Saturday, March 18, 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA, YATEMBELEA MIRADI YA UJENZI WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA KIWANDA CHA UCHAPAJI WA NYARAKA ZA SERIKALI.


 

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imeonesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ujenzi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali Mjini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria Mhe. Joseph Mhagama, leo 18 March 2023 katika ziara ambayo ililenga kujionea kile ambacho kimepangwa kwenye bajeti ya Serikali na kuangalia hatua zilizopigwa, changamoto zilizojitokeza na namna ya utatuzi wake.

“Ziara hii imetuwezesha kupata uhalisia wa hali jinsi ilivyo, ili iweze kutusaidia wakati wa kupanga bajeti, tuwe na uhalisia wa utekelezaji miradi” alisema.

Akizungumzia kuhusu Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Mhe. Mhagama amesema upo muhimu wa Idara hiyo kuwa na mifumo rasmi ya kujisimamia bajeti yake yenyewe (kama wakala) ili isaidie idara hiyo iweze kuingia katika soko shindani.

Aliongeza kusema Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ikiweza kujisimamia katika bajeti yake, itasaidia kuongeza Makusanyo mengi ambayo yanategemewa kutoka katika Idara hiyo.

Tunachangamoto kubwa sana katika utengenezaji wa nembo ya Taifa, “lazima tuwe na Mamlaka moja ya kutengeneza nembo ya Taifa na watu wengine wote waipate kupitia katika Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali, “alisema Mhe. Mhagama.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema anakubaliana na maelekezo ya Kamati. Wizara itatoa taarifa mbele ya Kamati hatua iliyofikia katika kuandaa mabadiliko ya sheria ili kuwezesha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa wakala.

Naye Mhe. Ahmed Ngwali Mjumbe wa Kamati, ameshauri Idara ya Mpiga Chapa Mkuu Wa serikali Kufanyia kazi mapendekezo ya Kamati mapema ili iweze kubadilishwa na kuwa wakala.

Awali Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bwn. George Lugome amesema Utakapokamilika mradi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali itasaidia kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu ikiwa ni sambamba na kuongeza ajira na kuwa sehemu ya mafunzo kwa watu wanasomea maswala ya uchapishaji.

Read More

Tuesday, March 14, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE “TUTUMIE RASILIMALI ZILIZOTOLEWA KUFANYA KAZI”


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene, amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kutumia rasilimali zilizotolewa kufanya kazi kwa bidii na ufanisi.

Mhe.Simbachawene ameyasema hayo mapema leo Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo kilichokutana kwa lengo la kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na makisio ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Aliendelea kusema kuwa, Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu sana mahala pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Watumishi, na alibainisha kuwa, Serikali inazingatia sana suala la Wizara na Taasisi zake kuwa na mabaraza ya wafanyakazi kwani, yanaanzishwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za Idara, Taasisi na Wizara  ili kuweza kusimamia kazi na rasilimali watu.

Alibainisha kuwa mabaraza haya yana majukumu ya kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi, masilahi ya wafanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi. Wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, pia wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya utendaji wa kazi yenye tija, staha na upendo.

Ameshauri menejimenti kupitia baraza hilo la wafanyakazi, kuwa na utaratibu mzuri wa kuwapongeza wafanyakaki wanaotekeleza majumu yao kwa uweledi, ”kuna watumishi ambao kufaya kazi kwa weledi na biidii, na kuwahudumia wananchi kwao ni kama sehemu ya ibada.” Alifafanua

Aliendelea kusema kuwa Utumishi wa umma wa zama hizi ni watu wenye ueledi,wasomi na wenye wasifu mkubwa,lakini wanashindwa kuuonesha kutokana na mazingira kutokuwa rafiki,aliwaasa watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi ya umma kwa bidii.”Jukumu kubwa kwa ninyi viongozi ni kuwahudumia wadogo ili waweze kuleta matoke.”alisema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi aliwashukuru watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza majukumu yao na kusimamia shughuli mbali mbali za serikali kwa kujituma na kwa ufanisi mkubwa.

 

Read More

Thursday, February 23, 2023

TANZANIA YA KWANZA KUSAINI MKATABA WA KITUO CHA HUDUMA YA DHARURA CHA MAAFA MIONGONI MWA NCHI ZA SADC

 


Tanzania imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu na oparesheni za dharura za kanda.

