Thursday, June 29, 2017

MAJALIWA: BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA KUWA HISTORIA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeadhimia kupambana vilivyo dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na kuhakikisha inakuwa historia nchini.

Pia ametoa wito kwa wazazi wote nchini waendelee kufuatilia nyendo za watoto ili wasijiingize kwenye mtego wa dawa za kulevya na wala wasisubiri vijana wao waanze kutumia.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni 29, 2017) kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani, iliyoadhimishwa mjini Dodoma.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya unadhibitiwa kikamilifu nchini.

Amesema katika kutimiza azma hiyo, ambayo pia inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuanzisha chombo cha kisheria cha kupambana na biashara hiyo, ambayo imeongeza adhabu kwa wanaoshiriki.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha chombo hicho kinachoongoza mapambano ya dawa za kulevya ili kiendelee kufanya kazi kwa weledi na kwa kutumia mbinu za kisayansi.

“Tunaponadi uchumi wa viwanda lazima tuwe na nguvu kazi yenye siha njema kuweza kushiriki kwenye kazi halali za kujenga Taifa letu na yeyote anayetaka kudhohofisha nguvu kazi ya Taifa letu au kuhujumu jitihada za uchumi wa viwanda atashughulikiwa bila huruma,” amesema.

Aidha, kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ni ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Vijana na Watoto ili Kuwaepusha na Dawa za kulevya.’

Waziri Mkuu amesema kauli mbiu hiyo imetokana nan a takwimu za waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ambao ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35.

“Hili ndilo kundi kubwa kwenye jamii jetu na ndilo tegemeo kubwa kwa ustawi wa nchi yetu. Hili ndilo kundi litakalotoa askari wa kulinda Nchi yetu, wanasiasa wa kuongoza Taifa letu na wataalamu mbalimbali wa kuisaidia Tanzania,” amesema.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu), Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema matumizi ya dawa za kulevya yamelisababishia Taifa madhara makubwa ya kiafya na  kiuchumi hivyo kila mwananchi ashiriki katika mapambano hayo.

Mapema Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la Kituo cha Kutoa Huduma ya Tiba kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya katika eneo la Itega mkoani Dodoma na kuwashauri wakazi wa mkoa huo kutojihusisha na biashara hiyo.
Read More

MAADHIMISHO YA KITAIFA YA SIKU YA KUPIGA VITA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI MJINI DODOMA

 Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke akizungumza katika  Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Gaudensia Simwanza wakati alipotembelea banda la  Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) katika  Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la Kituo cha Kutoa Huduma kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya mjini Dodoma Juni 29, 2017.  Kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.

Wasanii wa Kikundi cha Mchoyi cha Dodoma wakicheza ngoma ya kabila la Wagogo katika  Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za ulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhutubia katika  Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.

Baadhi ya wananchi na Viongozi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Baadhi ya wananchi na Viongozi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama dawa mbalimbali za kulevya katika maonyesho yaliyokwenda sambamba na Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwenye uwanja wa Nyerere mjini Dodoma Juni 29, 2017.Read More

MAJALIWA: ZUIO LA USAFIRISHAJI CHAKULA NJE LIKO PALE PALE


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali wa kuzuia usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi uko pale pale.

Pia amesema mahindi iliyokamatwa mkoani Kilimanjaro yakisafirishwa kwenda nje ya nchi yataingizwa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na magari yatabaki polisi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo ( Alhamisi Juni 29, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri  Mkuu wakati akijibu swali la Mheshimiwa Ritha Kabati  (Viti Maalumu) aliyetaka ufafanuzi kuhusu zuio la kusafirisha mazao nje ya nchi kwa mikoa yenye chakula cha ziada.

