Thursday, November 23, 2017

WAZIRI MKUU AMPA OFISA ARDHI MWEZI MMOJA KUFIDIA WANANCHI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya Namtumbo Bw. Maurus Yera awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo.

Wakazi hao 21 mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ya mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Lwinga akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.

Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango, ambapo walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi.

“Nataka wananchi hawa wawe wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya Krismasi ya mwaka huu. Serikali haiko tayari kuona wananchi wake waliotoa ardhi kupisha maendeleo wakisumbuliwa.”

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.

Pia Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa rushwa pale wanapohitaji kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi kwa kuwa ni haki yao kuhudumiwa.

Aliwataka wananchi kuwa na imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watendaji kuhakikisha miradi wanayosimamia inakuwa na thamani inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa na iwapo watabainika kwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Lazima kiasi cha fedha kinachotolewa kugharamia mradhi kilingane na thamani ya mradi husika. Mfano tumetoa sh. milioni 70 kugharamia mradi na kukuta mradi uliojendwa ni wa sh. milioni 30 aliyeshughulikia ujenzi huo nasi tutamshughulikia hatutamuacha salama.”

Awali, Waziri Mkuu alifungua ghala la kuhifadhiia mpunga na mchele katika wilaya ya Namtumbo lililojengwa na MIVARF na kisha alizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bibi Christine Mndeme alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao ya mahindi na mbaazi, ambapo Waziri Waziri Mkuu alisema sula hilo linashughulikiwa hivyo wananchi waendelee kuwa na subira.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.