Thursday, December 19, 2019

SEKTA YA UMMA KUSHINDANISHWA TUZO ZA MWAAJIRI BORA WA MWAKA – MHAGAMA


Na. OWM, Dar es salaam.

Tangu mwaka 2015 Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kilianzisha rasmi Tuzo ya Mwajiri Bora kwa kila mwaka,   lengo la tuzo hizo ni kuwatambua   Waajiri wenye mikakati bora ya usimamizi wa rasilimali watu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara na kuwahamasisha Waajiri kufuata taratibu za kitaifa na kimataifa katika uendeshaji wa biashara zao, ambapo makampuni wanachama kutoka sekta binafsi hushindanishwa kwa kila mwaka.

Kutokana na tuzo hizo kuwashirikisha kwa wingi wanachama wa chama hicho wa sekta binafsi, ambapo kwa mwaka huu , Katika ushindi wa jumla Tanzania Breweries Limited (TBL) wameweza Kuibuka kinara na kushika nafasi ya kwanza, wakifuatiwa na Geita Gold Mines na wa tatu wakiwa Puma Energy.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu  imedhamiria  Tuzo za mwakani 2020 kwa kushirikiana na ATE pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), kuishindanisha sekta ya Umma ili ushindani huo unaofanywa katika sekta binafsi uyashirikishe mashirika ya umma  kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya  kuweza kuboresha mazingira ya kazi na Ajira  na kuongeza  tija hapa nchini.

Akiongea katika wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), jijini Dar es salaam, tarehe 18 Desemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, aliye mwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amefafanua kuwa ustawi wa wafanyakazi sio kwa sekta binafsi peke yake ni pamoja na sekta ya umma, hivyo ili sekta binafsi iwe injini ya kuendesha uchumi wa Taifa,  ni lazima pia sekta ya Umma nayo iwekeze rasilimali watu ili kuweza kuongeza tija katika maeneo ya kazi.

“Niipongeze ATE kwa kuwa na Tuzo hizi, Tungependa kuona ni mashirika gani ya Umma yanafanya vizuri katika kuangalia ustawi wa wafanyakazi na kuleta tija nchini. Maamuzi ya kuwa na washindi wa jumla  katika makundi ya kisekta yataongeza chachu mpya ya mashindano ambayo itakuza sekta mbalimbali na hatimaye yataboresha na kuleta tija katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu” Amesisitiza, Mhe. Mhagama.

Waziri Mhagama ameitaka ATE kuendelea kutoa mafunzo katika maeneo ya kazi na juu ya sheria za kazi na Usimamizi wa rasilimali watu, ambapo kutokana na mafunzo hayo yatasaidia kupunguza migogoro mahala pa kazi na hivyo kujenga mazingira tulivu ya kibiashara ndani ya maeneo ya kazi. lakini pia mafunzo hayo yatawasaidia wafanyakazi kukidhi ushindani wa mazingira ya kibiashara  kwa sasa.

“Takwimu zinaonesha mafunzo ambayo yameratibiwa na kuandaliwa na ATE kuwa vijana  1, 437, waliidhinishwa na kupata nafasi kwa waajiri huku kwenye tovuti ya serikali wapo vijana 6,919,  walijiandikisha hadi Julai mwaka huu, hivyo nitoe rai kwa waajiri wapeni fursa  vijana ili waweze kujifunza kwa vitendo,  niipongeze Kampuni ya TCC kwa kuwa mstari wa mbele kutoa nafasi kwa vijana kujifunza kwa vitendo hapa nchini.” Amesema , Mhe. Mhagama.

Aidha. Amewataka waajiri kuendelea  kushirikiana na serikali katika kutekeleza mpango wa kitaifa wa miaka 5 wa kukuza ujuzi ambao hufadhiliwa na serikali kupitia tozo ya kukuza ujuzi mahala pa kazi ili kuweza kuongeza ujuzi kwa vijana na kutatua tatizo la ajira nchini huku akiwasisitiza kuzingatia sheria za kazi zinazo onya ajira kwa watoto.

