Thursday, March 20, 2025

WANANCHI WAKUMBUSHWA KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA ALAMA ZA TAIFA.


Wito umetolewa kwa Wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya Alama za Taifa ikiwemo Ngao ama Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa na Wimbo wa Taifa na kuendelea kujifunza matumizi sahihi ya alama hizo pamoja na matumizi  ya Gazeti la Serikali

Hayo yamesemwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bw. George Lugome kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha Habari Jijini Dar es Salaam.

Bw. Lugome amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na upotoshwaji wa Alama za Taifa na kukumbusha kuwa Alama hizi zipo kwa mujibu wa sheria “Na yeyote atakayechezea alama hizi atapata adhabu kwa mujibu wa sheria na adhabu yake kwa yeyote anayekiuka atatumikia kifungo cha miaka miwili Jela ama faini,ama vyote viwili kwa pamoja, ambapo sheria hii ya mwaka 1964 ipo kwenye mchakato wa kubadilishwa.” Alisisitiza.

Akizungumza kuhusu Nembo ya Taifa, Bw. Lugome alisema kuwa Nembo hiyo, ipo kwa Matumizi ya shughuli za Serikali pekee na sheria imesema Wazi, na aliongeza kwa kusema kuwa matumizi ya alama za Taifa ambayo siyo sahihi yanaharibu Haiba ya Taifa na Idara ya Mpiga Chapa ndo yenye jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa matumizi ya Alama hizi yanatumika kwa usahihi.

Aidha, Bwana Lugome Alifafanua kuwa uchapishaji holela wa alama hizi na  uchoraji wa nembo hizi kuonesha ubunifu wao, unachangia upotoshwaji na kuharibu uhalisia wake.

Kwa Upande wa Bendera ya Taifa, Bw. Lugome Alizungumza na kutolea ufafanuzi kuhusu rangi nne za Bendera ya Taifa zinazotumika

Akizungumzia Wimbo wa Taifa, Bw. Lugome alisema Wimbo wa Taifa Unavyoimbwa lazima uimbwe kwa beti zote mbili na kufuata Ala zilizowekwa na kusimama kikakamavu ambapo ni hali ya kuonesha utamaduni na Uzalendo kwa Taifa hili.

Kwa upande wa Gazeti la Serikali alisema kuwa, ni jarida Linaloratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na Kuhaririwa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, ambapo linachapishwa mara moja kwa wiki na kujikita katika kutoa taarifa Muhimu za Serikali hususan Utendaji wa Serikali na Taarifa Binafsi, na Jarida hili lipo kwa Mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, na kanuni za kudumu za Utumishi wa umma kanuni C27-30

 

Read More

Monday, March 17, 2025


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema Tanzania imebahatika kuongozwa na viongozi wanaojali utu na kutanguliza maslahi ya taifa mbele hivyo tunamshukuru Mungu kwa kuwafanya sehemu ya historia kwa sababu taifa linaendelea kushuhudia mazuri waliyofanya kwa ajili ya nchi.

 Waziri Lukuvi  ametoa kauli hiyo  wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mt. Yohaba Maria Muzevi Chato.

 “Leo tunadhimisha miaka Minne tangu tondokewe na mpendwa wetu Hayati Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli, kwa hali ya kibinadamu si rahisi kusahau kumbukumbu ya kuondokewa na mpendwa wetu kwa jamii inayomfahamu na kujumuika naye katika maswala mbalimbali ya kitaifa”.

 Aidha, amebainisha kuwa, Hayati Ally Hassani Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa uhai wake aliwahi kusema, “maisha ya mwanadamu ni hadithi tuu, basi ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa wale watakaosimuliwa”, hii inamaanisha viongozi waliopita wameishi vyema na ndio maana tuna ujasiri wa kusimulia yaliyomema katika kumbukizi zao na kuendelea kusimulia yaliyofanywa na Hayati Dkt, John Pombe Magufuli.

 “Hayati Dkt, John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi aliyejali watu na rasilimali za nchi yake na mchamungu hivyo tutaendelea kushirikiana na familia katika kumuenzi, kumuombea na kutangaza mema aliyoyafanya katika jamii na kama baba wa familia na kiongozi wa taifa letu,” alieleza.