Akizungumza mapema hii leo wakati wa hafla ya utiaji Saini iliyofanyika Jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.

Aliongeza kuwa, Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa  na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi tarehe 21 Juni, 2021.

“Lengo la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa.” Alifafanua.

Aliendelea kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi; Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.

 

Awali mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt Phiness Matto, alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri itavyowezekana.

“Natoa Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea nchi 11 kusaini mkataba huu” Alifafanua Dkt Matto.

Read More

Friday, February 17, 2023

DKT.JINGU:WAKULIMA TUONGEZE MSUKUMO WA KUFANYA KILIMO CHENYE TIJA.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ametoa rai kwa wakulima kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha teknolojia ili kuleta matokeo mazuri zaidi.

Wito huo ameutoa katika kikao cha Kamati ya Tathmini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichohusisha Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo kilichofanyika Februari 17, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Saalam.

Dkt. Jingu amesema dhamira ya Serikali ni kuona wakulima wanatumia rasilimali kidogo na kupata faida zaidi.

Aliongezea kuwa Serikali itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kufanya katika kuimarisha sekta ya Kilimo na Mifugo ili kuongeza ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

“Mwelekeo ni kwamba shughuli wanazofanya ziwe na mwelekeo wa kibishara kwa maana kilimo ni biashara na uvuvi ni biashara,” alisema Dkt.Jingu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema Uvuvi wetu bado tunatumia mbinu za zamani lakini sasa tunaenda kutoa boti mpya za kisasa zitakazofanya wavuvi waongeze tija.

Ameongeza kusema kuwa, jitihada hizo zinaenda sambamba na kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwenye vizimba katika ziwa Viktoria kwa kuwapatia vizimba vya samaki na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki.

“Lengo ni kuongeza uzalishaji wa samaki na kutimiza malengo tuliyopewa na Mhe. Rais wa kuongeza tani za uzalishaji wa samaki ifikapo Mwaka 2026,” alisema Dkt.Madalla

Aidha Serikali itaenda kutoa mikopo kwa wakulima wa zao la Mwani katika ukanda wa Pwani ili waweze kununua vifaa na waweze kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani.

"Tunaimani zao hili litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua kipato na kuboresha maisha hasa kwa wakina mama ambao ndiyo wakulima wakubwa wa zao la Mwani na vyote hivi ni katika utekelezaji wa Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili,"alisisitiza Dkt. Madalla

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema Mpango wa Usimamizi na Ushauri wa Program ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ni mpango jumuishi unaohusisha wizara kupitia Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi  ambayo yanajihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na uwekezaji.

 

Read More

Thursday, February 16, 2023

MEJA JENERALI MBUGE: TUTAENDELEA KUJIPANGA KATIKA KUKABILANA NA MAAFA NCHINI


 SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuweka mikakati madhubuti katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini ili kuhakikisha inapunguza madhara yatokanayo na maafa.

 

Kauli hiyo imetolea na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua kikao kazi cha wadau cha kupitia na kujadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya African Dream Jijini Dodoma.

 

Kikao kazi hicho kililenga kupitia na kujadili rasimu ya mpango huo wenye malengo ya  kusimamia mawasiliano na kuweka utaratibu wa matumizi ya huduma za mawasiliano ndani ya Serikali, Umma, Wadau wa Mawasiliano na Mashirika Binafsi.

 

Meja Jenerali Mbuge alisema, upo umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote wa masuala ya maafa nchini kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kuwa na mikakati madhubuti ya mawasilino wakati wa dharura.

 

“Hakikisheni kuwa mpango unazingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 na Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa 2022 ili kurahisisha utekelezaji wake,”alisisitiza Meja Jenerali Mbuge.

 

Akieleza kuhusu Mpango huo, alisema utarahisisha mawasilino ya haraka, sahihi na kwa wakati unaohitajika kwa kuzingatia mfumo huo uliojikita kidijiti na unahusisha vyombo vya habari ikiwemo matumizi ya radio, televisheni na mitandao ya kijamii.

 

Katika hatua nyingine Idara imeendelea kuchukua hatua za kupunguza madhara kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za dharura zinatolewa kwa wakati kwa kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya kitaifa na kisekta. Juhudi hizi zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi, Mashirika ya kimataifa na Asasi zisizo za kiserikali.

