Thursday, November 30, 2017

SERIKALI HAIJARUHUSU KOZI ZA FOUNDATION CHUO KIKUU HURIA


SERIKALI haijatoa ruhusa kwa Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee kutoa kozi ya ‘Foundation’ kama ambavyo imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii.

Baadhi ya mitandao ilitoa taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho: Waziri Mkuu aruhusu kozi za 'Foundation' Chuo Kikuu Huria kwa madai kuwa alitoa ruhusa hiyo jana (Alhamisi, Novemba 30, 2017) wakati akiwa mkoani Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.

Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Singida waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida, Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanyia maboresho Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.

“Kwa sasa Serikali inafanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani sera tuliyonayo haifafanui vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu wajiendeleze kwa njia ya mfumo wa elimu huria na masafa,” alisema.

“Programu kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation, zinahitaji pia kufafanuliwa kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea kuiboresha. Pindi itakapokamilika, tutaitolea taarifa kwa Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza kushirikiana na sekta zote ili kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,” alisema.

Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda alisema wamepokea barua kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwaarifu juu ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa kozi za Foundation katika chuo hicho.

“Tayari tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation ulioboreshwa ili kukidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na tunasubiri mrejesho kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema mwezi ujao,” alisema Prof. Bisanda.

Read More

WAZIRI MKUU ATAKA UDAHILI ELIMU YA JUU UONGEZWE

                 
 *Ashuhudia mkewe akitunikiwa Shahada ya Uzamili OUT


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uchumi wa kati na wa viwanda hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23.

“Hivi sasa, kiwango cha Tanzania cha udahili katika elimu ya juu ni asilimia nne. Kiwango hiki ni kidogo hata kuliko nchi kama Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, ambao licha ya hali ya vita nchini mwao kwa muda mrefu, wamefikia asilimia saba,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Novemba 30, 2017) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Singida na mikoa jirani waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida,

Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonyesha kwamba karibu nchi zote washirika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukiacha Burundi, zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya juu na kwa maana hiyo zimeizidi Tanzania.

Amesema, Chuo Kikuu pekee chenye kanuni za udahili (open entry), chenye kufundisha, kujisomea na hata kutathmini maendeleo ya wanafunzi (assessment on demand) ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. 

“Naungana na Mheshimiwa Rais kuwaomba mtumie fursa hiyo, kuisaidia nchi yetu kuongeza kiwango cha udahili wa wananchi wake katika elimu ya juu, kwa haraka na kasi itakayotuwezesha kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati na wa viwanda, ifikapo 2025.”

“Kwa kushirikiana na Baraza la Elimu Masafa Afrika (African Council for Distance Education (ACDE), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na hata vyuo vikuu vingine ndani na nje ya nchi yetu, ongezeni ubora na panueni wigo wa udahili, kwenye programu za sasa na zingine mtakazoziongeza,” alisisitiza. 

Aliwataka wahakikishe kuwa siku zote, mfumo wao wa utoaji elimu, yaani elimu huria na masafa (Open and Distance Learning (ODL) unajitanabaisha kama mfumo wa kisasa na mahiri katika kutoa elimu na mafunzo yenye ubora unaokubalika na kutambulika kitaifa, kikanda na kimataifa. 


“Kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendelelo na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, napenda nisisitize kuwa dira ya utendaji wenu, ijikite katika maeneo yaliyoainishwa, chini ya mwanvuli wa kaulimbiu ya Chuo “elimu bora na nafuu kwa wote.”

Waziri Mkuu amesema katika kutambua umuhimu wa elimu huria na masafa kwa maendeleo ya elimu hapa nchini, Serikali inaunga mkono azma ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuanzisha dawati maalumu kwa ajili ya kuimarisha Mfumo wa Elimu Huria na Masafa.

“Kupitia hafla hii, ninaagiza dawati kama hilo lianzishwe pia katika Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zao za ithibati zinazingatia na kukidhi matakwa ya viwango vya mfumo wa Elimu Huria na Masafa,” alisema Waziri Mkuu. 

