Tuesday, December 31, 2019

MIUNDOMBINU YA SHULE IKAMILIKE MAPEMA-MAJALIWA

*Kama kuna wahusika walioko likizo warudishwe haraka

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya shule ikamilike mapema na kama kuna watendaji walioko likizo warudi kwani Serikali inataka wanafunzi wote waanze masomo pamoja.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Desemba 31, 2019) wakati alipofanya ziara kukagua ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleoa wilayani Ruangwa. Amesisitiza ukamilishwaji wa miradi hiyo ili wananchi waanze kuitumia.

Waziri Mkuu amesema agizo alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Desemba 29, 2019 kuhusu usimamizi wa miundimbinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa liko pale pale kwa sababu Serikali haitaki kuona wanafunzi wakipishana katika kuanza masomo.

Miradi ambayo Waziri Mkuu ameitembelea ni ujenzi wa shule ya msingi ya Ng’au ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, ujenzi wa chuo cha VETA, hospitali ya wilaya ya Ruangwa na shule ya sekondari ya Lucas Maria. 

Waziri Mkuu amesema Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo hivyo ni lazima viongozi katika maeneo husika wahakikishe wanashirikiana katika kusimamia utekelezaji wake.

Amesema wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020, hivyo ni lazima usimamizi ukaongezwa katika baadhi ya maeneo ambayo miundombinu yake bado haijakamilika ili kuwahi masomo.

Akiwa katika shule ya Sekondari ya Lucas Maria Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Andrea Chezue ahakikishe mafundi wanafanya kazi usiku na mchana.

“Shule zinakaribia kufunguliwa na baadhi ya majengo kama bwalo, maabara, nyumba za walimu hayajakamilika mafundi hawapo eneo la ujenzi na Serikali imetoa fedha. Nataka kazi hii ikamilike mapema kwani hakuna sababu.”

Wakati huo huo, Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa wamepongeza na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wananchi hao wakiwemo vijana wanaojenga chuo cha VETA walitoa pongezi na shukrani hizo mbele ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza kukagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho. Mafunzo yatakayotolewa chuoni hapo ni pamoja na ufundi uashi, seremala, magari, ushonaji nguo na Tehama.

Kadhalika, vijana hao wamewashauri vijana wenzao wajitokeze na kuchangamkia fursa za ajira zinazopatikana katika maeneo yao kupitia miradi mbalimbali inayotokelezwa na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua darasa katika Shule ya Msingi Ng’ao, iliyopo wilayani Ruangwa, wakati akikagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maabara katika Shule ya Lucas Maria, iliyopo wilayani Ruangwa, wakati akikagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiuliza jambo kwa Mshauri wa Mradi Sudi Shomari, wakati alipotembelea mradi majengo ya VETA, yanayojengwa katika Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa, wakati akikagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua mradi wa majengo ya VETA, yanayojengwa katika Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa, wakati alipotembelea miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maabara ya hospitali mpya ya Wilaya ya Ruangwa, wakati alipokagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maabara ya hospitali mpya ya Wilaya ya Ruangwa, wakati alipokagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo, baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, wakati alipokagua miradi ya Halmashauri hiyo, Desemba 31, 2019.

Read More

Sunday, December 29, 2019

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WAKUU WA MIKOA

*Ataka ujenzi wa vyumba vya madarasa ukamilishwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati ili wanafunzi wote waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 waanze masomo kwa pamoja.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kusoma kwa pamoja kwa sababu wakipishana muda wa kuanza masomo baadhi yao wanashindwa kufanya vizuri jambo ambalo si sahihi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Desemba 29, 2019) wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020 kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Ruangwa.

Jumla ya watahiniwa  933,369  sawa  na  asilimia  98.55 ya  waliosajiliwa  walifanya  mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 na kati yao watahiniwa  759,737  wamefaulu ambao ni sawa na asilimia 81.50.

Kati  yao  wasichana  ni  395,738  ambao  ni  sawa  na  asilimia  80.87  na wavulana  ni  363,999  sawa  na  asilimia  82.20.  Mwaka  2018  watahiniwa waliofaulu  walikuwa  asilimia  77.72,  hivyo  kuna  ongezeko  la  ufaulu  kwa asilimia  3.78. 

