Friday, August 30, 2019

SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA UNHCR-MAJALIWA


SERIKALI ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika kutatua changamoto zinazotokana na uwepo wa wakimbizi nchini pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu kwenye nchi zao ili wakimbizi hao waweze kurejea makwao kuendelea na shughuli za maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Agosti 30, 2019) katika mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Bw. Filippo Grandikwenye Kituo cha Maonyesho cha Yokohama nchini Japan baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7).

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa UNHCR kuisaidia mikoa inayokaliwa na wakambizi kutokana na kuharibiwa kwa mazingira. “Hata hivyo Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na UNHCR kuimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na utulivu.”

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Bw. Filippo Grandi amesema amefurahishwa na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kupokea wakimbizi na usikivu wa Rais Dkt. John Magufuli katika kushughulikia changamoto za wakimbizi.  

Waziri Mkuu yupo nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye Mkutano wa Kilele wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7) ambao umehitimishwa leo.

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi  na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


 (mwisho)
Read More

Wednesday, August 28, 2019

WAZIRI MKUU AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA MAURITIUS


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Mauritius waje washirikiane na Watanzania katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya utalii, viwanda vya sukari, nguo na bidhaa za uvuvi. 

Ametoa kauli hiyo leo, (Jumatano, Agosti 28, 2019) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar katika Ukumbi wa Monyesho wa Pasfico Yokohama nchini Japan.

Waziri Mkuu amesema nchi ya Mauritius ina uwezo mkubwa sana katika uzalishaji wa sukari na wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Watanzania katika kilimo cha miwa na ujenzi wa viwanda vya sukari na Tanzania ina ardhi nzuri na kubwa inayofaa kwa kilimo hicho pamoja na soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Amesema uwekezaji katika sekta ya sukari utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli za kuhakikisha inamaliza tatizo la upungufu wa sukari nchini.

Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, Waziri Mkuu amesema Mauritius imefanya vizuri sana katika utalii na hasa ule wa kutumia fukwe za bahari. “Kwa vile Tanzania inazo fukwe za bahari na maziwa naamini ushirkiano katika eneo hilo utatuletea tija.”

Kuhusu usafiri wa anga, Waziri Mkuu amesema kuwa wakati  umefika sasa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza safari za kwenda Mauritius ili kuvutia watalii wengi wanaokwenda Mauritius   kufanya utalii wa fukweni waje  pia nchini.

Kuhusu viwanda vya nguo, Waziri Mkuu amewahamasisha wafanyabiashara wa Mauritius kuwekeza nchini hasa katika viwanda vya nyuzi za pamba na nguo kwani Tanzania hivi sasa inazalisha pamba nyingi na yenye ubora wa juu. 

“Watanzania wengi wameishia kuwekeza kwenye viwanda vya kuchambua pamba hivyo wanalazimika kuuza pamba yao nje ya nchi na wenzetu Mauritius wameenda mbali zaidi kwani wana viwanda vya nguo na viwanda vya nyuzi. Kwa sasa Serikali ya Tanzania imeweka mkakati wa kujenda viwanda vya nguo ili kuongeza tija.”

Amesema kwa sasa wamekuabaliana na Waziri wa Mkuu huyo wa Mauritius kuwakutanisha Mawaziri wa viwanda na Biashara wa Mauritius na Tanzania wakae pamoja kwa ajili ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kuwashawishi wafanyabiashara wa Mauritius waje wawekeze katika viwanda vya nguo na nyuzi nchini.

Kadhalika,Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu sekta ya Uvuvi, ambapo amesema Tanzania ina eneo kubwa la bahari na maziwa linalofaa kwa uvuvi wa kibiahara na lina samaki wengi lakini wanavuliwa kwa kiwango kidogo sana kutokana na uwekezaji duni katika sekta hiyo.

Amesema ingawa Serikali ya Awamu ya Tano inaandaa mazingira ya kufufa kampuni za uvuvi nchini, bado nafasi ipo kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi hasa nchini Mauritius kuja Tanzania kuwekeza kwenye uvuvi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo na Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya uwekezaji nchini  ili kupata taarifa za kutosha zitakazomwezesha kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi yake waje wawekeze nchini.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi na viongozi kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

(mwisho)
Read More

MAJALIWA AMWAKILISHA MAGUFULI KATIKA MKUTANO WA TICAD 7

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwa katika picha ya pamoja na viongozi waku wa Nchi za Afrika na Japan katika ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development (TCAD 7) uliofanyika kwenye Ukumbi wa hoteli ya Pacifico Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais waTogo,  Faure Gnassingbe (kulia)  wakipiga makofi katika ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development (TCAD7) uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe kwenye Ukumbi wa hoteli ya Pacifico  Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi  Wakuu wa Nchi za Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa  Saba wa  Tokyo International Conference on Africa Development (TCAD7) uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe kwenye Ukumbi wa hoteli ya Pacifico  Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi (kushoto) wakisikiliza hotuba ya  ufunguzi wa  Mkutano wa  Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development (TCAD7) uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe kwenye Ukumbi wa hoteli ya Pacifico  Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019.