“Tumedhibiti na kuzuia usafirishaji wa chakula hasa mahindi kwenda nje ya nchi ili kuliepusha Taifa kukumbwa na baa la njaa kutokana na baadhi ya mikoa kutopata mavuno ya kutosha,”

“Kuna maeneo kama ya Sengerema na Geita mahindi yamekauka, hivyo bado tuna upungu wa chakula. Na hata bei ya chakula ipo juu, hatuna namna nyingine zaidi ya kudhibiti utokaji wa chakula kwenda nje na nawasihi wananchi tushirikiane katika jambo hili,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kama kunaulazima wa kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi  wahusika wakaombe kibali katika Wizara ya Kilimo,  Mifugo na Uvuvi na kibali kiwe cha kusafirisha unga na si mahindi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema watumishi wote wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Mkuu Dodoma (CDA) waliokuwa wanaolalamikiwa na wananchi kutokana na utendaji wao wataondolewa wakati wenzao wakihamishiwa Manispaa ya Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na ukaguzi na uhakiki wa kina kwenye masuala ya fedha na utumishi ili waweze kujua CDA ilipovunjwa iliacha fedha kiasi gani na shughuli zake zilifikia hatua gani ili ziendelezwe.

Amesema majukumu yote ya CDA yatafanywa na Manispaa ya Dodoma na baada ya kukamilisha utaratibu huo mpango kazi wote utaendelea kama ulivyopangwa.Kuhusu waliolipia viwanja watakabidhiwa mara baada ya kukamisha utaratibu huo.


Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Mheshimiwa Matha Malata (Viti Maalumu) aliyetaka kupata tamko la Serikali kuhusu wananchi ambao waliolipia viwanja CDA ambao bado hawajakabidhiwa.


Read More

BUNGENI LEO JUNI 29,2017

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju bungeni mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Waziri  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akiwasilisha hati mezani, Bungeni mjini Dodoma Juni 29, 2017.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura (kushoto) na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Tekinolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya wakiteta  bungeni mjini Dodoma Juni 29, 2017.

Mbunge wa Mbulu Vijijini, Fratei Massay akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Bungeni mjini Dodoma Juni 29, 2017.  Kushoto ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia na katikati ni Mbunge wa Viti Maalum Rita Kabati.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali, Bungeni mjini Dodoma Juni 29, 2017.


Read More

Monday, June 26, 2017

WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU USAFIRISHAJI WA CHAKULA NJE YA NCHI


*Ahimiza nyumba za ibada zisaidie vita ya dawa za kulevya         
           
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi kuanzia leo. 

“Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini,” amesema. 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 26, 2017) wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid. 

“Jana nimeona kwenye televisheni taarifa kuhusu malori 10 yaliyokamatwa Tarakea yakiwa na mahindi tayari kuvushwa mpaka. Mheshimiwa RC akasema chakula hicho ni lazima yarudishwe kwa ajili ya usagaji.”

“Mimi nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.” 

Akitoa tahadhari kuhusu uuzwaji wa chakula nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali. “Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa la njaa huko mbele,” amesema.

Amesema mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo ambalo ni hatari sana. Hii ni kwa sababu chakula cha ndani hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa."

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wafanyabiashara wa ndani, wachukue mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu zenye mavuno kidogo. “Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu,” alisisitiza. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa dini waisadie Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kupitia kwenye nyumba za ibada. “Naomba tuendelee kushirikiana kupambana na janga hili la dawa za kulevya kwa ustawi wa nchi yetu. Naamini viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa katika mapambano haya, kwa kuwafunda vijana wetu kuishi katika maadili ya kidini na kutojiingiza kwenye janga hilo.”

Alisema Serikali kwa upande wake itaendeleza mapambano hayo bila ajizi wala mzaha. “Tunaomba wananchi wote watuunge mkono kwa kutoa taarifa sahihi za wanaojihusisha na uzalishaji, utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya pindi tu wanapowabaini.”

Wakati huo huo, akitoa tafsiri ya Qur’aan tukufu kwenye Baraza la Eid, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Juma alisema kila nguzo katika Uislamu inapaswa kufuatwa na kwamba mtu akiharibu nguzo moja tu anakuwa ameharibu nguzo zote tano.

Alisema siku ya kiyama, watatokea watu wenye thawabu kama milima ya Usambara ama Upareni na akawataka Waislamu wote nchini wadumu katika kutenda mema ili wapate thawabu.

Mapema, akitoa khutba katika swala ya Eid el Fitr iliyoswaliwa kwenye msikiti huohuo wa Masjid Riadha, Sheikh Mlewa Shaban alisema sikukuu ya Eid ni siku ya kujiepusha na madhambi kama ulevi, kamari na lugha chafu, bali aliwataka waumini wote waitumie siku hiyo kuwapa furaha maskini, yatima na wajane.

