Tuesday, September 26, 2023

WANANCHI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI MVUA ZA EL NINO.

 


Serikali imezitaka taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi  kuimarisha mifumo mbalimbali kama ya  usafiri, mawasiliano, nishati na maji  ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miundo mbinu ya mito mikubwa na mifereji ikiwa ni hatua ya kujiandaa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha mapema mwaka huu mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Kamati za Usimamizi wa Maafa ngazi ya Mkoa katika Kuzuia na Kupunguza madhara ya El Nino kilichofanyika Jijini Dar es salaam.

Mhe. Jenista amesema  matukio ya maafa yanatokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii ambapo Serikali za Mitaa, kuanzia Kitongoji, Mtaa au Kijiji na Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya zinawajibika moja kwa moja.

“Hatua za kuzuia madhara zinatekelezwa zaidi na viongozi na wataalam kwa  kushirikiana na wadau na wananchi katika maeneo haya. Tumekutana leo  kukumbushana wajibu muhimu mlio nao kwa kila mmoja kuwajibika katika  eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi. Tukumbuke kuwa  Mkoa unaingia kusaidia juhudi za Halmashauri husika pamoja na  kushirikisha uratibu wa msaada kutoka ngazi ya Taifa endapo madhara  yatakuwa yamezidi uwezo wa rasilimali katika eneo husika.

Pia  amewasisitiza wananchi  kila mmoja kuchukua hatua katika eneo lake, akisema  mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi yenye  jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali za jamii  yetu kutokana na matukio ya maafa.

Katika hatua nyingine amezitaka taasisi zinazohusika kuwa mstari wa mbele  kuchukua tahadhari na kujiandaa  kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi ili kuokoa maisha.

“Historia inaonesha madhara yanayoweza kutokea katika sekta kutokana na uwepo wa El Nino utakaosababisha mvua kubwa ni pamoja na  Mafuriko kuharibu miundombinu mbalimbali, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali,  Maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini, Magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea,” Amesema Mhe. Jenista.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,Albert Chalamila ameahidi kutekeleza maagizo yalyotolewa na Waziri huyo katika kuhakikisha miundo mbinu yote ya maji pamoja na maeneo hatarishi yanafanyiwa matengenezo ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Nino hivyo akawahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi watakapofika katika maeneo yao kufanya maboresho hayo.

“Hakikisha tunajidhatiti kutunza mazingira yetu na miundo mbinu hasa hii ya mito tunaweza kupata kipindu pindu na jambo tunalokabiliana nalo kwa sasa hapa Tabata ni wimbi la vibaka lakini tumeandaa timu  za ulinzi kupitia ulinzi shirikishi wa Sungusungu,”Ameeleza Mkuu wa Mkoa huyo.

Akitoa maoni yake mkazi wa Mji Mpya-Mnyamani ameiomba Serikali kuhakikisha inaweka miundo mbinu imara ya vivuko na barabara katika maeneo ya mitaa ili kusaidia wananchi kuvuka na kupata huduma wakati wa maafa.

Aidha Mkazi wa Tabata Bw. Shelemia Gwassy ameishukuru Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara ya kushitukiza katika maeneo ya Tabata na kukagua mito inayopitisha maji ikiwemo Mto Msimbazi, Mto Mpiji, Mto Ng’ombe na Mfereji wa Jangwani huku akiiomba kuweka utaratibu mzuri wa uzoaji taka katika makazi ya wananchi.

 

Read More

Monday, September 25, 2023

KAMATI ZA MAAFA MKOA ZAJENGEWA UWEZO WA KUZUIA ,KUJIANDAA NA KUKABILIANA NA MADHARA YA EL-NINO

 


Kamati za maafa Ngazi ya Mkoa zajengewa uwezo juu Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kufuatia utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023 kuonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 na kuendelea mpaka Mwezi Januari 2024.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa, Serikali ilianza kutekeleza hatua za kuzuia madhara haya toka mwezi Julai 2023 wakati taarifa ya awali ya dalili za uwezekano wa uwepo wa El Nino ilipotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Kikao kazi hichi kinafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 25 hadi 26 septemba, 2023 na kuhusisha wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa ngazi ya Mkoa wakiwemo; Wakuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyekiti wa Halmashauri pamoja na washiriki kutoka washiriki kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, wawezeshaji kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi Tanzania, TMA na DarMAERT Pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali na Viongzozi wa dini.