Read More

MAJALIWA AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA MAURITIUS, PRAVIND KUMAR

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar kabla ya mazungumzo yao  kwenye  Ukumbi wa Maonyesho wa Pacifico Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019. Wote wawili wako Japan kuhudhuria Mkutano wa  Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development -TICAD 7.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar kwenye ukumbi wa Maonyesho wa Pacifico Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019. Wate wawili wanahudhuria Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa – TICAD 7.  Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar kwenye ukumbi wa Maonyesho wa Pacifico Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019. Wate wawili wanahudhuria Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa – TICAD 7.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Japan,   Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) wakati alipotembelea banda la maonyesho la Tanzania kwenye Ukumbi wa Maonyesho wa Pacifico Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na maofisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Japan,   Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania  (TTB) wakati alipotembelea  banda la maonyesho la Tanzania kwenye Ukumbi wa Maonyesho wa Pacifico Yokohama nchini Japan, Agosti 28, 2019.


Read More

Tuesday, August 27, 2019

WAZIRI MKUU AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA TOSHIBA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Toshiba nchini Japani, ambapo amewashawishi waje nchini na wafungue ofisi kubwa na waanzishe viwanda vya bidhaa za elektroniki watakavyoona vinafaa hapa nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Agosti 27, 2019) baada ya kutembelea Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya Toshiba na kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na Kampuni hiyo.

Akizungumza na viongozi wa kampuni ya Toshiba, Waziri Mkuu amewashawishi waje nchini na wafungue viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki kama vile redio, televisheni, pasi na viwanda vingine watakavyoona wao vinafaa kujengwa nchini.

Waziri Mkuu amewahakikisha viongozi hao kwamba hawatojuta kuwekeza nchini Tanzania kutokana na sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara pamoja na soko la uhakika wa bidhaa zitakazozalishwa kwa kuwa Tanzania imezungukwa na nchi nyingi.

“Wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza Tanzania wakiwemo na wa kutoka Japan pamoja na kampuni ya Toshiba, watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha mazingira ya uwekezaji na kuyafanya yawe rafiki, nina uhakika wawekezaji watakaoamua kuwekeza Tanzania hawatajutia uamuzi wao huo”.

Waziri Mkuu amesema ujio wa kampuni kubwa kutoka nchini Japan utawapa Watanzania fursa ya kujifunza tekinolojia mpya na namna bora ya uendeshaji wa biahsara unaozingatia viwango vya  Kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sayansi ya Toshiba, Takano Lwakiri amemwambia Waziri Mkuu kuwa Kampuni yake iko tayari kupanua ofisi yake ya Tanzania na kufungua biashara, ambapo ameomba yafanyike mazungumzo yatakayotoa dira sahihi ya kufanikisha jambo hilo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development (TICAD 7) utakaoanza kesho Yokohama, nchini Japan, amesema anaamini kuwa utakuwa na mafanikio makubwa kutokana na ajenda zilizoandaliwa.

Waziri Mkuu amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kuhusu namna ya kuunganisha kibiashara shughuli za Serikali na sekta binafsi.

Amesema kwa kutumia mkutano huo wa TICAD 7 wafanyabiashara wa Tanzania wanayo fursa ya kunufaika kwa kuunganisha nguvu zao na makampuni makubwa ya nchini Japan kama Toshiba ili kupata uzoefu na teknolojia muafaka. 

Hivyo, Waziri Mkuu amewasihi wafanyabiashara kutoka Tanzania ambao watashiriki mkutano huo wafanye mazungumzo na wenzao wa Japan, wawashawishi ili waweze kushirikiana nao kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.

Waziri Mkuu yuko nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye mkutano wa TICAD 7 utakaoanza kesho, ambapo ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi na viongozi wengene wa Serikali na Taasisi za Umma.