 Aidha, Waziri Lukuvi amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa karibu na familia tangu wakati wa uhai wa mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mpaka sasa.

 “Upendo na ukaribu wake kwa familia umedhihirishwa kwa mambo mengi, mambo mengine tunayaona na yapo mengine familia wanayajua na sisi wengine hatuwezi kuyaona ndio maana katika matukio muhimu kama haya familia imekuwa ikimualika moja kwa moja, na Rais Dkt Samia Suluhu Hassani amekuwa akiitikia mialiko hiyo kwa kushiriki yeye mwenyewe au kutuma miongoni mwa wasaidizi wake kuja kumuwakilisha pale anapokuwa na majukumu mengine ya kitaifa” alisema Waziri Lukuvi.

 Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amesema Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania aliyeshika kijiti ameendeleza yale yote yaliyoanzishwa na Dkt. Magufuli na tumeshuhudia miradi mingi ikikamilika, mingine ikiwa katika hatua ya kuelekea ukamilifu na miradi mingi imeanzishwa kwa mwenendo ule ule na fikra zilezile kwa slogani yake kazi iendelee.

 “Ni adhima ya Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu kuwaenzi viongozi wakuu wa kitaifa waliomtangulia na hatuna budi kuwaenzi viongozi hao kwa vitendo katika utendaji washughuli zetu, hivyo ni wasihi tuendele kumuombea ndugu yetu Hayati, John Pombe Magufuli na familia yake ikiongozwa na mama Janeth Magufuli”

“Tuendelee pia kumuombea Rais wetu wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuliongoza taifa kwa utulivu na amani kama tunavyoshuhudia sasa Tanzania imetulia kwa sababu Mkuu wa Nchi anafanya kazi kwa niaba ya Watanzania wote,” alibainisha.

 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela amemshukuru mama Janeth Magufuli kwa jinsi alivyoweka utaratibu wa kumkumbuka Hayati John Pombe Magufuli lakini pia amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza misingi ya amani na utulivu.

 “Tuendelee kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aendele kuliongoza taifa kwa utulivu, amani na maendeleo kama tunavyoshuhudia sasa Tanzania ikiwa imetulia,” alihimiza

Nae, Askofu wa Jimbo katoliki Rulenge Ngara Mhashamu Severine Niwemugizi amesema Kanisa Katoliki lina utamaduni wa kuwakumbuka marehemu wote, ambao pia ni desturi ya kujifunza kutokana na maisha yao.

 “Tunajua Hayati Dkt, Magufuli alipenda nidhamu katika utumishi wa umma na kuwajibika ikiwa ni pamoja na kukata mambo mabaya rushwa, unyanyasaji na uonevu hivyo tuandike kitabu chetu tukiwa tunaishi, ili tukimaliza kuandika kiwe na kurasa zenye mambo mazuri tuweze kujifunza na yale mambo mabaya tuachane nayo,” alieleza.

 Akizungumza kwa niaba familia Bi, Jesca Magufuli, amemshukuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuunga mkono na kudumisha maono ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

 “Miaka minne iliyopita alipotembelea hapa Chato alituahidi kama familia kwamba hata tuacha na leo tunashuhudia uaminifu wake katika kutekeleza ahadi zake,” alisema Bi. Jesca.



Read More

Friday, March 14, 2025

“WATENDAJI OFISI YA WAZIRI MKUU ENDELEENI KURATIBU VYEMA TAARIFA ZA UTEKELEZAJI WA SERIKALI KWA MANUFAA YA TAIFA” WAZIRI LUKUVI


Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wamehimizwa kuratibu vyema taarifa za utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita na kuzisemea kazi hizo kwa wananchi ilia wapate uelewa wa uhakika wa miradi ya maendeleo iliyofanywa na Serikali katika maeneo yao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uaratibu) Mheshimiwa William Lukuvi wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi la Ofisi ya Waziri Mkuu, katika Ukumbi wa Ngome Jijini Dodoma.