“Wakuu wa Mikoa hakikisheni vyumba vya madarasa vinakamilika ili wanafunzi wote waliofaulu waanze masomo kwa pamoja. Kitendo cha wanafunzi kupishana kuanza masomo kinawafanya waliochelewa kutofanya vizuri katika mitihani yao.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao wahakikishe wanasimamia vizuri elimu kwa watoto wa kike na kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwakatisha masomo iwe kwa kuwaoa, kuwaozoesha au kuwapa ujauzito.

Amesema Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.

“Watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa au kumpa ujauzito.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona idadi kubwa ya watoto wa kike wanatimiza malengo yao kielimu, hivyo ni lazima wakaondolewa vishawishi  kwa kuboresha mazingira yao ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mabweni.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo na wilaya ya Ruangwa ambayo imepewa sh. bilioni 38 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kubuni mradi wa kimkakati wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao na pembejeo linalojengwa katika kijiji cha Lipande. Ujenzi huo unaogharimu sh bilioni 5.45.

Ghala hilo ambalo limeanza kutumika lina uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 litaiwezesha halmashauri kujiongezea mapato ya ndani na kusaidia kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu na wafadhili. Pia litapunguza gharama za usafirishaji wa korosho walizokuwa wanatozwa wakulima wakati wa kusafirisha mazao. 

Amesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano miradi mingi ya kimkakati imetekelezwa nchini ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), upanuzi wa bandari za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga, uboreshwaji wa viwanja vya ndege, ununuzi wa rada na ununuzi wa ndege mpya.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, kipaumbele chake kilikuwa ni kukuza kiwango cha uchumi kutoka cha chini kwenda cha kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya viwanda.



(mwisho)
Read More

MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA CCM WILAYA YA RUANGWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.
Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.

Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.





Read More

Thursday, December 19, 2019

WAZIRI MHAGAMA AKUNWA NA KASI YA UTATUZI WA MIGOGORO YA KAZI KWA NJIA YA USULUHISHI


Na. OWM, MOROGORO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mwaka jana kwa Tume hiyo, ambapo aliiagiza Tume hiyo  kuwa na mpango mkakati wa Kuhakikisha kuwa migogoro ya kazi nchini inatatuliwa kwa njia ya Usuluhishi bila kufika katika ngazi ya maamuzi, kutokana na utekelezaji wa agizo hilo asilimia 86.73 ya migogoro ya kazi 9,646 iliyosajiliwa nchini imetatuliwa kwa njia ya usuluhishi bila kufika kwenye ngazi ya maamuzi.

Waziri Mhagama ameyasema hayo leo, tarehe 19, Desemba 2019,  mjini Morogoro,  wakati akifungua kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume kilichowakutanisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo. Aidha, amefafanua kuwa njia bora ya kutibu mahusiano ya kiajira yaliyotetereka ni kupitia kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi.

“Nawapongeza Wasuluhishi na Waamuzi wa mashauri ya kikazi, jitahidini mfanye kazi kwa uadilifu, kwani hata kwenye mashauri yaliyohitaji kutatuliwa kwa njia ya maamuzi asilimia 78 ya mashauri 5,131 ya maamuzi yaliyosajiliwa yamepata maamuzi,mmefanya kazi nzuri kwa kuvuka nusu ya mashauri, pia  mmepunguza malalamiko ya watumishi kupata haki zao ambazo zimekuwa zikipotezwa  na baadhi ya wajanja katika sekta ya ajira bila kuwa na huruma kwa watanzania wenzao ”  Amesema Mhagama

Mhe. Mhagama ameeleza kuwa kitendo cha Tume hiyo kutekeleza agizo lake la kuanzisha kitengo cha Usuluhishi na kuteua Mkurugenzi anayeratibu Kitengo hicho kunadhihirisha dhamira ya Tume hiyo ya kuhakikisha migogoro ya kikazi haizalishwi kwa kuwa huchochea kutumika vibaya kwa rasilimali muda kati ya mwajiri na Mfanyakazi hali inayopelekea kuchelewesha Maendeleo.    

“Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza miradi ya Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii ikiwemo kujenga viwanda, kujenga reli ya kisasa, kujenga bwawa la Nyerere litakalozalisha Umeme, Utekelezaji wa Miradi hii maana yake kuna ajira zinazotengenezwa hivyo tutarajie na migogoro ya kazi pia kuzalishwa, kwa mantiki hiyo Tume haina budi kuendana pia na  kasi ya maendeleo ili kuifanya nchi yetu kuwa mahala salama ya uwekezaji na ufanyaji wa kazi ” Amesisitiza mhagama.

Aidha, Mhe. Mhagama ameitaka Tume hiyo kuendelea kufanya utafiti kwa sekta   zote zinazoongoza kwa migogoro ya kikazi ili kubaini chanzo cha migogoro hiyo na kuandaa Mkakati Maalum wa kuishughulikia, kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Kupitia Tume hiyo  imepewa jukumu la kutatua migogoro na kuweka msisitizo wa kuimaliza migogoro.

“Nimepitia ripoti yenu inaonesha bado sekta ya Ulinzi binafsi inaendelea kuwa kwenye kundi linaloongoza kwa migogoro, lakini sekta ya Hoteli pia kila mwaka ipo kwenye kundi hilo, lakini ziko sekta nyingine kama sekta ya Ujenzi kwa mwaka huu imeondoka lakini sekta ya  Viwanda imeingia kwenye sekta zinazoongoza za migogoro japo si kwa kiwango cha juu, kwa kuwa tumejipambanua tunajenga uchumi wa viwanda lazima muwe na mpango kazi ili kuweka mazingira wezeshi kwa Taifa letu” Amesisitiza Mhagama

Awali akiongea katika kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Shanes Nungu alibainisha kuwa Tume hiyo iliamua kutelekeza maagizo ya Mhe. Waziri Mhagama kwa kuboresha Mkakati Wa Mpango kazi Wa Tume ambao umesaidia kuwa na  mpango mkakati kwenye mtazamo Wa kupunguza migogoro  na unaolenga kumaliza migogoro, lengo nikutaka kutatua migogoro na kuweka msisitizo wa kuimaliza migogoro kwenye  sekta  zinazoongoza kuwa na migogoro mahala  pa kazi.

 "Wasuluhishi na Waamuzi wa mashauri ya Kikazi kwa pamoja wamekuwa wanajitahidi kumaliza na kuipunguza migogoro ya kikazi, kwani tumefanikiwa kumaliza migogoro hiyo kwa asilimia 86 kwenye hatua ya Usuluhishi na asilimia 78 kwenye hatua ya Uamuzi kwa migogoro na mashauri yote yaliyosajiliwa," alieleza Nungu.  
 
Naye, mjumbe kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) aliye mwakilisha  Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani hapa nchini, Maridadi Marwa amefafanua kuwa ILO wanaunga mkono utatuzi wa migogoro uishie kwenye hatua ya Usuluhishi, kwani utatuzi wa njia hiyo humaliza mgogoro kabisa kwani pande mbili zenye tofauti hukubaliana tofauti na hatua ya uamuzi ambapo mmoja huambiwa kashindwa hivyo ni bora kujikita katika utatuzi wa usuluhishi.
              
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi  ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo  Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo kimefanyika kwa mujibu wa Agizo la Rais Na.1 la mwaka 1970. Baraza hilo   huiwezesha Tume kuboresha Huduma na masuala ya utatuzi Wa migogoro ya kikazi kwa njia ya Usuluhishi na Uamuzi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza umuhimu wa kutatua migogoro ya kikazi kwa kutumia njia ya Usuluhishi wakati kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Shanes Nungu akiongea, wakati  wa kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini,  mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha wakutanisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini,  mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha wakutanisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimpongeza mmoja wa watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, wakati kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini,wakifuatilia  kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwa  katika picha ya pamoja na Watumishi wa  Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, wakati kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019




Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini,  mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha wakutanisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo.