(mwisho)
Read More

MAJALIWA ATEMBELEA KIWANDA CHA KUTENGENEZA MITAMBO YA UMEME CHA TOSHIBA NA MAKUMBUSHO YA SAYANSI YA KAMPUNI HIYO NCHINI JAPAN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Bibi Ririko Tanabe kuhusu historia ya kampuni ya Toshiba ya Japan wakati alipotembelea makumbusho ya Sayansi ya kampuni hiyo, Agosti 27, 2019 .
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akipata maelezo kutoka kwa  Bibi Ririko Tanabe   kuhusu redio ya kwanza  ilitengenezwa na kampuni ya Toshiba kwenye miaka ya 1930, wakati alipotembelea Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya Toshiba nchini Japan, Agosti 27, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa  Bibi Ririko Tanabe   kuhusu redio ya kwanza ya kucheza santuri iliyotengenezwa na kampuni ya Toshiba kwenye miaka ya 1930, wakati alipotembelea Makumbusho ya Sayansi ya kampuni ya Toshiba nchini Japan, Agosti 27, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya kampuni ya Toshiba nchini Japan baada ya kutembelea makumbusho hiyo, Agosti 27, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa kiwanda cha kutengeneza mitambo ya  kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na kampuni ya Toshiba nchini Japan wakati alipotembelea kiwanda hicho, Agosti 27, 2019. Kushoto ni Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Japan, John Kambona.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wafanyakazi wa Kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na kampuni ya Toshiba nchini Japan baada ya kutembelea kiwanda hicho, Agosti 27, 2019.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama chombo muhimu kinaunda  mitambo ya kuzalisha umeme wa maji na gesi (turbine) wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na Kampuni ya  Toshiba nchini Japan, Agosti 27, 2019. Wapili kulia ni Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Shinya Fujitsuka.


Read More

SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA WATENDAJI KATA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya Watendaji Kata na askari nchini ambao wamekuwa wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu waliowapa ujauzito wanafunzi na amesema watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ameyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilula Sokoni, kata ya Nyalumbu wilayani Kilolo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.
“Wanafunzi bado wanaendelea kupewa ujauzito na kukatishwa masomo yao huku watu waliohusika na vitendo hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu baadhi ya watendaji na askari wamezikalia kesi zao na kushindwa kuwafikisha polisi.”
“Watoto wa kike lazima walindwe ili wamalize masomo yao waje kulitumikia Taifa lao. Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi.”

Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na adhabu iliyowekwa na Serikali ni kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayemuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi hususan waishio vijijini wasikubali kurubuniwa na kugawa ardhi yao kwa watu mbalimbali wanaofika kwenye maeneo yao na kutaka wauziwe ardhi bila ya kuzihusisha mamlaka husika.

“Eneo lenu hili la Ilula ni zuri hivyo msikubali kurubuniwa kuuza ardhi yenu kwa sababau inathamani kubwa. Viongozi wa Kata na Vijiji hakikisheni mnaratibu vizuri na muandae mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro.”

Waziri Mkuu alisema wananchi hao wanatakiwa wawe makini na ardhi na mamlaka zinazohusika na ardhi lazima zihusishwe katika ugawaji wa ardhi kwa sababu wakigawa hovyo watasababisha vijana wao hapo baadaye wakose maeneo ya kilimo.

Akizungumzia kuhusu uboreshwaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu ameahidi ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Ilula ili kuwapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma hizo.

Alisema kituo kitakachojengwa kitakuwa na chumba cha kujifungulia, chumba cha maabara kwa ajili ya vipimo mbalimbali, huduma za mama na mtoto, mapasuaji, wodi ya wanaume na wanawake, aliwataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Waziri Mkuu alisema suala la kuboresha na kusogeza huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi zikiwemo za afya limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye anataka kuona wananchi wakiwa na afya nzuri ili waweze kushiriki ipasavyo katika shughuli zao za kimaendeleo.

Kabla ya kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa mradi wa maji Ilula na kuweka jiwe la msingi. Pia, Waziri Mkuu alikagua shughuli za ukarabati wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi  Ilula.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege aliwahimiza wananchi hao wajiunge katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu ya bure wao na familia zao.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi alisema kuwa awali eneo la Ilula lilikuwa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo yam ogogoro ya ardhi ambayo kwa kushirikiana na watendaji wenzake walifanikiwa kuitatua.


 (mwisho)
Read More

Monday, August 26, 2019

WAZIRI MHAGAMA AFUNGUA WARSHA YA WADAU KUJADILI FURSA ZA BOMBA LA MAFUTA –DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu Mhe.Jenista Mhagama akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge mara baada ya kufungua warsha ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati (Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akisalimiana na mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Bi. Mariagorete Charles mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo Agosti 26, 2019.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati (Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani Dodoma iliyofanyika tarehe 26 Agosti, 2019.