Ameongeza kusema Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wana majukumu makubwa hivyo wanapaswa kuwa kioo katika utekelezaji wa kazi vizuri na usimamizi wa shughuli za Serikali ili waweze kuratibu taarifa za mafanikio kwa wananchi.

“Tunalo jukumu la kuwaambia wananchi kazi zilizofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi na kwa kuzipambanua vizuri ikiwa ni sehemu ya uratibu ili wananchi wazijue kwa uhakika huko waliko,” alieleza Waziri.

Ili tuweze kuratibu lazima majukumu yaliyo ndani ya Ofisi yetu yaweze kusimamiwa vizuri sana kwa kuwa mfano katika idara zetu ili tuweze kusimamia idara na taasisi zilizo nje vizuri.

Amefafanua, Waziri Mkuu anaamini kwamba watendaji wa Ofisi yake wapo na wanamsaidia katika jukumu kubwa la kuratibu shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nikupongeze tena Katibu Mkuu Dkt. Yonazi kwa usimamizi mzuri na timu ya menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tuendele kushirikiana katika kufanya kazi lakini niwapongeze Wakuu wa Idara na Vitengo nimewatembelea mnafanya vizuri sana,” alisema Waziri.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi ameshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo kwa miongozo mizuri wanayotoa ili kuweza kutimiza majukumu ya kila siku.

“Viongozi wetu Wakuu wanafahamu kazi ambazo tumekuwa kukizifanya na kwa kupitia nyie tunaomba mtufikishie salamu za shukrani kwao,” alieleza

Naye Msaidizi wa Katibu wa (TUGHE) Mkoa wa Dodoma Bi, Maisha Mbilla amesema wanafahamu kwamba watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri na wanapata stahiki zao vizuri, na kuupongeza uongozi wa Ofisi hiyo.

“Hii inatutia faraja na moyo na tuna wajibu kama Chama Cha Wafanyakazi wakuongea na watumishi ili waendelee kufanya kazi kwa kufuata sheria kanuni na taratibu pamoja na miongozo ya Utumishi wa Umma,” alihimiza



Read More

Thursday, March 13, 2025

MIFUMO RAFIKI YA UPATIKANAJI WA NYARAKA IWEKWE KUWAFIKIA WANANCHI KWA WAKATI

 


Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali yatakiwa kuweka mifumo mizuri ya usambazaji wa nyaraka za wazi kwa wananchi kupitia mifumo ya kidigitali na hata kwa mifumo ya nyaraka ngumu ili wananchi wanufaike na taarifa hizo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe William Lukuvi alipofanya ziara katika Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Jijini Dodoma t ambapo amejionea maendeleo ya ujenzi na ufungaji wa mitambo mipya ya uchapishaji wa nyaraka za serikali.

Amesema, nyaraka nyingi na muhimu huchapwa kwenye Gazeti la Serikali hivyo mkiongeza uelewa kwa wananchi juu ya namna ya kulipata Gazeti la Serikali inarahisha taarifa hizo muhimu kufikia walengwa.

“Tunaweza kufanya jitihada hizi za kusambaza taarifa la Gazeti la Serikali kupatikana katika shule kwa njia za kidigitali kupita mifumo ya computa ambazo zimeanza kutumika katika utoaji wa elimu ili wanafunzi waweze kuzipata,” alifafanua

Nitoe rai kwa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali hasa kwenye nyaraka ambazo ni za wazi fanyeni uelimishaji ili taarifa Magazeti ya Serikali ziweze kuwafikia wananchi.

“Tunaamini Serikali kwa kununua mitambo hii ya kisasa itasaidia Watendaji wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kujiweka sawa kimafunzo na maadili ili utunzaji wa nyaraka na siri uzidi kuimarika,” alisisitiza

Hivyo basi Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali inaendelea kuwa  mhimili Mkuu wa Serikali kwa miaka yote katika uchapishaji wa nyaraka za Serikali hasa zinapokuwa nyaraka nyingi na nyeti na zinahitajika kwa uharaka.

Kwa upande wake Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bw. George Lugome amesema wanatengeneza mfumo wa mtandao ambao utamsaidia mteja kujaza taarifa zake na kufanya malipo kwa njia ya mtandao na tangazo kutoka katika gazeti la serikali.