 

“Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inajukumu la kuratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini,”alisema.

 

Idara ya maafa ilizindua nyaraka za usmamizi wa maafa nchini ikiwemo; Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura 2022 ambao umelenga kuhakikisha utendaji kazi, ushirikiano, na mwendelezo wa mawasiliano vinaimarika wakati wa maafa ili kuruhusu watoa huduma za dharura kufanya mawasiliano baina yao na ngazi nyingine za serikali wakati wote, hata pindi miundombinu ya mawasiliano itakapoharibiwa


Read More

Friday, February 10, 2023

WAZIRI MKUU AZINDUA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.

Amesema pamoja na uwepo wa sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, wakati akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Nyaraka zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022).

Nyaraka nyingine ni Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022), Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

Amesema miongozo na mipango hiyo ya usimamizi wa maafa inatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza.

Waziri Mkuu amesema nchi bado inao uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.

“Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu, tuwe sehemu ya watendaji wakati wa dharura zinapojitokeza badala ya kusubiri tuanze kulaumu. Wale wenye nguvu na uwezo wa kusaidia wajitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali badala ya kuwa watazamaji mfano ilipotokea ajali ya ndege wananchi walijitokezakusaidia.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya usimamizi wa maafa.

Pia, Waziri Mkuu amezielekeza wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine zitenge fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za usimamizi wa maafa katika maeneo yao. “Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya nendeni mkasimamie kikamilifu bajeti katika maeneo yenu ili kuwezesha usimamizi wa maafa.”

Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa watenge rasilimali kabla ya kutokea kwa maafa na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejijengea uwezo wa kukabiliana na maafa hayo, pia sekta zote zilizopewa majukumu ya kusimamia maafa zihakikishe zinaratibu upatikanaji wa msaada wa kitaalamu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.

Kwa upande wake, Muwakili Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi Veronica ameihakikishia Serikali kuwa UNDP pamoja na wadau wengine wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na maafa.

Amesema nyaraka hizo zilizozinduliwa leo zitasaidia katika upatikanaji wa taarifa za maafa kwa wakati na hivyo kuwawezesha wahusika kuchukua hatua haraka.

 

Read More

Tuesday, February 7, 2023

WAZIRI MKUU MGENI RASMI UZINDUZI WA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA.

 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa nchini tarehe 09 Februari, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage uliopo Hazina Jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipokutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya habari Bungeni Dodoma kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi.

Waziri Simbachawene alisema, katika kuendeleza juhudi za kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Maafa Nchini, Serikali imefanya mapitio ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2012), Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2012) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2015-2020). Hivyo, mapitio hayo yamewezesha kuandaliwa kwa nyaraka tano zitakazozinduliwa ikiwemo;Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022),Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa (2022) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027),Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

“Nyaraka zote tano zimeandaliwa kwa kushirikisha wadau ndani na nje ya Serikali. Nyaraka zinazozinduliwa zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na baadaye katika mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa,”alisema Waziri.

Alifafanua kuwa, mipango na mikakati iliyoandaliwa itaimarisha usimamizi wa maafa yanayosababishwa na majanga ya nguvu za asili kama vile mafuriko na matetemeko ya ardhi na majanga yanayochochewa na shughuli za kibinadamu.

Aidha, Majukumu ya utendaji yanazingatia taasisi yenye wajibu wa kisheria, ujuzi pamoja na rasilimali zinazohitajika. Mfumo uliopo umezingatia wajibu wa sekta kutambua hatari za maafa katika eneo lake, kutenga rasilimali za kisekta kabla ya tukio kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabili maafa endapo yatatokea.

Aliongezea kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha shughuli za kuratibu na kusimamia shughuli za maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na Kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na miongozo, mikakati na taratibu za kiutendaji zinazowezesha utekelezaji wa majukumu na kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano wa wadau.

Read More

Friday, February 3, 2023

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU NAMMA YA KUPATA CHAKULA CHA MSAADA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema maswala ya upungufu wa chakula yanachukuliwa kama maafa kwa mujibu ya sheria ya maafa iliyopo.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati akifafanua hoja iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Yahaya Ally Mhata Bungeni  katika Mkutano wa Kumi Kikao cha Nne cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu taratibu za kufuata ili kupata chakula cha bei nafuu.