 “Utafiti wa hali ya maambukizi mapya ya UKIMWI hapa nchini unabainisha kuwa katika maabukizi mapya 72,000 kwa mwaka 40% ya maabukizi hayo ni kwa vijana kati ya miaka 15-24, ambapo   80% ya maabukizi hayo ni kwa watoto wa kike ” Hivyo  waajiri mnayo kazi ya kufanya katika kuilinda nguvu kazi hii” Alisisitiza Mhagama.

Mhe. Mhagama amewataka waajiri kuendelea kuchangia katika mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ili kuweza kuwakinga wafanyakazi dhidi ya majanga yatokanayo na kazi. Pia amewasisitiza waajiri kuzingatia haki, usawa mahala  pa kazi ili kuondoa unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi hivyo katika kuhakikisha hilo linafanikiwa serikali tayari imeshazindua mkakati wa Kitaifa wa usawa wa kijinsia mahala pa kazi.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Mhe.  Stella Ikupa amewapongeza ATE kwa juhudi zao za kuunga juhudi za serikali za kuwawezesha watu wenye Ulemavu hivyo amewasihi waendelee kujenga mazingira rafiki mahala pa kazi ili watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji maalum waweze kufanya kazi  na kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Jayne Nyimbo amefafanua kuwa ushirikiano wanaoupata serikalini wa kushirikiana na sekta binafsi umesaidia kuboreshwa kwa tuzo hizo ambazo zimekuwa zikiboresha mazingira ya kazi na ajira hapa nchini.

Awali akiongea katika Hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt Aggrey Mlimuka amesema tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka kwa mwaka huu imefanyia kazi ushauri uliotolewa na seriikali mwaka na  Waziri Mhagama kuwa katika tuzo za mwaka huu ziongeze vipengele vipya vitatu (3) ambavyo viezifanya tuzo za mwaka huu kuwa na Jumla ya vipengele 38 kutoka vipengele 35.

"Vipengele vilivyoongezeka ni Mwajiri Bora anayeendeleza Mafunzo ya Ujuzi wa Kazi kwa wahitimu (Internship), Mwajiri Bora anayetoa mafunzo ya Uanagenzi (Apprentiship), Mwajiri Bora anayezingatia Haki Rasilimali ijulikanavyo kama “Local Content”, " Alisema, Dkt.  Mlimuka.

Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka hufanyika kila mwaka na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ambapo zilianza mwaka 2005. Wanachama i kutoka sekta binafsi na wengine wasio wanachama wa moja kwa moja wanaotoka makampuni ya biashara na baadhi ya mashirika ya umma wameshiriki Tuzo hizo za mwaka huu.
MWISHO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (MB) akihutubia wageni waalikwa wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019. 
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akitoa rai kwa Chama cha Waajiri (ATE) kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali  inazozifanya za kuwawezesha watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji maalum nchini, wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama hicho, katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waajiri Tanzania ATE, Jayne Nyimbo akieleza masuala yaliyotekelezwa na  chama hicho  wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama hicho katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam,  tarehe 18 Desemba, 2019.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi TUCTA Said Wamba akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi na kuwashukuru Chama cha Waajiri Tanzania ATE kwa kutambua mchango wa wafanyakazi wawapo mahala pa kazi. wakati wa hafla ya Tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama hicho katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam,  tarehe 18 Desemba, 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (MB) akitoa Tuzo kwa mwajiri bora wa mwaka 2019, ambaye ni Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL), ikipokelewa na Mkurugenzi wa Rasilimali watuwa Kampuni hiyo, David Magese wakati wa hafla yaTuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019, wanaoshuhuddia ni Mwenyekiti wa Bodi wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Jayne Nyimbo na Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt Aggrey Mlimuka.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemav) Mhe. Stella Ikupa (katikati), akitoa tuzo kwa mwajiri bora wa mwaka 2019 kwa nafasi ya mshindi wa pili Geita Gold mines,  iliyopokelewa na Bibi. Elizabeth Karua wakati wa hafla yaTuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Desemba, 2019,  (kulia), ni Mwenyekiti wa Bodi wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Jayne Nyimbo.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.