Ameongeza kusema “mfumo wa mtandao hauhusiki taarifa za mirathi ambazo uwasilishaji wake unahitaji Mhusika kuleta vielelezo vyake vya uthibitisho kwa mujibu sheria.”

Mpiga Mchapa amesema, kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika ununuaji wa mashine za kisasa utasaidia katika kuongeza uzalishaji na kuongeza maduhuli ya Serikali.



 

Read More

Wednesday, March 12, 2025

NAIBU WAZIRI UMMY AZINDUA MTANDAO WA UWEZESHAJI WA WATU WENYE ULEMAVU MAHALI PA KAZI

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masual aya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amezindua rasmi Mtandao wa Uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu Mahali pa Kazi nchini (National Business Disability Network – NBDN).

 Mhe. Nderiananga amefanya uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ambapo alikipongeza Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Shirika Lisilo la Kiserikali la Sightsavers International kwa kuona umuhimu wa kuwa na mtandao huo.

Alisema kuanzishwa kwa mtandao huo utahakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa na kushiriki kikamilifu katika soko la ajira akisema ni jambo la msingi kwa ustawi wa jamii na kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa haki za watu wenye ulemavu zinaheshimiwa na kuthaminiwa,” Alisema Naibu Waziri huyo.

 Aliongeza kwamba Serikali imeendelea kutekeleza Sera na Sheria mbalimbali zinazolinda haki za watu wenye ulemavu, zikiwemo Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Watu Wenye Ulemavu na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010.

 Vile vile alibainisha kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mahali pa kazi, ikiwa ni pamoja na unyanyapaa, ukosefu wa miundombinu rafiki, na uelewa mdogo wa waajiri kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu katika kuchangia maendeleo ya taasisi na taifa.

“Napenda kuwasihi waajiri wote wa sekta binafsi nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia masuala ya ujumuishaji kwa kutoa nafasi kwa watu wenye ulemavu, si kwa misingi ya hisani, bali kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Tunapaswa kuondoa vikwazo vyote vinavyowazuia watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika soko la ajira,”Alisisitiza.

 Aidha Naibu Waziri huyo alifafanua kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wote ili kuhakikisha kuwa ajenda ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu inatekelezwa kwa ufanisi.

 “Kwa pamoja, tunaweza kuleta mabadiliko chanya na kujenga jamii jumuishi inayotoa fursa sawa kwa wote. Hata hivyo, kupitia mtandao wa NBDN, nina imani kuwa changamoto hizi zitapungua kwa kiasi kikubwa kwa kuwa utatoa mwongozo na kusaidia waajiri kutekeleza sera za ujumuishaji kwa vitendo,”Alihimiza Mhe. Nderiananga.



 

Read More

Sunday, March 2, 2025

MHE. NDERIANANGA AGAWA FUTARI KWA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amegawa futari kwa watu wenye ulemavu 500 kutoka Wilaya Saba za Mkoa wa Kusini Unguja.

Akizungumza katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Mhe. Nderiananga aliwaomba  waumini wa dini ya kiislamu na watanzania wote kuutumia mwezi  Mtukufu wa Ramadhan kwa  kufanya ukarimu kwa wanyonge, wasiyojiweza na watu wenye ulemavu.

Mhe. Nderiananga amegawa futari hiyo kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia watu wenye ulemavu la Tanzania Foundation for Excellence in Disabilities (TFED) iliyoambatana na dua maalum  ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  katika utekelezaji wa majukumu yao  ili Taifa liwe na amani, umoja na mshikamano.

“Nimshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani  viongozi wetu hawa wamekuwa watu wema wametujali na kututhamini wakati wote. Sisi watu wenye ulemavu Watoto wa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi tumeona ushirikishwaji mkubwa katika serikali na sekta binafsi,” Mhe. Nderiananga.

Pia alimpongeza Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwani ni nia yake njema kwa watanzania wote kuwa na maendeleo huanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla.

Vilevile alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanya katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo kama ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami.

“Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya kazi kubwa sana hapa Zanzibar barabara  zimejengwa kila mahali watu wanaendelea  na shughuli  zao. Sekta ya afya Dkt. Mwinyi amewashangaza wengi kwa ujenzi wa hospitali za Wilaya zenye vifaa tiba vya kisasa, sekta ya maji na elimu ambapo tunashuhudia ujenzi wa shule katika maeneo yetu,”Alipongeza.

Aidha aliwasisitiza wazazi na walezi kutowaficha  watoto wenye ulemavu ndani na badala yake wawapeleke shule kwani Serikali iko tayari kwa ajili ya kuwahudumia kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na kuwa nguvu kazi ya Taifa.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayotarajiwa kuadhimishwa Machi 08 mwaka huu ameiomba jamii kuendelea kuiamini nafasi ya mwanamke katika uongozi akisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mfano wa kuigwa hivyo wanawake hawana budi kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali pindi wakati utakapowadia wa uchaguzi unatakaofanyika mwezi Oktoba 2025.

 

Read More

Thursday, February 27, 2025

WAZIRI LUKUVI AMEKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE KUTOKA SHIRIKA LA FAO

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa William Lukuvi amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliyopo katika Mtaa wa posta Jijini Dodoma.

Ujumbe huo kutoka FAO umefanya ziara ya wadau wa ufadhili wa Mfuko Nyumbulifu wa Uchangiaji kwa Hiari (Flexible Voluntary Contribution - FVC) iliyohusisha  Waheshimiwa Mabalozi wa Ubelgiji na Uswisi, Wawakilishi wa Kudumu FAO katika Umoja wa Mataifa, Rome, Washauri Waandamizi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa (IDC) na Viongozi Waandaamizi wa FAO Makao Makuu.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuwezesha washirika (partners) kupata uelewa wa utekelezaji wa programu na miradi inayofadhiliwa kupitia Flexible Voluntary Contribution (FVC) nchini Tanzania, kuongeza uelewa, muonekano na fursa zinazopatikana kwenye FVC kama mfuko nyumbulifu wa utoaji misaada ili kuweza kufikia malengo ya kimkakati Kitaifa na Kimataifa kupitia FAO.



Read More

Wednesday, February 26, 2025

TAARIFA ZA AWALI ZA TAADHARI ZA MAAFA ZITOKE KWA WAKATI

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi ameelekeza Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kujiratibu vizuri katika kufikisha taarifa zote za taadhari ya maafa kwa wakati ili utekelezaji wake ufanyike mapema kabla ya madhara kutokea.

Kauli hiyo ametoa leo alipotembelea Kituo cha Ufuatiliaji wa Majanga Katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

" kwa nafasi mliyonayo na teknolojia mnazotumia mnaweza kujua na kutoa taarifa zote za tahadhari bila urasimu, ili kuepuka athari kubwa za maafa zinazoweza kutokea baadae."alisisitiza Waziri Lukuvi.

Aidha muangalie na uwezekano wa kurahisisha mawasialiano ya taarifa zote za tahadhari ziweze kupatikana kila siku kwa njia ya simu ili kila mtu anayeenda kwenye shughuli ajue na achukue tahadhari.

“huduma hii iwe bure na ipatikane muda wote ili wananchi waingie wasome na wachukue tahadhari, na tutakuwa tumefanya kazi yetu vyema,” alisema

Naye Mkurugenzi Msaizidizi anaye simamia  Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi: Jane Kikunya amelezea kuhusu ufanyaji kazi wa kituo hicho kwamba kinajukumu kubwa la kufuatilia majanga ikiwa ni pamoja kushirikiana na taasisi mbalimbali katika ngazi ya kitaifa katika kutoa taarifa za awali za tahadhari kwa ngazi mbalimbali.

Amefafanua kwamba katika Ngazi ya Mikoa kuna vituo vya maafa vinapaswa kuanzishwa na jukumu hilo limeainishwa katika sheria ya maafa ya mwaka 2022 ambayo imeeleza kila Mkoa, kuwa na kituo cha usimamizi wa maafa ili kufanya ufuatiliaji wa majanga yanayoweza kutokea katika eneo la Mkoa husika.

Hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu inafanya ufuatiliaji wa uanzishwaji wa vituo hivyo ambapo wameweza kukutana na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa ambao kisheria wamepewa jukumu la usimamizi wa vituo hivyo ili kujengeana uelewa wa miongozo na namna ya uanzishaji na usimamizi wa vituo hivyo.

“Vituo hivyo vya Mikoa vitaunganishwa na mifumo ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ili waweze kufanya ufuatiliaji kwa karibu,” alibainisha Bi. Jane.



Read More

Saturday, February 22, 2025

WAZIRI LUKUVI AMSHUKURU RAIS SAMIA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha kiu na ndoto za Iringa kwa kuanza ujenzi bararaba ya kiwango cha lami kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na upanuzi wa ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Iringa.

Waziri ametoa Kauli hiyo wakati aliposhiriki katika tukio la kurejesha wa safari za ndege za shirika la ndege Tanzania (ATCL) Mkoani Iringa iliyoongozwa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Amesema wazo la Ujenzi lilikuwa la Muda Mrefu tangu enzi za TANU lakini Mungu amemleta Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yote mawili utekelezaji wake umefanyika, hivyo hatuna budi kumshukuru.

“Tunatarajia ujenzi wa babarara ya Pawaga kuanzia Pawaga Kuja Mjin, tunategemea barabara hiyo ikikamilika tuanze kusafirisha mpunga unaozalishwa kutoka Pawaga  kusafirishwa na shirika la ndege la Tanzania (ATCL),” alibainisha.



Read More

Tuesday, February 18, 2025

WAZIRI LUKUVI AKUTANA NA WADAU WA SEKTA BINAFSI

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa William Lukuvi amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa Sekta binafsi katika kikao kilichoratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es salaam, kilicholenga kujadili ushiriki wa Sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara kwa kuangalia fursa za uchumi ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati ya kutumia fursa hizo vizuri na kushauri Serikali katika maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Akizungumza katika kikao hicho Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Bi. Angelina Ngalula amesema Sekta binafsi ndio injini ya kusukuma uchumi, inayochukua fursa zote zinazofunguliwa na serikali kama mabadiliko makubwa ya sheria na taratibu, kutolewa kwa tozo inalenga kutoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza na kupata mafanikio.

“Katika Kipindi cha Miaka Minne ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani umefanya kazi kubwa sana katika uwekezaji wa miundombinu ambayo imesaidia katika kuchochea biashara," alieleza Bi. Angelina

Akichangia kuhusu Sekta ya Kilimo Bi. Jacqueline Mkindi amesema sekta ya kilimo na mifugo imenufaika sana kwa sababu ya nguvu ya serikali kutangaza diplomasia ya uchumi na kueleza kuwa umeongeza uhitaji wa bidhaa za Tanzania nje ya Nchi.




Read More

Wednesday, February 12, 2025

WAKURUGENZI WA UFUATILIAJI NA TATHMINI NGAZI YA WIZARA WAKUTANA KUPITIA TAARIFA YA UTENDAJI WA SERIKALI



Imeelezwa kwamba jukumu la Ufuatiliaji na Tathmini ni muhimu katika kuboresha utendaji wa Serikali kwa ujumla hivyo kusaidia kutoa msukumo wa kuboresha Miundo na Mifumo kwaajili ya kuandaa Miongozo ya Ufuatiliaji na Tathmini Ili kuimarisha U&T ndani ya Serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Sakina Mwinyimkuu alipomuwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. James Henry Kilabuko, katika Kikao kazi cha wakurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini na Maafisa kutoka katika Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini ndani ya wizara kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa lengo la kupitia Taarifa ya Utendaji wa Serikali (Government Performance Report kwa Mwaka wa Fedha 2023/24).

Alisema dhumuni kubwa ni kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji huduma bora kwa wananchi hivyo wataalam wa Vitengo mnapaswa kusimamia na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika mipango ya serikali.