Alisema kuwa, Ofisi yake inajukumu ya kuratibu upatikanaji wa chakula cha msaada kwa kushirikiana na sekta tofauti tofauti ikiwemo hatua zote muhimu za uzalishaji, upatikanaji hadi matumizi kwa walaji.

Alifafanua Ofisi ya Waziri Mkuu inajukumu la kutoa kibali kwa ajili ya chakula cha bei nafuu au msaada linaratibiwa kwa kuielekeza Wizara ya Kilimo kuchukua hatua kupitia NFRA.

 “Kimsingi jukumu la kutoa chakula cha bei nafuu au msaada ni jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo inalitekeleza kwa kuelekeza Wizara ya Kilimo ili ielekeze NFRA kupeleka eneo la kukipeleka kile chakula na kwenda kukiuza kwa bei nafuu iliyopangwa,” alisisitiza waziri.

Read More

KATIBU MKUU KASPAR MMUYA ATETA NA WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU

 


Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wametakiwa kutumia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali pamoja na Busara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

 

Hayo yamesema na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  Bw. Kaspar Mmuya.

 

Bw. Mmuya alisema ameitumikia Ofisi hiyo na kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja kwa lengo la kuleta matokeo chanya.

 

“Kwa majukumu ya Ofisi hii jinsi yalivyo yalitupa nafasi sisi wengine ya kujua wizara nyingine zinafanya nini katika kutekeleza majukumu ya Serikali kwa ujumla,”alisema Katibu Mkuu huyo.

 

Pia amewahimiza  watumishi wa Ofisi hiyo kuishi kwa upendo na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu hatua itakayochochea maendeleo ya Taifa na shughuli za Serikali kufanyika katika hali ya ubora na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Sambamba na hilo, Bw. Mmuya alimshukuru Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu kwa kumfundisha, kumuongoza na kumpa ushirikiano wakati wote alipokuwa akitumikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu katika ofisi hiyo.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu  Dkt. John Jingu alisema kuwa Katibu Mkuu Mmuya alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa matokeo hivyo  watumishi kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa  kufanya kazi kama timu katika kuitumikia Nchi, kuishi na watu vizuri.

 

 “Tujitahidi kila wakati kufanya kazi kwa matokeo, uliyaishi matokeo na unaendelea kutukumbusha tuyaishi hayo, kila mtu ana nafasi yake lakini lazima kuheshimiana na kujua umuhimu wa kuwajibika, tuendelee kufanya kazi kwa matokeo weledi ushirikino na nidhamu sisi ni timu moja tushirikiane.” Alisisitiza Dkt. Jingu.

 

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Katibu wa  TUGHE tawi la  Ofisi hiyo Bw. Dotto Kyaolang amemshukuru Katibu Mkuu Mmuya kwa kutoa dira ya utendaji kazi na kumtakia afya njema na utendaji mwema katika kituo chake kipya cha kazi.

 

 

Read More

Sunday, January 29, 2023

DKT.JINGU: MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YATUMIKE KATIKA MIPANGO YA MAENDELEO.

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Utatibu Dkt. John Jingu ameeleza ni muhimu kuyatumia matokeo ya sensa ya watu na maakazi ya mwaka 2022 katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu.

Ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha 9 cha Kamati ya Ushauri ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa ajili ya kupitia baadhi ya ripoti za matokeo ya Sensa zilizo kamilika kabla ya kuzinduliwa.Kikao kilifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Dar es Salaam.

Jukumu kubwa la Kamati hiyo ni kuishauri Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa inayoongozwa na Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar namna bora ya utekelezaji wa masuala ya sensa.

=MWISHO=

Read More

Thursday, January 26, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE: IMARISHENI MIFUMO WA USHUGHULIKIAJI WA MATUKIO YA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO.

Serikali yahimiza jamii  kuanzia ngazi ya familia kuimarisha mfumo wa ushughulikiaji wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ndani na nje ya shule unaowajumuisha wasimamizi wa shule, wazazi, walezi na jamii kwa lengo kuendelea kutokomeza matukio ya ukatili nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika Mkutano wa Kitaifa wa tafakuri ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) uliofanyika katika Ukumbi wa Saint Gaspar Jijini Dodoma.