Alisema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa mikoa 14 inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

 

“Kikao kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.” alisisitiza Mhe. Nderiananga.

Naibu Waziri aliongezea kuwa, kazi hiyo imezingatia uwajibikaji wa pamoja ambapo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeshirikiana na Wizara za kisekta na Taasisi za Serikali na Wadau kuendelea kuimarisha hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Mikoa husika.

Ametumia nafasi hiyo kuzikumbusha kamati za maafa zote kuendelea kujiandaa na kukabili maafa nchini kwa kuimarisha mifumo ya utendaji, rasilimali zilizopo huku wakitambua masuala ya menejimenti ya maafa ni jukumu la kila mmoja hivyo upo umuhimu wa kuunganisha nguvu ya pamoja.

“Ni jukumu letu sote katika nafasi zetu kama wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa kutekeleza kimamilifu hatua za kuchukua katika sekta zenu kwa kuzingatia kuwa madhara yanaweza kuongezeka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kwa wakati. Natarajia kuwa baada ya kikao kazi cha leo, Kamati hasa ngazi ya Halmashauri zote za Mkoa zitaimarisha utekelezaji wa hatua za kuzuia madhara ili kuhakikisha tunaokoa maisha na mali kwa ustahimilivu wa taifa,”alisema.

Alizikumbusha Taasisi zinazohusika kuendelea kuwa mstari wa mbele wakati wa tukio la maafa zinapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi ili kuokoa maisha.

“Taasisi hizo ni pamoja na zile zinazohusika na huduma ya utafutaji na maokozi, usalama wa wananchi, afya na makazi ya muda na huduma zingine za kijamii. Aidha, taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi pamoja na kuimarisha mifumo kama vile usafiri, mawasiliano, nishati na maji zinakumbushwa kujiimarisha ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa. Taasisi saidizi zina wajibu wa kuwezesha taasisi zenye jukumu ongozi katika kuokoa maisha na mali ili zitekeleze majukumu kwa ufanisi pamoja na kupunguza athari kwa jamii”,Alisisitiza

Sambamba na hilo aliwaeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha juhudi zinazochukuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha uchumi na huduma za kijamii katika ujenzi wa Taifa letu zinakuwa stahimilivu dhidi ya maafa. Ni dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa zitachangia katika juhudi zake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali pamoja na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 kwa manufaa makubwa kwa wananchi na tija iliyokusudiwa.

 

“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 kuhusu masuala ya Menejimenti ya maafa nchini kifungu cha 107, kinaeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha Serikali inaendelea kusimamia kikamilifu vyombo vinavyoshughulika na maafa kuwa na mpango wa utayari wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali haraka pindi maafa yanapotokea kwa kuchukua hatua mbalimbali” alibainisha Mhe. Nderiananga.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameeleza kuwa mkoa umejiandaa katika kukabiliana na maafa na kueleza wataendelea kutoa elimu kwa umma juu ya uwepo wa mvua hizo huku akitahadharisha wakazi wa Malinyi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia ni maeneo yanayoathiriwa na maafa ya mvua mara kwa mara.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa ametahadharisha wakazi wa maeneo yanayoathiriwa kwa wingi, kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalam ikiwemo kuhama maeneo hatarishi na kutotupa taka zinazosababisha kuziba kwa mifereji ya maji na kuimarisha kingo zote.

 

 

Read More

Friday, September 22, 2023

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA: ENDELEENI KUZINGATIA UBORA KATIKA UZALISHAJI WA MBEGU

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameupongeza uongozi wa Wakala wa Taifa wa Uzalishaji na Uendelezaji wa mbegu za kilimo (ASA) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuzalisha na uendelezaji wa mbegu nchini huku akiwasihi kuendelea kuzingatia ubora na weledi katika majukumu ya kuzalisha mbegu bora hizo ili kuendelea kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha nchini. 

Ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kikazi kufuatili shughuli za utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Uvuvi ya AFDP ambayo inaratibiwa na ofisi yake na kutekeleza katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Morogoro.

Akiwa katika ziara hiyo alitembelea Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira, Wakala wa Taifa wa Uzalishaji na Uendelezaji wa mbegu za kilimo (ASA) Pamoja na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) zilizopo Mkoani Morogoro.

Mhe.Ummy amesema upo umuhimu wa kuendelea kuunga mkono Programu ya kuendeleza sekta ya Kilimo na Uvuvi nchini kwa kuzingatia inaongeza tija hasa katika kuhakikisha kunakuwa na mbegu bora nchini. 

“Ofisi ya Waziri Mkuu tunaendelea kufanya uratibu na kutathmini ya programu hii ambayo ni ya miaka sita hivyo endeleeni kufanya kazi vizuri, kwa weledi huku mkiunga jitihada za Mhe Rais za kuona Tanzania inakuwa ghala kubwa la chakula, Serikali haita waacha nyumba, inaendelea kuunga mkono jitihada hizi.” alisema Mhe. Nderiananga

Aidha aliwataka kuendelea kuzingatia ubora na viwango katika utekelezaji wa majukumu ya uzalishaji wa mbegu bora na zinazoendana na mahitaji halisi.

 “Eneo la mbegu ni muhimu sana, bila kuwa na mbegu nzuri hatuwezi kuwa na matokeo ya chakula kizuri, hivyo ninawapongeza mnafanya kazi nzuri endeleeni maana tunategemea sana sekta yetu ya kilimo ili kuendelea kuwa na uhakika wa chakula nchini,”alisisitiza.

Kwa upande wake Mchumi Mwandamizi kutoka wa Wakala wa Taifa wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mbegu za Kilimo (ASA) Bw. Edmund Kayombo akizungumza kuhusu wakala hiyo amesema umeendelea kutoka huduma za kuongeza uzalishjaji na usambazanji mbegu bora, kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora na kushirikiana na kituo cha utafiti ili kuhakikisha mbegu mpya zinazaliwashwa na kusambazwa kwa wakulima.

“Wakala wa Mbegu za kilimo una jumla ya mashamba 14 ikiwemo mashamba ya kilimi yaliyopo Nzenga, Msungula (Kasulu), Chalinze, Nane nane - Morogoro, Tanganyika, Dabaga kilosa, Arusha (Tengelu), Namtumbo (Songera), Njombe, ambayo yanajumla ya ukubwa wa hekta 16,909,” alisema Kayombo.

Read More

TANESCO WATAKIWA KUKAMILISHA KWA WAKATI UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA DODOMA

 


Shirika la Umeme Nchini TANESCO limetakiwa kukamilisha kwa wakati mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya umeme wa chini unaoendelea katika mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba.

Dkt. Yonazi alisema kuwa,TANESCO wana jukumu la usimamizi wa karibu na ulazima katika ujenzi wa Miundombinu ya nishati ya umeme  katika Mji wa Serikali kwani baada ya muda mfupi ujao mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa kutokana na Agizo la Serikali kuzitaka Ofisi zote za Serikali Jijini Dodoma kuhamia Mtumba mapema ifikapo January Mosi mwakani.

Sambamba na hilo Dkt. Yonazi Amelitaka Shirika hilo kuvipa vipaombele viwanda vya ndani kwakununua bidhaa zinazofaa kununuliwa nchini katika viwanda hivyo.

 “Mnafahamu kuwa kuna changamoto ya kiuchumi duniani kote hivyo hatuwezi kununua nje kila kitu; vitu ambavyo vinaweza kununuliwa ndani ya nchi vununuliwe ndani ya nchi, ili kupunguza upelekaki wa fedha za Tanzania nje, ni vizuri kuhusisha viwanda vya ndani ambavyo vinawezekana kutoa huduma vitoe huduma.” Alifafanua Dkt. Yonazi

Akiendelea Kusisitiza kuhusu suala la Ubora na muonekano wa Ujenzi unaendelea katika Mji wa Serikali Dkt. Yonazi alisema ni muhimu kuzingatia maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya huduma nyingine akitolea Mfano Miundombinu ya Umeme, Maji na mawasiliano na kutoa wito kwa kila Mkandarasi katika eneo kufuata Mpangokazi ambao ulikuwa umewekwa, na alisisitiza suala zima la kuzingatia muda wa umaliziaji wa kazi.