“Mtu asiseme mwezi wa Ramadhan umepita, sasa narudia mambo yangu ya zamani. Adhabu za Mwenyezi Mungu hazina mipaka na wale waliotulizana watapata thawabu yao, kumbukeni neema na Mwenyezi Mungu na mcheni Mwenyezi Mungu.”

“Kitu tunachopaswa kufanya kila wakati ni kumcha Mwenyezi Mungu. Lazima tupendane, tuondoe tofauti zetu na tuujenge Uislam. Hatuwezi kuujenga uislam kama hatupendani. Lazima tuilinde ibada yetu kwa sababu hatuna garantii, ni lini tutaondoka,” alisema.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally; Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe; Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira; IGP Mstaafu, Bw. Said Mwema; Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Jaffary Michael; Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
Read More

WAZIRI MKUU AKIWA MOSHI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa nasaha kwa waumini (hawapo pichani) waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.
  
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally wakati wa stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mara baada ya Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa mkoani Kilimanjaro Tarehe 26 Juni, 2017.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally mara baada ya stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa pole na neno la faraja kwa wanafamilia, nyumbani kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpa pole mjane wa marehemu, mama Ndehorio P. Ndesamburo alipofika nyumbani kwao eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017.Kaka wa marerehemu Dk. Philemon Ndesamburo, Bw. Zablon Sindato Kihwelu akimshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika nyumbani kwao eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Anna Mgwira (wa tatu kushoto), mjane wa marehemu na Kaka wa marehemu wakiomba dua na wanafamilia kwenye kaburi la Dk. Philemon Ndesamburo, aliyezikwa nyumbani kwake eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro. Wa kwanza kulia ni mtoto wa marehemu.

Read More

Friday, June 23, 2017

OFISI YA WAZIRI MKUU YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua akiongea na  wafanyakazi wa ofisi hiyo (hawako pichani) wakati wa mkutano wa kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma uliofanyika    leo jijini Dar es salaam tarehe 23 Juni, 2017.
Ofisi ya Waziri Mkuu imeadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia Juni 16-23 Barani Afrika,  kwa mwaka huu kauli mbiu  ni “Kuimarisha Ushirikishwaji wa Jamii katika Utoaji Huduma: Vijana washirikishwe kuleta Mabadiliko Barani Afrika”.
Kwa kuzingatia kauli mbiu hiyo yenye kujikita katika kushirikisha jamii katika utoaji huduma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua amekutana na wafanyakazi wa ofisi hiyo leo jijini Dar es salaam tarehe 23 Juni, 2017,   ambapo wamejadili jinsi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa umma kwa kuzingatia weledi, uadilifu na ufanisi ili kuhakikisha Dira na Dhima ya Ofisi hiyo inafikiwa.
Dira ya Ofisi hiyo ni kutoa huduma kwa umma katika mazingira shindani ya kiuchumi ili kuwa na maendeleo emdelevu, aidha Dhima ya ofisi hiyo ni Kuratibu na kusimamia utoaji wa huduma zenye kuleta matokeo yanaotarajiwa katika sekta zote ili kujenga mazingira ya kiuchumi kwa maendeleo enndelevu.Ofisi ya Waziri imekuwepo tangu mwaka 1962. Mwaka 1977, Ofisi ilipewa hadhi yake kisheria kwa kuzingatia Katiba ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilianzisha wadhifa wa Waziri mkuu. 

Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano wa Kuadhinmisha wiki ya utumishi wa umma uliofanyika    leo jijini Dar es salaam tarehe 23 Juni, 2017.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano wa Kuadhinmisha wiki ya utumishi wa umma uliofanyika    leo jijini Dar es salaam tarehe 23 Juni, 2017.


Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano wa Kuadhinmisha wiki ya utumishi wa umma uliofanyika    leo jijini Dar es salaam tarehe 23 Juni, 2017.

Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano wa Kuadhinmisha wiki ya utumishi wa umma uliofanyika    leo jijini Dar es salaam tarehe 23 Juni, 2017.

