Sunday, December 8, 2019

KAGUZI 1,187 ZA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI ZAFANYIKA NCHINI


Na. OWM, Dodoma.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,  Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu,  imefanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria
Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi, ambapo maeneo 1,187 yalikaguliwa na kusajiliwa na Idara na Taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo , Idara  ya  kazi, OSHA, NSSF, PSSSFna WCF,  ili kuhakikisha wafanyakazi  nchini wanakuwa  ni wenye afya na wanakuwa    na mahali pa  kazi salama.

Akiongea, Jijini Dodoma, wakati wa kupokea ripoti ya ukaguzi huo kwenye  Kikao  na Wakuu wa Idara na Taasisi  za Ofisi hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,  Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Andrew Massawe amefafanua kuwa ukaguzi huo ni muhimu kwa kuwa  kuwekeza kwenye Afya na Usalama kazini kunasaidia  kuzuia madhara kwa wafanyakazi  na  kuilinda nguvu kazi muhimu kwa Taifa letu.

Aidha, Katibu Mkuu, Massawe amefafanua kuwa iwapo sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi itatekelezwa ipasavyo itasaidia kuleta hamasa na ari ya kufanya kazi kwa bidii miongoni mwa wafanyakazi, kuimarisha mahusiano mazuri na jamii, kuongeza ubora wa bidhaa au huduma inayotolewa na wizara, Idara  za serikali , kampuni au taasisi husika.

Ameongeza kuwa ameipokea ripoti hiyo ambayo itamsaidia kuweka mikakati ya kuzuia vihatarishi vinavyoweza kujitokeza ili kuweza kuzuia wafanyakazi wasiweze kupata ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

“Ni vyema waajiri na wafanyakazi na umma kwa ujumla kushirikiana na serikali katika ukaguzi wa utekelezaji wa sheria hii ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi,  ili tuweze kuimarisha afya na usalama kazini na mstakabali wa kazi, kwa kuwa tayari serikali tumefanya  juhudi katika kuboresha mazingira ya kazi na kuweka mifumo ya afya na usalama kazini iliyo imara na inayoleta tija katika sehemu za kazi” amesisitiza Massawe.

Katika kuhakikisha kuwa nchi  inapunguza au kuondoa vifo, ajali, magonjwa na madhara yatokanayo na kazi, mnamo mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu ulifanyika ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi nchini kwa kuhusisha  Idara na taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu ndio yenye jukumu la kuboresha na kusimamia Usalama na Afya mahali pa Kazi kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA). Wakala huo ulianzishwa mnamo tarehe 31 Agosti, 2001 chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997, ambapo miongoni mwa majukumu yake ni Kusimamia Utekelezaji wa Sheria hiyo ili kuweza kuongeza  tija na uzalishaji mali hivyo kukuza pato la taifa
MWISHO.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,  Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Andrew Massawe pamoja na  Wakuu wa Idara na Taasisi za Ofisi hiyo  wakiipitia ripoti ya  ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi  nchini uliofanywa na Idara na Taasisi za Ofisi  hiyo,  wakati alipokutana nao  kupokea ripoti  hiyo, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Taasisi za  Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,  Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), wakifuatilia kikao na katibu Mkuu wa ofisi hiyo Andrew Massawe (hayupo pichani) cha kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi  uliofanywa na  Ofisi  hiyo, Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,  Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Andrew Massawe akifafanua umuhimu wa ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi wakati alipokutana na Wakuu wa Idara na Taasisi za Ofisi hiyo mara baada ya kupokea ripoti  ya ukaguzi  wa utekelezaji wa sheria hiyo  nchini, ulifanywa na  ofisi hiyo, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Taasisi za  Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,  Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), wakifuatilia kikao na katibu Mkuu wa ofisi hiyo Andrew Massawe (hayupo pichani) cha kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ya Usalama na Afya mahali pa kazi nchini, uliofanywa na   Ofisi  hiyo, Jijini Dodoma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.