Saturday, June 30, 2018

NHC MNA JUKUMU LA KUWAFIKIA WATU WA CHINI -MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina jukumu kubwa la kuhakikisha sekta hiyo inakua na kuwafikia watu wa kipato cha chini.

Amesema ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inahimiza uchumi wa viwanda, hivyo sekta ya nyumba ina mchango mkubwa sana katika kuchochea ukuaji wa viwanda.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 30,2018) wakati akizindua mradi wa Singidani Commecial Complex, mjini Singida. Jengo hilo la biashara na ofisi limejengwa na NHC kwa ajili ya kupangisha wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema sekta ya nyumba ni mtambuka kwa kuwa huchochea ukuaji wa uchumi, kutoa ajira na kukuza uwekezaji wa viwanda vya vifaa vya ujenzi kama saruji, mabati, nondo, marumaru na vinginevyo, ambavyo  vinafungua fursa kubwa ya ukuaji wa viwanda.

Hivyo, Waziri Mkuu amesema wadau mbalimbali wanapaswa kuitazama sekta ya nyumba kama sekta mtambuka katika kuleta maendeleo endelevu ya uchumi na jamii kwa ujumla.

“Napenda kutoa pongezi kwa Shirika la Nyumba la Taifa kwa kujenga jengo hili zuri na la kisasa kabisa hapa mjini Singida. Vilevile, jengo hili limeboresha na kupendezesha mandhari ya mji wa Singida kwa kiwango kikubwa kabisa,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema amefurahi kusikia jengo hilo limesanifiwa na ujenzi wake kusimamiwa na Watanzania wenyewe, wakandarasi washauri wakiwa ni NHC wenyewe na kwamba Watanzania zaidi ya 600 walipata ajira wakati wa ujenzi.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Felix Maagi alisema mradi wa jengo hilo la ofisi na biashara la Singidani lililogharimu sh. bilioni 3.4 ulianza Januari 26, 2015 na kukamilika Februari 17, 2018 na linatarajia kuliingizia shirika pango ya sh. milioni 420 kwa mwaka. Tayari asilimia 50 ya jengo hilo  limepangishwa.

Mkurugenzi huyo alisema mbali na mradi huo wa Singidani, pia shirika limeendelea kukua na kuimarika katika utendaji wake ambapo thamani ya mali zote imeongozeka kutoka sh. trilioni 1.7 mwaka 2011 mpaka kufikia sh. trilioni 4.8 mwaka 2018.

Bw. Maagi alisema mapato ya shirika yamekua kutoka sh. bilioni 40 kwa mwaka 2011 hadi kufikia sh. bilioni 154 mwaka 2018.” Pia shirika linalipa gawio la Serikali kila mwaka na gawio hilo limekua kutoka sh. milioni 250 mwaka 2011 hadi sh. bilioni 1.2 kwa mwaka 2018,”

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, wabunge wa mkoa wa Singida, viongozi wa dini na maafisa wa Serikali.
Read More

MAJALIWA AFUNGUA JENGO LA BIASHARA LA NHC LA SINGIDANI MJINI SINGIDA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Viongozi wa Dini wakati alipowasili kwenye viwanja vya Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida, kufungua jengo hilo Juni 30, 2018. Kulia ni Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida,  Issa Ramadhani Simba na watatu kulia ni Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida.

Baadhi ya wananchi na wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza kabla ya kufungua Jengo la Biashara la NHC la Singidani mjini Singida Juni 30, 2018.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Felix Manyama Maagi akisoma taarifa ya Shirika hilo mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika tukio la ufunguzi wa Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na NHC mjini Singida Juni 30, 2018.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema  Nchimbi akitoa salamu za mkoa mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika tukio la  ufunguzi wa Jengo la Biashara la Singidani lililopo Singada mjini Juni 30, 2018.