Read More

Thursday, June 22, 2017

MSIWATOZE KODI YA MAJENGO WAZEE WA MIAKA 60

*Ataka TRA wafanye sensa ya majengo kwenye miji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka maafisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasitoze kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.

"TRA ijipange kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai Mosi 2017. Katika kutekeleza jukumu hilo, zingatieni sheria. Tusisikie mnawadai kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama makazi yao," amesema. 

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Juni 22, 2017) wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa wilaya ya Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA, wilayani humo, mkoani Geita. 

Waziri Mkuu amewataka maafisa hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu. "Msiende vijijini. Nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za mijini.  Piteni kwenye mitaa, muainishe aina zote za nyumba zinazostahili kulipiwa kodi. Mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha wananchi kulipia kodi hizo," amesema huku akishangiliwa.

Pia amewataka wananchi wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia.  "Ukipewa risiti uiangalie kama ina kiwango halisi cha fedha uliyotoa. Kuna watu wachache wasio waaminifu wanaamua kukupa risiti lakini imeandikwa bei ndogo kuliko ile uliyolipia, ukitoa laki moja anakuparisiti ya sh 10,000."

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw.  Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana na ulikamilika Juni 12, mwaka huu. 

"Ujenzi wa jengo hili umegharimu sh. bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya walipakodi wa Chato kutoka watu 150 mwaka 2010/2011 hadi kufikia watu 600 mwaka 2016/2017", alisema. 

Pia alisema wamejenga ofisi hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA ambako ni umbali wa zaidi km.120.

Alisema hivi karibuni watakamilisha ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara, Iringa, ikiwemo kujenga ofisi kwenye mikoa mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe na Manyara. "Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa mpya wa kikodi wa Kahama," alisema. 

Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru. 

Alisema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya sh. trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo. 
Read More

MWINYIMVUA: VIJANA WASHIRIKISHWE KULETA MABADILIKO BARANI AFRIKAWatumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wameaswa kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia maadili na utendaji katika Utumishi wa Umma wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Dkt. Hamisi Mwinyimvua alipokutana na wafanyakazi wa ofisi yake Dodoma kwa lengo la kuiadhimisha Wiki hiyo inayofanyika kila mwaka kuanzia Juni 16-23 Barani Afrika ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni 

“Kuimarisha Ushirikishwaji wa Jamii katika Utoaji Huduma: Vijana washirikishwe kuleta Mabadiliko Barani Afrika”.

“Kila mtumishi wa umma anapaswa kuwa mwadilifu na mchapakazi hivyo niwaombe watumishi wote muwe mfano kwa kuwa waadilifu katika utendaji wenu kwa kuzingatia sheria zote za utumishi wa umma ili kuisaidia Serikali na kuwafikia wananchi kiujumla.”alieleza Dkt.Mwinyimvua

Katika kuiadhimisha wiki hii ya utumishi wa Umma ni wakati pekee wa kujitathimini eneo la kiutendaji na kuona maeneo yenye mapungufu ili yafanyiwe maboresho kwa haraka lengo likiwa kuondokana na mazoea yaliyokuwepo na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Issa Nchansi amewataka watumishi  kuzingatia mambo nane muhimu yaliyoainishwa katika Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma ikiwemo; Utoaji wa huduma bora, Utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, uwajibikaji kwa umma,kuheshimu sheria, matumizi sahihi ya taarifa na uadilifu sehemu ya kazi.

Naye, Katibu Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge) Bi. Maimuna Tarishi aliwaomba watumishi wote kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu kwa kuwawezesha vijana kielimu, kiuchumi na kijamii ili waweze kuzalisha na kuwa tegemeo la taifa.

“Niwaombe watumishi wote kuiangalia hili kundi la vijana wanaoajiriwa na Serikali kwa kuwatia moyo na kuwaunga mkono katika utekelezaji wa kazi zao” alisisitiza Tarishi

Sambamba na hili, Katibu Mkuu, Tarishi alisema  kuwa ili kuwe na utendaji wenye matokeo lazima kuitumia wiki hii kukumbushana majukumu na nafasi zetu katika kuitumikia serikali.