“Ninaungana na Waziri mwenye dhamana kuagiza kuwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) washirikiane na TCU na NACTE kuhakikisha kuwa taratibu za ithibati zinatekeleza azma ya Serikali kama ilivyoainishwa kwenye Sera ya Elimu ya Mafunzo 2014, hususan juu ya suala la kuwatambua watu waliopata ujuzi bila kupitia mfumo (rasmi) wa elimu na mafunzo,” alisisitiza.

Waziri Mkuu pia alishuhudia mke wake, Mary Majaliwa akitunukiwa Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Masters’ of Education in Administration, Planning and Policy Studies) na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Waziri Mstaafu, Mizengo P. Pinda.
Read More

MAJALIWA MGENI RASMI MAHAFALI YA 33 YA CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda,  baada ya kuwasili kwenye Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mjini Singida ambapo alikuwa mgeni rasmi, Novemba 30, 2017. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida Novemba 30, 2017. Kushoto ni Mkuu wa Chuo Kikuu hicho na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (mwenye miwani mbele) akiwa na wahitimu wenzake katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida, Novemba 30, 2017.
 Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akimtunuku Shahada ya Uzamili Katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Master Of Education in Administration, Planning and Policy Studies), Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (kushoto) katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida, Novemba 30, 2017. Wapili kulia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Watatu kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinoloji, Profesa Joyce Ndalichako.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akitelemka kutoka kwenye jukwaa baada ya kutunukiwa Shahada ya Uzamili Katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Master of Education in Administration, Planning and Policy Studies) na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu MStaafu, Mizengo Pinda (kulia)  huku  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia.

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (mwenye miwani mbele) akiwa na wahitimu wenzake katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida, Novemba 30, 2017. 

Mke wa  Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa   akipokea ua kutoka kwa mwanae, Saad Majaliwa Kassim baada ya kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Master of Education in Administraion, Planning and Policy Studies) katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida Novemba 30, 2017.Read More

Wednesday, November 29, 2017

WAZIRI MKUU AMKABIDHI IGP WALIOTAKA KUTOA SEMI TELA 44 BILA YA KUKAMILISHA TARATIBU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwakamata, Bw. Bahman wa kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni ya Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa bandarini magari makubwa aina ya semi tela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.

“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.”

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 29, 2017) alipofanya ziara ya ghafla bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kuutapeli uongozi wa TPA kutaka kutoa magari hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.

Hatua hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata msamaha wa  kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.

Amesema Serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kulipakodi  ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi bila ya kubugudhiwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kufuata sharia za nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao.
Waziri Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa magari hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya nchini Uturuki.

“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani  (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakin huyu bwana hajafanya hivyo”

Waziri Mkuu amesema kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo ni kinyume cha sheria na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.  

Amesema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha mahusiano mazuri iliyopo kati ya Tanzania na Uturuki kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.

“Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania sasa huu ujanjaunja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi unajenga sura mbaya kwa wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja.”

Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mawakala wa Forodha kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na Serikali haitawavumilia wababaishaji kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimueleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria na taratibu.

Read More

WAZIRI MKUU ABAINI SEMI TRELA 44 ZIKITAKA KUTOLEWA BANDARINI BILA YAKUFUATA UTARATIBU

Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa (mwenye Tai nyekundu) amefanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Dar es salaam leo November 29, 2017 nakubaini Kampuni ya NAS ikitaka kutuo Semi Tela Arobaini na nne bilayakufuata utaratibu.


Read More

MAJALIWA AWASILI SINGIDA

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenuyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Martha Mlata baada ya kuwasili Ikulu Ndogo ya Singida Novemba 29, 2017. Kesho Mheshimiwa Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya Chuo Kikuu Huria chaTanzania yatakayofanyika mjini Singida.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary (kuila) wakimsikiliza mwimbaji wa Kwaya ya Africa Inland Church Tanzania, Loice Jonathan (kushoto) baada ya kuwasili kwenye Ikulu ndogo ya Singida Novemba 29, 2017. Kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yatakayofaanyika  mini Dodoma. Watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi.