Kikundi cha Kwaya cha Polisi Jamii cha Mjini Singida kikiimba mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  katika uzinduzi wa Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida Juni 30, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati alipofungua Jengo la Biashara la Singidani lilijengwa na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) mjini Singida Juni 30, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika  la Nyumba la Taifa  (NHC) mjini Singida Juni 30, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la  Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida Juni  30, 2018.  Watatu kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi. Watatu kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Felix Manyama Maagi na kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum Neema Mgaya.  Wanne kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida Juma Kilimba na wapili kulia ni Mbunge wa Singida Mjini Mussa Sima. (

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakimsikiliza, Kaimu Mkurugenzi wa Ubunifu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Margaret Ezekiel wakati alipotoa Maelezo kuhusu Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na NHC mjini Singida na kufunguliwa na Waziri Mkuu Juni 30, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wabunge walioshiriki katika ufunguzi wa Jengo la Biashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) la SIngidani mjini Singida Juni 30, 2018. Waliokaa, watatu kushoto ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Watano kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, Wasita kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Juma Kilimba na  kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Felix Manyama Maagi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi baada ya kufungua Jengo la Biashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida, Juni 30, 2018.

Read More

MAJALIWA AFUNGUA JENGO LA BIASHARA LA NHC SINGIDA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (kushoto) wakifurahia baada ya Waziri Mkuu kufungua Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) mjini Singida Juni 30, 2018. Kulia ni Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima na wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Juma Kilimba.

Read More

OFISI YA WAZIRI MKUU YASHIRIKI KATIKA BONANZA LA SHIMIWI JIJINI DODOMA

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifanya mazoezi ya viungo kabla ya kuingia katika mchezo wa mpira wa miguu wakati wa Bonanza la SHIMIWI lililofanyika Juni 30, 2018 Jijini Dodoma.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifanya mazoezi ya viungo kabla ya kuingia katika mchezo wa mpira wa miguu wakati wa Bonanza la SHIMIWI.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifanya mazoezi ya viungo kabla ya kuingia katika mchezo wa mpira wa miguu wakati wa Bonanza la SHIMIWI.

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Matamwe Jimmy akiwapongeza wachezaji na washiriki wa michezo ya Bonanza walioshiriki katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Mmoja wa wachezaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Alex Ndimbo akisubiri kupokea pasi ya mpira wakati wa mechi kati yao na Timu kutoka Wizara ya Kilimo wakati wa Bonanza la SHIMIWI lililofanyika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakishangilia mara baada ya timu yao kutoka sare kwa bao moja na Timu ya Wizara ya Kilimo wakati wa Bonanza la SHIMIWI lililofanyika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Nigel Msangi Msangi (waliosimama mwenye koti jeusi) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi yake mara baada ya kumalika kwa Bonanza la SHIMIWI Jijini Dodoma.

Read More

Friday, June 29, 2018

TANZANIA NI KIMBILIO KWA WALIOKOSA AMANI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuvumiliana na kustahamiliana ndiko kunakolifanya Taifa la Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na kimbilio la wale waliovurugikiwa na amani katika nchi zao. 

Kadhalika, uwepo wa amani nchini si tu unatoa fursa ya kutekeleza majukumu ya kiuchumi na kijamii bila hofu bali pia ni sababu muhimu ya wenzetu wengine kutoka nje kuona fursa ya kuwekeza na kushirikiana nasi katika kujenga maendeleo ya nchini. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 28, 2018) wakati akizindua Umoja wa Kimataifa wa  Wabunge Wapenda Amani tawi la Tanzania (IAPP), kwenye mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa Bungeni, jijini Dodoma.

Amesema amani na utulivu ni tunu kubwa sana katika jamii yoyote ile Duniani na Tanzania muda wote imeendelea kuenzi tunu hiyo iliyojengwa kwenye misingi imara kupitia waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Shirikisho la Amani kwa Wote  (Universal Peace Federation (UPF), ambalo lilianzishwa kwa lengo la kumkomboa binadamu kutoka katika udhalili wa kukosa mahitaji muhimu. 

“Hili linadhihirika kupitia mipango ya shirikisho hilo ya kushirikiana na jamii nyingine katika kuimarisha sekta zenye kugusa maisha ya watu wengi kama vile kilimo, mazingira, afya, elimu, miundombinu na nyinginezo,” amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mipango hiyo utategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na utulivu katika jamii husika, ambapo amewahakikishia kwamba Serikali ipo tayari na itaendelea kushirikiana nao katika nyanja hizo za kijamii na maeneo mengine kwa ajili ya kulinda maslahi ya pande zote mbili na kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nitoe rai kwa Waheshimiwa Mawaziri wa sekta husika kwamba hakikisheni mnaanzisha mazungumzo na wawakilishi wa UFP nchini kwa lengo la kuona namna nzuri ya kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia shirikisho hilo hususan katika sekta za kilimo, elimu, afya, mazingira na miundombinu,” amesema. 