 “Tunakumbuka Agizo la Serikali linataka watumishi kuhamia Mtumba ifikapo Tarehe 1 Januari 2024, hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba majengo yanakwenda vizuri katika umaliziaji na kuweka huduma ambazo ni muhimu.” Alibainisha

Akiongea katika ziara hiyo, Mhandisi Richard Kafura kutoka Shirika la Umeme nchini TANESCO alisema,Ujenzi wa mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia TANESCO kwa kushirikiana na mkandarasi DERMO Contruction Limeted. Ambapo mpaka sasa ujenzi wa mifereji ya kupitishia miundombinu ya umeme na Mfumo wa umeme wa ardhini unaendelea kutekelezwa na Mkandarasi.

 
Read More

Thursday, September 14, 2023

DHANA YA UFUATILIAJI NA TATHMINI ITEKELEZWE KWA VITENDO – NAIBU WAZIRI UMMY

 


 

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewasihi wataalam na wabobezi mbalimbali wa eneo la Ufuatiliaji na Tathmini kuitekeleza dhana hiyo kwa vitendo.

 

Naibu Waziri Nderiananga ameyasema hayo mapema leo jijini Arusha wakati akitoa hotuba ya kufunga Kongamamno la pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ambapo amesema umefika wakati sasa wa kutekeleza dhana hiyo kwa vitendo, kwa kushirikisha wadau wote muhimu ndani na nje ya nchi.

Aidha, Mhe. Nderiananga Alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendeleza juhudi mbalimbali za kuimarisha eneo la Ufuatiliaji na Tathmini, kwa kuboresha mifumo na Miundo ya Utumishi ili kuendana na mahitaji ya sasa ya upimaji wa Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma.

“Hii ni pamoja na kukamilisha Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini, Kukamilisha Mwongozo wa Kujenga na kutekeleza Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini kuanzia ngazi ya Taasisi ya Umma, Sekta na Kitaifa, Kuoanisha mifumo ya Taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuunda Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathimini (National Intergrated M&E Dashboard).” Alisema

Aliendelea kueleza kuwa mfumo Jumuishi wa Ufuatilijai na Tathmini utawezesha Mifumo mbalimbali ya utoaji taarifa za utendaji kazi Serikalini kusomana.

“Jitihada hizi ziende bega kwa bega na kuboresha mitaala yetu ili tuweze kupata wataalamu wenye weledi katika kusimamia vizuri utendaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ikiwemo miradi ya maendeleo.” Alisisitiza Naibu Waziri Nderiananga.

Kwa upande wa Sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya Tanzania, Naibu Waziri Nderiananga amewashauri kuendelea kuwa na utayari wa kushirikiana na Serikali ili kuongeza ufanisi wa Ufuatiliaji, Tathmini na upimaji wa utendaji na matokeo.

“Kama ambavyo mmeona uzoefu wa nchi mbalimbali, eneo la Ufuatiliaji na Tathmini si la mtu mmoja, hivyo linahitaji ushirikishwaji wa Wadau wote, Serikali yetu ipo tayari kushirikiana na wadau katika kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora wanazostahili na kwa wakati.” Alisisitiza

Kwa upande wake Bi, Joanita Magongo, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Uongozi amesema baadhi ya maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na sera ya Taifa ya ufuatiliaji na tathmini ikamilishwe ili kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini.

Bi, Magongo amesema maeneo hayo ni pamoja na ukamilishwaji wa mfumo jumuishi wa kielektroniki wa ufuatiliaji na tathmini (Intergrated National M&E System) mfumo ambao umependekezwa uwe na uwezo wa kupokea maoni na kutoa mrejesho kwa wadau.