Waziri ameeleza kwamba Mfumo wa Ushughulikiwaji wa matukio ya ukatili utasaidia Taifa kupunguza kwa kiasi kubwa changamoto iliyopo katika jamii ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa Watoto.

“tuendelee kuunga mkono juhudi za Serikali kwa hali na mali ili kuhakikisha makundi yote ndani ya jamii yanalindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto alisema,” alisema Waziri Simbachawene.

Akieleza kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989, wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto 2008 na Sheria ya Mtoto Na. 21, 2009, ambao unaoelezea masuala ya ukatili kwa watoto ni kinyume cha haki zao za msingi za kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kutokubaguliwa.

Aidha umeeleza kuwa,vitendo vya ukatili vinarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 ambayo nchi imeridhia kutekeleza.

Waziri amehimiza kuendeleza juhudi za kukabiliana na ukatili huo katika zama za utandawazi kuwa na msukumo mpya na wa pamoja ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.

Amesema kuwa, athari za utandawazi zimedhoofisha mifumo ya ulinzi na usalama wa watoto hivyo kufanya kundi hilo kutokuwa salama kwani tatizo la ukatili bado ni changamoto katika ngazi zote.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake  na Makundi Maalum  Mhe. Dorothy Gwajima amesema wizara ya Maendeleo ya jamii imekuwa ikiratibu utekelezaji wa MTAKUWWA toka kuzinduliwa kwake mwaka 2016, na baada ya kukamilika kwake Wizara pamoja na Wadau wa maendeleo walifanya tathimini ya utekelezaji wake kuanzia 2017/2018 hadi 2021/2022 kupitia Mtaalam mwelekezi Chuo Kikuu cha Dodoma.

Waziri amesema taarifa ya tathimini imekamilika na imebainisha utekelezaji wa MTAKUWWA kwenye maeneo yote nane yalliyopo kwenye mpango huu, na imebainishwa maeneo muhimu yatakayoenda kutekelezwa kwenye mpango kazi ujao.

“Niwaombea wadau tuwe na subira tukiwa tunaendelea mapitio ya pamoja mpaka itakapotangazwa kwamba serikali pamoja na wadau,”aliomba Waziri Gwajima

Naye Mkurugenzi wa Shirika la ICS Tanzania Bwn.  Kudely Sokoine  Joram amesema wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha mapambano haya yanatokomezwa huku akiipongeza Serikali kwa hatua inazochukua katika kukabiliana na changamoto ya ukatili wa makundi haya muhimu huku akitaja maeneo muhimu ikiwemo la kuimarisha mifumo ya ulinzi wa Wanawake na Watoto, kujenga uwezo wa Kamati za ulinzi wa Wanawake na watoto pamoja na kusaidia uratibu wa Masuala yote.

Read More

Thursday, January 19, 2023

"TATUENI CHANGAMOTO ZA WANANCHI," WAZIRI SIMBACHAWENE.

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amewataka watendaji wa Serikali kuendelea kutatua changamoto za wananchi zinazowakabili ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kujenga uwezo kwa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Idara ya  Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikalini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi uliopo Njedengwa Jijini Dodoma Januari 19, 2023.

Waziri alihimiza kila mtendaji wa Serikali kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akitatua changamoto za wananchi katika eneo lake la kazi.

Aliongezea kuwa ni muhimu kwa watendaji kuwajibika kwa kuyafikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita huku wakileta matokeo chanya yatokanayo na utendaji mzuri wa kazi zao za umma.

"Hakikisheni mnakuwa watu wa  msaada kwa wengine katika kuyatekeleza majukumu yenu, muwe watengeneza furaha na hii iwe kipimo kwa kila mwenye kukufikia huku ukizingatia taratibu za utumishi wa umma na sheria zilizopo,"alisema Waziri Simbachawene

Aidha aliwaasa waendelee kutumia taaluma zao kuleta matokeo chanya kwa Serikali na jamii huku wakijitathimini utendaji wa kila siku.

 “Ni sahihi kujitathimini kila iitwapo leo ili kuona namna unavyoleta matokeo chanya kwenye utendaji wako wa kila siku, matokeo utayoyapata  yatatusaidia kuongeza tija ,” alisisitiza Waziri Simbachawene.