Read More

SEKTA YA UMMA KUSHINDANISHWA TUZO ZA MWAAJIRI BORA WA MWAKA – MHAGAMA


Na. OWM, Dar es salaam.

Tangu mwaka 2015 Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kilianzisha rasmi Tuzo ya Mwajiri Bora kwa kila mwaka,   lengo la tuzo hizo ni kuwatambua   Waajiri wenye mikakati bora ya usimamizi wa rasilimali watu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara na kuwahamasisha Waajiri kufuata taratibu za kitaifa na kimataifa katika uendeshaji wa biashara zao, ambapo makampuni wanachama kutoka sekta binafsi hushindanishwa kwa kila mwaka.

Kutokana na tuzo hizo kuwashirikisha kwa wingi wanachama wa chama hicho wa sekta binafsi, ambapo kwa mwaka huu , Katika ushindi wa jumla Tanzania Breweries Limited (TBL) wameweza Kuibuka kinara na kushika nafasi ya kwanza, wakifuatiwa na Geita Gold Mines na wa tatu wakiwa Puma Energy.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu  imedhamiria  Tuzo za mwakani 2020 kwa kushirikiana na ATE pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), kuishindanisha sekta ya Umma ili ushindani huo unaofanywa katika sekta binafsi uyashirikishe mashirika ya umma  kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya  kuweza kuboresha mazingira ya kazi na Ajira  na kuongeza  tija hapa nchini.

Akiongea katika wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), jijini Dar es salaam, tarehe 18 Desemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, aliye mwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amefafanua kuwa ustawi wa wafanyakazi sio kwa sekta binafsi peke yake ni pamoja na sekta ya umma, hivyo ili sekta binafsi iwe injini ya kuendesha uchumi wa Taifa,  ni lazima pia sekta ya Umma nayo iwekeze rasilimali watu ili kuweza kuongeza tija katika maeneo ya kazi.

“Niipongeze ATE kwa kuwa na Tuzo hizi, Tungependa kuona ni mashirika gani ya Umma yanafanya vizuri katika kuangalia ustawi wa wafanyakazi na kuleta tija nchini. Maamuzi ya kuwa na washindi wa jumla  katika makundi ya kisekta yataongeza chachu mpya ya mashindano ambayo itakuza sekta mbalimbali na hatimaye yataboresha na kuleta tija katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu” Amesisitiza, Mhe. Mhagama.

Waziri Mhagama ameitaka ATE kuendelea kutoa mafunzo katika maeneo ya kazi na juu ya sheria za kazi na Usimamizi wa rasilimali watu, ambapo kutokana na mafunzo hayo yatasaidia kupunguza migogoro mahala pa kazi na hivyo kujenga mazingira tulivu ya kibiashara ndani ya maeneo ya kazi. lakini pia mafunzo hayo yatawasaidia wafanyakazi kukidhi ushindani wa mazingira ya kibiashara  kwa sasa.

“Takwimu zinaonesha mafunzo ambayo yameratibiwa na kuandaliwa na ATE kuwa vijana  1, 437, waliidhinishwa na kupata nafasi kwa waajiri huku kwenye tovuti ya serikali wapo vijana 6,919,  walijiandikisha hadi Julai mwaka huu, hivyo nitoe rai kwa waajiri wapeni fursa  vijana ili waweze kujifunza kwa vitendo,  niipongeze Kampuni ya TCC kwa kuwa mstari wa mbele kutoa nafasi kwa vijana kujifunza kwa vitendo hapa nchini.” Amesema , Mhe. Mhagama.

Aidha. Amewataka waajiri kuendelea  kushirikiana na serikali katika kutekeleza mpango wa kitaifa wa miaka 5 wa kukuza ujuzi ambao hufadhiliwa na serikali kupitia tozo ya kukuza ujuzi mahala pa kazi ili kuweza kuongeza ujuzi kwa vijana na kutatua tatizo la ajira nchini huku akiwasisitiza kuzingatia sheria za kazi zinazo onya ajira kwa watoto.

