Saturday, June 29, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MKAZO WA KUONDOA VIJANA KWENYE URAIBU WA DAWA ZA KULEVYA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inaendelea kuweka nguvu katika kuondoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya kwa kuhakikisha inawapa tiba vijana hao ili warudi katika hali zao za kawaida.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipotembelea Mabanda ya Taasisi mbalimbali kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Dunia 2024 zinazofanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana.

"Tumeshuhudia vijana wengi waliotoka kwenye uraibu wa dawa za kulevya wamerudi kuwa rai wazuri wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na wameamua kujitokea kuokoa vijana wenzao," alisema Waziri Mhagama

Waziri Mhagama alifafanua kwamba, serikali imeshajenga kituo Jijini Dodoma cha urekebishaji ambacho kitakuwa kinatoa tiba ya kutoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya na kufundisha mafunzo ya ujuzi.

Aidha Serikali inaendelea kutekeleza kwa nguvu kubwa kwenye matamko ya kisera ili kuweza kuhakikisha inaokoa vijana kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

"pia tunaamini Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine tukifanya kwa pamoja tunaweza kupata mafanikio makubwa sana," alisema

Waziri Mhagama alisema  tafiti zilizofanyika mtumiaji akitumia dawa za kulevya anatumia masaa sita kwa kilevi ambacho kinamsababishia kulala na kutojitambua masaa sita, jambo ambalo linamnyima uwezo wa kufanya kazi, anapopata fahamu anakuwa dhaifu na hawezi ufanya kazi yoyote na anapokosa fedha ya kununua madawa inamsababisha kuingia kwenye matendo ya jinai.

Awali katika zoezi hilo Waziri Mhagama aliambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi.

 

 



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.