Akieleza umuhimu wa mafunzo hayo aliwataka kuhakikisha mafunzo  yanawafikia watendaji katika ngazi zote ili kuendelea kuongeza uelewa kwa watumishi wa umma.

" Mafunzo haya yawafikie watumishi wote katika Idara na vitengo vyetu bila kumuacha nyuma mtu yeyote ili kuleta chachu katika utendaji na  kuondokana na tabia ya mazoea," alisema.

Aliongezea kuwa matokeo ya Mafunzo haya yatumike kuboresha mifumo ya uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali ili kuwa na uwezo wa kupima utendaji wa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali kisayansi.

Aidha uwekwe utaratibu ambao utawezesha uchambuzi wa Taarifa za kisekta na kutoa mrejesho wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa au kupewa msukumo zaidi.

 "Ili kuendelea kuboresha shughuli za uratibu naamini uwepo Idara mpya ya Ufuatiliaji na Tathmini itasimamia hili na kuhakikisha kunakuwa na mrejesho kwa Wizara na Taasisi zote ili kuimarisha uwajibikaji," alihimiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu  amesema mafunzo haya yanalenga watendaji wa serikali kufanya kazi kwa ufanisi kwa weledi na kwa namna ambayo itakidhi mahitaji pia yatajikita katika majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu  katika eneo la uratibu wa shughuli za serikali, na jukumu la kufanya kazi ya ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa  shughuli za Serikali.

 

Read More

Tuesday, January 17, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE, ARIDHISHWA NA HATUA ZA UJENZI KIWANDA KIPYA CHA MPIGA CHAPA MKUU WA SERIKALI

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu  ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kiwanda  cha kupiga chapa cha serikali ambacho mpaka sasa msingi wa jengo na ujenzi wa boma la jengo; kuta, kupiga plasta na kupauwa vimeshafanyika.

“Hiki kiwanda tunatarajia kukifunga mitambo na mashine za kisasa ili kiweze kufanya jukumu la kuchapa nyaraka za Serikali na  shughuli za Mpiga Chapa ziweze kufanyika kwa ufanisi.”

Kauli hiyo ameitoa alipotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kilichopo Kisasa katika Jiji la Dodoma.

Ofisi hii ni muhimu sana kwa nchi, ni lazima iwe Ofisi bora kwa sababu nyaraka nyingi za siri za serikali zinapaswa kuchapwa na Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali,

Waziri Simbachawene amempongeza Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho cha mpiga chapa wa serikali kwa kiasi cha billioni 1.88

“Serikali imetoa pia kiasi cha million kiasi cha millioni 350 ambazo zitatumika kufanyia ukarabati kiwanda na Mashine za Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kiasi kingine cha shilingi billioni 1.4 kwa ajili ya kununua malighafi kwa viwanda vinavyondelea na uzalishaji, cha Dodoma na Dar es salaam.”

Amefafanua kiwanda kipya cha Dodoma cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali imetoa kiasi cha shilingi billioni 3.9 ambayo itasaidia kununua mitambo mipya na ya kisasa ili kuhakikisha nyaraka zote muhimu za serikali zinachapishwa katika kiwanda hicho.

“Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa na Mhuri ni vitu ambavyo vimewekwa katika uangalizi wa Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.”

Naye Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bwn. George Lugome ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali  kwa kuiwekea majengo yenye uwezo wa kuwa na miundo mbinu mizuri na mashine za kisasa ambazo zitasaidia kuchapa nyaraka zenye alama ya siri.

“Sheria ya alama za Taifa ya mwaka 1971 inatamka wazi kabisa kwa yoyote anayekiuka au anaibadili nembo ya Taifa au alama za Taifa anastahili kupewa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela,” amesema Bwn, Lugome.

Ametoa wito kwa taasisi binafsi zinazotaka kujihusisha na uchapaji wa nyaraka  kuhakikisha wanathibitishwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Usalama ya Serikali ili waweze kupata kibali.

 Read More

JAMII YA WATANZANIA IPEWE ELIMU YA KUTOSHA JUU YA URAHIBU WA DAWA ZA KULEVYA.

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe.  George Simbachawene ametoa wito kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma juu ya athari za dawa za kulevya kwa vijana na wanachi wote kwa ujumla.