Read More

WAZIRI MKUU ,KASSIM MAJALIWA AWASILI NCHINI JAPAN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi wakati alipowasili kwenye hoteli ya Yokohama  Bay  nchini Japan Agosti 26, 2019, ambako anatarajiwa  kushiriki kwenye mkutano wa  TICAD 7 na kufanya ziara ya kikazi nchini humo. Kulia ni Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Japan, John Kambona.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi wakati alipowasili kwenye hoteli ya Yokohama  Bay  nchini Japan Agosti 26, 2019, ambako anatarajiwa  kushiriki kwenye mkutano wa  TICAD 7 na kufanya ziara ya kikazi nchini humo. Kulia ni Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Japan, John Kambona.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya maofisa wa serikali ya Tanzania wakati alipowasili  kwenye hoteli ya Yokohama  Bay  nchini Japan Agosti 26, 2019, amabako anatarajiwa  kushiriki kwenye mkutano wa  TICAD 7 na kufanya ziara ya kikazi nchini humo.


Read More

Sunday, August 25, 2019

MAFUNZO YA UJASIRIMALI NA USIMAMIZI WA BIASHARA KUWANUFAISHA VIJANA MKOANI GEITA


Na; Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imedhamiria kuwawezesha vijana kupitia programu ya mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamaizi wa Biashara kwa lengo la kuwawezesha kukuza na kurasimisha biashara zao.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa programu ya mafunzo hayo katika Mkoa wa Geita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa mafunzo hayo ni mahususi kwa vijana na yatawawezesha vijana kupata elimu juu ya masuala mbalimbali ya ujasiriamali na biashara ikiwemo urasimishaji wa biashara, kutambua ushindani, upatikanaji wa mitaji,  masuala ya uchambuzi wa masoko, mikakati na uendeshaji wa biashara.
“Mafunzo haya yanamanufaa sana kwenu ninyi vijana kwa kuwa yatawawezesha kukua kwa kasi katika biashara zenu mnazoziendesha na hivyo kuwajengea wigo mpana wa kuendeleza shughuli za kiuchumi mnazozifanya,” alisema Mhagama
Alifafanua kuwa Ujasirimali ni moja ya nguzo za sera ya taifa ya uwezeshaji ambayo inalenga kuinua viwango vya ujuzi na uzoefu wa masuala ya biashara nchini.
Alieleza kuwa, kupitia programu hiyo vijana 4,000 watanufaika na Mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo vijana nchini kuwa na uelewa juu ya masuala ya biashara ikionesha utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli katika kuwawezesha vijana.
“Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuwajengea uwezo vijana kote nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kujiajiri, kuajiri wenzao kwa ujumla pamoja,” alisisitiza Mhagama
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali katika kuwawezesha vijana inatekelezwa kwa vitendo kupitia programu mbalimbali ikiwemo ya ukuzaji ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, mmoja wapo ikiwemo ya Mafunzo ya Ujasirimali kwa vijana.
Sambamba na hayo, Mhe. Mhagama aliwasihi vijana walioshiriki mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kuwa ni chachu ya mageuzi katika kuboresha biashara zao. Pia aliwataka vijana hao kueneza ujuzi waliopata kupitia mafunzo hayo kwa vijana wenzao.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa maagizo kwa viongozi wa Mkoa huo kuhakikisha vijana wanashiriki kwa wingi katoka mafunzo hayo kwa kuwa yataleta matokeo chanya kwa jamii na yatakuwa ni chachu kwa vijana katika kujiletea maendeleo sambamba na kuwawezesha kuchangia pato la Taifa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Hamim Gwiyama ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa vijana maana wao ndio nguvu kazi ya taifa, hivyo kijana akiwa na ujuzi wa mambo mbalimbali ya biashara ni faida kwake kutambua njia bora za kukuza shughuli zao za uzalishaji mali.
“Katika Mkoa wa Geita vijana walikuwa na mawazo kuwa dhahabu ndio biashara pekee itakayowapa faida, ila kupitia mafunzo haya wataweza kutambua kuwa biashara yoyote wakisimamia vizuri itakuwa na manufaa kwao,” alisema Gwiyama
Naye, Mmoja wa Vijana walioshiriki katika Mafunzo hayo Bw. Salim Hassan aliweza kutoa shukrani zake kwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yameweza kuwatoa katika sehemu moja na kuwapeleka hatua nyingine.
“Leo tumepata stadi za msingi katika masuala ya ujasirimali na biashara, tumeweza kuelewa umuhimu wa kutunza kumbukumbu, usimamizi wa fedha, taratibu za kurasimisha biashara na jinsi ya kutafuta masoko,” alisema Hassan
AWALI
Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, Jijini Dodoma Julai 29, 2019. Mafunzo hayo yanasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) katika Mikoa nane (8) ya Tanzania Bara ikiwemo Dodoma, Ruvuma, Geita, Mwanza, Lindi, Mbeya, Arusha na Tanga. Tayari vijana kutoka Mkoa wa Dodoma na Ruvuma wamekishwa nufaika na mafunzo hayo.
Read More

MAJALIWA AENDA JAPAN KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Agosti 25, 2019 ameondoka nchini kwenda Japan kwa ziara ya kikazi ya siku saba. Pichani, Mhe. Majaliwa akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako (kushoto)  na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.  Avemaria Semakafu (wapili kushoto) kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  kabla ya kuondoka.