Awali, Mwenyekiti Mwanzilishi wa IAPP, Bw. Mussa Ntimizi amesema Shirikisho la Amani kwa Wote  litasaidia nchi kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo kama ya kilimo, afya kwa sababu hakuwezi kuwa na amani bila maendeleo.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Bw. William Ngeleja amesema Shirikisho la Amani kwa wote  limetenga dola bilioni tatu kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya katika nchi 10 za Bara la Afrika na Tanzania ikiwemo.

Katika hafla hiyo Waziri Mkuu amepewa tuzo ya Balozi wa Amani na Mwenyekiti wa Shirikisho la Amani kwa Wote (UPF), Dkt. Thomas Walsh. Viongozi wengine walipewa tuzo hiyo ni pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo,Bw. William Ngeleja Katibu Msaidizi wa umoja huo Bibi Anna Lupembe, Mweka hazina Bibi Ritta Kabati.

Baada ya kukabidhi tuzo hizo, Dkt. Walsh shirikisho lao linahitaji kufanya kazi nna Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia kwa ajili ya kuboresha maendeleo na amani. Amesema katika Taifa kukiwa na maendeleo amani lazima itakuwepo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Shirikisho la Amani kwa Wote (UPF), Dkt. Thomas Walsh, Katibu wa Shirikisho la Amani kwa Wote Kanda ya Afrika (UPF_Afrika), Bw. Adama Doumbia, Katibu wa Shirikisho la Amani kwa Wote Tanzania (UPF_Tanzania), Bw Stylos Simbamwene, 

Read More

SERIKALI YATENGA 4.3bn/- KUJENGA VITUO VYA KUHIFADHI DAMU SALAMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 4.3 ili kujenga vituo vya kuhifadhi damu (satellite blood banks) kwenye mikoa 12.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Njombe. Mingine ni Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 4, mwaka huu.

Amesema lengo la mpango huo ni kuboresha upatikanaji wa damu hasa kwa akinamama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. “Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara, wodi za wazazi, nyumba za watumishi na wodi za watoto,” amesema.

Amesema kukamilika kwa majengo hayo, kutaboresha huduma za uzazi kwa akinamama na watoto wachanga. “Hatua hii itawezesha upatikanaji wa huduma kamili za uzazi na kupunguza vifo vya mama na watoto. Katika mwaka 2018/2019, eneo litakalopewa kipaumbele ni kuimarisha upatikanaji vifaa na watumishi katika vituo 208 vinavyoendelea kuboreshwa,” amesema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi watumishi wa afya, waongeze juhudi ya kuhamasisha wananchi wajitolee damu na pia akawaomba wananchi nao wawe na utamaduni wa kuchangia damu ili kuwezesha upatikanaji wa damu salama itakayohifadhiwa kwenye benki hizo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa nchini kwa kutenga shilingi bilioni 14 ili kuanzisha huduma ya kuchunguza mwili bila upasuaji (PET Scan) katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road. 
Amesema kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hicho na kwamba Serikali itaweza takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kulipia wagonjwa waliokuwa wakienda nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hiki.

Amesema Serikali itasogeza huduma ya tiba ya saratani katika ngazi ya Hospitali za Kanda ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya Kanda ya Kaskazini KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, jijini Mbeya.

“Vilevile, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa tiba na madaktari bingwa. Jumla ya shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha hospitali hizi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for Results - EP4R) itaimarisha miundombinu kwenye shule zenye uhitaji mkubwa.

“Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatumia shilingi bilioni 155.58 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe 25, ununuzi wa vifaa vya maabara, ujenzi wa mabwalo 85, vyumba vya madarasa 2,000 na motisha kwa Halmashauri kutokana na ufanisi katika utekelezaji wa vigezo vya EP4R,” amesema.

Amesema kwa sasa, Serikali inatarajia kuajiri walimu 4,785 wa shule za msingi zenye uhitaji mkubwa na kwamba tayari imeshatangaza nafasi za ajira kwa walimu 2,000 wa masomo ya sayansi, hisabati na lugha ambao watapangwa kwenye shule za sekondari zenye uhitaji mkubwa.