Ameongeza kuwa maandalizi ya mfumo huo yaende sambamba na maandalizi ya mkakati wa mawasiliano kwa ajili uelewa wa kina kwa wadau.

“Taasisi zote za Serikali ziimarishe Vitengo vya ufuatiliaji na tathmin kwa kuhakikisha vinapatiwa rasilimali za kutosha ili kuwezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuongeza ufanisi,” alisema Bi, Magongo.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza jukumu la Ufuatiliaji na Tathmini sambamba na taarifa za ufuatiliaji na tathmini kuandaliwa na kujadiliwa katika sekta husika kila robo mwaka.

 

Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliji na Tathmini lililofanyika kwa siku nne Jijini Arusha, lilihusisha washiriki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo mada mbalimbali za kitaalamu ziliwasilishwa na Tuzo na vyeti vya Pongezi vilitolewa kwa washiriki mbalimbali.

 

Read More

Wednesday, September 13, 2023

UFUATILIAJI NA TATHMINI HAVIEPUKIKI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI NA MIPANGO YA MAENDELEO

 


IMEELEZWA KUWA, Suala la Ufuatiliaji na Tathmini lina umuhimu mkubwa katika kuangalia utekelezaji wa Mipango kuanzia ngazi ya mamlaka za chini hadi ngazi ya taifa katika utendaji hususan kwenye miradi, ikilinganishwa na namna gani inakwenda sawasawa au inatekelezwa kama ilivyopangwa.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Cosmas Ngangaji katika siku ya pili ya Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini linaloendelea jijini humo ambapo amesema kuwa Suala Ufuatiliaji na Tathmini linajikita zaidi katika vitendea kazi vinavyotakiwa kutumika pamoja na michakato inayotumika kama inafanya kazi na kuleta matokeo chanya hususan katika sekta ya Umma.

Akitolea mfano wa dhana ya tathmini ya utoaji wa huduma za kijamii, Bw. Ngangaji alisema kuwa, miradi mingi ya Serikali inatakiwa kuwekewa misingi endelevu ili wananchi waweze kupata huduma sahihi na kwa wakati.

Akiongea katika kongamano hilo Bw. Mussa Mshirazi Mbarouk kutoka Tume ya Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisema, suala la Ufuatilijai na Tathmini ni suala linalohitaji kujifunza mara kwa mara ili kusaidia kujenga uwezo katika utendaji wa shughuli za kila siku.

Kongamano la Pili la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini linaloendelea Jijini Arusha limeingia katika siku ya pili ambapo mada mbalimbali zimeendelea kuwasilishwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uelewa wa Tathmini, majadiliano bayana juu ya matokeo halisi na mbinu muhimu za kuleta mbadiliko.

 

Read More

Tuesday, September 12, 2023

NAIBU WAZIRI MKUU DKT. DOTO BITEKO ASISITIZA UMUHIMU WA UFUATILIAJI NA TATHMINI SERIKALINI

 


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kama Serikali haitafanya Tathmini ya Shughuli zake haitakuwa na uwezo wa kujipima na vihatarishi vya utekelezaji wa mipango yake. 

Mhe. Naibu Waziri Mkuu Dkt. BITEKO ameyasema hayo mapema leo jijini Arusha alipofungua Kongamano la Pili la Kitaifa la Ufuatilijai, Tathmini na Mafunzo ambapo amesema Serikali imegawanyika katika maeneo mengi kama vile Serikali Kuu na Serikali za Mitaa hivyo ufuatiliaji na tathmini ni eneo muhimu na linalopaswa kutiliwa mkazo. Kutokana na umuhimu huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisistiza Serikali kuwa na Uratibu wa shughuli zake.

