Monday, June 8, 2026

DKT. YONAZI AONGOZA KIKAO CHA MAKATIBU MAKUU CHA MAANDALIZI YA AFCON 2027


 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Dkt.Jim Yonazi ameongoza Kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) kwa ajili ya kupitia hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maandalizi ya michuano hiyo mikubwa itakayofanyika mwaka 2027 katika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya.

Dkt. Yonazi ameongoza kikao hicho leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wajumbe wa kikao hicho kuendelea kufanya maandalizi kwa weledi huku wakishirikisha sekta zote muhimu katika kufanikisha michuano hiyo na kufikia malengo yanayotarajiwa ili kuipa nchi heshima inayostahili.

“Kila sekta iendelee kutekeleza jukumu lake kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya, “ alisema Dkt. Yonazi

Aidha, Dkt. Yonazi amewashukuru wajumbe wote na kusema kuwa Ofisi yake itaendelea kuratibu shughuli hizo kwa ushirikiano wa pamoja.

Read More

SERA ZA KISEKTA ZATAKIWA KUENDANA NA DIRA 2050


Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imewakumbusha wataalamu wa uchambuzi wa sera nchini kuimarisha jitihada za kuhakikisha sera zote zinaendana na Dira 2050 ili kuwezesha utekelezaji wenye tija na kuleta matokeo tarajiwa kwa wananchi.

Wito huo umetolewa leo Jijini Arusha na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Bw. Paul Sangawe, alipokuwa akifungua kikao kazi maalum cha kuwajengea uwezo wataalamu wa uchambuzi wa sera kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Bw. Sangawe amesema kuwa, sera zina mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa, hivyo ni muhimu kuendana na Dira 2050.

“Ni muhimu sera zetu ziendane na Dira 2050 ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa hai na matokeo yanayokusudiwa yanaonekana kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Sangawe.

Aidha, ameipongea Taasisi ya Uongozi kwa mchango wanaotoa katika kuratibu sera na kujenga uwezo wa wataalam wa uchambuzi wa sera. 

Katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo Dira 2050, hatua iliyofikiwa katika mapitio ya sera, nafasi ya sheria katika utekelezaji wa sera na uzoefu kutoka nchi nyingine.

Washiriki wa kikao hicho kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo na kueleza umuhimu wa mafunzo hayo kuwa endelevu. Aidha, akitoa ufafanuzi Mkurugenzi alieleza kuwa, mafunzo hayo yatakuwa endelevu. 

Vilevile, amewahakikishia wajumbe hao kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo Tume ya Mipango katika kuhakikisha uratibu wa sera unaimarishwa nchini.

 





Read More

OWM, DIT YAINGIA MAKUBALIANO KUIMARISHA USIMAMIZI WA MAAFA NCHINI

 


SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeingia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa maafa nchini kwa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu.

Akizungumza mapema hii leo (08 Juni, 2026) katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga mifumo madhubuti ya kiutendaji inayoongozwa na maarifa, sayansi na teknolojia ikiwemo matumizi ya Akili Unde (AI) katika kukabiliana na maafa.

Amesema makubaliano hayo yanatekeleza pia mapendekezo ya Mkutano wa Nane wa Umoja wa Mataifa wa Jukwaa la Dunia la Upunguzaji wa Vihatarishi vya Maafa uliofanyika Geneva, Uswisi, mwezi Juni 2025, na yanaashiria mabadiliko ya kimkakati katika namna Serikali inavyoshughulikia changamoto za maafa kutoka mfumo wa kusubiri majanga hadi mfumo wa kujikita katika kinga, maandalizi na tahadhari.

“Vyuo vikuu na taasisi za utafiti, ikiwemo Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, zina jukumu muhimu la kuzalisha maarifa na suluhisho za kisayansi zitakazosaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini,”amesema.

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa makubaliano hayo, Serikali itaandaa Mpango Kazi wa utekelezaji pamoja na Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Usimamizi wa Maafa itakayobainisha maeneo ya kipaumbele yanayohitaji ufumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia.

Dkt. Yonazi amesisitiza kuwa mafanikio ya makubaliano hayo yatapimwa kwa matokeo halisi yatakayochangia kuongeza usalama wa wananchi, kulinda rasilimali za taifa na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya maafa.