Nitoe rai kwa wataalam kutofanya kazi kwa mazoea, uoga au kutojiamini, kwani kwa kufanya hivyo serikali haitafikia malengo nhivyo kupunguza umuhimu wa kuanzisha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini. Hivyo

 “ni vema kufanya ufuatiliaji na tathmini kuwa nyenzo ya msingi ya kusaidia utendaji wa taasisi, sekta na nchi kwa ujumla,”alifafanua Bi, Sakina

Ikumbukwe kwamba

Kikao kazi hicho kitafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 12 hadi 13 februari 2025 kimelenga kutoa mafunzo ya Miongozo ya Ufuatiliaji na Tathmini (U&T) katika taasisi za Serikali yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu



Read More

Saturday, February 8, 2025

WAZIRI LUKUVI AMPA KONGOLE MHE. WAZIRI MKUU

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa William Lukuvi amemshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuendelea kusimamia na kuratibu shughuli za Serikali.

Waziri Lukuvi ametoa pongezi hizo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Ngome Jijini Dodoma.

Alisema kuwa kazi ya Waziri Mkuu kwa Mujibu wa Katiba ni kuratibu shughuli zote za Serikali na chini yake yupo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na watendaji wa Ofisi yake ambayo wanatekeleza majukumu hayo kwa weledi na ufanisi mkubwa.

“Wakati wa uratibu wa shughuli za Maafa watendaji mmefanya kazi kwa ushirikiano Mkubwa chini ya Uongozi wa Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mambo yameenda vizuri nchi nzima,” alisema Waziri Lukuvi

Aidha alifafanua kuwa kazi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu Serikali ili kuwafahamisha namna Serikali inavyoendelea kutekeleza majukumu na kuhudumia wananchi.

"...kwa kuwa tuna nafasi ya kupata taarifa na kuzifanyia uchambuzi ili kujulisha umma kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari basi tuendelee kuratibu vyema taarifa na kuzitoa kwa usahihi ndiyo jukumu letu kubwa na lamsingi lazima tujipange ili ziweze kutoka kwa wakati alisema,” Waziri Lukuvi.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi katika maneno ya utangulizi amesema Viongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamewatengeneza mazingira mazuri kwa watendaji kufanya kazi kwa furaha na amani.

Pia ameahidi kuimarisha ushirikiano miongoni mwao ili kuyafikia maelengo ya ofisi na Serikali kwa ujumla.

"Tuimarishe ushirikiano miongoni mwetu ili kazi zetu ziende kwa wepesi na ufanisi kwa kuamini kila mmoja ana mchango chanya kuhakikisha malengo yanatimia," alisema Dkt. Yonazi.

 


Read More

Tuesday, February 4, 2025

DKT. YONAZI AWAKUMBUSHA WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU KUENDELEA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WELEDI



Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya sera, bunge na uratibu Dkt. Jim Yonazi amewakumbusha watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ushirikiano, upendo, furaha na amani ili kuyafikia malengo ya ofisi hiyo.

Dkt. Yonazi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi Ofisi yake wakati wa mkutano wake na watumishi hao uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo Njedengwa Jijini Dodoma.

Dkt. Yonazi amesema ipo haja ya kila mtumishi kujifanyia tathmini katika utendaji wake wa kazi huku akizingatia miongozo na kanuni za utumishi wa umma na kusema kuwa, kila mtumishi anawajibika katika kuhakikisha ofisi inapata matokeo iliyoyakusudia na kwa ufanisi.

“Ni wakati sahihi kila mmoja kuilinda furaha aliyonayo awapo mahali pa kazi, isingefaa utoke nyumbani huna furaha na ufike eneo la kazi ukose furaha, ni vyema kuja eneo la kazi na kuipata furaha mara mbili  kwa kuzingatia mazingira yaliyorafiki katika kutekeleza majukumu,” alisema Dkt. Yonazi

Aliongezea kuwa kila mtumishi wa umma awe na desturi ya kuheshimu nafasi ya mwingine bila kujali tofauti zinazoweza kuwepo miongoni mwa watumishi hao.