Amesema kuwa Serikali imetangaza nafasi za ajira kwa mafundi sanifu maabara 160 ambao nao pia watapangwa kwenye shule zenye uhaba wa wataalamu hao.
Read More

TANZANIA YAONGOZA KWA WANYAMA PORI AFRIKA

*Ni baada ya Serikali na wananchi kulinda rasilimali za nchi 

IMEELEZWA kuwa jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za nchi na ushirikiano kutoka kwa wananchi zimesababisha ongezeko kubwa la idadi ya wanyama pori, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye wanyama wengi barani Afrika. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa bungeni wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma. 

Amesema ili kuitumia vema fursa ya kuwa na vivutio vingi ikiwemo wanyamapori wengi na kuleta tija kwa nchi, Serikali imeendelea kuandaa utambulisho wa Tanzania Kimataifa (Destination Branding), lengo likiwa ni kuitambulisha Tanzania kama kituo mahsusi cha utalii duniani.

“Tunalenga kuvutia wageni wa kimataifa waje kuitembelea Tanzania, kuongeza wigo wa kutangaza vivutio na kufanya vivutio vya utalii vifahamike duniani. Pia, Serikali inakamilisha mchakato wa kuanzisha Channelmaalum katika Television ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema maandalizi ya kuanzisha studio ya kutangaza utalii kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea vizuri, ambapo studio hiyo itawezesha kutambua, kufuatilia na kuwasiliana moja kwa moja na watu wanaofuatilia Tanzania na vivutio vyake.

Pia, Serikali inakusudia kuanzisha chombo kitakacho simamia fukwe za bahari, mito na maziwa lengo la hatua hiyo ni kuimarisha utalii wa fukwe Bara na Visiwani kwa kujenga hoteli, maeneo ya mapumziko na michezo mbalimbali. 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya migogoro ya matumizi ya ardhi miongoni mwa watumiaji kwa kuunda timu ya kisekta ikijumuisha watendaji wa sekta mbalimbali zinazohusika kwenye masuala hayo. 

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kupima mipaka ya vijiji, kutunga na kurekebisha sera, sheria na kuandaa mipango mbalimbali ya kuboresha matumizi na utawala wa ardhi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa mipango ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. “Ni matumaini yangu kwamba programu hii ikitekelezwa, ardhi itatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na pia kudhibiti migogoro ya ardhi,”. 

Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali itaendelea kutatua migogoro inayojitokeza na pia kutoa elimu kwa umma ili watumiaji wote wa ardhi waweze kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa katika vijiji. 

Amesema katika juhudi za kudhibiti migogoro kwenye maeneo mbalimbali ya utawala, jumla ya vijiji 11,256 kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini vimepimwa, hiyo ni sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote, huku lengo likiwa ni kupima mipaka ya vijiji vyote na kuvipatia vyeti vya kijiji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo. 

“Hatua hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji. Ili kuharakisha kasi ya upimaji nchini, Serikali itaendelea kutumia makampuni binafsi ya upimaji na upangaji makazi kwa vibali maalum,”.

Akizungumzia kuhusu hifadhi ya mazingira, Waziri Mkuu amesema misitu inaendelea kukatwa hovyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya mkaa na kuni, ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kote nchini.

Amesema Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu mahsusi wa kuwawezesha na kuwaratibu wajasiramali wanaojishughulisha na nishati mbadala ili kuwa na uzalishaji wa kutosha wa nishati hiyo na iweze kusambazwa katika maeneo yote nchini. 

Aidha, Serikali itaendelea kuboresha na kukamilisha Mkakati wa Tungamotaka (National Biomass Energy Strategy) na kusambaza kwa wadau nchini ili kuratibu vyema upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo. 

Read More

SERIKALI YAWATAKA WATENDAJI KUWAJIBIKA

*Ni katika ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali katika ngazi zote wawajibike ipasavyo kwenye ukusanyaji wa mapato na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha na rasilimali za Taifa. 

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaimarisha ukaguzi katika ngazi zote na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba miradi na kazi zitakazofanyika zinawiana na thamani ya fedha (Value for money) za umma zinazotolewa na Serikali.  

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa bungeni wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma. 

Vilevile, Waziri Mkuu amesema taasisi zote za Serikali zinasisitizwa kutumia mifumo ya kieletroniki kukusanya mapato na wafanyabiashara wote wanahimizwa kutumia mashine za EFD na kulipa kodi kwa hiari.

Amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba malengo ya ukusanyaji wa mapato na matumizi yanazingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. “Viongozi na watendaji wote wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma katika eneo la ukusanyaji wa mapato,”. 