Read More

Friday, August 23, 2019

WAZIRI MKUU: ZIARA MKOANI LINDI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa Kata ya Rutamba, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Wananchi wa Kata ya Rutamba, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.


Read More

Thursday, August 22, 2019

MATUKIO KATIKA PICHA VIJANA MKOANI GEITA WAPATIWA ELIMU YA UJASIRIAMALI

Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Silas Daudi akitoa mada kuhusu Mpango wa Biashara kwa vijana wanajihusisha na shughuli mbalimbali za biashara na ujasiriamali katika Mkoa wa Geita ikiwa ni awamu ya tatu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa Vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 yanayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Baadhi ya Wajasiriamali wakifuatilia kwa makini mada iliyokuwa ikiwasilishwa na mmoja ya watoa mada wakati wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Julius Tweneshe akielezea mada kuhusu taratibu za kufungua kampuni wakati wa mafunzo hayo.
Sehemu ya wajasirimali kutoka Mkoa wa Geita wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Afisa Uwezeshaji kutoka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bw. Halidi Mbwana akitoa mada kuhusu masuala ya utafutaji wa vyanzo vya mapato kwa vijana walioshiriki mafunzo hayo Mkoani Geita.
Baadhi ya Wajasiriamali walioshiriki kwenye mafunzo hayo wakijadiliana kazi kwenye vikundi.
Sehemu ya Sekretarieti wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wawezeshaji wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Geita Agosti 22, 2019.


Read More

Wednesday, August 21, 2019

UN YAIPONGEZA TANZANIA KWA MATUMIZI MAZURI YA RASILIMALI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,anaye maliza muda wake hapa Nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez kwa ajili ya kumuaga Waziri Mkuu  Ofisini kwake ,Magogoni jijini Dar es Salaam leo Agosti 21,2019.

UMOJA wa Mataifa (UN) umeipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyotumia vizuri rasilimali zake za ndani na hivyo kuiwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo sambamba na kupunguza utegemezi kutoka nje.

Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumatano, Agosti 21, 2019) na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Mratibu huyo Mkazi wa Umoja wa Mataifa ambaye alikwenda kumuaga Waziri Mkuu, amesema kuwa Tanzania imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.

“Katika kipindi changu cha miaka mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania, nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa na taasisi zake nchini.”

Katika hatua nyingine, Bw. Rodriguez ameisifu Serikali ya Tanzania kwa namna ilivyoweza kuandaa na kuendesha vizuri mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu.

Mbali na kuisifu Serikali pia kiongozi huyo amevipongeza vyombo vya habari kwa jinsi vilivyoshirikiana na Serikali kuripoti matukio mbalimbali ya mkutano huo. “Nawapongeza na wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa Serikali wakati wote wa mkutano wa SADC.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amemshukuru kiongozi kwa pongezi alizozitoa ambazo ni ishara kwamba anatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kutumia vizuri rasimali zake.

Waziri Mkuu amesema “maelezo yaliyotolewa na Bw. Rodriguez yanaakisi kauli za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba Tanzania si nchi masikini na inayo uwezo wa kutoa misaada kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo. Watanzania waendelee kuiunga mkono Serikali yao.”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kiongozi huyo kwani alikuwa kiungo kizuri kabaina ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa. Pia atakumbukwa sana kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kipindi cha utumishi wake nchini Tanzania.

Awali, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Balozi Thamasanqa Dennis Mseleku ambaye alikwenda kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania.

Waziri Mkuu alimpongeza Balozi huyo kwa ushirikiano na mchango alioutoa kwa Serikali ya Tanzania katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo zikiwemo za kiuchumi, elimu, afya, maendeleo ya jamii pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya nchini mbili hizo.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mseleku ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa uliompatia katika kipindi chake cha utumishi akiwa nchini na kwamba alitamani aendelee kubaki Tanzania.

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutana na Balozi wa Afrika Kusini, Thamasanqa Dennis Mseleku   kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania amekutana naye   ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam leo Agosti 21.2019.
Read More