“Ni vyema kila mtu akajali mwingine na ikumbukwe hakuna mtu mwenye uwezo mdogo wa kufanya kazi, jambo la msingi ni kuhakikisha ule uwezo uliopewa na Mwenyezi Mungu na Mafunzo mbalimbali unatumia vizuri na kuhakikisha unaleta matunda mazuri na kuleta maendeleo kwa Nchi yetu” alisema Dkt, Yonazi.

Sambamba na hilo aliwaeleza watumishi hao kuwa kila mmoja ni kiongozi katika eneo lake la kazi hivyo abebe dhamana hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa.

“.....kila mtumishi aliyepo hapa ndiye Katibu Mkuu kwenye eneo lake, kwa kubeba imani ya kwamba ni Katibu Mkuu anapaswa kuwa na nidhamu na bidii katika kazi ikiwa ni pamoja na kuwa mwaminifu,” alisema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. James Kilabuko katika neno lake la utangulizi amewaasa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuzingatia sheria za utumishi wa Umma huku akiwasihi kuimarisha umoja na mshikamano ili kuiletea Serikali maendeleo yake.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Waziri Mkuu Bi, Numpe Mwambenja ameomba watumishi kuendelea kujitathimini mienendo yao katika utumishi wa Umma kwa kufanya kazi vizuri na nidhamu na kuheshimu viongozi huku wakiheshimiana wao kwa wao.

Bi. Numpe alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna unavyojali maslahi ya watumishi na ustawi wao kwa ujumla na kuwasihii watumishi kuendelea kutimiza wajibu kwa kuzingatia kauli ya “hakuna haki bila wajibu”.






Read More

Wednesday, January 8, 2025

WAZIRI LUKUVI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI JENGO JIPYA LA MAHAKAMA YA WILAYA MKOANI

 


Imeelezwa kwamba hali ya amani utulivu na ushirikiano unaosimamiwa na Viongozi Wakuu wa Nchi imesaidia katika kuleta chachu kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi ametoa kauli hiyo leo  wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Mkoani ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Amefafanua kwamba uongozi wao bora; hatuna budi kuendelea kuwaombea viongozi wetu, kila mmoja kwa dini yake ili Mwenyezi Mungu awape afya na nguvu ya kuendelea kutuongoza kwa mshikamano.

Waziri Lukuvi amesema, “chini ya uongozi wao Tanzania Bara imetulia na Tanzania Visiwani imetulia na hivyo kuwezesha haya kufanyika na kuendelea kuchochea maendeleo makubwa, mwenye macho haambiwi tazama.”

Sote ni mshahidi wa hatua kubwa za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia uongozi wa awamu ya nane chini ya Mhe. Daktari Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Waziri Lukuvi amesema, mafanikio ya Serikali ya awamu ya nane yanaonekana wazi katika nyanja za siasa na utawala bora, uchumi, huduma za kijamii na namna utamaduni wa watu wa Visiwa vya Zanzibar unavyoenziwa na kuheshimika wakati wote.

Aidha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua za makusudi kuja na mradi wa ujenzi wa jengo hili la Mahakama ya Wilaya pamoja na majengo mengine ya Mahakama za Mikoa na Wilaya kule Unguja na hapa Pemba ili kukabiliana na changamoto za miundombinu ya majengo.

“Ujenzi wa jengo hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 alisema,” Waziri Lukuvi.

Kwa upande wake Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Mkuu wa Zanzibar amesema Rais. Mhe. Daktari Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewaheshimisha kwa kuwajengea majengo saba ya Mahakama za Mkoa na wilaya katika visiwa vyote vya unguja na pemba.

“Tumekusudia kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga mifumo imara ya usimamizi wa haki ili kuboresha huduma zetu za mahakama kuwa za kisasa ,” alisema Mhe, Jaji, Khamis.

Naye Mhe, Valentina Katema, Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, amesema miundo mbinu ya majengo ya mahakama ipo katika muundo zamani hivyo kusababisha kushindwa kuendesha shughuli zake katika mazingira ya kisasa.

”Ujenzi wa majengo mapya ya Mahakama itasaidia, kupunguza msongamano wakati wa utoaji wa huduma na kusaidia wananchi kupewa huduma kwa kuendana na  mahitaji ya kisasa,” alisema Mrajis.



Read More