Waziri Mkuu amesema Serikali itasimamia ipasavyo utekelezaji wa bajeti sambamba na kuongeza uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha zilizoelekezwa katika vipaumbele mbalimbali kama ilivyoidhinishwa na Bunge. 

Amesema katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali itashirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote kwa ujumla ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, sh. trilioni 20.47 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya Bajeti na sh. trilioni 12.01, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau wa kilimo, mifugo, uvuvi na sekta nyingine watumie fursa mbalimbali zinazopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDPII),ili kutimiza ndoto ya Taifa kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Aidha, Waziri Mkuu ameziagiza taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa  ASDP II, ziimarishe usimamizi na ufuatiliaji ili utekelezaji wa mpango huo uwe na mafanikio makubwa.

Amesema mpango huo unaweka mkazo katika maeneo makuu manne, ambayo ni usimamizi endelevu wa matumizi ya ardhi na maji katika kilimo; kuongeza tija na faida katika kilimo, mifugo na uvuvi; kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza thamani ya mazao na kuwajengea uwezo wadau wa sekta katika uratibu, ufuatiliaji na tathmini.

Juni 4, 2018, Rais Dkt. John Magufuli alizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II), ikiwa na lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika mnyororo wote wa thamani ili kuvipatia malighafi viwanda vitakavyoanzishwa na kupata ziada ya  kuuza katika masoko ya nje ya nchi na kupata faida kubwa
.

Read More

MUHOGO SASA RASMI KWENYE MAZAO YA BIASHARA-MAJALIWA

*Ni baada ya kupata soko kubwa nchini China 
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya China imetoa fursa ya kufungua soko la muhogo mkavu kutoka Tanzania, tukio ambalo  linafungua ukurasa mpya wa zao la muhogo kuwa miongoni mwa mazao ya biashara. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodomakatika hotuba yake aliyoitoa wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge. 

Amesema ili kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na fursa hiyo, Mei, 2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China.  

Amesema kufuatia hatua hiyo, mwezi huu wa Juni 2018, tani 74 za muhogo mkavu kutoka Tanzania zimeingia China kupitia Bandari ya Qingdao iliyopo katika jimbo la Shandong. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kiasi cha muhogo kilichofanikiwa kuingizwa katika soko la China bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ambayo yanazidi tani 150,000 kwa mwaka. 

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wachangamkie fursa ya kilimo cha muhogo ambacho kimeonesha kuwa na tija kubwa, pia amevitaka vituo vya utafiti wa kilimo viwawezeshe wakulima kupata mbegu bora na mbinu za kisasa ili waongeze uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko hilo. 

Waziri Mkuu amesema kutokana na zao la muhogo kuonekana kuwa na matumizi menginezaidi ya chakula, Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuchakata muhogo na kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwamba umekuwa na mafanikio katika maeneo mengi nchini kwa sababu wakulima wadogo na wa kati wapo kwenye ushirika, hivyo kuwa na nguvu ya soko na bei nzuri ya mazao yao. 

“Mathalani, kwa kutumia mfumo huo, mwezi huu bei ya ufuta imeongezeka kutoka shilingi1,500 hadi shilingi 2,800 kwa kilo na kuua mfumo usio rasmi wa uuzaji wa zao hilo ujulikanao kama ‘chomachoma’ ambao  ulimpunja mkulima kwa ujazo na bei,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema mfumo huo unasaidia kuzuia upotevu wa mazao unaotokana na uhifadhi dhaifu, pia unasaidia kuhifadhi mazao ili kusubiri kuuza wakati muafaka na kuyaongezea thamani mazao kabla ya kuyauza. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa mfumo huo unatekelezwa kikamilifu na kuleta tija kwa wakulima. 