 “Utafiti wa hali ya maambukizi mapya ya UKIMWI hapa nchini unabainisha kuwa katika maabukizi mapya 72,000 kwa mwaka 40% ya maabukizi hayo ni kwa vijana kati ya miaka 15-24, ambapo   80% ya maabukizi hayo ni kwa watoto wa kike ” Hivyo  waajiri mnayo kazi ya kufanya katika kuilinda nguvu kazi hii” Alisisitiza Mhagama.

Mhe. Mhagama amewataka waajiri kuendelea kuchangia katika mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ili kuweza kuwakinga wafanyakazi dhidi ya majanga yatokanayo na kazi. Pia amewasisitiza waajiri kuzingatia haki, usawa mahala  pa kazi ili kuondoa unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi hivyo katika kuhakikisha hilo linafanikiwa serikali tayari imeshazindua mkakati wa Kitaifa wa usawa wa kijinsia mahala pa kazi.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Mhe.  Stella Ikupa amewapongeza ATE kwa juhudi zao za kuunga juhudi za serikali za kuwawezesha watu wenye Ulemavu hivyo amewasihi waendelee kujenga mazingira rafiki mahala pa kazi ili watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji maalum waweze kufanya kazi  na kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Jayne Nyimbo amefafanua kuwa ushirikiano wanaoupata serikalini wa kushirikiana na sekta binafsi umesaidia kuboreshwa kwa tuzo hizo ambazo zimekuwa zikiboresha mazingira ya kazi na ajira hapa nchini.

Awali akiongea katika Hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt Aggrey Mlimuka amesema tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka kwa mwaka huu imefanyia kazi ushauri uliotolewa na seriikali mwaka na  Waziri Mhagama kuwa katika tuzo za mwaka huu ziongeze vipengele vipya vitatu (3) ambavyo viezifanya tuzo za mwaka huu kuwa na Jumla ya vipengele 38 kutoka vipengele 35.

"Vipengele vilivyoongezeka ni Mwajiri Bora anayeendeleza Mafunzo ya Ujuzi wa Kazi kwa wahitimu (Internship), Mwajiri Bora anayetoa mafunzo ya Uanagenzi (Apprentiship), Mwajiri Bora anayezingatia Haki Rasilimali ijulikanavyo kama “Local Content”, " Alisema, Dkt.  Mlimuka.

Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka hufanyika kila mwaka na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ambapo zilianza mwaka 2005. Wanachama i kutoka sekta binafsi na wengine wasio wanachama wa moja kwa moja wanaotoka makampuni ya biashara na baadhi ya mashirika ya umma wameshiriki Tuzo hizo za mwaka huu.
MWISHO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (MB) akihutubia wageni waalikwa wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019. 
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akitoa rai kwa Chama cha Waajiri (ATE) kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali  inazozifanya za kuwawezesha watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji maalum nchini, wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama hicho, katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waajiri Tanzania ATE, Jayne Nyimbo akieleza masuala yaliyotekelezwa na  chama hicho  wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama hicho katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam,  tarehe 18 Desemba, 2019.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi TUCTA Said Wamba akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi na kuwashukuru Chama cha Waajiri Tanzania ATE kwa kutambua mchango wa wafanyakazi wawapo mahala pa kazi. wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama hicho katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam,  tarehe 18 Desemba, 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (MB) akitoa Tuzo kwa mwajiri bora wa mwaka 2019, ambaye ni Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL), ikipokelewa na Mkurugenzi wa Rasilimali watuwa Kampuni hiyo, David Magese wakati wa hafla yaTuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019, wanaoshuhuddia ni Mwenyekiti wa Bodi wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Jayne Nyimbo na Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt Aggrey Mlimuka.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemav) Mhe. Stella Ikupa (katikati), akitoa tuzo kwa mwajiri bora wa mwaka 2019 kwa nafasi ya mshindi wa pili Geita Gold mines,  iliyopokelewa na Bibi. Elizabeth Karua wakati wa hafla yaTuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019,  (kulia), ni Mwenyekiti wa Bodi wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Jayne Nyimbo.