Read More

Tuesday, November 28, 2017

TUTAWASHUGHULIKIA WOTE WANAOTUMIA VIBAYA FEDHA ZA UKIMWI-MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Novemba 28, 2017)  amefungua kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Juliasi Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Novemba 28, 2017)  amefungua kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Juliasi Nyerere jijini Dar es Salaam.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitawavumilia watu wote wanaotumia vibaya fedha za umma ambazo zinapaswa kuleta maendeleo kwa wananchi, zikiwemo na za Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi

Amesema mfuko huo unalenga kufanikisha ukusanyaji wa fedha za kutosha amabazo ni muhimu kwa Taifa wakati huu tunapoazimia kumaliza ukimwi ifikapo mwaka 2030..

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Jumanne, Novemba 28, 2017) wakati akifungua kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Nitoe wito kwa Bodi ya Mfuko huu na watendaji wake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha hizi ili ziweze kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa Mfuko huu. “

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhamasisha wananchi, wadau na sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kujenga nchi ya viwanda ili waweze kufikia uchumi wa kati, jambo ambalo haliwezi kufikiwa iwapo wananchi wake watakuwa hawana afya bora.

“Hatutaweza kufikia malengo haya kama Taifa iwapo watu wetu hawatakuwa na afya bora kwani nguvu kazi kwa ajili ya Tanzania ya Viwanda itatokana na wananchi wenye nguvu na afya bora.”

“ Hivyo kama Serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora za afya ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora. Tutaendelea kuwakinga wananchi wetu hususan ni vijana ili Taifa letu liwe na nguvu kazi ya kutosha hasa wakati huu tunapoanza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.”

Pia Waziri Mkuu amesema kwamba kwa sasa Watanzania wengi wana uelewa mkubwa wa ukimwi lakini changamoto iliyopo ni kubadili tabia na kuachana na tabia hatarishi zinazosababisha kupata maambukizo mapya.

Amesema jambo hilo ni hatari kubwa kwa nchi yetu kwa sababu bado wananchi wengi wanaendekeza tabia ya kuwa na wapenzi wengi tena kwa wakati mmoja na hakuna uaminifu katika ndoa.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu “changia mfuko wa udhamini wa udhibiti ukimwi, okoa maisha”.

Kongamano hilo lilihudhuliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Walemavu Bibi Stella Ikupa Alex, Naibu Waziri Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile, Makamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS).
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt Leonard maboko, Mwenyekiti wa Baraza la Wanaoishi na virusi vya Ukimwi (NACOPHA), wawakilishi wa wadau wa maendeleo na wadau  wa ukimwi nchini.


Read More

Saturday, November 25, 2017

WAZIRI MKUU AKABIDHI KOMBE LA UBINGWA KWA TIMU YA AFISI KUU

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikabidhi kombe  kwa nahodha wa timu ya Afisi Kuu .Bwana  Vuai Jecha baada ya timu yake kuibuka mshindi kwakuifunga timu ya Kwahani mabao 3 kwa 1. katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Aman Zanziba, Novemba 25,2017


Waziri Mkuu .Kassim Majaliwa mwenye nguo nyeupe akiwa katika picha ya pamoja na timu ya Afisi Kuu Zanzibar


Read More

Friday, November 24, 2017

MAKATIBU WAKUU OFISI YA WAZIRI MKUU WAKUTANA NA MENEJIMENTI YA OFISI HIYO DODOMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora akizungumza jambo kwa wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya ofisi hiyo (hawapo pichani) walipokutana kujadili   utekelezaji wa ofisi hiyo Novemba 24, 2017 kulia kwake ni Katibu Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge) Bi. Maimuna Tarishi.

Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia kikao cha Makatibu wakuu Ofisi hiyo walipokutana kujadili utekelezaji wa majukumu yao Mjini Dodoma Novemba 24, 2017.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Issa Nchasi akichangia hoja wakati wa kikao cha Menejimenti ya Ofisi hiyo walipokutana na Makatibu wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kujadili utekelezaji wa majukumu yao Novemba 24, 2017 Mjini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Packshard Mkongwa akifafanua jambo kwa Makatibu wakuu wa ofisi hiyo (hawapo pichani) wakati wa kikao cha menejimenti kilichofanyika Dodoma.

