Thursday, June 25, 2026

SERIKALI YAZITAKA TAASISI ZOTE KUJIANDAA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO


SERIKALI imesema itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini ili kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga mbalimbali ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu, kuharibu mali na kurudisha nyuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa hii leo na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, wakati akifunga Jukwaa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa lililojadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Niño Jijini Dodoma.

Amesema Tanzania imeendelea kukabiliwa na matukio ya maafa yanayosababisha athari kubwa kwa wananchi na uchumi wa Taifa, hali inayolazimu kuwepo kwa maandalizi madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo kabla hazijatokea.

“Nchi yetu imekuwa ikishuhudia matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii. Majanga hayo yamesababisha vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu,” amesema Dkt. Kilabuko.

Amesema kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ya Aprili 28, 2026 kuhusu uwezekano wa kujitokeza kwa hali ya El Niño, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura kwa ajili ya kuzuia na kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea kuanzia Agosti 2026 hadi Juni 2027.

Kwa mujibu wa Dkt. Kilabuko, rasimu hiyo imejadiliwa na wadau mbalimbali ili kuiboresha kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana wakati wa matukio ya El Niño yaliyowahi kutokea nchini, hususan ya mwaka 2023/2024.

Amesema ushirikishwaji wa wadau ni hatua muhimu itakayoiwezesha Serikali kuwa na mpango shirikishi na unaotekelezeka katika kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali endapo maafa yatatokea.

“Ni vema kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yetu huku tukijielekeza kwenye athari tarajiwa na hatua za kuchukua ili kuwa na mpango thabiti utakaoiwezesha Serikali na wadau kuchukua hatua stahiki za kuzuia au kupunguza madhara,” amesema.

  


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.