Read More

Wednesday, December 18, 2019

WAZIRI MHAGAMA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA NSSF MAAGIZO YA WAZIRI MKUU MIRADI YA NYUMBA KIGAMBONI

Na. OWM Dar es Salaam,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameridhishwa na utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa aliyoyatoa mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu,  baada ya  kukagua miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam.

Akiongea mara baada ya kukagua miradi ya nyumba za NSSF leo (18, Desemba, 2019), Mhe. Mhagama amesema kuwa Mhe. Waziri Mkuu alielekeza menejimenti ya NSSF Kuharakisha kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo ili ziweze kutumiwa na watanzania.

Waziri Mkuu alielekeza menejimenti ya NSSF kuwasiliana na vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati, Taasisi za Umma ili kuangalia uwezekano wa wanafunzi wa  elimu ya juu na watumishi wa umma pamoja na watanzania wenye nia ya kutaka kupanga nyumba hizo waweze kupangishwa kwenye nyumba hizo 161 zilizoko  Tuangoma na  720 zilizoko Mtoni Kijichi.

“Nimefurahishwa katika taarifa yenu kuwa mmewasiliana na vyuo kadhaa ikiwemo DUCE ambao wameonesha nia ya kuomba nafasi za wanafunzi 3000, lakini pia DIT wanahitaji nafasi za wanafunzi 300, tunawasubiri IFM na taasisi nyingine za elimu ya juu na Umma,kwa kuwa kwa Mradi wa Kijichi unazo nyumba 720 ambazo zinaweza kupangishwa na wananfunzi 7,200 kwa mantiki hii inaonesha tunao uwezo wa kukidhi mahitaji ya vyuo vikuu ” Amesema Mhe.Mhagama.

Mhe. Mhagama, ameongeza kuwa katika kuhakikisha nyumba hizo zinakuwa mkombozi wa malazi kwa wanafunzi wa vyuo, hivyo ameishauri menejimenti ya NSSF kuwapa kipaumbele wanafunzi wa kike kwa kuzingatia kuwa takwimu za hivi karibuni zimebainisha kuwa maabukizi mapya ya virusi vya UKIMWI asilimia 40 ni kwenda kwa vijana ambapo asilimia 80 ya vijana ni watoto wa kike wa vyuo vikuu, huku mojawapo ya kichocheo cha maabukizi hayo ni  kutokana na kutokuwa na malazi salama.

Waziri Mkuu, alielekeza TARURA kuhakiksha wanatengeneza  miundombinu ya barabara katika miradi ya nyumba za NSSF, ambapo tayari wamekamilisha taratibu za  awali za ujenzi wa barabara hizo na wataalamu wa NSSF tayari wamehakiki gharama za ujenzi wa barabara hizo ili kuona kama zinaendana na uhalisia wa ujenzi utakaofanyika kupitia SUMA JKT.

“Katika kuboresha barabara za mitaa za hizi nyumba nimeonakazi inayoendelea  na wameniambia DIT wanafanya kazi yao ya kuweka  taa za sola kwenye barabara za mitaa yote ya nyumba hizi na watafanya kazi kwa wakati kama tulivyokubaliana” amesema Mhagama.

Aidha, agizo jingine kwa menejimenti ya NSSF ilikuwa ni kuboresha miundo mbinu ya Umeme, maji taka na maji safi, ambapo tayari taasisi zinazohusika na miundombinu hiyo ikiwemo TANESCO na DAWASA wamekamilisha taratibu za awali za utekelezaji na wameahidi kukamilisha shughuli zake kwa wakati ili nyumba ziweze kutumika.
Waziri Mhagama amefafanua kuwa agizo lingine ambalo NSSF wamelitekeleza ni  Mthamini Mkuu wa Serikali kutathimini nyumba hizo na kutoa   bei halisi ya soko kwa sasa ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa watumishi wa Umma kununua na kupanga katika nyumba hizo.

“Nimefurahishwa na taarifa mliyonipatia kuwa mthamini mkuu wa serikali atakabidhi ripoti yake leo kwa NSSF na naamini sasa watu wengi ambao wameonesha nia ya kupanga au kununua tutawapatia huduma kwa kuwa tunalo kundi la wanafunzi, watumishi wa umma na watu binafsi wenye uwezo wa kununua nyumba hizo”, Amesisitiza Mhagama.