Makatibu wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu Bi.Maimuna Tarishi na anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof.Faustin Kamuzora wakisikiliza hoja za wajumbe wa kikao cha Menejimenti cha ofisi hiyo walipokutana kujadili utekelezaji wa majukumu yao Novemba 24, 2017 Dodoma.

Afisa Tehama Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Innocent Mboya akifafanua jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Ofisi hiyo walipokutana Katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.

Read More

TUTAMALIZA KERO YA MAJI TUNDURU-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa miradi miwili ya maji katika vijiji viwili vya Rahaleo na Mbungulaji kwenye kata ya Kalulu yenye thamani ya sh. Milioni 112 na kuahidi kumaliza kero ya maji wilayani Tunduru.

Amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 24, 2017) mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji hivyo kwa lengo la kumaliza changamoto ya umatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo hayo.

Amesema ujenzi wa miradi hiyo ni utekelezaji wa Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani yenye lengo la  kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

“Nataka maji haya yaende kwa wananchi si wananchi wayafuate, hivyo mara baada ya kukamilika ujenzi wa mradi huu Halmashauri ijenge mtandao wa mabomba yatakayosafirisha maji kutoka eneo la mradi hadi kwenye vioksi na kuyafikisha katika makazi ya wananchi.”

Pia ametoa wito kwa wazee wa vijiji hivyo kwa kushirikiana na vijana kuhakikisha wanalinda mradi huo kwa kutokata miti kwenye maeneo yote yanayozunguka vyanzo vya maji ili kuepusha ukame. Ameagiza ipandwe miti kwenye maeneo hayo ili kuhifadhi mazingira.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao ikiwa ni pamoja na kufanya kazi ya kuwatumikia wasnanchi bila ya ubaguzi wa dini, rangi na itikadi za vyama.
Amesema Serikali haitaki kusikia mwananchi anakwenda kufuata huduma katika ofisi zao na kuzungushwa kwa muda mrefu bila ya kuhudumiwa. “Serikali hii haitaki wananchi wake hususan wanyonge wasumbuliwe tukikubaini tunakuondoa.”

Waziri Mkuu ameongeza kwamba “Serikali hii haidekezi wala kuwaonea aibu watumishi wasiowajibika katika kuwatumikia wananchi. Serikali hii haitamuhifadhi mtu atakayeshindwa kufanya kazi, tunataka kazi tu na asiyefanya kazi na asile ndiyo maana tunawaondo watumishi  wazembe wote.”
Read More

WAZIRI MKUU AUNGANA NA WANASONGEA KUOMBOLEZA KIFO CHA GAMA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisaini kitabu cha maombolezo,Nyumbani kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Songea .Leonidas Gama. Waziri Mkuu aliungana na wanafamilia pamoja na wananchi wa Songea katika kijiji cha Lukuyi Wilayani Songea leo Novemba 25/2017 katika kuomboleza msiba.

Waziri Mkuu Kassim. Majaliwa leo Noemba 25/2017 ameungana na wanafamilia, wananchi wa Songea katika kuomboleza kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Songea, Bw. Leonidas Gama, nyumbani kwa marehemu Likuyu wilayani Songea.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na wanafamilia, wananchi wa Songea katika kuomboleza kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Songea, Bw. Leonidas Gama, nyumbani kwa marehemu Likuyu wilayani Songea.

Bw. Gama   amefariki dunia jana (Ijumaa, Novemba 24, 2017) katika Hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma alikokuwa akipatiwa matibabu. Marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumatatu, Novemba 27, 2017 katika kijiji cha Likuyu wilayani Songea.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu amesema kifo hicho ni pigo kwa Serikali kwa sababu marehemu alishirikiana nayo vizuri tangu akiwa mtumishi wa umma na hata baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Songea.

Waziri Mkuu amesema msiba huo umeleta mtikisiko mkubwa kwa sababu baada ya kurudi nchini kutoka India alikokuwa akipatiwa matibabu aliwaeleza kuwa hali yake kwa sasa ni nzuri. ”Ametuachia pengo kubwa ambalo hatuna namna ya kuliziba.”