Ushirikiano huo unaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoweka msisitizo katika matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Prof.Preksedis Marco Ndomba amesema kuwa taasisi imeandika historia kwa kusaini hati ya ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo ameeleza kuwa mchakato huu ulianza muda mrefu na matunda yake yameanza kuonekana jambo ambalo ni mafanikio makubwa.

“Tunaahidi juu ya kufanikisha  makubaliano hayo kwa kuwa, uwezo huo tunao, utalaam upo wa kutosha kwa kushirikiana kwenye masuala ya viatarishi kitaifa ili kufanikisha adhima hii ya Serikali,” Alisema Profesa Ndomba.

 

Read More

Friday, June 5, 2026

SERIKALI YAZINDUA KITUO CHA OPERESHENI NA MAWASILIANO YA DHARURA MWANZA


SERIKALI imezindua rasmi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura cha Mkoa wa Mwanza, hatua inayolenga kuimarisha uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa na majanga katika mkoa huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo , Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Said Mtanda, amesema kituo hicho ni nyenzo muhimu katika kufuatilia na kudhibiti matukio ya dharura kwa ufanisi zaidi.

Amesema kupitia kituo hicho, mkoa unaweza kufuatilia matukio ya dharura kwa karibu, kukusanya na kuchambua taarifa kwa wakati pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa.

“Kupitia kituo hiki, taarifa muhimu zinafika kwa mamlaka husika kwa haraka ili kuwezesha maamuzi stahiki kufanyika kwa wakati,” anasema Mhe.Mtanda.

Ameongeza kuwa kituo hicho kinaunganishwa moja kwa moja na Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, hatua inayorahisisha mtiririko wa taarifa na kuimarisha uratibu wa shughuli za kukabiliana na maafa kati ya ngazi ya mkoa na taifa.

Kwa mujibu wa Mhe. Mtanda, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kujenga mfumo jumuishi wa usimamizi wa maafa wenye uwezo wa kutoa mwitikio wa haraka na wenye ufanisi katika kukabiliana na majanga.

Aidha, amewataka watumishi na viongozi kutumia mafunzo wanayopata kujenga uelewa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano wa kiutendaji ili kuboresha zaidi usimamizi wa maafa katika Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, amesema kituo hicho kina umuhimu mkubwa kwa mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla.

Amesema kituo hicho kinakuwa kitovu cha ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa za matukio ya dharura na maafa, ambapo kinaunganishwa moja kwa moja na Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kufanya maamuzi ya haraka na sahihi.

“Kupitia kituo hiki, Serikali inaweza kufuatilia vihatarishi mbalimbali, kutoa tahadhari za mapema, kuratibu rasilimali za kukabiliana na maafa na kuimarisha mawasiliano kati ya wadau wote wanaohusika na usimamizi wa maafa,”alisema.

Ameongeza kuwa, “Huu ni uwekezaji muhimu katika kuimarisha utayari wa mkoa na taifa kwa ujumla. Sambamba na hilo, timu ya mkoa ya kukabiliana na dharura tunayoizindua leo ndiyo nguzo kuu ya kukabiliana na matukio ya maafa kwa wakati.”

Vilevile amesema uzinduzi wa kituo hicho unakuja katika wakati muafaka ambapo serikali inaendelea kujiandaa na kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema kufuatia taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu uwezekano wa kutokea kwa hali mbaya ya hewa, ikiwemo athari zinazoweza kusababishwa na El NiƱo.

Read More

Thursday, June 4, 2026

TIMU KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU YAFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU TAWALA MWANZA KUHUSU MASUALA YA USIMAMIZI WA MAAFA


 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Mwanza Bw. Henry Mwaijega amekutana na kufanya mazungumzo timu ya Idara ya Usimamizi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu walipomtembelea ofisini kwake leo Jijini Mwanza.

Timu hiyo ipo mkoani Mwanza kwa lengo la kuongoza mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa mkoa pamoja na wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utayari, uratibu na uwezo wa kukabiliana na majanga katika ngazi ya mkoa.

Pamoja na mafunzo hayo, wanatarajia kuzindua Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura cha mkoa wa Mwanza tarehe 05 juni, 2026.

Read More