“Unaweza kukuta Serikali za Mitaa na Serikali kuu kila mtu anafanya jambo lake hakuna vinavyosomana, tujifanyie tathmini ili tusije kuwa watu wa kuduwaa kunini hili limetokeaje.” Alisisitiza

Dkt.Biteko aliongeza kusema kuwa asiyejifanyia tathmini atakuwa ni mtu wa hasara hivyo kujifanyia tathmini kunaifanya serikali kubaini matatizo mapema na kuweza kuyatafutia ufumbuzi kabla hayajaleta hasara. Dkt. Biteko ametoa wito kwa washiiriki wa kongamano hilo hasa watendaji wa serikali kufanya ufuatiliaji na tathmini bila kuweka mbele rasilimali fedha.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri Mkuu Dkt. BITEKO amewataka maafisa masuhuli wote nchini kuviwezesha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara na taasisi zao kwa kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wa kutosha, vitendea kazi na rasilimali fedha ili viweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulika na masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema, wakati kongamano hili likifanyika kwa mara ya Pili hapa nchini, Serikali imefanyia kazi kwa Asilimia mia, (100%) utekelezwaji wa agizo la uanzishwaji wa Idara za Ufuatilijaia na Tathmini katika Wizara na Serikali.

Awali akiongea wakati wa Ufunguzi wa Kongamano hilo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, alisema kwa kufuatilia mwendeno wa utekelezaji wa kujipima matokeo, Taasisi za Umma zinaweza kujihakikishia kuwa zipo katika njia sahihi za utekelezaji katika kufikia malengo yake, hivyo Ufuatiliaji na Tathmini ni njia nzuri ya kujifunza na kuwajibika.

 

Read More

Sunday, September 10, 2023

DKT. YONAZI “WANAUME MUWE MSTARI WA MBELE KUSHIRIKI MASUALA YA LISHE”

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewaasa wanaume kuwa mstari wa mbele katika kushiriki masuala ya lishe kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanawake ili kuwa na taifa lenye lisha bora kuanzia ngazi ya familia.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wanakijiji wa Mpandapanda katika Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya katika kuadhimisha Siku ya afya na Lishe ngazi ya kijiji ambapo iliadhimishwa kijijini hapo.

Katibu Mkuu Dkt. Yonazi amesema kuwa wanaume wamekuwa mstari wa nyuma katika utekelezaji wa afua za lishe hivyo kukwamisha jitihada zinazofanywa na wakinamama katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora.

“Niwaombe wanaume wote kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na lishe bora kwa kushirikiana pamoja tutakuwa na watoto wenye afya bora na kuwa na Taifa lenye Lishe bora ili kuchochea maendeleo yetu,” Alisema

Akieleza kuhusu jukumu la ofisi yake amesema, itaendelea kuratibu masuala ya lishe nchini kwa kushirikia na wadau kwa kuzingatia miongozo iliyopo.

“Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu shughuli za Serikali na kuhakikisha miongozo ya masuala ya lishe inatekelezwa ipasavyo ili kila mmoja kujua majukumu yake na kuwa na nia thabiti katika utekelezaji wa masuala ya lishe nchini,” Alisisitiza Dkt. Yonazi

Kwa uapnde wake Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha Taifa linakuwa na afya bora kwa kuwa na mikakkati inayotekelezeka.

“Tuna ahidi kuendelea kutoa ushirikino wa kila hali kwa kuhakikisha tunaboresha afua za lishe, ninaipongezea Tanzania kwa kuwa na rasilimali zote muhimu, huku nikiupongeza mkoa wa mbeya kwa kuwa na vyakula bora na muhimu kwa afya zetu niwasihii endeleeni kula vyakula vyenye virutubisho kwa kuzingatia mazingira yenu yanaruhusu, yatumieni katika kuimarisha afya kwa kila rika,” alisema Khan .

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Ben Malisa akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo alisema mkoa umeendelea kutekeleza masuala ya lishe kwa kuhakikisha inatatua changamoto za masuala hayo ikiwemo ya udumavu na utapiamlo ambapo alisema ajenda ya lishe imeendelea kupewa kipaumbele mkoani humo.