Ameongeza kuwa alipokea taarifa za msiba huo kwa huzuni na mshtuko mkubwa kwa sababu siku mbili kabla ya Waziri Mkuu kuanza ziara yake mkoani Ruvuma, Bw. Gama alimpigia simu na kumjulisha kwamba yeye anatangulia Songea kumpokea.

“Kifo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kwamba Bw. Gama ametangulia nasi tutafuata, hivyo wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Gama alikuwa kiongozi na mwanga wa maendeleo.”

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba wanafamilia, mke wa marehemu na watoto na wananchi wa jimbo la Songea waendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bibi Christine Mndeme alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wake na kwenda kuwafariji wafiwa licha ya majukumu mengi na makubwa aliyonayo.

Awali msemaji wa familia Bw. Issa Fusi alimshukuru Waziri Mkuu pamoja na viomgozi mbalimbali waliojitokeza na kuwafariji baada ya kutokea kwa msiba huo.”Kaka yetu tulimpenda sana kazi ya Mungu haina makosa.”
Read More

MAJALIWA: TANESCO KAWAHUDUMIENI WANANCHI VIJIJINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liwafuate wananchi walioko katika vijiji vinavyotarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuwahudumia.

Amesema Serikali imetenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nicety hiyo nchini, hivyo ni vema wakawatembelea wananchi katika maeneo yao na kuwahudumia huko huko.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Novemba 24, 2017) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo Tunduru, ambapo aliwasisitiza watumishi wa TANESCO kutokaa maofisini na badala yake wakawahudumie wananchi katika vijiji vyao.

Alisema katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza miradi ya kusambaza umeme vijini kupia REA, TANESCO wanatakiwa kwenda vijijini na kuwaandikisha wananchi wanaohitaji huduma hiyo pamoja na kufungua vituo vya muda vya malipo.

Waziri Mkuu alisema hatua hiyo itawapunguzia wananchi gharama za kusafiri hadi kwenye makao makuu ya wilaya kufuata huduma mbalimbali ikiwemo ya kulipia gharama za kuunganishiwa umeme katika nyumba zao.

Alisema Serikali imedhamiria kusambaza huduma ya nishati ya umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vya wilaya ya Tunduru ambapo wananchi hao wataunganishiwa umeme huo kwa gharama ya sh. 27,000 tu.

Pia Waziri Mkuu aliesema  wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliongeza kwamba  lengo la Serikali ya awamu ta tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa.
Waziri Mkuu alisema huduma hiyo ni muhimu kwani mbali ya kutumika katika matumizi ya majumbani, pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha zahanati, shule ,viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.
Awali Waziri Mkuu alitembea na kukagua shughuli za ujenzi wa mradi wa kituo cha afya kinachojengwa katika eneo la Nakayaya wilayani Tunduru pamoja na kukagua ghala la kuhijfadhia korosho na kisha kupokea taarifa ya kiwanda cha kubangulia korosho cha Korosho Afrocan Limited.

Read More

WAZIRI MKUU AKIWA KATIKA ZIARA YA KIKAZI NAMTUMBO,TUNDURU MKOANI RUVUMA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja  Afisa Ardhi wa Wilaya ya Namtumbo Bwana  Maurus  Year kuhakikisha ametatua tatizo la Ardhi lilodumu miaka kumi katika Wilaya ya Namtumbo. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Novemba 23,2017  katika mkutano wa hadhara Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.

Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa akiongea na Wananchi wa kijiji cha Chomolo Wilaya ya Namtumbo wakati walipo simamisha msafara wake Novemba 24,2017 alipokuwa akielekea katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Tunduru Mkoani  Ruvuma.
Wananchi wa Wilaya ya Namtumbo wakimsikiliza kwa makini Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa  akihutubia Mkutano wa hadhara katika Uwanja wa michezo wa Rwinga uliopo Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma Novemba 23,2017.Read More

Thursday, November 23, 2017

CHUO KIKUU ARDHI MARUFUKU KUKODI MAKAMPUNI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekipiga marufuku Chuo Kikuu Ardhi kukodi makampuni ya kufanya kazi mbalimbali kwa niaba yake.

Amesema kitendo hicho kinaharibu kazi na sifa ya chuo hicho kwa kuwa baadhi ya makampuni wanayoyapa kazi hayakidhi vigezo.

