesha teknolojia mbalimbali na bidhaa mpya za kilimo na madini katika maonesho hayo.”

Amesema kupitia maonesho hayo, wachimbaji hao wadogo, pia waliweza kukutana na wataalamu wanaosimamia sekta ya madini na mabenki kwa lengo la kujifunza matumizi ya teknolojia mpya sambamba na kufahamu taratibu mbalimbali za kupata mikopo ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji madini.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani na kukuza uchumi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji na kwamba hatua stahiki hazina budi kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo isiendelee.

Akitoa mfano Waziri Mkuu amesema: “Miradi mingi ya maji nchini imekwama au kutoleta tija kutokana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Hivyo, niwasihi Wabunge wenzangu muwahamasishe wananchi na wadau kutoa maoni yatakayosaidia kujenga na kuboresha vema sheria zinazokusudiwa kulinda mazingira yetu pamoja na vyanzo vya maji.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amebainisha faraja aliyoipata wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani Lushoto na kukuta mazingira yametunzwa vizuri na uoto wa asili umehifadhiwa, na akaagiza Halmashauri nyingine ziige mfano huo wa utunzaji mazingira.

“Katika ziara yangu ya hivi karibuni wilayani Lushoto, nilifarijika mno kuona jitihada kubwa zinazofanywa na wananchi wa wilaya hiyo katika kuhifadhi mazingira. Nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi wa Halmashauri za Wilaya ya Lushoto na Bumbuli kwa utunzaji mzuri wa mazingira. Naziagiza Halmashauri nyingine nchini ziige mfano huo mzuri wa kuhifadhi mazingira,” amesema.

Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, mwakani.

(mwisho)
Read More

SERIKALI YATOA SH. BILIONI 83 KUIMARISHA ELIMU

*Ni kuanzia Julai hadi Oktoba mwaka huu, kwa msingi na sekondari
*Waziri Mkuu aonya wanaoshiriki wizi wa mitihani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai na Oktoba, mwaka huu, Serikali imetoa jumla ya sh. bilioni 83.2 ili kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini.

Waziri Mkuu amesema, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa kwenye shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 zilienda kwenye shule za sekondari ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila malipo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 16, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, 2019.

“Katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini, Serikali inapeleka fedha za elimumsingi bila malipo moja kwa moja shuleni. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai hadi Oktoba, 2018 shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa katika shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 kwenye shule za sekondari,” amesema.

Amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimumsingi bila malipo, uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza umeimarika na kwamba kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu kwenye mitihani ya kumaliza darasa la saba.

“Kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu katika mitihani ya kumaliza darasa la saba, ambapo mwaka 2016 ilikuwa wastani wa asilimia 70 na mwaka 2018 ilikuwa ni wastani wa asilimia 78. Hali hiyo, imeongeza mahitaji mbalimbali, ikiwemo miundombinu katika shule zetu za msingi na sekondari,” amesema.

Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu inaendelea na mikakati ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu muhimu ya shule.

“Kwa mfano, kupitia programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R), shilingi bilioni 53.4 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.  Aidha, shilingi bilioni 9.2 zimeelekezwa katika uimarishaji wa miundombinu ya elimu kupitia programu ya kuboresha elimu ya shule za msingi (EQUIP-T),” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri katika mfumo mzima wa elimu nchini kwa kushirikiana na wadau wote.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya taifa hazina budi kuhakikisha zinasimamia kikamilifu mitihani hiyo ili kuepuka udanganyifu.

“Natambua kuwa mitihani ya taifa kwa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne inaendelea. Hata hivyo, katika kipindi cha hivi karibuni kumezuka matukio ya kuvuja kwa mitihani.”

“Naziagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya taifa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mitihani hiyo ili kuepuka udanganyifu. Itakapobainika kuwepo kwa udanganyifu wa mitihani, hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayehusika,” amesisitiza.

(mwisho)
Read More

MAJALIWA: SERIKALI IMETUNGA SHERIA KUONGEZA UDHIBITI SEKTA NDOGO YA FEDHA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 ili kuongeza udhibiti wa sekta ndogo ya fedha.

“Kwa muda mrefu sekta ndogo ya fedha haikuwa na udhibiti wa kutosha. Hali hiyo ilisababisha kuwepo na uendeshaji usio rasmi wa shughuli mbalimbali za kifedha kama vile, taasisi zinazochukua amana, vikundi vya fedha vya jamii na wakopeshaji binafsi,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 16, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, mwakani.

Amesema shughuli hizo ambazo nyingi ziliendeshwa katika utaratibu usio rasmi, ziliwaletea wananchi athari mbalimbali ikiwemo kupoteza mali zao zilizowekwa kama dhamana kwenye taasisi hizo.

Amesema baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya wa kutokuwepo udhibiti wa kutosha kwenye sekta hiyo ndogo ya fedha kuendesha vitendo mbalimbali vya kihalifu ikiwemo utakatishaji fedha.

“Kutokana na sababu hizo, Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 kwa lengo la kuongeza udhibiti wa sekta hiyo ndogo ya fedha na kuiwezesha kuchangia ipasavyo katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kulinda mali na fedha za wananchi wetu,” amesema.

Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018) ambao umesomwa kwa hatua zake zote na kupitishwa na Bunge, ukisubiri kibali cha Mheshimiwa Rais ili uwe sheria kamili.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hali ya usalama barabarani bado ina changamoto nyingi licha ya takwimu kuonesha kupungua kwa matukio na vifo vinavyosababishwa na ajali hizo.
Akitoa mfano kuhusu matukio ya ajali nchini, Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016 matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 9,856 ikilinganishwa na matukio 5,578 katika mwaka 2017 ambayo ni pungufu kwa matukio 4,278 sawa na asilimia 43.

Akifafanua zaidi, amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2018, matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 3,209 ikilinganishwa na matukio 5,578 katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana.

Amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matukio ya usalama barabarani ikiwemo kuendesha operesheni za kuhakikisha sheria zote za usalama barabarani zinafuatwa kikamilifu.

(mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU AKUTANA NA MAKAMU MWENYEKITI WA BUNGE LA CHINA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma Novemba 16, 2018. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma Novemba 16, 2018. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma Novemba 16, 2018. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mahagama, akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma Novemba 16, 2018.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma Novemba 16, 2018.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa katika picha ya pamoja  na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng na ujumbe aliombatana nao,  Ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma Novemba 16, 2018.

Read More