Thursday, November 9, 2017

HATUJASHINDWA KUCHUNGUZA MATUKIO YA KIHALIFU-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesisitiza kwamba vyombo vya dola vya ndani ya nchi havijashindwa kuchunguza matukio ya kihalifu yaliyotokea nchini, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuwa na subira.

Amesema Serikali hairidhishwi na matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyofanywa na watu wasiolitakia mema Taifa, ambayo yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini na baadhi yake yamesababisha vifo na wengine kujeruhiwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 9, 2017) wakati akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma.

Bw. Mbowe alitaka apew kauli ya Serikali juu ya hatua zilizochukuliwa kuhusu tukio la kushambuliwa na mbunge wa Singida Mashariki Bw. Tundu Lissu, ambapo alishauri uchunguzi huo ufanywe na vyombo vya kimataifa, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya ndani vya dola.

“Vyombo vya ndani vya dola vina uwezo mkubwa wa kusimamia usalama wa nchi na vinaendelea na uchunguzi wa matukio hayo yaliyofanywa na watu wasiolitakia mema Taifa letu. Nawaomba wananchi waendelee kuwa na imani na vyombo vyetu vya dola na mara uchunguzi utakapokamilika taarifa itatolewa.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi waendelee kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa mbalimbali juu ya vitendo vya kihalifu vinavyotokea kwenye maeneo yao kwa lengo la kudumisha amani na utulivu nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma imeanza kutekelezwa kwa kuwapandisha madaraja watumishi wanaostahili sambamba na kulipa malimbikizo yao mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema baada ya kumaliza ulipaji wa malimbikizo ndipo Serikali itaendelea na hatua ya uboreshaji wa mishahara kwa watumishi wote wa umma, hivyo amewaomba waendelee kuwa na subira na imani na Serikali. Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilindi, Bw. Omary Kigua aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itapandisha mishahara ya watumishi wa umma.

Pia Waziri Mkuu amezungumzia changamoto ya masoko kwa mazao ya mbaazi na tumbaku ambayo yanashughulikiwa na Serikali na tayari baadhi ya nchi zimeanza kuonyesha nia ya kununua mazao hayo, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuwa na uvumilivu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu Bibi Munde Tambwe aliyeiomba Serikali kumpatia ufafanuzi juu ya kukosekana kwa soko la tumbaku ambayo imelundikana katika maghala na Bibi Pauline Gekul Mbunge wa Babati aliyelalamikia kukosekana kwa soko la zao la mbaazi.

Akizungumzia kuhusu zao la tumbaku, Waziri Mkuu amesema changamoto hiyo imetokana na wakulima wa zao hilo kuongeza uzalishaji tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali na wanunuzi. “Nawaomba wakulima waendelee kuwa wavumilivu Serikali inafanya mazungumzo na nchi za lran, Korea Kusini, Misri na Indonesia ili waweze kununua tumbaku hiyo na kuwaondolea usumbufu wakulima.”


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.