Waziri Mkuu  ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 23, 2017) kwenye ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu Ardhi.

“Kama kuna umuhimu wa kufanya kazi na kampuni ni bora muanzishe kampuni ya kwenu itakayofanya kazi vizuri ili kujiepusha na matatizo.”

Pia Waziri Mkuu amekiagiza chuo hicho kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa na Dunia.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi holela, uharibifu wa mazingira na majanga ya asili kama mafuriko.

Amesema Serikali inaamini kuwa matokeo ya kazi zinazofanywa na chuo hicho zikiwemo tafiti ni chachu ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa imeweka mkazo wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kupato cha kati ifikapo 2025, hivyo wanahitajika wataalamu wa kutosha na wenye weledi.

“Hivyo Chuo Kikuu cha Ardhi kama taasisi ya Serikali inawajibu mkubwa wa kutayarisha wataalamu mbalimbali wa sekta za ujenzi, ukadiriaji majenzi na uhandisi wa mazingira.

Pia Waziri Mkuu amewataka watumie fursa hiyo ya kuadhimisha miaka 10 ya chuo hicho kujitafakari na kuona ni kwa namna gani wanaweza kuwekeza zaidi ili kuongeza tija ya uwepo wa taasisi hiyo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Wekeni mikakati madhibuti itakayowezesha chuo kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Siku zote mjikite katika kutafuta kuwa na ubora zaidi ya wakati uliopita.”

Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema Serikali inakkitegemea chuo hicho katika kufanikisha ajenda yake ya uchumi wa viwanda kwa kuwa kinatoa wataalamu wengi.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya, Mwenyekiti wa Baraza la chuo Bibi Tabitha Siwale, Makamu Mkuu wa chuo Profesa Evaristo Liwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.
Read More

CHUO KIKUU ARDHI MARUFUKU KUKODI MAKAMPUNI-MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati )akimuelekeza jambo Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi (kushoto)Profesa Evaristo Liwa.kulia kwa Waziri Mkuu,ni Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi. Profesa Joyce Ndalichako.Waziri Mkuu leo Novemba 23 /2017 alikuwa mgeni Rasimi katika Sherehe za Miaka 10 ya Chuo cha Aridhi  Dar es salaam
Waziri Mkuu. Kassim Maliwa,(kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu  Aridhi Tanzania. David Cleopa Msuya .wakati wa uzinduzi wa Sherehe ya miaka Kumi ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo yameanza leo Novemba 23/2017 Jijini Dar es salaam.katikati ni Rais wa Jumuia ya wahitimu Chuo Kikuu cha Aridhi


Read More

WAZIRI MKUU AMPA OFISA ARDHI MWEZI MMOJA KUFIDIA WANANCHI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya Namtumbo Bw. Maurus Yera awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo.

Wakazi hao 21 mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ya mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Lwinga akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.

Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango, ambapo walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi.

“Nataka wananchi hawa wawe wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya Krismasi ya mwaka huu. Serikali haiko tayari kuona wananchi wake waliotoa ardhi kupisha maendeleo wakisumbuliwa.”

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.

Pia Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa rushwa pale wanapohitaji kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi kwa kuwa ni haki yao kuhudumiwa.

Aliwataka wananchi kuwa na imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watendaji kuhakikisha miradi wanayosimamia inakuwa na thamani inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa na iwapo watabainika kwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Lazima kiasi cha fedha kinachotolewa kugharamia mradhi kilingane na thamani ya mradi husika. Mfano tumetoa sh. milioni 70 kugharamia mradi na kukuta mradi uliojendwa ni wa sh. milioni 30 aliyeshughulikia ujenzi huo nasi tutamshughulikia hatutamuacha salama.”

Awali, Waziri Mkuu alifungua ghala la kuhifadhiia mpunga na mchele katika wilaya ya Namtumbo lililojengwa na MIVARF na kisha alizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bibi Christine Mndeme alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao ya mahindi na mbaazi, ambapo Waziri Waziri Mkuu alisema sula hilo linashughulikiwa hivyo wananchi waendelee kuwa na subira.
Read More