Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Dorothy Mwaluko amelielekeza
Jukwaa la Taifa la Usimamizi wa Maafa nchini kutoa ushauri wa kitaalamu unaojikita
katika hatua ya kabla ya maafa kutokea na sio kujikita wakati wa maafa
yanapotokea kama ilivyozoeleka, kwa kuwa ushauri wa namna ya kuzuia na kujiandaa
na maafa kabla ya maafa kutokea huweza kupunguza madhara ya maafa na rasilimali
zinazohitajika katika upunguzaji wa madhara hayo.
Ameyasema hayo leo Jijini
Dodoma tarehe 16 Desemba, 2019, wakati akifungua kikao cha Jukwaa hilo ambapo amebainisha kuwa wakati
wa kukabili majanga na maafa kunakuwepo na mipango mingi ambayo hutekelezwa na
wadau wa Usimamizi wa maafa na kwa uchache wakati wa urejeshaji hali wa maafa,
lakini mipango ya kujiandaa na kuzuia maafa ambayo hufanyika kabla ya maafa
kutokea kwa ajili ya kuzuia au kupunguza
madhara ya maafa yatakapotokea huwa
haitekelezwi.
“Tumekuwa na maafa hapa
nchini ambayo yameleta madhara nchini, itakumbukwa ajali ya moto mjini Morogoro hivi
karibuni, tujiulize kuna mipango inayoendelea katika kuzuia majanga hayo, yapo
maafa ya mvua yanaendelea kutokea, lakini je ipo mipango ya kabla ya maafa
kutokea, lakini pindi maafa yakitokea wadau wa usimamizi wa maafa hujitokeza
na kuanza kukabili maafa, sasa nataka nguvu nyingi ielekezeni kwenye mipango ya
kabla ya maafa kutokea na hata ikibidi ainisheni majanga yanayoweza kutokea
kwenye maeneo husika ili jamii iweze kujiandaa na kuyazuia maafa husika kabla
yakutokea“ Amesisitiza Mwaluko.
Aidha, amelielekeza
Jukwaa hilo kuupitia Mkakati wa Taifa wa Kupunguza athari za maafa na
kuhakikisha kuwa unaendana na uhalisia wa hali ya majanga yanayotokea katika
jamii ili uweze kutekelezeka kwa kuweka malengo yenye uhalisia, huku
akisisitiza kuwa ni vyema mkakati huo ukatafsiriwa kwa Kiswahili ili uweze
kutumiwa vyema na walengwa kuanzia ngazi ya msingi ya maafa ambayo ni kamati za
vijiji.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu, Mwaluko amelielekeza Jukwaa hilo kuwa
na ushirikiano miongoni mwa wadau wa jukwaa hilo kwa kila mdau kuainisha
majukumu yake na namna anavyoyatekeleza majukumu yake, ili kuweza kujua jukumu
la kila mdau na anafanya nini na kwa
wakati gani na hatimaye mipango ya kuimarisha Usimamizi wa maafa iwe inayotekelezeka.
“Kupunguza madhara ya
maafa ni suala mtambuka lenye mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo.Wakati
mwingine wananchi wamekuwa wakipata madhara kwa kukosa uelewa hivyo ni vyema kila
mdau kuwajibika katika majukumu yake kwa kutoa fursa ya uratibu wa usimamizi wa
maafa kwa ushirikiano wa wataalamu
wa fani mbalimbali” Amesema, Mwaluko
Awali akiongea katika
kikao hicho, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Maafa , Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kanali Jimmy Matamwe, ameeleza kuwa Jukwaa hilo ni chombo cha kisheria ambacho kipo kwa ajili ya kutathmini na kutoa ushauri wa kitaalam kwa serikali kuhusu
majanga ya aina zote, ambapo Jukwa hilo linaundwa kwa kuzingatia Kifungu cha 40 cha
Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.7 ya mwaka 2015.
Kikao
hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kupitia ufadhili
wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kidunia ya Utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa ya
GFCS (Global Framework for Climate Services Adaptation Programme
in Africa (APA) II).
Jukwaa hilo
ambalo linajumuisha wataalamu wa fani mbali mbalimbali kwa kujumuisha sekta ya umma na sekta binafsi,
mashirika ya kimataifa na umoja wa mataifa na asasi za kiraia jukumu lake la msingi ni kutoa ushauri maeneo ya kipaumbele
katika usimamizi wa maafa kwa uratibu na ushirikishawaji wa wadau ili
kufanikisha kujumuisha upunguzaji wa madhara ya maafa katika mipango na sera za
maendeleo ya taifa na katika misaada ya kibinadamu.
MWISHO.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.