“Hali ya Lishe kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano imeendelea kuimarika kutokana na juhudi kubwa za utoaji wa elimu ya Lishe katika jamii. Kiwango cha watoto wa umri chini ya miezi sita walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee kimeongezeka kutoka asilimia 27.3 mwaka 2014 hadi asilimia 71 mwaka 2018,”alisema Ben Malisa

Alibainisha kuwa takwimu zinaonesha kwa mwaka 2022 hali ya Lishe imeimarika ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo kiwango cha udumavu katika Mkoa wa Mbeya kimepungua kutoka asilimia 33.8 hadi 31.5 ingawa kiwango hiki bado kipo juu ya kiwango cha Kitaifa ambacho ni asilimia 30.

Aidha, kiwango cha uzito pungufu kimepungua kutoka asilimia 9.8 hadi 1.4, ukondefu umepungua kutoka asilimia 2.7 hadi 0.6 na uzito uliozidi umepungua kutoka asilimia 5.3 hadi 5.2.

Aliongezea kuwa Juhudi kubwa zimefanyika katika kipindi cha miaka kumi ili kuboresha Afua za Lishe katika Mkoa kupunguza kiwango cha udumavu na aina nyingine zote za utapiamlo. Afua shirikishi za Lishe zinazolenga siku 1000 za mwanzo wa maisha ya mtoto kuhakikisha athari ya muda mrefu katika Lishe, ukuaji na maendeleo ya watoto zinatekelezwa kulingana na Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe wa Sekta Mbalimbali (NMNAP II, 2022-26).

Read More

Monday, September 4, 2023

MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI UTASAIDIA KUIMARISHA UTENDAJI-DKT YONAZI

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt Jim Yonazi amesema, mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali ni mfumo mahususi wa uboreshaji wa utendaji Serikalini kwa lengo la kuona ni namna gani Rasilimali za Serikali zinaboreshwa na Kutumika vizuri.

Hayo ameyasema Mapema leo Ofisini kwake Jijini Dodoma alipokuwa katika mahojiano maalum na chombo kimoja cha Habari, katika kuelekea Kongamano la wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Jijini Arusha Wiki Ijayo, ambapo Dkt. Yonazi ameeleza kuwa, Uratibu wa Shughuli za Utendaji wa Serikali katika eneo la Ufuatiliaji na Tathmini una nia ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali unafanikiwa na malengo yanafikiwa.

Aliendelea kusema kuwa Dhana hii, ni dhana ambayo inalenga katika kuangalia utekelezaji wa Miradi ya Serikali Nchi nzima na kuona kama malengo yaliyowekwa katika Miradi hiyo yanafanikiwa. “Ili malengo hayo yaweze kufanikiwa ni lazima tufanye Ufuatiliaji tujue nini kinaendelea, tufanye Tathmini dhidi ya ile mipango ambayo ilikuwa imewekwa, lakini vilevile tuangalie kwamba tunajifunza nini kutokana na kile ambacho tumekiona kutoka katika Ufuatiliaji na Tathmini,” Alifafanua.

Aidha, Dkt. Yonazi Alimshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na wazo la kuanzisha mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini Nchi nzima,na kuweka vitengo na Idara mahususi kwa ajili ya kazi hiyo katika Wizara na Taasisi za Serikali kwa lengo la kuzipa uzito mkubwa ripoti zinazotokana na Ufuatiliaji na Tathmini katika maamuzi, mijadala na mipango ya Serilikali ili kufikia malengo tarajiwa.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Sakina Mwinyimkuu  amesema pamoja na kongamano hilo kuhusisha wataalam na wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi, wananchi kwa Ujumla wanaalikwa kupata fursa ya kufahamu namna ambayo serikalini inatekeleza miradi kwani kwa kiasi kikubwa miradi mingi inakwenda kwa wananchi “Mwananchi ndiyo mdau wa kwanza kwani yeye ndo anaweza kujua mradi flani unatekelezwa vizuri katika eneo husika, kwa hivyo tunaona pia ni fursa kwa mwananchi kuweza kufahamu na kutoa hali halisi ya utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.” Alisisitiza.

Kongamano hilo la Pili la Kitaifa la wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Jijini Arusha linaongozwa na Kauli mbiu inayosema “Kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya kujifunza na kuboresha Utendaji wa Serikali.”

Read More