“Tuwe na utendaji wenye matokeo na si kuhesabu siku, miezi hadi mwaka bali tuwajibike kwa uadilifu kila muda tuwapo Serikalini.”
Read More

WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU WAASWA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU


Baadhi ya watumishi Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua (hayupo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika Ukumbi wa Mikutano ofisi hiyo Dodoma ili kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea Barani Afrika.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Issa Nchansi akieleza kanuni za maadili kiutendaji kwa watumishi wa ofisi hiyo wakati wa kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma walipokutana na watumishi wote Dodoma ili kujadili masuala ya kiutumishi Juni 22, 2017.

Mchumi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Novatus Tesha akisoma Kanuni za Maadili ya Utendaji Katika Utumishi wa Umma wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambapo ofisi hiyo imeadhimisha kwa kukutana na watumishi wake kujadili masuala ya msingi ya kiutumishi Juni 22, 2017.

Msaidizi wa Waziri Mkuu (Hotuba) Bw. Abdalah Mtibora akiuliza swali kwa Mwenyekiti wa mkutano (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma tarehe 22Juni, 2017.

Mhasibu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi.Kissa Mwakipesile akieleza hoja yake kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu ofisi hiyo Bw.Issa Nchansi (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Juni 22, 2017 Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Dodoma.

Afisa Tehama Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Innocent Mboya akifafanua jambo kwa washiriki wa mkutano wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Juni 22, 2017 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Dodoma.

Read More

Wednesday, June 21, 2017

MAJALIWA AFUTARISHA CHATO , AKIWA NJIANI AZUNGUMZA NA WANANCHI WA KIGONGO FERI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza  na wananchi wa eneo la Kigongo feri Wilaya ya Misungwi, wakati aliposimama kwa muda akiwa njiani kuelekea Chato kwa ziara ya siku mbili Juni 21,2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Meja Jenerali Mstaafu,  Ezekiel Kyunga wakati alipowasili mjini Chato mkoani Geita  Juni 21, 2017 kwa ziara ya siku mbili mkoani humo.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishiriki  katika swala ya magaharibi katika  futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu mjini  Chato, mkoani Geita, Juni 21, 2017. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifuturu pamoja na Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC)  Dayosisi ya Geita (kushoto) na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alhaj Yusuph Kabaju(kulia) katika futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli, mjini  Chato, mkoani Geita  Juni 21, 2017.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Meja Jenerali Mstaafu,  Ezekiel Kyunga wakati alipowasili mjini Chato mkoani Geita  Juni 21, 2017 kwa ziara ya siku mbili mkoani humo.

Read More

WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS MAGUFULI KWENYE FUTARI CHATO

*Ahimiza nyumba za ibada zisitumiwe vibaya    
           
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini wahakikishe nyumba zao za ibada hazitumiki kuleta migogoro. 

Ametoa ombi hilo jana usiku (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na mamia ya waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu pamoja na viongozi wa dini walioshiriki ibada ya futari wilayani Chato, mkoani Geita. 

Akizungumza na waumini hao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais alishapanga kufika Chato ili kushiriki nao ibada ya iftar lakini ametingwa na majukumu ya kitaifa akaona ni vema amtume yeye ili amwakilishe.

“Mheshimiwa Rais alishapanga kuja Chato kufuturu pamoja na wana-Chato lakini kadri siku zinavyozidi kwenda anajikuta anabanwa na majukumu mengi ikiwemo kukutana na wageni wa kimataifa, kwa hiyo akaona ni vema nije kumwakilisha katika shughuli hii,” alisema.

“Mheshimiwa Rais anawaombea heri katika siku zilizobakia za mfungo wa Ramadhan ili mmalize salama na Mungu akijalia muweze kusherehekea pamoja, na pia anawatakia heri wale watakaoendelea na sita tushawal.”

Akisisitiza kuhusu amani na utulivu nchini, Waziri Mkuu alisema: “Hatupendi kusikia kuwa msikiti fulani wamechapana viboko kwa sababu ya kugombea uongozi au kwenye kanisa fulani waumini wamepigana wakigombea mchungaji wao.”