Hayo ameyasema alipotembelea na kujionea eneo la Hekta saba ambalo linatarajiwa kujengwa jengo la Makao Makuu ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kati, katika eneo la Itega Jijijni Dodoma.

 “lazima tuvunje ukimya na tuongeze udhibiti wa matumizi ya bangi, hatuwezi kudhibiti matumizi ya bangi kwa kutegemea mamlaka pekee yake lazima tuweke mfumo na uratibu kwa kuanza kudhibiti kuanzia ngazi ya kijiji, Kata na Wilaya.” Amesema Simbachawene.

 Tufike mahali tuone tunauwa Taifa; Vitu vingi vinavyotokea kwenye familia, na matokeo ya ajabu ya unyanyasaji msukumo wake ni matumizi ya madawa ya kulevya na ukipata urahibu unashindwa kuisadia jamii, unashindwa kuwajibika kwenye familia unashindwa kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Waziri Simbachawene, ameongeza kuwa aina mpya ya Urahibu wa kucheza Kamari (Kubeti) ambayo inawakumba watu wote, na ina madhara kama urahibu wa madawa ya kulevya, lazima tujipange.

Kila mmoja ni shahidi watu wanapokuwa wanafanya Kamari ya kubahatisha, kwenye michezo ya mpira, hata kufanya kazi hawawezi, muda wote ni kuangalia mkeka tuu(kubeti)

Aidha kuna umuhimu wa kuziunganisha kwa kuziimarisha Taasisi zetu hizi za Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na Mamlaka wa Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kisera na kisheria ili ziweze kushirikiana vizuri katika utendaji wa kazi.

Naye Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  Jenerali Gerald Kusaya amesema  katika Mwaka huu wa fedha serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeweza kupeleka Vyuo vya Ufundi warahibu  walioachana na matumizi ya  dawa za kulevya wapatao 245 wanaolipiwa ada zote na Ofisi ya Waziri Mkuu na kila mmoja amechagua kitu anachotaka kusoma ili watakapomaliza warudi mtaani na waweze kuanza kujitegemea na kujenga uchumi wa nchi.

Katika kuhitimisha ziara hiyo kamishna Jenerali Kusaya ameomba serikali kuwasaidia  warahibu wanaohitimu mafunzo ya Ufundi stadi na stadi za kazi kupewa vitendea kazi vitakavyowasaidia pindi watakaporudi kwenye jamii yao

Jumla ya warahibu wapatao 12,800 wanatarajia kuhitimu mafunzo kutoka kwenye vyuo vya ufundi wakiwa na ujuzi wa stadi mbalimbali za kazi na kuweza kujitegemea na kujenga uchumi.

 

 

Read More

Monday, January 16, 2023

TAASISI ZINAZOENDELEA NA UJENZI WA OFISI ZATAKIWA KUKAMILISHA MAJENGO YAO KWA WAKATI JIJINI DODOMA


Serikali imeziagiza Taasisi zote zinazoendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi zao Jijini Dodoma kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa kuzingatia taratibu zote za ujenzi ikiwemo ubora, muda, bajeti iliyotengwa na thamani ya fedha ili kuleta tija inayotarajiwa.

Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George simbachawene wakati wa hafla ya kukabidhi Vibali vya Ujenzi wa Ofisi za Taasisi za Serikali Dodoma iliyofanyika katika Ukumbi wa Hazina mapema.

 

Waziri Simbachawene amesema, kila Taasisi ya Serikali ihakikishe inajenga majengo ya Ofisi zake ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamishia Makao makuu yake Dodoma na kuifanya Dodoma kuwa eneo lenye ufanisi.

 

“Taasisi zote zilizoelekezwa kuhamia Dodoma kwa mujibu wa ratiba niliyoitoa leo zihakikishe zinatekeleza maagizo hayo na Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe wanasimamia mpango kazi wa utekelezaji wake,”alisema Mhe.Simbachawene.

 

Aliongezea kuwa, Mpango huu ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 151 chini ya kifungu (a), (b) na (c) vinavyoielekeza Serikali kutunga Sheria ya kuitambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi na kuhakikisha kwamba majengo ya Wizara na Taasisi yanajengwa Dodoma badala ya Dar es Salaam.