Pia, Waziri Mkuu aliagiza  Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni kupewa kipaumbele kwa nyumba 439 za Dungu ambapo Mkuu wa wilaya  na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni walielekezwa kuwasaidia watumishi wa wilaya na Halmashauri hiyo  kuingia mikataba rafiki itakayowawezesha watumishi  hao kupewa kipaumbele katika kununua au kupanga kwenye nyumba hizo mara ukarabati utakapo kamilika.

“Nimeridhishwa na utekelezaji wa shughuli za miundo mbinu kwa hapa Nungu na hivyo menejimenti ya NSSF wasilianeni na Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni kuwa uboreshaji wa majengo unaenda vizuri ili watumishi tunaowalenga waweze kutumia nyumba hizo, ” Amesema Mhagama.

Pia Mheshimiwa Mhagama amefurahishwa  na hatua ya LATRA kuanza kutekeleza agizo la kuanzisha njia za mabasi ya daladala   kupitia kwenye nyumba za NSSF Mtoni Kijichi na Dungu ili kuwezesha wapangaji na wananchi watakaonunua na kupanga  nyumba hizo kupata usafiri wa umma, kama ilivyokuwa imeelekezwa na Mhe. Waziri Mkuu.

Aidha, Mhe. Waziri pamoja na kuwapongeza NSSF kuanza kutekeleza maagizo hayo, pia amewataka wazingatie muda uliowekwa wa kukamilisha kazi hiyo, hivyo amewataka kufanya kazi usiku na mchana kwa kuzingatia ubora wa kazi.

“Zingatieni uhalisia wa gharama zinazotumika katika ujenzi wa mradi huu ili fedha za wanachama zitumike vyema kwa kuonekana fedha zimewekezwa kwenye miradi yenye tija ” Amesema Mhe. mhagama

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, amesema NSSF imeyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Waziri Mhagama  na kwamba watafanya kwa weledi na ubora ili kuhakikisha kwamba majengo yote yanakamilika haraka na kuuzwa au kupangishwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini NSSF, Balozi Ali Idd Siwa amemhakikishia Mhe. Waziri Kuwa watatoa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha kuwa maagizo aliyoyatoa yanatekelezwa kwa wakati ili kuhakikisha nyumba hizo zinawanufaisha watanzania.

Miradi ya nyumba za NSSF, wilayani Kigamboni Jijini Dar es salaam, ipo katika maeneo ya Tuangoma   jumla ya nyumba 161, Dungu nyumba 439 na Mtoni Kijichi   jumla ya nyumba 720.
MWISHO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akikagua shughuli za uboreshaji miundombinu katika  miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam leo tarehe 18, Desemba, 2019
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akisistiza kwa menejimenti ya NSSF, umuhimu wa miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya  kukagua uboreshaji wa miundombinu wa  nyumba hizo leo tarehe 18, Desemba, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akieleza kuhusu miundombinu ya maji  wakati akikagua shughuli za uboreshaji miundombinu katika  miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam leo tarehe 18, Desemba, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiongea na vijana wa SUMA JKT wanahusika na uboreshaji wa miundo mbinu miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya  kukagua uboreshaji wa miundombinu hiyo  leo tarehe 18, Desemba, 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Balozi Ali Siwa,(katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, wakati akikagua  miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam leo tarehe 18, Desemba, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akikagua shughuli za uboreshaji miundombinu katika  miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam leo tarehe 18, Desemba, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akisistiza kwa menejimenti ya NSSF, umuhimu wa miradi ya nyumba za NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya  kukagua uboreshaji wa miundombinu wa  nyumba hizo leo tarehe 18, Desemba, 2019.

Sehemu ya muonekano wa Nyumba za Miradi ya NSSF zilizopo katika wilaya ya Kigamboni  Jijini Dar es Salaam leo tarehe 18, Desemba, 2019.

Read More