Amesema hatua hizo ni pamoja na ushirikishwaji wa wadau, kuimarisha ushirika, kuweka miundombinu ya masoko na kuboresha muundo wa taasisi na vitendeakazi vya Bodi ya Stakabadhi za Ghala. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watendaji Serikalini kuhakikisha kuwa mazao mengi zaidi yanaingizwa katika stakabadhi za ghala ili kuwe na tija kwa wakulima.
Read More

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA AKISOMA HOTUBA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA 11 WA BUNGE JIJINI DODOMA

Bendi ya JKT Makutupora ikiongoza  Wimbo wa Taifa wakati Bunge lilipoahirishwa  jijini Dodoma Juni 29, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipiga makofi baada ya Bendi ya JKT Makutopora kuongoza Wimbo wa Taifa wakati wa kuahirisha  Mkutano wa 11 wa Bunge  jijini Dodoma Juni 29, 2018. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Madini,  Angela Kairuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mahagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa  11 wa Bunge,  jijini Dodoma Juni 29, 2018.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa  11 wa Bunge,  jijini Dodoma Juni 29, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipongezwa na baadhi ya wabunge baada ya kusoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma Juni 29, 2018.

Read More

RAIS AAGIZA SH. MILIONI 308 ZITUMIKE KUBORESHA BARABARA

*Ni zile zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Mashujaa 

RAIS Dkt. John Magufuli ameagiza sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha  miundombinu ya barabara jijini Dodoma.

Ametaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari  katika barabara ya Kisasa na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya Emmaus-African Dream yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha lami.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu leo (Ijumaa, Juni 29, 2018), wakati akizindua kituo cha polisi kinachohamishika katika hafla iliyofanyika eneo la Kisasa, jijini Dodoma. Kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huadhimisha siku ya mashujaa. 

“Sasa kutokana na msongamano uliopo ambao unaweza kusababisha ajali, Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Magufuli ameamua fedha zote zilizoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zitumike kuboresha barabara,” amesema

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt Magufuli anawataka  Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika  maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.

Kufuatia uamuzi huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mkoa waratibu zoezi hilo kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameliagizaJeshi la Polisi lianze kujikita kwenye matumizi ya mifumo ya kiulinzi ya kielektroniki yaaniCity Surveillance Sytemsili limudu kudhibiti hali ya sasa ya uhalifu. 

Amesema kutokana na kuwepo kwa mapinduzi makubwa ya kiteknolojia duniani, hususani kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo eneo la ulinzi wa raia na mali zao, hivyo ni wakati muafaka sasa kwa Jeshi la Polisi lianze kutumia teknolojia za kisasa.

“Usimikaji wa mifumo hiyo si tu utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao lakini pia utaongeza imani kwa wafanyabiashara na watalii wanaotembelea nchi yetu,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amewasisitiza wakazi wa eneo hilo kukitumia vizuri kituo hicho ni kwa kupeleka taarifa za uhalifu. “Aidha, naomba niwasisitize kituo hiki ni cha muda, hivyo  uongozi wa eneo hili ni lazima uje na mkakati wa kupata kituo cha kudumu,”.

Ufunguzi wa kituo hicho ambacho ni kati ya vituo vitano vilivyogharimu sh. milioni 250 vilivyotolewa na Benki ya Equity mkoani Dodoma; umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.

Wengine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Giles Mroto na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Equity, Joseph Iha.
Read More

MAJALIWA AZINDUA KITUO CHA POLISI KINACHOHAMKISHIKA , ENEO LA KISASA JIJINI DODOMA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza wakati alipozindua Kituo cha Polisi kinachohamishika katika eneo la Kısasa jijini Dodoma, Juni 29, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni (wapili kushoto) na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (kushoto) baada ya kuzindua Kituo cha Polisi kinachohamishika kwenye eneo la Kısasa jijini Dodoma Juni 29, 2018. Wengine pichani kutoka kulia ni Meya wa Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Giles Mroto na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni akizungumza kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  katika tukio la kuzindua Kituo cha Polisi kinachohmishika, eneo la Kisasa jijini Dodoma Juni 29, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Kituo cha Polisi kinachohamishika  katika eneo la Kısasa jijini Dodoma, Juni 29, 2018.   Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambno ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni na wapili kulia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity, Joseph Iha baada ya kuzindua Kituo cha Polisi kinachohamishika kilichojengwa kwa ufadhili wa benki hiyo eneo la Kisasa jijini Dodoma Juni 29, 2018.


Baadhi ya wananchi wa Dodoma wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza kabla ya kuzindua Kituo cha Polisi kinachohamishika, eneo la Kisasa jijini Dodoma Juni 29, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Askari wa Jeshi la Polisi,  E8687 Koplo Martin (kushoto) kuhusu pikipiki zilizokamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma kuwa ziliibwa.  Watatu kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde na wasita kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani yaNchi, Mhandisi Hamadi Masauni.
Read More