“Tutumie nyumba zetu za ibada kudumisha amani na mshikamano wetu. Napenda niwahakikishie kuwa Serikali yenu chini ya Rais John Pombe Magufuli itaendelea kuheshimu dini zote.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini hao kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhan ni wa toba kwa kila muumini. “Huu mwezi mafundisho yake yanasisitiza amani, uvumilivu na kusameheana. Nipende kuwasihi kwamba tuendelee kudumisha utulivu tulionao,” aliongeza.

“Nipende kusisitiza kwenu wana-Geita na wana-Chato kwamba jukumu kubwa mlilonalo ni kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, busara na uongozi wa kimungu katika maamuzi yake. Niwasihi ndugu zangu Waislamu na Wakristo, tuendelee kuwaombea viongozi wote wa kitaifa kila siku ili wafanye kazi kwa kuongozwa na Mungu,” alisema.

Awali, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Sheikh Ally Moto alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa ya kuweza kushiriki ibada ya iftar pamoja na watoto yatima na wajane.

Alisema wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na ili kudumisha amani wilayani humo, waumini wa Kiislamu na Kikisto wameunda Kamati ya Amani ya wilaya hiyo inayojulikana kama Interfaith Committee

Naye Mbunge wa Chato ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alisema anamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuandaa futari hiyo ambayo imejumuisha wana Chato kutoka pembe nne za wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Geita, Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Geita alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais Magufuli na kuwapongeza viongozi wakuu wa kitaifa kutokana na utendaji wao unaogusa mioyo ya Watanzania.

“Ninyi wote watatu ni viongozi ambao Mungu amewaweka kuongoza nchi yetu. Katika miezi hii 18, mmefanya mambo makubwa, ni imani yetu kuwa ataendelea kuwaongoza katika utendaji kazi wenu,” alisema.

Akitoa shukrani, Sheikh wa Mkoa wa Geita, Sheikh Yusuph Kabaju ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa wana-Geita kujumuika pamoja katika futari hiyo na kuahidi kudumisha amani ya Tanzania.

“Tunakushukuru kwa kutuunganisha wana Geita katika futari hii japo umeamua kufanyia ibada hii hapa Chato. Maneno ya Quran tukufu yanasema malipo ya waliofunga anayapata pia yule aliyefuturisha waliofunga,” alisema.

Sheikh Kabaju pia alisoma dua ya kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli pamoja na viongozi wa kitaifa. Pia aliombea amani kwa ajili ya Taifa la Tanzania.

Read More

WAZIRI MKUU AMUAGIZA MKURUGENZI WA MISUNGWI AITISHE KIKAO KESHO SAA 4


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw. Eliud  Mwaiteleke  aitishe kikao na wananchi wa Kigongo na kutafuta ufumbuzi wa tatizo la eneo la kujenga soko. 

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi na wajasiriamali wanaotumia kivuko cha feri cha Kigongo waliokuwa wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema. 

"Mkurugenzi haya mambo ya mipango, mipango na kupanga hayaleti tija kwa wananchi. Hivi hamjui kuwa wananchi wanahitaji kuwa na soko katika eneo hili ili waweze kuuza mazao yao au samaki?"

"Ninakuagiza Mkurugenzi, kesho Alhamisi, saa 4 njoo na Afisa Biashara wako, Mwenyekiti wa kijiji na watu wako pamoja na Diwani wa hapa, itisheni kikao na muonyeshwe eneo la soko ili mliingize kwenye mipango yenu," alisema. 

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.

Awali, Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi huyo ili aeleze amejipanga vipi kwenye Halmashauri yake kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo. 

Akitoa majibu mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Mwaiteleke alisema hawajawahi kupata mpango kutoka kwenye kata hiyo na kwa hiyo akawasihi wananchi waibue mpango huo na kuuwasilisha kwenye Halmashauri ili wao waweze kutenga fedha za kujenga soko.

Mapema, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Bw. Sebastian Kisumo alimweleza Waziri Mkuu kwamba eneo hilo linakabiliwa na tatizo la soko pamoja na uhaba wa maji. 


Kuhusu maji, Waziri Mkuu alisema Serikali imetenga sh. bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao utasambaza maji kwenda Misungi,  Usagara hadi Kigongo Feri. 
Read More