Aidha Waziri ameagiza Ofisi ya Katibu Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Mamlaka husika kuendelea kuratibu Mpango wa Serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii Dodoma.

Sambamba na hilo, Serikali imekamilisha ratiba na mwongozo utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado zinaendelea kutekeleza majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli zao Jijini Dodoma kwa awamu.

“Katika utekelezaji wa suala hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwamba Taasisi 42 zihamie Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2022/23; Taasisi 36 zitahamia Dodoma katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/24 na Taasisi 19 zitahamia katika mwaka 2024/25 wakati Taasisi 27 zimeelekezwa, kwa kuzingatia aina ya majukumu zilizonazo, kuendelea kutekeleza majukumu yake Mkoani Dar es Salaam.” Alieleza.

Alisisitiza kuwa, hatua hii itakamilisha sehemu kubwa ya Mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma ambapo hadi sasa tayari Taasisi 65 zilishahamia Dodoma tangu mwaka 2016 hadi 2022.

Waziri ameziagiza Taasisi nyingine ambazo bado hazijaanza maandalizi ya ujenzi wa Ofisi za serikali Dodoma ziwasilishe Ofisi ya Waziri Mkuu Mahitaji ya Viwanja vya ujenzi wa Ofisi za taasisi Dodoma kwa ajili ya uratibu wa pamojal.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya kuwezesha taasisi kuwepo.

 

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa mnayoifanya kwa kupanga makao makuu ya serikali yetu yanakuwa ni mji wa kisasa na mji uliopangwa.”alisema Mhe. Rosemary

 

Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt, John Jingu akitoa taarifa ya utekelezajia amesema Ofisi ya waziri Mkuu imeidhinisha vibali 55 kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2018 kati ya hizo taasisi 20 zimekamilisha ujenzi, taasisi 16 zinaendelea na ujenzi na taasisi 19 zimeanza maandalizi ya ujenzi.

“Majengo haya yanajengwa katika maeneo mbalimbali, na ujenzi huu unazingatia mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.”

Read More

Wednesday, January 11, 2023

SERIKALI YATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO YA MAJI MKOANI MBEYA

Serikali Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu imetoa msaada kwa wananchi walioathirika na Maafa ya Mafuriko ya Maji Mkoani Mbeya, yaliyosabisha nyumba kubomoka, kuharibika kwa vifaa, vyakula, uharibifu wa mifugo na mazao yaliyoko mashambani.

“Msaada huo unajumuisha Magodoro 300 kwa kuanzia, mablanketi 1200 ya wakubwa na wadogo, mikeka 600, madumu ya maji, sufuria bakuli sahani pamoja na vijiko kwa kila familia ambayo imeathirika.”

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipotembelea maeneo yaliyoathirika wa mafuriko ya mvua katika kata saba Mkoani Mbeya kutokana na Mvua zilizonyesha  terehe 07/01/2023.

“Kwa mujibu wa sheria no. 6 ya Maafa ya Mwaka 2022 sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tunayo dhamana ya kuwaunganisha wadau ili kuwasaidia watu walioathirika na tutafanya hivyo kwa kutumia Ofisi zetu za Mkoa na wilaya, naomba wadau wote wa ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya kutusaidia ili kuhakikisha watu hawa wanarudi katika hali yao.”

Natoa pole kwa wote walioathirika, TARURA kwa kushirikiana TANROAD Halmashauri ya jiji  la Mbeya na Halmashauri ya Mbeya vijijini wahakikishe wanaenda kuona kwenye vyanzo kuangalia ni eneo gani maji yametoka kwenye mkondo wake wa asili.

Akimkaribisha Waziri wa Nchi, Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson ameishukuru serikali kwa mchango iliyoutoa kwa  waathirika wa mafuriko ya Mvua Mkoani Mbeya .

“Naomba sisi kama Halmashauri tusitoe vibali vya ujenzi kwenye  maeneo ambayo ni mikondo ya maji, kwa sababu athari za mafuriko zinarudisha nyuma  maendeleo ya uchumi kwa wananchi”

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera katika taarifa yake amesema watu waliopata athari za mafuriko ya maji, kaya 281 zenye watu idadi ya watu 1405 ambao wanahitaji chakula takribani tani 50 kwa miezi mitatu ili ziweze kuwasaidia.

 

Read More