Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, ametoa wito kwa Viongozi,
Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kubeba malengo
ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kama sehemu ya wajibu wao wa kitaifa ili
kuweza kufikia maono yaliyopo kufikia mwaka 2050.
Dkt. Yonazi ametoa wito huo wakati ufunguzi wa
Kikao cha Mazingativu ya Menejimenti, Wakuu wa taasisi na Watumishi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na taasisi zake kinachofanyika leo Jijini
Arusha.
“Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 tayari
imeshazinduliwa, Dira hii ni ramani ya mustakabali wa nchi yetu, ikitupa
taswira ya nchi ambayo tunaihitaji kuwa nayo katika ndani ya miaka 25 ijayo,
ili kufanikisha maono haya kila mmoja wetu anawajibu na anajambo la kulifanya,
ni wajibu wetu kujiuliza kwamba nitachangia nini kuhakikisha nchi yangu
inafikia maono haya kufikia mwaka 2050” ameeleza Dkt. Yonazi.
Aidha, amebainisha kuwa, kila mmoja mahali
pake pa kazi anawajibu kwa kuhakikisha nchi ya Tanzania inakuwa nchi bora na
mahali bora pa kuishi kwa kuweka misingi bora ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza kuhusu kikao hicho, Dkt. Yonazi
amebainisha kuwa, kikao hicho ni sehemu ya utamaduni wa Ofisi ya Waziri Mkuu
kutenga muda kila mwaka kwa ajili ya kujitafakari, kujifunza na kujipanga upya
kwa lengo la kuboresha utendaji katika kutekeleza majukumu ya Ofisi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha,
Joseph Mkude akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA. Amos Makalla ametoa
wito kwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa wabunifu katika kufikiri na
kutekeleza majukumu yao, ili kuweza kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na
matarajio ya wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Dunia ya sasa inabadilika kwa
kasi kubwa na changamoto zake zinahitaji mbinu mpya za kuzikabili, ni wajibu
wetu kuwa wabunifu katika kufikiri na kutekeleza majukumu yetu, ili tuweze
kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wananchi kwa ufanisi zaidi.
Hivyo, kubadilika kulingana na wakati ni muhimu ili kuendana na mabadiliko ya
kidunia, kitaifa na kijamii, tukizingatia misingi hii, tutakuwa na Ofisi yenye
weledi, inayothamini maendeleo endelevu na inayokabiliana na changamoto kwa
mafanikio” alisema.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo amebainisha kuwa
“Kwa kuwa jukumu la uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zote za
Serikali lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nitumie fursa hii kutoa rai kuwa
tuendelee kulitekeleza jukumu hili kwa ufanisi wa hali ya juu. Kila taasisi
inapaswa kuonesha matokeo halisi katika maeneo yake ya utekelezaji, tuweke
mkazo zaidi katika kuhakikisha kwamba kazi zetu zinajikita kwenye matokeo
yanayogusa maisha ya wananchi, badala ya kuishia kwenye michakato au
utekelezaji usioonesha matokeo”.
Mbali na hayo Mhe. Mkude
ametoa wito wa kushiriki uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwani
Uchaguzi huo ni fursa ya kipekee kushiriki katika kuimarisha misingi ya
demokrasia na utawala bora.
“Kila Mtanzania anatakiwa kutimiza haki na
wajibu wake wa kikatiba kwa kupiga kura, ili kuchagua viongozi watakaoliongoza
Taifa letu katika ngazi zote, aidha, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha
tunadumisha amani, mshikamano na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi, ili
Tanzania iendelee kubaki kuwa mfano bora wa utulivu, mshikamano na demokrasia
barani Afrika” ameongeza.
Kikao hicho kinaendelea Jijini Arusha, na mada
mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo ikiwemo Matumizi ya Akili Unde (AI) mahala pa
kazi na mustakabali wa ajira kutokana na maendeleo ya kasi ya sayansi na
teknolojia, masuala ya afya ya akili, fursa za uwekezaji kwa watumishi na
maandalizi ya maisha baada ya kustaafu, masuala ya itifaki na ustaarabu na Dira
ya Maendeleo ya Taifa 2050, ili kuweza kujiimarisha katika nyanja mbalimbali
kitaaluma, kimaisha na kiutumishi.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.